2010–2019
Mtumaini Bwana na Wala Usijitegemee
Aprili 2017


Mtumaini Bwana na Wala Usijitegemee

Tunaweza kuyaweka maisha yetu kumlenga Mwokozi kwa kumjua Yeye, naye atayaongoza mapito yetu.

Nikiwa safirini katika Asia, dada mpendwa alinijia. Akanikumbatia, na kuniuliza, “Kwa hakika unaamini kuwa injili hii ni ya kweli?” Dada mpendwa, ninaamini ni ya kweli. Ninamtumaini Bwana.

Katika Methali 3:5–6, tunasoma ushauri huu:

Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe.

“Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako.”

Maandiko haya yanakuja na mawaidha mawili, onyo, na ahadi tukufu. Mawaidha mawili: “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote” na “katika njia zako zote mkiri yeye,.” Onyo: “Usitegemee akili zako mwenyewe.” Na ahadi tukufu: “Naye atayanyosha mapito yako.”

Acha kwanza tujadili onyo. Vielelezo vya picha vinatupa mengi ya kutafakari. Onyo linakuja katika neno “usijitegemee”—“usitegemee akili zako mwenyewe.” Kwa Kiswahili neno egema lina maana ya lala upande kimwili au kuelekea upande mmoja. Tunapoegema kimwili upande mmoja au mwingine, tunaondoka toka katikati, tunakuwa hatuna usawa, na tunaanguka. Wakati kiroho tunapojitegemea sisi wenyewe, tunajiondoa kumtegemea Mwokozi. Kama tunaegema, hatupo katikati; hatupo sawa; hatulengi kwa Kristo.

Akina dada, kumbukeni, katika maisha yetu kabla ya ulimwengu kuwepo, tulisimama pamoja na Mwokozi. Tulimwamini Yeye. Tulipaza sauti ya kuunga mkono, kwa shauku, na furaha kwa mpango wa furaha uliowekwa mbele na Baba yetu wa Mbinguni. Hatukuegemea. Tulipigana na shuhuda zetu na “kujipanga wenyewe na majeshi ya Mungu, na majeshi hayo yalishinda.”1 Vita hii kati ya mema na uovu imeletwa duniani. Kwa mara nyingine tuna majukumu matakatifu kusimama kama mashahidi na kumwamini Bwana.

Lazima kila mmoja aulize: Ni jinsi gani najiweka kati na kutotegemea akili zangu mwenyewe? Ni jinsi gani nitagundua na kufuata sauti ya Mwokozi wakati sauti za ulimwengu zikiwa zinalazimisha? Ni jinsi gani nitaendelea kumwamini Mwokozi?

Naomba nipendekeze njia tatu za kuongeza elimu ya kumwamini Mwokozi. Utagundua kwamba kanuni hizi sio mpya, bali ni za msingi. Zinaimbwa katika kila Msingi, zikipigwa mwangwi katika masomo ya Wasichana, na ni majibu kwa maswali mengi ya Muungano wa Usaidizi wa Kina Mama. Zinalenga katikati—na si kanuni za—kuegemea.

Kwanza, tunaweza kuja kumjua Bwana na kumtegemea Yeye “tunaposherekea maneno ya Kristo; kwani tazama, maneno ya Kristo yatawaelezea vitu vyote mnavyostahili kutenda.”2

Miezi kadhaa iliyopita, tulikuwa na masomo ya maandiko kwa familia. Mjukuu wangu wa kiume wa miaka miwili alikuwa amekaa kwenye paja langu tukiwa tunasoma. Mimi nilikuwa katika hali nzuri ya ubibi, nikifurahia kutembelewa na familia ya mwanangu.

Tulipomaliza kusoma maandiko, nilifunga kitabu changu. Mjukuu wangu alijua kwamba punde utakuwa muda wa kulala. Alitazama kwa macho yake yenye matamanio na aliongea ukweli wa milele: “Maandiko zaidi, Nana.”

Picha
Mwana mkujuu wa Dada Cordon

Mwana wangu, mzazi mwema, alinionya mimi, “Mama usiwe kiungo dhaifu. Anataka tu hasiende kulala.”

