Mkutano Mkuu
Baraka za Ufunuo Unaoendelea kwa Manabii na Ufunuo Binafsi ili Kuongoza Maisha Yetu
Mkutano mkuu wa Aprili 2020


Baraka za Ufunuo Unaoendelea kwa Manabii na Ufunuo Binafsi ili Kuongoza Maisha Yetu

Ufunuo unaoendelea umepokelewa na bado unaendelea kupokelewa kupitia njia za Bwana ambazo ameziweka.

Leo nitazungumza juu ya ufunuo unaoendelea kwa manabii na ufunuo binafsi ili kuongoza maisha yetu.

Nyakati zingine tunapokea ufunuo hata kama hatujui makusudi ya Bwana. Muda mfupi kabla Mzee Jeffrey R. Holland hajaitwa kuwa Mtume mnamo Juni ya 1994, nilipata tukio zuri la kiufunuo kwamba yeye angeitwa. Mimi nilikuwa mwakilishi wa eneo na sikuona sababu ya kupewa ufahamu huo. Lakini sisi tulikuwa wenza tukiwa wamisionari vijana mapema miaka ya 1960 huko Uingereza, na nilikuwa na mapenzi makubwa kwake. Nililichukulia tukio lile kama rehema nyororo kwangu. Katika miaka ya hivi karibuni, nimejiuliza kama Bwana alikuwa akiniandaa kuwa Kumi na Wawili mdogo kwa mmisionari huyu mwenza wa kushangaza ambaye alikuwa mmisionari mwenza wangu mdogo wakati tukiwa wamisionari vijana.1 Nyakati zingine ninawaonya wamisionari vijana wawe wakarimu kwa wamisionari wenza wao wadogo kwa sababu hawajui kamwe ni lini hao wadogo watakuwa wenza wao wakubwa.

Ninao ushuhuda imara kwamba Kanisa hili lililorejeshwa linaongozwa na Mwokozi wetu, Yesu Kristo. Yeye anajua ni nani awaite kama Mitume Wake na katika mpangilio gani awaite. Yeye pia anajua namna ya kumwandaa Mtume Wake mkubwa kuwa nabii na Rais wa Kanisa.

Tulibarikiwa asubuhi hii kumsikia nabii wetu mpendwa, Rais Russell M. Nelson, akitoa tangazo zito kwa ulimwengu linalohusiana na kuadhimisha miaka mia mbili ya Urejesho wa utimilifu wa injili ya Yesu Kristo.2 Tangazo hili la msingi lililotolewa na Rais Nelson limeweka wazi kwamba Kanisa la Yesu Kristo asili yake, uwepo wake, na mwelekeo wake wa baadaye unatokana na kanuni ya ufunuo endelevu. Tangazo hili jipya linawakilisha mawasiliano ya Baba mwenye upendo kwa watoto Wake.

Katika siku ya zamani, Rais Spencer W. Kimball alielezea hisia kama hizi nilizonazo leo. Yeye alisema: “Kati ya vitu vyote, ambavyo … tunapaswa kushukuru zaidi [kwavyo] ni kwamba hakika mbingu ziko wazi na kwamba kanisa lililorejeshwa la Yesu Kristo limejengwa juu ya mwamba wa ufunuo. Ufunuo unaoendelea hakika ndicho kiini cha injili ya Bwana na Mwokozi aliye hai, Yesu Kristo.”3

Nabii Henoko aliona mapema siku ambazo sisi tunaishi. Bwana alitambulisha kwa Henoko uovu mkuu ambao utakuwepo na kutoa unabii juu ya “dhiki kuu” itakayotokea. Hata hivyo, Bwana aliahidi, “lakini watu wangu nitawalinda.”4 “Na haki nitaishusha kutoka mbinguni; na ukweli nitaueneza kutoka duniani, ili kutoa ushuhuda wa Mwanangu wa Pekee.”5

