2010–2019
Lolote Atakalowaambia, Fanyeni.
Aprili 2017


Lolote Atakalowaambia, Fanyeni.

Wakati tunapoamua kufanya “Lolote Mungu atakalotuambia” sisi, tunajitolea kwa bidii kufuata mapenzi ya Mungu.

Mwokozi alifanya muujiza Wake wa kwanza ulioandikwa kwenye karamu ya harusi huko Kana ya Galilaya. Mariamu, mama Yake; na wanafunzi wake walikuwa pale pia. Mariamu inavyoonekana alihisi kiasi fulani cha wajibu katika mafanikio ya karamu hiyo. Wakati wa sherehe, kulitokezea shida—wenyeji wa harusi waliishiwa na divai. Mariamu alikuwa na wasiwasi na akamwendea Yesu. Walizungumza kwa kifupi, kisha Mariamu akawageukia watumishi na kusema:

“Lolote atakalowaambia, fanyeni.

“Basi kulikuwako huko mabalasi sita ya mawe. … [Mabalasi haya hayakutumika kuhifadhi maji kunywa lakini yalikuwa ni ya kufuata utaratibu wa kutawadha chini ya Sheria za Musa.]

“Yesu akawaambia [wale watumishi], Jalizeni mabalasi maji. Nao wakayajaliza hata juu.

“Akawaambia, Sasa tekeni, mkampelekee mkuu wa meza. Wakapeleka.

“[Kisha] mkuu wa meza … alipoyaonja yale maji yaliyopata kuwa divai” alishangazwa ya kwamba divai iliyokuwa bora zaidi ililetwa mwishoni mwa karamu.1

Kwa kawaida tunakumbuka tukio hili kwa sababu kugeuza maji kuwa divai ilikuwa ni maonyesho ya uwezo wa Mungu—ilikuwa ni muujiza. Huo ni ujumbe muhimu, lakini tunao tena ujumbe muhimu katika historia ya Yohana. Mariamu “chombo cha thamani na kilichochaguliwa,”2 akiwa ameitwa na Mungu azae, na kumlea Mwana wa Mungu. Alifahamu mengi kumhusu Yeye kuliko mtu mwingine yeyote duniani. Alijua ukweli wa kuzaliwa Kwake kimiujiza. Alifahamu kwamba Yeye alikuwa bila dhambi na “na kwamba hakuzungumza kama wanaume wengine, wala hangefundishwa; kwani hakuhitaji mtu yeyote amfundishe.”3 Mariamu alifahamu kuhusu uwezo Wake wa ajabu wa kusuluhisha shida, ikiwa ni pamoja na moja ya kibinafsi kama kutoa divai ya karamu ya harusi. Alikuwa na imani imara katika Yeye na nguvu Zake za kutoka kwa Mungu. Maelekezo yake, rahisi na ya moja kwa moja kwa watumishi hayakuwa na tahadhari, ujuzi au mipaka: “Lolote atakalowaambia, fanyeni.”

Mariamu alikuwa msichana wakati malaika Gabrieli alipojitokeza kwake. Mwanzoni alikuwa “amefadhaika” kwa kuitwa “aliyepewa neema” na “heri … miongoni mwa wanawake … akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani.” Gabrieli alimhakikishia ya kwamba hakuwa na chochote cha kuogopa—habari aliyoleta ilikuwa njema. “Angechukua mimba … Mwana wa Aliye Juu” na “kuzaa mtoto mwanaume … [ambaye] ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele.”

Mariamu alishangaa na kuwaza kwa sauti, “Litakuwaje neno hili, maana sijui mume?”

Malaika alimwelezea, lakini kwa ufupi tu, akimhakikishia ya kwamba “hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.”

