Mkutano Mkuu
Kuwasaidia Masikini na Wenye Huzuni
mkutano mkuu wa Oktoba 2022


Kuwasaidia Masikini na Wenye Huzuni

Kanisa la Yesu Kristo limejikita kwenye kuwahudumia wenye uhitaji na pia limejikita kwenye kushirikiana na wengine katika juhudi hiyo.

Akina kaka na akina dada, mpendwa wetu Rais Russell M. Nelson atatuhutubia baadaye katika kikao hiki. Ameniomba niwe mnenaji wa kwanza.

Mada yangu leo inahusu kile Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho na waumini wake wanachotoa na kufanya kwa ajili ya masikini na wenye huzuni. Nitazungumza pia juu ya utoaji sawa na huo kutoka kwa watu wengine wema. Kutoa kwa wenye uhitaji ni kanuni katika dini zote za ki-Ibrahimu na zingine vilevile.

Miezi kadhaa iliyopita, Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho lilitoa ripoti kwa mara ya kwanza juu ya kiwango cha kazi zetu za kibinadamu ulimwenguni kote.1 Matumizi yetu ya 2021 kwa wenye uhitaji katika nchi 188 ulimwenguni kote yalikuwa $906 milioni—takribani dola bilioni. Kwa nyongeza, waumini wetu walijitolea kwa masaa zaidi ya milioni 6 ya huduma katika kusudi hilohilo.

Takwimu hizo, hata hivyo, ni ripoti isiyo kamili ya utoaji na usaidizi wetu. Hazijumuishi huduma binafsi waumini wetu wanayotoa mmoja mmoja wakati wakihudumiana katika nafasi walizoitwa na waumini wa kujitolea mpaka kwenye huduma ya muumini. Na ripoti yetu ya 2021 haitaji kile waumini wetu wanachofanya mmoja mmoja kupitia mashirika yasiyo na idadi ya hisani ambayo hayana uhusiano rasmi na Kanisa. Ninaanza na haya.

Mnamo 1831, chini ya miaka miwili ya kanisa lililorejeshwa kuundwa, Bwana alitoa ufunuo huu ili kuongoza waumini wa kanisa na, ninaamini, watoto wake wote, ulimwenguni kote:

“Kwani tazama, si vyema kwamba niamuru katika mambo yote; kwani yule alazimishwaye katika mambo yote, huyo ni mvivu na siyo mtumishi mwenye busara. ….

“Amini ninawaambia, wanadamu yawapasa kujishughulisha kwa shauku katika kazi njema, na kufanya mambo mengi kwa hiari yao wenyewe, na kutekeleza haki nyingi;

“Kwani uwezo upo ndani yao, ambamo wao ni mawakala juu yao wenyewe. Na kadiri wanadamu watakavyofanya mema hawatakosa thawabu zao.”2

Kwa zaidi ya miaka 38 kama Mtume na kwa zaidi ya miaka 30 ya kazi ya kuajiriwa, nimeona juhudi nyingi za ukarimu za mashirika na watu ambao ufunuo huu unawaelezea kama “kazi njema” na “[wana]tekeleza haki nyingi.” Kuna mifano isiyohesabika ya huduma kama hiyo ya kibinadamu kote ulimwenguni, kupita mipaka yetu wenyewe na kupita ufahamu wetu wa kawaida. Nikitafakari hili, namfikiria nabii wa Kitabu cha Mormoni‑Mfalme Benjamini, ambaye mahubiri yake yalijumuisha ukweli huu wa milele: “Mnapowatumukia wanadamu wenzenu mnamtumikia tu Mungu wenu.”3

Ustawi mkubwa na huduma ya kibinadamu kwa wanadamu wenzetu vimefundishwa na kufanyiwa kazi na Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho pamoja na sisi kama waumini wake. Kwa mfano, tunafunga kila mwanzo wa mwezi na kuchangia angalau kiasi kinacholingana cha milo ambayo haikuliwa ili kuwasaidia wenye uhitaji katika mikusanyiko yetu. Kanisa pia linatoa michango mikubwa kwa ajili ya huduma za kibinadamu na zinginezo kote ulimwenguni.