Rais Ezra Taft Benson alifundisha kwa nguvu kubwa kwamba Kitabu cha Mormoni, jiwe la teo la dini yetu, kimejitokeza duniani katika kutimiza tangazo la Bwana kwa Henoko. Baba na Mwana na malaika na manabii waliomtokea Nabii Joseph Smith “walielekezwa na mbingu kurejesha uwezo muhimu kwenye ufalme.”6

Nabii Joseph Smith alipokea ufunuo baada ya ufunuo. Baadhi umetolewa wakati wa mkutano huu. Mafunuo mengi yaliyopokelewa na Nabii Joseph yamehifadhiwa kwa ajili yetu sisi katika Mafundisho na Maagano. Vitabu vyote vitakatifu vya Kanisa vinayo mawazo na mapenzi ya Bwana kwa ajili yetu katika kipindi hiki cha mwisho cha maongozi ya Mungu.7

Kama nyongeza kwa maandiko haya makuu ya kimsingi, tumebarikiwa kuwa na ufunuo unaoendelea kwa manabii walio hai. Manabii ni “mawakala wenye mamlaka kutoka kwa Bwana, walioruhusiwa kuzungumza kwa niaba Yake.”8

Baadhi ya mafunuo yana umuhimu mkubwa sana, na mengine yanaboresha uelewa wetu juu ya kweli muhimu za kiungu na kutoa mwongozo kwa ajili ya siku yetu.9

Tunashukuru sana kwa ajili ya ufunuo uliotolewa kwa Rais Spencer W. Kimball wenye kutoa ukuhani na baraka za hekaluni kwa wanaume wote wenye kustahili walio waumini wa Kanisa mnamo Juni 8, 1978.10

Nimehudumu na wengi wa Kumi na Wawili waliokuwepo na kushiriki wakati ufunuo huo wa thamani ulipopokelewa. Kila mmoja wao, katika maongezi ya faragha, alithibitisha mwongozo wenye nguvu na umoja wa kiroho Rais Kimball na wao waliouona. Wengi walisema ulikuwa ni ufunuo wenye nguvu zaidi ambao wamewahi kupokea kabla au baada ya wakati huo.11

Wale miongoni mwetu ambao sasa tunahudumu katika Akidi ya Mitume Kumi na Wawili tumebarikiwa katika siku yetu wakati mafunuo ya kipekee yamekuja kupitia manabii wa hivi karibuni.12 Rais Russell M. Nelson amekuwa wakala mwenye mamlaka kutoka kwa Bwana hususani katika mafunuo yanayohusiana na kuzisaidia familia kujenga mahali patakatifu pa imani katika nyumba zao, kukusanya Israeli waliotawanyika pande zote za pazia, na kuwabariki waumini waliopewa endaumenti katika mambo matakatifu ya ibada za hekaluni.

Wakati mabadiliko muhimu ya kubariki nyumba zetu yalipotangazwa kwenye mkutano mkuu wa Oktoba 2018, nilishuhudia “kwamba katika mashauriano ya Baraza la Urais wa Kwanza na Akidi ya Mitume Kumi na Wawili ndani ya hekalu, … baada ya mpendwa wetu nabii kumwomba Bwana kwa ajili ya ufunuo … , uthibitisho wenye nguvu ulipokelewa na wote.”13

Wakati huo, mafunuo mengine kuhusiana na ibada takatifu za hekaluni yalikuwa yamepokelewa lakini hayakuwa yametangazwa au kutekelezwa.14 Mwongozo huu ulianza na ufunuo binafsi wa kinabii kwa Rais Russell M. Nelson na uthibitisho mwepesi na wenye nguvu kwa wale wanaoshiriki katika mchakato. Rais Nelson mahususi aliwashirikisha akina dada wanaoongoza makundi ya Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama, Wasichana, na Msingi. Mwongozo wa mwisho, ndani ya hekalu, kwa Urais wa Kwanza na Akidi ya Mitume Kumi na Wawili ulikuwa mzito sana kiroho na wenye nguvu. Sote tulijua tulikuwa tumepokea mawazo, mapenzi na sauti ya Bwana.15

Ninatamka kwa moyo wote kwamba ufunuo unaoendelea umepokelewa na bado unaendelea kupokelewa kupitia njia za Bwana ambazo ameziweka. Ninashuhudia kuwa tangazo jipya ambalo Rais Nelson amelitangaza asubuhi hii ni ufunuo wa kuwabariki watu wote.

