Kuhusu Kuunganishwa Hekaluni

Kuhusu Kuunganishwa Hekaluni

Familia ni Muhimu kwa Mpango wa Mungu

Familia: Tangazo kwa Ulimwengu” linasema kwamba “ndoa kati ya mwanamume na mwanamke imetakaswa na Mungu, na kwamba familia ni muhimu katika mpango wa Muumba kwa maisha ya milele ya watoto Wake” (Ensign au Liahona, Nov. 2010, 129).

Shangwe kuu za maisha hupatikana kwenye familia yenye upendo. Hii ni kweli licha ya vikwazo na changamoto za maisha. Kujenga familia imara kunahitaji juhudi. Lakini juhudi sawa na hiyo inaweza kuleta shangwe katika maisha haya na katika milele yote. Hata katika familia ambapo uhusiano ni mgumu, injili ya Yesu Kristo inaweza kuleta tumaini, faraja na uponyaji.

Katika mpango wa furaha wa Baba yetu wa Mbinguni, mume na mke wanaweza kuwa pamoja milele. Mamlaka ya kuzileta pamoja familia milele yanaitwa nguvu ya kuunganisha. Ni nguvu ileile ambayo Yesu aliwapa Mitume Wake wakati wa huduma Yake duniani (Mathayo 16:19). Hivyo basi ndoa ya milele inaitwa kuunganishwa. Watoto waliozaliwa au kuasiliwa kwenye ndoa hizo za milele wanaweza pia kuunganishwa na familia zao milele.

Tofauti na ndoa ambazo hudumu tu “hadi kifo kitakapowatenganisha,” kuunganishwa hekaluni kunahakikisha kwamba kifo hakiwezi kuwatenganisha watu wanaopendana. Ili ndoa ziendelee baada ya kifo, lazima ziunganishwe katika mahala sahihi na kwa mamlaka sahihi. Mahala sahihi ni hekaluni na mamlaka sahihi ni ukuhani wa Mungu (Mafundisho na Maagano 132: 7, 15–19).

Mume na mke waliounganishwa hekaluni wanafanya maagano matakatifu na Bwana na kwao wenyewe. Maagano haya huwahakikishia kwamba uhusiano wao utaendelea baada ya maisha haya ikiwa watakuwa wakweli kwenye misimamo yao. Wanafahamu kwamba hakuna chochote, hata iwe kifo, kinaweza kuwatenganisha. Wale waliooana wanapaswa kuzingatia muungano wao kama uhusiano wao wa thamani zaidi duniani. Hata hivyo, mwenza ndiye mtu pekee tofauti na Bwana ambaye tumeamriwa kumpenda kwa moyo wetu wote (Mafundisho na Maagano 42:22).

Hekalu la Payson Utah, Chumba cha Kuunganishia

Ndoa ya Milele Ni Muhimu

Rais Spencer W. Kimball (1895–1985) alifundisha: “Ndoa pengine ni muhimu mno kati ya maamuzi yote na ina matokeo yenye athari kubwa mno, kwani haihusiki tu na shangwe ya mara moja, lakini pia na shangwe za milele. Inawaathiri siyo tu watu wawili wanaohusika, lakini pia familia zao, hususani watoto wao na watoto wa watoto wao, na kuendelea kwa vizazi vingi” (“The Importance of Celestial Marriage,” Ensign, Oct. 1979, 3).

Agano la ndoa ya milele pia linahitajika kwa ajili ya kuinuliwa. Kuinuliwa ni uzima wa milele—aina ya maisha ambayo Mungu anayaishi. Yeye ni mkamilifu. Anaishi kwenye utukufu mkuu. Anayo maarifa yote, uwezo wote, na hekima yote. Yeye ni mwenye upendo, mkarimu na mwenye huruma. Yeye ni Baba wa Mbinguni wa kila mtu duniani. Tunaweza siku moja kuwa kama Yeye. Hii ndiyo kuinuliwa.

Kuinuliwa ni kipawa kikuu ambacho Mungu anaweza kuwapa watoto Wake (Mafundisho na Maagano 14:7). Ni zawadi kwa wale wote wanaothibitisha kuwa waaminifu kwa Bwana. Wale walio waaminifu wataishi katika daraja la juu la ufalme wa selestia.

