Maandiko Matakatifu
Enoshi 1


Kitabu cha Enoshi

Mlango wa 1

Enoshi anasali kwa bidii na kupokea msamaha wa dhambi zake—Anaisikia sauti ya Bwana mawazoni mwake ikiahidi wokovu kwa Walamani katika siku za hapo usoni—Wanefi walijaribu kuwakomboa Walamani—Enoshi anamshangilia Mkombozi wake. Karibia mwaka 420 K.K.

1 Tazama, ikawa kwamba mimi, Enoshi, nikijua kwamba Baba yangu alikuwa mtu wa haki—kwani alinifundisha kwa lugha yake, na pia katika malezi na maonyo ya Bwana—na jina la Mungu wangu libarikiwe kwa hayo—

2 Na nitakuelezea kuhusu mweleka ambao niliupata nao mbele ya Mungu, kabla ya kupokea msamaha wa dhambi zangu.

3 Tazama, nilienda kuwinda wanyama porini; na maneno ambayo nilikuwa nimezoea kumsikia baba yangu akizungumza kuhusu uzima wa milele, na shangwe ya watakatifu, yakapenya ndani ya moyo wangu.

4 Na nafsi yangu ikapata njaa; na nikapiga magoti mbele ya Muumba wangu, na nikamlilia kwa sala kuu na nikamsihi kwa nafsi yangu; na kwa siku nzima nikamlilia; ndiyo, na wakati usiku ulipofika bado nilipaza sauti yangu hata ikafika mbinguni.

5 Na sauti ikanijia, ikisema: Enoshi, umesamehewa dhambi zako, na wewe utabarikiwa.

6 Na mimi, Enoshi, nilijua kwamba Mungu hawezi kusema uwongo; kwa hivyo, hatia yangu iliondolewa mbali.

7 Na nikasema: Bwana, je, inafanywa vipi?

8 Na akaniambia: Kwa sababu ya imani yako katika Kristo, ambaye wewe hujamwona kamwe wala kumsikia. Na miaka mingi itapita kabla yeye hajajidhihirisha katika mwili; kwa hivyo, nenda, imani yako imekufanya mkamilifu.

9 Sasa, ikawa kwamba baada ya kusikia maneno haya nilianza kushughulika na ustawi wa ndugu zangu, Wanefi; kwa hivyo, nilimlilia Mungu kwa nafsi yangu yote kwa niaba yao.

10 Na nilipokuwa nikishindana hivyo rohoni, tazama, sauti ya Bwana ikanijia mawazoni mwangu tena, ikisema: Nitagawanyia ndugu zako kulingana na bidii yao katika kutii amri zangu. Nimewapatia nchi hii, na hii ni nchi takatifu; na siwezi kuilaani ila tu kwa sababu ya dhambi; kwa hivyo, nitagawanyia ndugu zako kulingana na yale ambayo nimesema; na nitawateremshia juu ya vichwa vyao wenyewe huzuni ya dhambi zao.

11 Na baada ya mimi, Enoshi, kusikia maneno haya, imani yangu kwa Bwana ikawa haitikisiki; na nikamwomba kwa vilio vingi kwa niaba ya ndugu zangu, Walamani.

12 Na ikawa kwamba baada ya kuomba na kumtumikia kwa bidii, Bwana akaniambia: Kwa sababu ya imani yako, nitakutendea kulingana na mahitaji yako.

13 Na sasa tazama, hii ndiyo ilikuwa tamaa ambayo niliyotamani kutoka kwake—kwamba kama hivyo ndivyo inavyopaswa kuwa, kwamba watu wangu, Wanefi, wataanguka katika uvunjifu wa sheria, na kwa njia yo yote waangamizwe, na, Walamani wasiangamizwe, kwamba Bwana Mungu angehifadhi kumbu kumbu ya watu wangu, Wanefi; hata kama ni kwa nguvu za mkono wake mtakatifu, ili katika siku za usoni ifunuliwe kwa Walamani, ili, pengine, waweze kuletwa katika wokovu—

14 Kwani kwa sasa majaribio yetu ya kuwarudisha katika imani ya kweli yalikuwa ni bure. Na wakaapa katika hasira zao, kwamba, kama itawezekana, wataangamiza maandishi yetu pamoja nasi, na pia desturi zote za baba zetu.