Licha ya yote ambayo Kanisa letu linafanya moja kwa moja, huduma nyingi za kibinadamu kwa watoto wa Mungu ulimwenguni kote hufanywa na watu na mashirika yasiyo na muunganiko rasmi na Kanisa letu. Kama vile mmoja wa Mitume wetu alivyosema: “Mungu hutumia zaidi ya mtu mmoja ili kukamilisha kazi yake kuu na ya muujiza. … Ni kazi kubwa sana, ngumu sana, kwa mtu mmoja yeyote.”4 Kama waumini wa Kanisa lililorejeshwa, tunahitaji kutambua zaidi na kushukuru zaidi kwa huduma ya wengine.

Kanisa la Yesu Kristo limejikita kwenye kuwahudumia wenye uhitaji na pia limejikita kwenye kushirikiana na wengine katika juhudi hiyo. Hivi karibuni tumetoa zawadi kubwa kwenye Programu ya Chakula Ulimwenguni ya Umoja wa Mataifa. Kwa zaidi ya miongo mingi ya kazi yetu ya kibinadamu, mashirika mawili yanasimama kama washirika wakuu: miradi ya ushirikiano na mashirika ya Msalaba Mwekundu na Mwezi Mwekundu kwenye jozi za nchi imewapatia watoto wa Mungu nafuu kubwa wakati wa majanga ya asili na migogoro. Vivyo hivyo, tuna rekodi ya muda mrefu ya usaidizi pamoja na Huduma ya Faraja ya Katoliki. Mashirika haya yametufunza sana kuhusu darasa la faraja ulimwenguni.

Pia tumekuwa na ushirikiano wenye tija na mashirika mengine, ikiwa ni pamoja na Msaada wa Kiislamu, Maji kwa ajili ya Watu na MSAADA wa Isra, nikitaja machache. Wakati kila shirika la kibinadamu likiwa na eneo lake la utendaji kazi, tunashiriki lengo moja la kupunguza mateso miongoni mwa watoto wa Mungu. Yote haya ni sehemu ya kazi ya Mungu kwa watoto Wake.

Ufunuo wa siku za leo unafundisha kwamba Mwokozi wetu Yesu Kristo, ni “nuru ya kweli imwangazayo kila mtu ajaye ulimwenguni.”5 Kama matokeo, watoto wote wa Mungu huangazwa kumtumikia Yeye na kutumikiana kwa maarifa yao yote na uwezo wao wote.

Kitabu cha Mormoni kinafundisha kwamba “kila kitu kinachokaribisha na kushawishi kufanya mema, na kumpenda Mungu, na kumtumikia, kinaongozwa na Mungu.”6

Kinaendelea:

“Kwani tazama, Roho ya Kristo imetolewa kwa kila mtu, ili ajue mema na maovu; kwa hivyo, ninawaonyesha njia ya kuhukumu; kwani kila kitu kinachokaribisha kufanya mema, na kushawishi kuamini katika Kristo, kinasababishwa na uwezo na thawabu ya Kristo. …

“Na sasa, ndugu zangu, … mnajua nuru ambayo kwake mnaweza kuhukumu, nuru ambayo ni nuru ya Kristo.”7

Hapa kuna mifano ya baadhi ya watoto wa Mungu wakiwasaidia watoto wengine wa Mungu kwa mahitaji yao ya msingi ya chakula, huduma za matibabu na kufundisha.