Bwana alifunua kupitia Joseph Smith:

“Katika utukufu wa selestia kuna mbingu au daraja tatu; na ili kupata la juu zaidi, mwanadamu lazima aingie katika utaratibu huu wa ukuhani [ikimaanisha agano jipya na lisilo na mwisho la ndoa]; na kama hakufanya hivyo, hawezi kulipata” (Mafundisho na Maagano 131:1–3).

Tunapoheshimu maagano yetu, tunaweza kuwa na uhakika kwamba tutakuwa na wapendwa wetu milele. Bwana ameahidi:

“Kama mtu ataoa mke kwa njia ya neno langu, ambalo ndilo sheria yangu, na kwa agano jipya na lisilo na mwisho, na ikafungwa kwao na Roho Mtakatifu wa ahadi, na yeye aliyepakwa mafuta, na yeye niliyempa uwezo huu na funguo za ukuhani huu; … na kama [wao] watatii katika agano langu, … itafanyika kwao katika mambo yote ambayo mtumishi wangu ameyaweka juu yao, kwa muda, na kwa milele yote; na yatakuwa na nguvu kamili wakati wakiwa nje ya ulimwengu” (Mafundisho na Maagano 132:19).

Bwana anafahamu kwamba si watoto wake wote watapata fursa ya kuwa na ndoa katika maisha haya. Yeye ameahidi kwamba wale wote wanaoikubali injili na kujitahidi kutunza maagano yao watapata fursa ya kuwa na ndoa na kuwa na watoto aidha katika maisha haya au yajayo.

Vizazi Vyote Vimeunganika

Tangazo la familia linaeleza kwamba “mpango mtakatifu wa furaha unawezesha uhusiano wa familia kuendelezwa zaidi ya kaburi. Ibada na maagano matakatifu yanayopatikana katika mahekalu matakatifu yanawezesha watu binafsi kurudi katika uwepo wa Mungu na kwa familia kuunganishwa milele.”

Nguvu ya kuunganisha pia inaendelea kutoka kwa wazazi hadi kwa watoto, kupita vizazi vyote kuanzia mwanzo wa ulimwengu. Rais Joseph Fielding Smith (1876–1972) alifundisha kwamba watoto waliozaliwa ndani ya agano—na wale ambao wameunganishwa na wazazi wao hekaluni—“wana haki juu ya baraka za injili zaidi ya vile ambavyo wale ambao hawakuzaliwa ndani ya agano wanastahili kupokea. Wanaweza kupokea mwongozo mkubwa, ulinzi mkubwa, msukumo mkubwa kutoka kwa Roho wa Bwana; na ndipo hakuna nguvu inayoweza kuwaondoa kutoka kwa wazazi wao” (Doctrines of Salvation, comp. Bruce R. McConkie [1955], 2:90).

Watoto waliozaliwa kwa wazazi waliounganishwa hekaluni wanazaliwa ndani ya agano. Hivyo, wao ni sehemu ya familia ya milele, kulingana na uaminifu wao. Watoto ambao hawakuzaliwa kwenye agano pia wanaweza kuwa sehemu ya familia ya milele wakati wazazi wao wa asili au waliowaasili wanapounganishwa. Ibada ya kuwaunganisha watoto kwa wazazi hufanyika hekaluni pekee. Ili kutoa baraka hizi kwa watu wote, tunaweza pia kuunganishwa kwa niaba ya wale ambao wamefariki. Kwa njia hii, familia zote zinaweza kuwa pamoja milele.

Ahadi kwamba familia zetu zinaweza kuwa pamoja baada ya kifo huleta maana zaidi kwenye maisha. Inatuhimiza tuwe waaminifu na wakweli. Inaboresha na kukuza uhusiano wa familia. Inatusaidia tupate shangwe na tumaini wakati tunapokabiliana na changamoto za maisha. Na kufahamu kwamba tunaweza kuwa pamoja tena huleta faraja na amani pale tunapokabiliana na mateso au kifo cha wapendwa wetu.

Ibada ya kuunganisha ni kipawa cha juu cha Mungu kwa watoto Wake. Inatuwezesha turejee kuishi Naye pamoja na wapendwa wetu wote milele. Inatoa baraka za ajabu kwa maisha haya na yajayo. Ni ukumbusho wa daima kwamba familia ni muhimu kwa mpango wa Mungu na kwa furaha yetu hapa na katika milele. Inatoa amani, tumaini, na shangwe kwa wote wanaoipokea kwa uaminifu.