Lakini wakati mjukuu wangu akihitaji maandiko zaidi, tulisoma maandiko zaidi! Maandiko zaidi yalituelimisha uelewa wetu, rutubisha roho zetu, yalijibu maswali yetu, kuongeza kumtegemea Bwana, na kutusaidia sisi kuyaweka maisha yetu katikati Yake. “Kumbukeni kuyapekua kwa bidii, ili mfaidike.”3

Pili, tunaweza kuja kumjua Bwana na kumtegemea Yeye kwa njia ya maombi. Ni baraka jinsi gani kuomba kwa Mungu wetu! “Ombeni kwa Baba kwa nguvu zote za moyo.”4

Nina kumbukumbu nzuri za maombi ambazo nazithamini. Katika moja ya mapumziko yangu ya chuo wakati wa kiangazi, nilipata kazi huko Texas. Nilitakiwa kuendesha kwa mamia ya kilomita kutoka Idaho kwenda Texas kwenye gari yangu nzee, gari niliyoipa jina la Vern. Vern ilijazwa mizigo hadi juu, na nilikuwa tayari kwa tukio jipya.

Nikiwa natoka mlangoni, nikamkumbatia mama yangu mpendwa na alisema, “Acha tuombe kabla hujaondoka.”

Tulipiga magoti na mama yangu akaanza kuomba. Alimwomba Baba wa Mbinguni kwa ajili ya usalama wangu. Aliomba kwa ajili ya gari langu ambalo haikuwa na kiyoyozi, akiomba kwamba gari lifanye kazi vizuri. Aliwaomba malaika wawe pamoja nami kiangazi chote. Aliomba na kuomba na kuomba.

Amani ambayo ilitokana na maombi yale ilinipa mimi msukumo wa kumtegemea Bwana na kutotegemea akili zangu mwenyewe. Bwana aliiongoza njia yangu katika maamuzi mengi niliyoyafanya kiangazi kile.

Tunapojenga tabia ya kumfuata Baba wa Mbinguni katika maombi, tutakuja kumjua Mwokozi. Tutakuja kumtegemea Yeye. Matamanio yetu yatakuwa kama ya Kwake. Tutaweza kujilinda sisi wenyewe na kwa baraka za wengine ambazo Baba wa Mbinguni yupo tayari kutoa kama tutaomba kwa imani.5

Tatu, tunaweza kuja kumjua Bwana na kumtegemea Yeye tunapowatumikia wengine. Ninashiriki hadithi ifuatayo kwa ruhusa ya Amy Wright, ambaye alikuja kuelewa kanuni ya kuhudumia hata wakati wa ugonjwa wa kuhatarisha maisha. Amy aliandika:

“Mnamo Oktoba 29, 2015, niligundulika nina saratani. Saratani yangu ilikuwa na asilimia 17 ya kupona. Hali haikuwa nzuri. Nilijua kwamba nitaendelea kupigania maisha yangu. Nilijizatiti kutoa kila kitu nilichokuwa nacho siyo kwangu mwenyewe bali, muhimu zaidi, kwa familia yangu. Mnamo Desemba, nilianza tibakemikali. Nilikuwa naelewa dalili nyingi za madawa ya vita ya-saratani, lakini sikujua kwamba iliwezekana kwa mtu kuwa mgonjwa na kuendelea kuishi.

“Wakati fulani, niliitangaza dawa ya saratani kama ukiukwaji wa haki za binadamu. Nilimwambia mume wangu tosha. Nimeshindwa! Nilikuwa siendi tena hospitali. Kwa hekima zake, mume wangu mpendwa kwa uvumilivu alinisikiliza na kisha akajibu, ‘Sawa, hivyo tunahitaji mtu wa kumtumikia.’”

Nini? Alikosa kuelewa kwamba mke wake alikuwa na saratani na hakuwa hata na chembe ya kinyaa au wakati wa kuhisi maumivu makali?

Amy aliendelea kuelezea: “Dalili zangu zilizidi kuwa mbaya hadi kufikia kuwa na siku NZURI moja au mbili kwa mwezi ambazo niliweza kufanya kazi kama kiumbe hai anayepumua. Zilikuwa siku zile wakati familia yetu ilitafuta njia za kuhudumu.”

