Maandiko Matakatifu
Musa 3


Mlango wa 3

(Juni–Oktoba 1830)

Mungu aliviumba vitu vyote kiroho kwanza kabla havijakuwepo kama ilivyo kawaida juu ya nchi—Alimuumba mwanaume, mwenye mwili wa kwanza, kuwepo juu ya nchi—Mwanamke ni msaidizi wa kufaa kwa mwanaume.

1 Hivyo mbingu na dunia zikamalizika, na jeshi lake lote.

2 Na siku ya saba Mimi, Mungu, nikamaliza kazi yangu, na vitu vyote nilivyovifanya; nami nikapumzika siku ya saba kutokana na kazi zangu zote, na vitu vyote nilivyovifanya vikamalizika, na Mimi, Mungu, nikaona kuwa ni vyema;

3 Na Mimi, Mungu, nikaibariki siku ya saba, na kuitakasa; kwa sababu katika siku hiyo nilipumzika kutokana na kazi zangu zote ambazo Mimi, Mungu, niliziumba na kuzifanya.

4 Na sasa, tazama, ninakuambia, kwamba hivi ndivyo vizazi vya mbinguni na vya duniani, wakati vilipoumbwa, katika siku ile ambayo Mimi, Bwana Mungu, nilipozifanya mbingu na dunia,

5 Na kila mmea wa kondeni kabla ya kuwepo duniani, na kila mche wa kondeni kabla haujachipua. Kwa maana Mimi, Bwana Mungu, niliviumba vitu vyote, nilivyovizungumza, kiroho, kabla ya kuwekwa kikawaida juu ya uso wa dunia. Kwa maana Mimi, Bwana Mungu, sikuifanya mvua inyeshe juu ya uso wa dunia. Na Mimi, Bwana Mungu, nilikuwa nimewaumba wanadamu wote; na bado hapakuwa na mtu wa kuilima nchi; kwa maana ni mbinguni ndiko nilikowaumba wao; na bado hapakuwa na mwenye mwili juu ya dunia, wala majini, wala angani;

6 Lakini Mimi, Bwana Mungu, nikasema, na ukungu ukapanda duniani, nao ukatia maji uso wote wa ardhi.

7 Na Mimi, Bwana Mungu, nikamuumba mtu kwa mavumbi ya ardhi, na nikampulizia puani pumzi ya uhai; na mtu akawa nafsi hai, mwenye mwili wa kwanza juu ya dunia, na mtu wa kwanza pia; hata hivyo, vitu vyote viliumbwa kwanza; lakini kiroho viliumbwa na kufanyika kulingana na neno langu.

8 Na Mimi, Bwana Mungu, nikapanda bustani ya Edeni ya mashariki, na huko nikamweka huyo mtu niliyemfanya.

9 Na Mimi, Bwana Mungu, nikafanya kila mti kuota kutoka ardhini, kikawaida, kama ambavyo inapendeza machoni mwa mtu; na mtu aweze kuona. Nayo pia ikawa nafsi hai. Kwa kuwa ilikuwa kiroho siku ile niliyoiumba; kwani ilibakia katika mazingira ambayo Mimi, Mungu, niliumba, ndiyo, hata vitu vyote nilivyovitengeneza kwa ajili ya matumizi ya mwanadamu; na mwanadamu akaona kuwa ni vizuri kwa chakula. Na Mimi, Bwana Mungu, nikaupanda mti wa uzima pia katikati ya bustani, na pia mti wa ujuzi wa mema na maovu.

10 Na Mimi, Bwana Mungu, nikaufanya mto kutoka Edeni ili kuitilia maji bustani; na kutokea hapo ukagawanyika, na kuwa katika vichwa vinne.

11 Na Mimi, Bwana Mungu, nikaita jina la ule wa kwanza Pishoni, nao unaizunguka nchi yote ya Havila, ambako Mimi, Bwana Mungu, niliiumba dhahabu nyingi;

12 Na dhahabu ya nchi ile ilikuwa ni njema, na kulikuwako na bedola na kito cha shoham.

13 Na jina la mto wa pili lilikuwa Gihoni; ndiyo uizungukayo nchi yote ya Ethiopia.

14 Na jina la mto wa tatu lilikuwa Hidekeli; ndiyo upitao mbele ya mashariki ya Ashuru. Na mto wa nne ulikuwa Frati.

15 Na Mimi, Bwana Mungu, nikamtwaa mtu huyo, na kumweka katika Bustani ya Edeni, ili ailime, na kuitunza.

16 Na Mimi, Bwana Mungu, nikamwagiza huyo mtu nikisema: Kutoka katika kila mti wa bustani waweza kula.

17 Lakini kutoka katika mti wa ujuzi wa mema na maovu, usile, hata hivyo, wewe waweza kujichagulia mwenyewe, kwani imetolewa kwako, lakini, kumbuka kwamba nimekataza, kwa maana siku utakayokula kutoka katika mti huo hakika utakufa.

18 Na Mimi, Bwana Mungu, nikamwambia Mwanangu wa Pekee, kwamba siyo vyema kwa mtu huyo kuwa peke yake; kwa sababu hiyo, nitamfanyia msaidizi wa kumfaa.

19 Na kutoka katika ardhi, Mimi, Bwana Mungu, nikamfanya kila aina ya mnyama wa kondeni, na kila ndege wa angani; na akawaamuru kwamba waje kwa Adamu, ili kuona atawaitaje; nao pia walikuwa nafsi hai; kwa maana Mimi, Mungu niliwapulizia pumzi ya uzima, na nikaagiza jina lolote Adamu atakalokiita kiumbe kilicho hai, ndilo litakuwa jina lake.

20 Na Adamu akatoa majina kwa wanyama wote wa kufugwa, na kwa ndege wa angani, na kwa kila mnyama wa kondeni; lakini kwa Adamu, hakuonekana msaidizi wa kumfaa.

21 Na Mimi, Bwana Mungu, nikamletea usingizi mzito Adamu; naye akalala, na nikatwaa ubavu wake mmoja na nikaufunika na nyama mahali pake;

22 Na ule ubavu ambao Mimi, Bwana Mungu, niliutwaa kutoka kwa mtu huyo nikaufanya mwanamke, na nikamleta kwa mtu huyo.

23 Na Adamu akasema: Sasa ninajua huyu ni mfupa wa mifupa yangu, na nyama ya nyama yangu; naye ataitwa Mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanaume.

24 Kwa hiyo mwanaume atamwacha baba yake na mama yake, naye ataambatana na mke wake; nao watakuwa mwili mmoja.

25 Na wote wawili walikuwa uchi, huyo mtu na mke wake, wala hawakuona aibu.