Tunatoa Mwaliko kwa Wote Kufurahia Karamu hii mezani kwa Bwana

Pia tunatamka hamu ya mioyo yetu ya kuungana tena na wale ambao wamekuwa walihangaika na shuhuda zao, wamekuwa hawashiriki ipasavyo, au majina yao kuondolewa kutoka kwenye kumbukumbu za Kanisa. Tunatamani kushiriki karamu pamoja nanyi, “juu ya maneno ya Kristo,” mezani pa Bwana, ili tujifunze mambo ambayo sote tunapaswa kufanya.16 Tunakuhitaji wewe! Kanisa linakuhitaji wewe! Bwana anakuhitaji wewe! Sala ya moyo wetu ni kwamba utajiunga nasi katika kumwabudu Mwokozi wa ulimwengu. Tunajua kwamba baadhi yenu mnaweza kuwa mlipata kukosewa, kutokirimiwa, au tabia nyingine ambayo siyo kama ya Kristo. Pia tunajua kwamba baadhi wamekuwa na changamoto kwenye imani yao kwamba yawezekana hawakupata shukrani kamili, kueleweka, au kukatiwa shauri.

Baadhi ya waumini wetu wa muda mrefu na waaminifu wameteseka kwa changamoto ya imani yao kwa muda mrefu. Ninapenda hadithi ya W. W. Phelps, ambaye aliacha Kanisa na kushuhudia dhidi ya Joseph Smith katika mahakama ya Missouri. Baada ya kutubu, alimwandikia Joseph, “Ninaijua hali yangu, wewe unaijua, na Mungu anaijua, na ninataka kuokolewa kama marafiki zangu watanisaidia.”17 Joseph alimsamehe, akamrudisha kazini, na kwa upendo akaandika, “Marafiki mwanzoni ni marafiki tena mwishoni.”18

Kaka zangu na dada zangu, bila kujali hali yako, tafadhali jua kwamba Kanisa na waumini wake watakukaribisha tena!

Ufunuo Binafsi ili Kuongoza Maisha Yetu

Ufunuo binafsi unapatikana kwa ajili ya wale wote ambao kwa unyenyekevu wanatafuta mwongozo kutoka kwa Bwana. Ni muhimu kama ufunuo wa kinabii. Ufunuo binafsi, wa kiroho kutoka kwa Roho Mtakatifu umesababisha mamilioni kupokea ushuhuda muhimu wa kubatizwa na kuthibitishwa kuwa waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

Ufunuo binafsi ni baraka muhimu inayopokelewa kufuatia ubatizo wakati tunapokuwa “tumetakaswa kwa kumpokea Roho Mtakatifu.”19 Ninaweza kukumbuka ufunuo maalumu wa kiroho wakati nilipokuwa na umri wa miaka 15. Kaka yangu mpendwa alikuwa akitafuta mwongozo kutoka kwa Bwana wa namna ya kumjibu mpendwa baba yetu, ambaye hakutaka kaka yangu akahudumie misheni. Mimi niliomba kwa nia thabiti pia na kupokea ufunuo binafsi juu ya ukweli wa injili.

Jukumu la Roho Mtakatifu

Ufunuo binafsi unategemea kweli za kiroho zinazopokelewa kutoka kwa Roho Mtakatifu.20 Roho Mtakatifu ndiye mfunuaji na mshuhudiaji wa ukweli wote, hususani ule wa Mwokozi. Pasipo Roho Mtakatifu, tusingeweza kujua kwamba Yesu ndiye Kristo. Jukumu lake la msingi ni kutoa ushahidi juu ya Baba na Mwana na vyeo Vyao na utukufu Wao.