Katika moja ya siku zile, familia ya Amy iligawa vifaa vya tibakemikali kwa wagonjwa wengine, vifaa vilijaa vitu vya kusaidia kupunguza dalili. Wakati Amy akishindwa kulala, angefikiria njia ya kumchangamsha mtu mwingine. Njia nyingine zilikuwa kubwa, lakini nyingine yalikuwa maelezo au jumbe za kutiia moyo na upendo. Katika usiku ule wakati maumivu yake yalikuwa makali na kushindwa kupata usingizi, alilala kitandani pamoja na iPad yake na kutafuta ibada ambazo zilitakiwa kukamilishwa kwa niaba ya mababu zake waliokufa. Kimiujiza maumivu yangepungua, na yeye alipata uwezo wa kuvumilia.

“Huduma,” Amy anashuhudia, “iliokoa maisha yangu. Ambapo mimi hatimaye nikapata nguvu za kusonga mbele ilikuwa furaha niliyoigundua katika kujaribu kupunguza mateso ya wale walio karibu yangu Nikatarajia miradi ya huduma zetu kwa furaha kubwa na matarajio. Hadi siku hii ilionekana kama ajabu ya uongo. Ungeweza kufikiria kwamba mtu ambaye alikuwa na kipara, aliye na sumu, na anayepigania maisha yake alikuwa amejiridhisha katika kufikiria kwamba kwa sasa yote ni kuhusu mimi. Hata hivyo, nilipojifikiria, hali yangu, mateso na maumivu yangu, ulimwengu ukawa giza na kuvunjika moyo. Wakati kuzingatia kwangu kuliwageukia wengine, palikuwa na nuru, tumaini, nguvu, ujasiri, na furaha. Ninajua kwamba hii inawezekana kwa sababu ya kudumisha, uponyaji, na nguvu kuwezesha za Upatanisho za Yesu Kristo.”

Amy alikuja kumwamini Bwana alipokuja kumjua. Kama angeegema hata kidogo kwenye akili zake mwenyewe, angekataa wazo la kuhudumu. Huduma ilimsaidia kuvumilia maumivu na mateso na kuishi andiko hili: “Mnapowatumikia wanadamu wenzenu, mnamtumikia tu Mungu wenu.”6

Yesu Kristo ameushinda ulimwengu. Na kwa sababu Yake, kwa sababu ya Upatanisho Wake usio na mwisho, wote tuna sababu ya kuamini, tukijua kwamba yote yatakuwa sawa mwishowe.

Akina dada, kila mmoja wetu anaweza kumwamini Bwana na kuacha kujitegemea.. Tunaweza kuyaweka maisha yetu kumlenga Mwokozi kwa kumjua Yeye, naye atayaongoza mapito yetu.

Tupo duniani kuonyesha uaminifu kama huo Kwake ambao unaturuhusu sisi kusimama pamoja na Yesu Kristo wakati alipotangaza, “Nipo hapa, nitume mimi.”7

Picha
Kristo na Uumbaji

Wapendwa dada zangu, Rais Thomas S. Monson alishuhudia kwamba “baraka tulizoahidiwa hazina kipimo. Ingawa dhoruba ya mawingu inaweza kukusanyika, ingawa mvua inaweza kunyesha juu yetu, elimu yetu ya injili na upendo wetu kwa Baba yetu wa Mbinguni na Mwokozi wetu itatufariji na kutuhimili … tukiwa tunatembea kwa ukamilifu. … Hapatakuwa na kitu chochote katika ulimwengu huu kinachoweza kutushinda.”8

Ninaongeza ushuhuda wangu kwa ule wa nabii wetu. Kama tunamwamini Baba yetu wa Mbinguni na Mwokozi na kuacha kutegemea akili zetu wenyewe, watayaongoza mapito yetu na watanyoosha mikono yao ya huruma kwetu. Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari: Mnamo Aprili 1, 2017, Dada Cordon alipumzishwa kama Mshauri wa Kwanza katika Urais Mkuu wa Msingi.