Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 46


Sehemu ya 46

Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii kwa Kanisa, huko Kirtland, Ohio, 8 Machi 1831. Katika wakati huu wa mwanzo wa Kanisa, mpangilio wa aina moja wa kuendesha ibada za Kanisa ulikuwa bado hujaanzishwa. Hata hivyo, desturi ya kuwaruhusu waumini pekee na wachunguzi wa dhati wa Kanisa kwenye mikutano ya Sakramenti na mikutano mingine ya Kanisa limekuwa jambo la kawaida. Ufunuo huu unaonyesha mapenzi ya Bwana juu ya kuongoza na kuendesha mikutano na mwongozo Wake juu ya kutafuta na kutambua vipawa vya Roho.

1–2, Wazee wataendesha mikutano kama watakavyoongozwa na Roho Mtakatifu; 3–6, Watafuta ukweli yapaswa wasitengwe kwenye ibada za sakramenti; 7–12, Mwombeni Mungu na tafuteni vipawa vya Roho; 13–26, Hesabu ya baadhi ya vipawa hivyo yatolewa; 27–33, Viongozi wa Kanisa wamepewa uwezo wa kutambua vipawa vya Roho.

1 Sikilizeni, Enyi watu wa kanisa langu; kwani amini ninawaambia kwamba mambo haya yalizungumzwa kwa manufaa na mafundisho yenu.

2 Lakini licha ya mambo yale ambayo yameandikwa, daima imekuwa ikitolewa kwa wazee wa kanisa langu kutoka mwanzo, na daima itakuwa hivyo, kuendesha mikutano yote kama inavyoelekezwa na kuongozwa na Roho Mtakatifu.

3 Hata hivyo mnaamriwa kamwe msimtupe yeyote nje ya mikutano yenu ya jumuiya, ambayo hufanyika mbele ya walimwengu.

4 Pia mnaamriwa msimtupe yeyote aliye wa kanisa nje ya mikutano yenu ya sakramenti; hata hivyo, kama kuna yeyote aliyekosa, acheni asipokee hadi atakapofanya suluhu.

5 Na tena ninawaambia, hamtamtupa yeyote nje ya mikutano yenu ya sakramenti ambaye anautafuta ufalme kwa dhati—ninalisema hili juu ya wale ambao si wa kanisa.

6 Na tena ninawaambia, juu ya mikutano yenu ya uthibitisho, kwamba endapo kutakuwa na yeyote ambaye si wa kanisa, ambaye huutafuta ufalme kwa dhati, msimtupe nje.

7 Lakini mnaamriwa katika mambo yote kumwomba Mungu, awapaye kwa ukarimu, na kile ambacho Roho hushuhudia kwenu hata hivyo nataka ninyi mkifanye katika utakatifu wote wa moyo, mkitembea wima mbele zangu, mkifikiria mwisho wa wokovu wenu, mkifanya mambo yote kwa sala na shukrani, ili msiweze kudanganywa na pepo wachafu, na mafundisho ya maibilisi, au amri za wanadamu; kwani baadhi ni za wanadamu na nyingine za mapepo.

8 Kwa hivyo, kuweni waangalifu msije kudanganywa; na ili msidanganywe takeni sana karama zilizo kuu, daima mkikumbuka ni kwa nini zinatolewa;

9 Kwani amini ninawaambia, hutolewa kwa manufaa ya wale ambao hunipenda Mimi na hushika amri zangu zote, na yule atafutaye kufanya haya; ili wote waweze kufaidika wale wanitafutao au kuniomba, kwamba wanaomba na hawaombi kwa ishara ili wapate kuvitumia kwa tamaa zao.

10 Na tena, amini ninawaambia, ningetaka kwamba daima mkumbuke, na daima yawekeni katika akili zenu vipawa hivyo ni vipi, ambavyo hutolewa kwa kanisa.

11 Kwani wote hawapokei vipawa vyote; kwani kuna vipawa vingi, na kwa kila mtu kipawa kimetolewa na Roho wa Mungu.

12 Kwa wengine wamepewa kimoja, na wengine wamepewa kingine, ili wote waweze kufaidika.

13 Kwa wengine kinatolewa na Roho Mtakatifu kujua kwamba Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu, na kwamba alisulubiwa kwa ajili ya dhambi za ulimwengu.

14 Kwa wengine kimetolewa kuamini juu ya maneno yao, ili hao pia waweze kuwa na uzima wa milele kama wataendelea kuwa waaminifu.

15 Na tena, kwa wengine imetolewa na Roho Mtakatifu kujua tofauti za huduma, kama itakavyo mpendeza Bwana yeye yule, kulingana na matakwa ya Bwana, akilinganisha rehema zake kulingana na hali za wanadamu.

16 Na tena, hutolewa na Roho Mtakatifu kwa wengine kujua tofauti za kutenda kazi, kama ni za Mungu, kwamba mafunuo hayo ya Roho yaweze kutolewa kwa kila mtu kwa faida ya wote.

17 Na tena, amini ninawaambia, kwa mwingine amepewa na Roho wa Mungu, neno la hekima.

18 Kwa mwingine neno la maarifa, ili wote waweze kufundishwa kuwa wenye hekima na kuwa na maarifa.

19 Na tena kwa wengine wamepewa kuwa na imani ya kuponywa;

20 Na wengine wamepewa kuwa na imani ya kuponya.

21 Na tena, kwa wengine wamepewa kufanya miujiza;

22 Na kwa wengine wamepewa kutoa unabii;

23 Na kwa wengine kuzitambua roho.

24 Na tena, wengine wamepewa kunena kwa lugha;

25 Na mwingine amepewa tafsiri ya lugha.

26 Na vipawa hivi vyote hutoka kwa Mungu, kwa manufaa ya watoto wa Mungu.

27 Na kwa askofu wa kanisa, na kwa watu wa aina hiyo ambao Mungu atawateua na kuwatawaza kulisimamia kanisa na kuwa wazee wa kanisa, watapewa kuvitambua vipawa hivyo vyote isije pakawepo mtu miongoni mwenu akitabiri na wala isiwe kutoka kwa Mungu.

28 Na itakuwa kwamba yule aombaye katika Roho atapokea katika Roho;

29 Kwamba baadhi waweza kupewa kuwa na vipawa vyote, ili paweze kuwa na kiongozi, ili kwamba kila muumini aweze kufaidika navyo.

30 Yule ambaye anaomba katika Roho aomba kulingana na mapenzi ya Mungu; kwa sababu hiyo hufanyika kwake kama aombavyo.

31 Na tena, ninawaambia, mambo yote lazima yafanyike katika jina la Kristo, lolote mfanyalo katika Roho;

32 Na ni lazima mtoe shukrani kwa Mungu katika Roho kwa baraka zozote mbarikiwazo.

33 Na ni lazima mtende wema na utakatifu mbele zangu daima. Hivyo ndivyo. Amina.