15 Kwa hivyo, mimi nikijua kwamba Bwana Mungu anaweza kuhifadhi maandishi yetu, nilimlilia sana bila kukoma, kwani alikuwa ameniambia: Chochote utakachoomba kwa imani, ukiamini kwamba utapokea kwa jina la Kristo, utakipokea.

16 Na nilikuwa na imani, na nikamlilia Mungu kwamba angehifadhi yale maandishi; na akaagana na mimi kwamba atayafunua kwa Walamani katika wakati wake.

17 Na mimi, Enoshi, nilijua kwamba itakuwa kulingana na agano alilofanya; kwa hivyo nafsi yangu ikapumzika.

18 Na Bwana akaniambia: Baba zako nao pia wameniomba kitu hiki; na kitatendwa kulingana na imani yao; kwani imani yao ilikuwa kama yako.

19 Na sasa ikawa kwamba mimi, Enoshi, nilienda miongoni mwa watu wa Nefi, nikitoa unabii kuhusu vitu vitakavyokuja, na nikishuhudia kuhusu vitu ambavyo nilikuwa nimevisikia na kuona.

20 Na ninashuhudia kwamba watu wa Nefi walijaribu kwa bidii kuwarejesha Walamani katika imani ya kweli ya Mungu. Lakini kazi zetu zilikuwa bure; na chuki yao ilikuwa imeimarishwa, na walitawaliwa na maumbile yao maovu na wakawa wachokozi, wakali, na watu wapendao umwagaji wa damu na kuabudu sanamu na uchafu; wakila wanyama wa porini; na kuishi katika mahema, na kuzunguka nyikani, na kuvaa ngozi za wanyama viunoni mwao na kunyoa nywele zao; na ustadi wao ulikuwa ni wa upinde, na upanga, na shoka. Na wengi wao hawakula chochote isipokuwa nyama mbichi, na walijaribu kila mara kutuangamiza.

21 Na ikawa kwamba watu wa Nefi walilima ardhi, na kupanda kila aina ya nafaka, na matunda, na makundi ya wanyama, na makundi yote ya kila aina ya ngombe, na mbuzi, na mbuzi wa mwitu, na pia farasi wengi.

22 Na kulikuwa na manabii wengi sana miongoni mwetu. Na watu walikuwa watu wenye shingo ngumu, wagumu katika kufahamu.

23 Na hakukuwa na chochote ila ukali mwingi, mahubiri na kutoa unabii kuhusu vita, na mabishano, na maangamizo, na kuwakumbusha kila mara kuhusu mauti, na kipindi cha umilele, na hukumu na nguvu za Mungu, na hivi vitu vyote—kuwavuruga kila mara ili wamwogope Bwana. Nasema hapakuwa na mambo chini ya vitu hivi, na mazungumzo dhahiri, ili kuwafanya wasiangamie kwa haraka. Na ninaandika jinsi hii juu yao.

24 Na niliona vita vingi miongoni mwa Wanefi na Walamani maishani mwangu.

25 Na ikawa kwamba nilianza kuzeeka, na miaka mia moja, sabini na tisa ilikuwa imepita tangu baba yetu Lehi aondoke Yerusalemu.

26 Na nikaona kwamba ni lazima ninakaribia kuelekea kaburini, nikiwa nimewezeshwa na nguvu za Mungu ili nihubiri na niwatolee watu hawa unabii, na nitangaze neno kulingana na ukweli ulio katika Kristo. Na nimeutangaza katika maisha yangu yote, na nimeufurahia zaidi ya yote ulimwenguni.

27 Na hivi karibuni naelekea mahala pa pumziko langu, ambapo ni pamoja na Mkombozi wangu; kwani najua kwamba nitapumzika na yeye. Na ninafurahia siku ile ambayo huu mwili wenye kutokufa utajivika, na kusimama mbele yake, kisha nitaona uso wake kwa furaha, na ataniambia: Njoo kwangu, heri wewe, umetayarishiwa mahali katika nyumba za Baba yangu. Amina.