Roho Mtakatifu anaweza kumshawishi kila mmoja katika njia yenye nguvu.21 Ushawishi huu hautakuwa endelevu isipokuwa mtu amebatizwa na kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu pia hutumika kama wakala wa kusafisha katika mchakato wa toba na msamaha.

Roho anawasiliana katika njia za ajabu. Bwana alitumia maelezo haya ya kupendeza:

“Nitakujulisha wewe akilini mwako na katika moyo wako, kwa njia ya Roho Mtakatifu, ambaye atakujia na ambaye atakaa moyoni mwako.

“Sasa, tazama, hii ni roho ya ufunuo.”22

Ingawa athari yake inaweza kuwa ina nguvu nyingi, mara nyingi zaidi huja kimya kimya, kama sauti tulivu, sauti ndogo.23 Maandiko yanajumuisha mifano mingi ya namna Roho anavyoshawishi akili zetu, ikijumuisha kusema amani akilini mwetu,24 kutawala akili zetu,25 kuangaza akili zetu,26 na hata sauti kutujia mawazoni mwetu.27

Baadhi ya kanuni ambazo hutuandaa sisi kupokea ufunuo zinajumuisha:

  • Kusali kwa ajili ya mwongozo wa kiroho. Kwa heshima na unyenyekevu tunahitaji kutafuta na kuomba28 na kuwa wavumilivu na kuwa tayari kukubali.29

  • Kujiandaa kwa ajili ya mwongozo wa kiungu. Hili linahitaji kwamba tuwe katika uwiano na mafundisho ya Bwana na katika ukubalifu kwa amri Zake.

  • Kupokea sakramenti kwa kustahili. Tunapofanya hivi, tunashuhudia na kufanya agano na Mungu kwamba tunajichukulia juu yetu jina la Mwanaye Mtakatifu na kwamba tutamkumbuka Yeye na kushika amri Zake.

Kanuni hizi hutuandaa sisi kupokea, kutambua, na kufuata misukumo na mwongozo wa Roho Mtakatifu. Hii inajumuisha “mambo ya amani … yale ambayo huleta shangwe [na] … uzima wa milele.”30

Maandalizi yetu ya kiroho yanaongezeka sana wakati tunapojifunza mara kwa mara maandiko na kweli za injili na kutafakari katika akili zetu mwongozo tunaoutafuta. Lakini kumbuka kuwa mvumilivu na kuamini katika wakati wa Bwana. Mwongozo unatolewa na Bwana mwenye maarifa yote wakati ambapo Yeye “kwa makusudi anachagua kutufunza sisi.”31

Ufunuo katika Miito na Majukumu Yetu

Roho Mtakatifu pia atatupa ufunuo katika miito na majukumu yetu. Katika uzoefu wangu, mwongozo wa kipekee wa kiroho mara nyingi huja wakati tunapojaribu kuwabariki wengine katika kutimiza wajibu wetu.

Ninaweza kukumbuka kama askofu kijana nilipokea simu ya kukata tamaa kutoka kwa wanandoa muda mfupi tu kabla ya kupanda ndege kwa ajili ya miadi ya kibiashara. Nilimlilia Bwana kabla ya kufika kwao ili nijue namna ambavyo ningeweza kuwabariki. Ilifunuliwa kwangu chanzo cha tatizo na jibu nililopaswa kuwapa. Mwongozo ule wa kiufunuo uliniruhusu mimi kutimiza wajibu mtakatifu wa wito wangu kama askofu licha ya muda mfupi niliokuwa nao. Maaskofu ulimwenguni kote nao pia wana aina hii ya uzoefu sawa na wangu. Kama rais wa kigingi, si tu nilipokea ufunuo muhimu lakini pia nilipokea maonyo binafsi ambayo yalikuwa muhimu ili kukamilisha makusudi ya Bwana.