Mariamu kwa unyenyekevu alijibu ya kwamba angelifanya kile Mungu angeomba, bila ya kutaka kujua bayana na hakika licha ya kuwa na maswali chungu nzima kuhusu maana ya haya katika maishan yake. Aliweka sharti bila kuelewa hasa kwa nini Yeye alikuwa anataka hilo kutoka kwake au mambo yangeenda vipi. Alikubali neno la Mungu bila masharti na mbeleni,4 akiwa na ufahamu kidogo wa yale yaliyokuwa mbele. Kwa imani tu katika Mungu, Mariamu alisema, “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema.”5

Wakati tunapoamua kufanya “Lolote Mungu atakalotuambia” sisi, tunajitolea kwa bidii kufuata mapenzi ya Mungu. Matendo rahisi ya imani kama haya kana vile kujifunza maandiko, kufunga kila, na kuomba kwa moyo wa dhati uongeza kina cha uwezo wetu wa kiroho wa kukabiliana na matakwa maishani mwetu. Baada ya muda, tabia rahisi za imani huleta matokeo ya ajabu. Inabadilisha imani yetu kutoka kwa mche hadi kuwa nguvu kwa wema katika maisha yetu. Kisha, changamoto zinapotupata, kule kukita mizizi katika Kristo uthabiti kwa nafsi zetu. Mungu hugadimu udhaifu wetu, kuimarisha furaha yetu, na kufanya “mambo yote [ku]fanya kazi pamoja kwa [yetu] mema.”6

Miaka michache iliyopita, nilizungumza na askofu kijana aliyekuwa akitumia masaa kadhaa kila wiki, akiwashauri washiriki wa kata yake. Alitoa wazo la kushangaza. Shida ambazo washiriki wa kata yake walikumbana nazo, alisema, zilikuwa ni zile waumini wa Kanisa wanakumbana nazo kila mahali—masuala kama jinsi ya kuanzisha ndoa yenye furaha; mapambano na kusawazisha kazi, familia na majukumu ya Kanisa; changamoto na kutii neno la hekima, ajira, au picha za ngono; au kupata amani kuhusu sera za Kanisa au swali la kihistoria ambalo hawakulielewa.

Ushauri wake kwa washiriki wa kata mara nyingi ilijumuisha kurejelea mambo ya msingi ya imani kama: kujifunza Kitabu cha Mormoni—kama tulivyoshauriwa kufanya na Rais Thomas S. Monson—kulipa zaka, na kuhudumu Kanisani kwa kujitolea. Mara nyingi, hata hivyo, majibu yao kwake yalikuwa yenye nadharia ya kushuku. “Sikubaliani nawe, Askofu. Sisi sote tunajua hayo ni mambo mema ya kutenda. Sisi huzungumzia mambo hayo kila wakati Kanisani. Lakini sina uhakika ya kwamba unanielewa. Je, kufanya mojawapo ya hayo mambo inahusikaje na mambo ambayo yananikumba mimi?”

Ni swali la haki. Baada ya muda, nimechunguza ya kwamba wale ambao hutenda kwa makusudi “vitu vilivyo vidogo na rahisi”7—kutii kupitia njia zinazoonekana kuwa ndogo—wanabarikiwa na imani na nguvu ambayo inazidi gharama halisi ya utiifu, na kwa hakika, inaweza kuonekana kama haiwahusu kabisa. Inaweza kuonekana kuwa vigumu kuona uhusiano kati ya vitendo vya kila siku vya utiifu na suluhu kwa shida kubwa na ngumu tunazokumbana nazo sisi sote. Lakini vina uhusiano. Katika uzoefu wangu, kufanya mazoea madogo ya imani kila siku ipasavyo, ni njia pekee bora ya kujiimarisha dhidi ya shida za maisha, haijalishi ni nini. Matendo madogo ya imani, hata wakati yanapoonekana yasiyokuwa ya maana au kutohusika hasa na shida ambazo zinatusumbua, hutubariki katika yale yote tunayofanya.

Kumbuka Naamani, “jemadari wa jeshi la … Shamu” na “mtu hodari wa vita,” mwenye ukoma. Mtumishi msichana alizungumzia kuhusu nabii aliyekuwa Israeli ambaye angeweza kumponya Naamani, na hivyo alisafiri na kundi la watumishi, wanajeshi, na zawadi za kupeana Israeli, hatimaye aliwasili nyumbani kwa Elisha. Mtumishi wa Elisha, sio Elisha mwenyewe, alimjulisha Naamani kwamba amri ya Bwana ilikuwa tu “Enenda ukaoge katika Yordani [Mto] mara saba.” Jambo rahisi. Pengine agizo hili rahisi kwa mtu huyu mkubwa wa vita lilionekana kuwa lisilio na mantiki, rahisi mno, au chini ya heshima yake kiasi cha kwamba aliona pendekezo hilo pekee la kukera. Angalau sana, maelekezo ya Elisha hayakuleta maana kwake Naamani, “Akageuka, akaondoka kwa hasira.”

