Maandiko Matakatifu
Mosia 2


Mlango wa 2

Mfalme Benjamini anahutubia watu wake—Anawakumbusha kuhusu haki, wema, na ustawi wa kiroho wa utawala wake—Anawashauri wamtumikie Mfalme wao wa Mbinguni—Wale ambao wanamuasi Mungu, watateseka kwa huzuni iliyo kama moto usiozimika. Karibia mwaka 124 K.K.

1 Na ikawa kwamba baada ya Mosia kutenda kulingana na vile baba yake alivyomwamuru, na kutangaza nchini kote, kwamba watu walikusanyika pamoja nchini kote, ili waende kwenye hekalu kusikia maneno ambayo mfalme Benjamini atawaelezea.

2 Na walikuwa idadi kubwa, hata kuwa wengi sana kwamba hawakuhesabika; kwani walikuwa wameongezeka zaidi na kuwa wengi katika nchi.

3 Na pia walichukua malimbuko ya mifugo yao, ili watoe dhabihu na sadaka za kuteketezwa kwa moto kulingana na sheria ya Musa;

4 Na pia kwamba wamtolee Bwana Mungu wao shukrani, ambaye alikuwa amewaleta kutoka nchi ya Yerusalemu, na ambaye alikuwa amewakomboa kutoka mikono ya maadui zao, na kuwachagulia watu wenye haki kuwa walimu wao, na pia mtu mwenye haki kuwa mfalme wao, ambaye alikuwa ameanzisha amani katika nchi ya Zarahemla, na ambaye aliwafundisha kutii amri za Mungu, ili washangilie na kujazwa na upendo kwa Mungu na kwa watu wote.

5 Na ikawa kwamba walipowasili kwenye hekalu, walipiga hema zao kando yake, kila mtu kulingana na jamii yake, akiwa na mke wake, na wanawe, na mabinti zake, na wana wao, na mabinti zao, kutoka mkubwa hadi kwa aliye mdogo, kila jamii ikiwa imetengana na nyingine.

6 Na wakapiga hema zao na kuizingira hekalu, kila mtu akielekeza mlango wa hema lake kwenye hekalu, ili wakae ndani ya hema zao na kusikia maneno ambayo mfalme Benjamini angewazungumzia;

7 Kwani umati ulikuwa mkubwa sana hata kwamba mfalme Benjamini hangeweza kuwafundisha wote katika kuta za hekalu, kwa hivyo akaamuru mnara ujengwe, ili watu wake wasikie maneno ambayo angewazungumzia.

8 Na ikawa kwamba alianza kuwazungumzia watu wake kutoka mnarani; na wote hawangeweza kusikia maneno yake kwa sababu ya wingi wa umati; kwa hivyo akasababisha kwamba maneno aliyozungumza yaandikwe na kupelekwa miongoni mwa wale ambao hawakuwa karibu na sauti yake, ili wao pia wapokee maneno yake.

9 Na haya ndiyo maneno aliyozungumza na kusababisha yaandikwe, akisema: Ndugu zangu, nyote ambao mmekusanyika pamoja, ninyi ambao mtasikia maneno yangu ambayo nitawazungumzia leo; kwani sijawaamrisha kuja hapa ili kuchezacheza na maneno ambayo nitawazungumzia, lakini kwamba mnisikilize, na mfungue masikio yenu ili msikie, na mioyo yenu ili mfahamu, na akili zenu ili siri za Mungu zifunguliwe machoni mwenu.

10 Sijawaamuru kuja hapa ili mniogope, au kwamba mnidhanie kwamba mimi mwenyewe ni zaidi ya binadamu.

11 Lakini mimi niko kama ninyi, kwa unyonge wa kila aina mwilini na akilini; walakini nimechaguliwa na watu hawa, na kutakaswa na baba yangu, na nikaruhusiwa kwa mkono wa Bwana kwamba niwe mtawala na mfalme wa watu hawa; na nimelindwa na kuhifadhiwa kwa uwezo wake usio na kipimo, ili niwatumikie kwa uwezo wote, na nguvu ambazo Bwana amenipatia.

12 Ninawaambia kwamba kwa vile nimekubaliwa kuwatumikia ninyi maishani mwangu, hata hadi sasa, na sijatazamia kupata faida ya dhahabu au fedha au aina yoyote ya utajiri kutoka kwenu;

13 Wala sijaruhusu kwamba mfungwe gerezani, wala ninyi wenyewe kuwafanya wengine watumwa, wala kuua, au kupora, au kuiba, au kuzini; wala hata mimi sijawaruhusu kwamba mtende aina yoyote ya uovu, na nimewafundisha ninyi kwamba mtii amri za Bwana, katika vitu vyote ambavyo amewaamuru—

14 Na hata mimi, mwenyewe, nimefanya kazi kwa mikono yangu mwenyewe ili niwatumikie ninyi, na kwamba msilemewe na makodi, na kwamba msipatwe na chochote ambacho hamuwezi kuvumilia—na ninyi ni mashahidi leo, kwa vitu vyote ambavyo nimewazungumzia siku hii.