Ninakuhakikishieni kwamba mwongozo wa kiufunuo unaweza kupokelewa na kila mmoja wetu tunapofanya kazi kwa unyenyevu katika shamba lake la mizabibu. Sehemu kubwa ya mwongozo wetu hutoka kwa Roho Mtakatifu. Nyakati zingine na kwa makusudi fulani, huja moja kwa moja kutoka kwa Bwana. Mimi binafsi ninashuhudia kwamba hii ni kweli. Mwongozo kwa ajili ya Kanisa, kwa ujumla wake, huja kwa Rais na nabii wa Kanisa.

Sisi, kama Mitume wa sasa, tumepata fursa ya kufanya kazi na kusafiri pamoja na nabii wetu wa sasa, Rais Nelson. Ninafupisha kile ambacho Wilford Woodruff alikisema kuhusu Nabii Joseph Smith; kwa kweli ni sawa kwa Rais Nelson. Nimejionea “utendaji kazi wa Roho wa Mungu pamoja naye, na mafunuo ya Yesu Kristo kwake na kutimia kwa mafunuo hayo.”32

Ombi langu la unyenyekevu kwenu ni kwamba kila mmoja wetu atafute ufunuo unaoendelea ili kuongoza maisha yetu na kumfuata Roho wakati tunapomwabudu Mungu Baba katika jina la Mwokozi wetu, Yesu Kristo, ambaye juu yake ninatoa ushahidi katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Mwaka 1960, wakati umri kwa ajili ya huduma ya umisionari kwa wavulana uliposhushwa kutoka umri wa miaka 20 mpaka 19, mimi nilikuwa mmoja wa wale wenye umri wa miaka 20; Mzee Jeffrey R. Holland alikuwa mmoja wa wale wenye umri wa miaka 19.

  2. Ona “Urejesho wa Utimilifu wa Injili ya Yesu Kristo: Tangazo la Miaka Mia Mbili kwa Ulimwengu,” katika Russell M. Nelson, “Msikilize Yeye,” Liahona, Mei 2020, 91. Tangazo hili linaungana na mengine matano ambayo yametolewa katika kipindi hiki cha maongozi ya Mungu na Urais wa Kwanza na Akidi ya Mitume Kumi na Wawili.

  3. Teachings of Presidents of the Church: Spencer W. Kimball (2006), 243; ona pia Mathayo 16:13–19.

  4. Musa 7:61.

  5. Musa 7:62. Bwana akaendelea, “Na haki na ukweli nitavifanya viifagie dunia kama vile kwa gharika, ili kuwakusanya wateule wangu kutoka pande nne za dunia” (Musa 7:62; ona pia Zaburi 85:11).

  6. Ezra Taft Benson, “The Gift of Modern Revelation,” Ensign, Nov. 1986, 80.

  7. Ona Ezra Taft Benson, “The Gift of Modern Revelation,” 80.

  8. Hugh B. Brown, “Joseph Smith among the Prophets” (Sixteenth Annual Joseph Smith Memorial Sermon, Logan Institute of Religion, Des. 7, 1958), 7.

  9. Ona Hugh B. Brown, “Joseph Smith among the Prophets,” 7. Katika mambo yote, mafunuo yanakubaliana na neno la Mungu lililotolewa kwa manabii waliopita.

  10. Ona Tamko Rasmi 2; ona pia 2 Nefi 26:33. Ufunuo hutekeleza mafundisho yaliyowekwa katika Kitabu cha Mormoni kwamba “wote ni sawa kwa Mungu,” ikijumuisha “weusi na weupe, wafungwa na walio huru, wanaume na wanawake” (2 Nefi 26:33). Ufunuo huu wa ajabu ulipokelewa na kuthibitishwa katika chumba kitakatifu cha ghorofani cha Hekalu la Salt Lake na Baraza la Urais wa Kwanza na Akidi ya Mitume Kumi na Wawili.