Lakini watumishi wa Naamani walimkaribia kwa upole na kusema kuwa angelitenda “jambo kubwa” ikiwa Elisha angalimuambia. Walibaini ya kwamba kwa vile aliombwa tu kutenda jambo ndogo na rahisi, mbona asifanye hivyo, hata kama hakuelewa ni kwa nini? Naamani alizangatia upya uamuzi wake na pengine kwa shaka, lakini kwa utiifu “akashuka … , akajichovya mara saba katika Yordani” na kimiujiza akapona.8

Baadhi ya zawadi za utiifu huja haraka; zingine huja tu baada ya kujaribiwa. Katika Lulu ya Thamani Kuu, tunasoma kuhusu bidii kubwa ya Adamu katika kuweka amri ya kutoa dhabihu. Wakati malaika walimuuliza Adamu kwa nini alikuwa anatoa dhabihu, alijibu, “Mimi sijui, ila Bwana ameniamuru.” Yule malaika alimuelezea ya kwamba dhabihu zilikuwa “mfano wa dhabihu ya Mzaliwa Pekee wa Baba.” Lakini maelezo yalikuja tu baada ya Adamu kuonyesha sharti lake la kumtii Bwana kwa “siku nyingi” bila kujua kwa nini, alihitajika kutoa dhabihu hizo.”9

Mungu daima atatubariki kwa ajili ya utiifu wetu ulio imara katika injili Yake na uaminifu kwa Kanisa Lake, lakini ni nadra kwake kutuonyesha ratiba ya kufanya hivyo mbeleni. Yeye hatuonyeshi picha mzima kutoka mwanzoni. Hapo ndipo imani, tumaini, na kuamini katika Bwana hutokezea.

Mungu anatuomba tuvumilie Naye—tumwamini na tumfuate. Anatusihi “msishindane kwa sababu hamwoni.” Anatuonya ya kwamba tusitegemee majibu rahisi au suluhu za haraka kutoka mbinguni. Suluhu hupatikana wakati tunaposimama imara katika “majaribu ya imani [yetu],” bila kujali ni vigumu kiasi gani kuvumilia majaribu hayo au ni pole pole kiasi gani jibu linakuja.10 Sizungumzi kuhusu “utiifu bila ya kujua au kuelewa”11 lakini kuhusu imani makini katika upendo kamili na majira kamili ya Bwana.

Majaribu ya imani yetu daima yatahusu kubakia mkweli kwa vitendo rahisi, vya kila siku vya imani. Kisha, na kisha tu, ndipo anaahidi kwamba tutapokea majibu ya kiuungu ambayo tumekuwa na hamu nayo. Mara tunapodhihirisha kutaka kwetu kutenda kile anachotuomba bila ya kutaka kufahamu lini, aje, na kwa nini ndipo tunaporuhusiwa “[ku]vuna zawadi ya imani [yetu], na bidii [yetu], na subira, na uvumilivu.”12 Utiifu wa kweli hukubali amri za Mungu bila masharti na mbeleni.13

Kila siku, kwa kufahamu au la, sisi sote humchagua “[tu]takayemtumikia [sisi].”14 Tunaonyesha bidii yetu kumtumikia Bwana kwa kujihusisha kwa uaminifu katika vitendo vya kila siku vya kujitolea. Bwana ameahidi ya kwamba ataongoza njia zetu,15 lakini ili aweze kufanya hivyo, ni lazima tutembee, tukiamini ya kwamba anajua njia kwa sababu Yeye ndiye “njia.”16 Sharti tujaze mabalasi yetu wenye furifuri. Tunapomwamini na kumfuata Yeye, kama maji kwa divai, maisha yetu yanabadilika. Tunakuwa zaidi ya kile kwa namna nyingine tungaliweza kuwa. Muamini Bwana, na “lolote atakalowaambia, fanyeni.” Katika jina la Yesu Kristo, amina.