15 Lakini, ndugu zangu, sijatenda vitu hivi ili nijivune, wala sisemi vitu hivi ili niwalaumu; lakini nawaambia vitu hivi ili mjue kwamba sina lawama katika dhamira yangu mbele ya Mungu siku ya leo.

16 Tazama, nawaambia kwamba kwa sababu niliwaambia kuwa nimewatumikia maishani mwangu, sitamani kujivuna, kwani nimekuwa tu katika utumishi wa Mungu.

17 Na tazama, nawaambia vitu hivi ili mpate hekima; ili mjifunze kwamba mnapowatumikia wanadamu wenzenu mnamtumikia tu Mungu wenu.

18 Tazama, mmeniita mfalme wenu; na kama mimi, ambaye mnaniita mfalme wenu, ninajichosha kuwatumikia, je, haiwapasi nanyi kujichosha kutumikiana?

19 Na tazama pia, kama mimi, ambaye mnaita mfalme wenu, ambaye amewatumikia siku zake zote ninyi, na walakini amekuwa katika utumishi wa Mungu, ninastahili shukrani kutoka kwenu, Je, inawapasa jinsi gani ninyi kumshukuru Mfalme wenu wa mbinguni!

20 Ninawaambia, ndugu zangu, kwamba kama mtamtolea shukrani zote na sifa ambazo nafsi zenu zote zina uwezo wa kuwa nazo, Mungu aliyewaumba, na aliyewaweka na kuwahifadhi, na kuwasababisha ninyi kufurahi, na kuwezesha kwamba ninyi muishi kwa amani kati yenu—

21 Ninawaambia kwamba kama mtamtumikia yule ambaye aliwaumba tangu mwanzo, na anawahifadhi siku kwa siku, kwa kuwaazima pumzi, kwamba muishi na mtembee na kutenda kulingana na nia zenu, na hata kuwasaidia muda kwa muda—nasema, kama mtamtumikia kwa nafsi zenu zote kwa jumla bado mtakuwa watumishi wasioleta faida.

22 Na tazama, yote ambayo anahitaji kutoka kwenu ni kutii amri zake; na amewaahidi kwamba kama mtatii amri zake mtafanikiwa nchini; na kamwe hageuki kutoka kwa yale aliyosema; kwa hivyo, kama mtatii amri zake atawabariki na kuwafanikisha.

23 Na sasa, kwanza, amewaumba, na kuwapatia uhai wenu, ambao anawadai.

24 Na cha pili, anahitaji kwamba ninyi mtende yale ambayo amewaamuru; kwani kama mtatenda hivyo, atawabariki papo hapo; na kwa hivyo amewalipa. Na hivyo basi bado anawadai, na hata sasa, na baadaye hadi milele na milele; kwa hivyo, je, mna nini ambacho mnajivunia?

25 Na sasa nauliza, je mnaweza kujiongezea chochote wenyewe? Ninawajibu, Hapana. Hamwezi kusema mko hata kuzidi mavumbi ya dunia; ingawa mliumbwa kutoka mavumbi ya dunia; lakini tazama, ni yake yule aliyewaumba.

26 Na mimi, hata mimi, ambaye mnaniita mfalme wenu, sio bora zaidi ya vile mlivyo; kwani mimi pia nilitoka katika mavumbi. Na mnaona kwamba mimi ni mzee, na ninakaribia kuupeleka mwili huu kwenye udongo.

27 Kwa hivyo, kama vile nilivyowaambia kwamba niliwatumikia, nikiwa na dhamira iliyo safi kwa Mungu, hata hivyo wakati huu mimi nimesababisha kwamba mkusanyike pamoja, ili nisipatikane na lawama, na kwamba damu yenu isiwe juu yangu, nitakaposimama mbele ya Mungu ili nihukumiwe kwa vile vitu alivyoniamrisha kuwahusu.

28 Nawaambia kwamba nimesababisha mkusanyike pamoja ili nitoe damu yenu kutoka mavazi yangu, wakati huu ambao ninakaribia kaburi langu, ili niende kwa amani, na roho yangu isiyokufa iungane na kwaya za juu katika kuimba sifa za Mungu aliye wa haki.