  11. Wengi wa Mitume walionesha kwamba ufunuo ule ulikuwa wenye nguvu sana na mtakatifu kwamba maneno yoyote yaliyotumika kuelezea yasingetosha, na kwa njia nyingine, yangepunguza kina na uhalisia wa ufunuo huo.

  12. Ona “Familia: Tamko kwa Ulimwengu,” Liahona, Mei. 2017, 145. Tangazo hili lilisomwa na Rais Gordon B. Hinckley kwenye Mkutano Mkuu wa Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama uliofanywa mnamo Septemba 23,1995, Jijini Salt Lake, Utah. Ona pia Thomas S. Monson, “Karibuni kwenye Mkutano,” Liahona, Nov. 2012, 4–5. Rais Monson alitangaza hitaji la kupunguzwa kwa umri kwa ajili ya huduma ya umisionari.

  13. Quentin L. Cook, “Uongofu wa Kina na wa Kudumu kwa Baba wa Mbinguni na Bwana Yesu Kristo,” Liahona, Nov. 2018, 11.

  14. Mafunuo yanayohusu ibada takatifu za hekaluni yalianza kutekelezwa katika mahekalu yote kuanzia Januari1, 2019. Ni muhimu kuelewa kwamba maelezo hayo maalumu ya kina kuhusu ibada za hekaluni yanajadiliwa tu ndani ya hekalu. Hata hivyo, kanuni zinafundishwa. Mzee David A. Bednar kwa uzuri kabisa alifundisha upekee wa maagano na ibada za hekaluni na jinsi gani kupitia hizo “nguvu za Uchamungu zinaweza kumiminika katika maisha yetu.” (“Acha Nyumba Hii Ijengwe kwa Jina Langu,” Liahona, Mei 2020, 86).

  15. Mchakato na mikutano hii ilifanyika katika Hekalu la Salt Lake mnamo Januari, Februari, Machi, na Aprili 2018. Ufunuo wa mwisho kwa Urais wa Kwanza na Akidi ya Mitume Kumi na Wawili ulikuwa Aprili 26, 2018.

  16. Ona 2 Nefi 32:3.

  17. Saints: The Story of the Church of Jesus Christ in the Latter Days, vol. 1, The Standard of Truth, 1815–1846 (2018), 418.

  18. Saints, 1:418.

  19. 3 Nefi 27:20.

  20. Roho Mtakatifu ni mshirika wa Uungu (ona 1 Yohana 5:7; Mafundisho na Maagano 20:28). Yeye ana mwili wa kiroho katika umbile na sura ya mwanadamu (ona Mafundisho na Maagano 130:22). Ushawishi wake unaweza kuwa kila mahali. Yeye ameungana katika umoja na Baba yetu wa Mbinguni na Yesu Kristo, Mwokozi wetu.

  21. Kwa uelewa mpana wa Nuru ya Kristo na tofauti kati ya Nuru ya Kristo na Roho Mtakatifu, ona 2 Nefi 32; Mafundisho na Maagano 88:7, 11–13; “Light of Christ,” Bible Dictionary. Ona pia, Boyd K. Packer, “Nuru ya Kristo,” Liahona, Mei 2005, 8–14.

  22. Mafundisho na Maagano 8:2–3.

  23. Ona Helamani 5:30; Mafundisho na Maagano 85:6.

  24. Ona Mafundisho na Maagano 6:23.

  25. Ona Mafundisho na Maagano 128:1.

  26. Ona Mafundisho na Maagano 11:13.

  27. Ona Enoshi 1:10.

  28. Ona Mathayo 7:7–8.

  29. Ona Mosia 3:19.

  30. Mafundisho na Maagano 42:61.

  31. Neal A. Maxwell, All These Things Shall Give Thee Experience (2007), 31.

  32. Wilford Woodruff, katika Teachings of Presidents of the Church: Joseph Smith (2007), 283.