29 Na zaidi ya hayo, ninawaambia kwamba nimesababisha mkusanyike pamoja, ili niwatangazie kwamba siwezi kuendelea kuwa mwalimu wenu, wala mfalme wenu;

30 Kwani hata sasa, mwili wangu wote unatetemeka ninapojaribu kuwazungumzia; lakini Bwana Mungu ananisaidia, na ameniruhusu niwazungumzie, na ameniamuru kwamba niwatangazie leo, kwamba mwana wangu Mosia ni mfalme na mtawala wenu.

31 Na sasa, ndugu zangu, nataka mtende kama vile tayari mmetenda. Hadi sasa mmetii amri zangu, na pia amri za baba yangu, na mmefanikiwa, na mmelindwa kwamba msiangukie mikono ya maadui wenu, hata hivyo mkitii amri za mwana wangu, au amri za Mungu ambazo mtapewa naye, mtafanikiwa nchini, na maadui wenu hawatapata uwezo juu yenu.

32 Lakini, Enyi watu wangu, jihadharini kwamba pasiwe na mabishano miongoni mwenu, na mchague kutii pepo mchafu, ambaye alizungumziwa na baba yangu Mosia.

33 Kwani tazama, ole kwa yule anayechagua kumtii huyo pepo; kwani akichagua kumtii, na kuishi na afariki katika dhambi zake, yeye anakunywa adhabu kwa nafsi yake; kwani yeye hupokea kwa mshahara wake adhabu isiyo na mwisho, kwa sababu ya kuvunja sheria ya Mungu kinyume cha ufahamu wake.

34 Ninawaambia, kwamba hakuna yeyote miongoni mwenu, ila tu watoto wenu wadogo ambao hawajafunzwa kuhusu vitu hivi, asiyejua kwamba mnadaiwa milele na Baba wenu wa mbinguni, kumtolea yote mliyo nayo na vile mlivyo; na pia mmefundishwa kuhusu maandishi ambayo yana unabii ambao umezungumziwa na manabii watakatifu, hata hadi wakati baba yetu, Lehi, alipotoka Yerusalemu;

35 Na pia, yote ambayo yamezungumzwa na baba zetu hadi sasa. Na tazama, pia, walizungumza yale ambayo waliamriwa na Bwana; kwa hivyo, ni ya haki na kweli.

36 Na sasa, nawaambia, ndugu zangu, kwamba baada ya kujua na kufundishwa vitu hivi vyote, kama mtakosa na kutenda kinyume cha yale yaliyozungumzwa, kwamba mnajitenga na Roho wa Bwana, kwamba hana nafasi ndani yenu ili awaongoze katika njia za hekima ili mpate baraka, mafanikio, na kuhifadhiwa—

37 Ninawaambia, kwamba, yule mtu anayetenda haya, huyo ndiye ambaye anamuasi Mungu kiwazi; kwa hivyo anachagua kumtii pepo mchafu, na kuwa adui wa haki yote; kwa hivyo, Bwana hana nafasi ndani yake, kwani yeye haishi katika hekalu zisizo takatifu.

38 Kwa hivyo kama mtu huyu hatatubu, na aishi na afe akiwa adui wa Mungu, matakwa ya haki takatifu huzindua nafsi yake isiyokufa kwa hatia yake mwenyewe, ambayo humsababisha kutetemeka mbele ya Bwana, na hujaza kifua chake na hatia, na uchungu, na huzuni, ambayo ni kama moto usiozimika, ambao miale yake hupaa juu milele na milele.

39 Na sasa ninawaambia, kwamba huruma haina dai juu ya mtu huyo; kwa hivyo hukumu yake ya mwisho ni kuvumilia mateso yasiyo na mwisho.

40 Ee ninyi, watu wote wazee, na pia ninyi vijana, na ninyi watoto wachanga mnaoweza kuelewa maneno yangu, kwani nimezungumza wazi kwenu ili muweze kuelewa, naomba kwamba muamke kwa ukumbusho wa mahali pa kuogofya ya wale walioanguka kwenye dhambi.

41 Na zaidi, ningetamani mtafakari juu ya hali ya baraka na yenye furaha ya wale wanaotii amri za Mungu. Kwani tazama, wanabarikiwa katika vitu vyote, vya muda na vya kiroho; na kama watavumilia kwa uaminifu hadi mwisho watapokewa mbinguni, kwamba hapo waishi na Mungu katika hali ya furaha isiyo na mwisho. Enyi kumbukeni, kumbukeni kwamba vitu hivi ni vya kweli; kwani Bwana Mungu ameyazungumza.