Miaka kumi iliyopita, Kanhdaris, mume na mke wa dhehebu la Sikh huko Umoja wa Falme za Kiarabu, binafsi walianzisha juhudi kubwa ya kuwalisha wenye njaa. Kupitia hekalu la Guru Nanak Darbar Sikh, kwa sasa wanahudumia zaidi ya milo 30,000 isiyo na nyama kila wikiendi kwa yeyote ambaye huingia ndani ya milango yao, bila kujali dini au mbari. Dkt. Kanhdari anaeleza, “Tunaamini kwamba sote ni wamoja; sote ni watoto wa Mungu mmoja na tuko hapa kuwahudumia binadamu.”8

Utoaji wa dawa na matunzo ya meno kwa wenye uhitaji ni mfano mwingine. Huko Chicago, nilikutana na daktari wa huduma za dharura mwenye asili ya Syria na Marekani, Dkt. Zaher Sahloul. Ni mmoja wa waanzilishi wa MedGlobal, ambayo inawaleta pamoja wataalamu wa tiba ili kujitolea muda wao, ujuzi, maarifa na uongozi kuwasaidia wengine walio katika migogoro, kama vile kwenye vita ya Syria, ambapo Dkt. Sahloul alihatarisha maisha yake katika kutoa huduma za matibabu kwa raia. MedGlobal na mashirika kama hayo (ikiwa ni pamoja na wataalamu wengi Watakatifu wa Siku za Mwisho) wanaonesha kwamba Mungu huwapa msukumo wataalamu wenye imani ili kuleta faraja inayohitajika kwa masikini ulimwenguni kote.9

Wengi wa watoto wa Mungu wasio na ubinafsi wanajihusisha katika juhudi za kufundisha, pia ulimwenguni kote. Mfano mzuri, unaojulikana kwetu kupitia juhudi zetu za kibinadamu, ni shughuli ya mtu anayejulikana kama Bwana Gabriel, ambaye amekuwa mkimbizi kutokana na migogoro mingi ya mara kadhaa. Hivi karibuni aligundua kwamba mamia elfu ya watoto wakimbizi wa Afrika Mashariki walihitaji msaada ili kuweka hai matumaini yao na kuchangamsha akili zao. Aliwakusanya walimu wengine kwenye mkusanyiko wa wakimbizi kwenye kile walichokiita “shule za miti,” ambapo watoto walikusanyika kwa ajili ya masomo chini ya kivuli cha mti. Hakuwasubiri wengine waanzishe au waongoze bali yeye binafsi aliongoza juhudi ambazo zimetoa fursa za kujifunza kwa maelfu ya watoto wa shule ya msingi wakati wa miaka ya hofu ya kuhamishwa.

Ndiyo, mifano hii mitatu haina maana kwamba kila kilichosemwa au kufanywa na mashirika au watu binafsi kinachoonekana kuwa kizuri au cha Mungu hakika ni cha Mungu. Mifano hii huonesha kwamba Mungu huyapa msukumo mashirika na watu wengi ili kufanya mengi mazuri. Pia inaonesha kwamba wengi wetu tunapaswa kutambua mazuri yaliyofanywa na wengine na kuyaunga mkono kwani tuna muda na nyenzo za kufanya hivyo.

Hapa ni mifano ya baadhi ya huduma zinazoungwa mkono na Kanisa na ambazo waumini wetu na watu wengine wema na mashirika pia yanaunga mkono kwa matoleo binafsi ya muda na pesa.

Ninaanza na uhuru wa dini. Katika kuunga mkono hilo, tunafanyia kazi mapendeleo yetu wenyewe, lakini pia mapendeleo ya dini zingine. Kama vile Rais wetu wa kwanza, Joseph Smith, alivyofundisha, “Tunadai haki ya kumwabudu Mungu Mwenyezi kulingana na mwongozo wa dhamiri yetu sisi wenyewe, na tunawaruhusu watu wote haki hiyo, na waabudu namna, mahali, au chochote watakacho.”10

Mifano mingine ya msaada wa kibinadamu wa Kanisa lililorejeshwa na misaada mingine ambayo pia huungwa mkono kwa kujitolea kwa waumini wetu ni shule zetu maarufu, vyuo vya kati na vyuo vikuu na michango yetu mikubwa isiyo maarufu ambayo sasa inachapishwa kwa ajili ya faraja ya wale wanaoteseka kutokana na maangamizo na kuhamishwa kwa sababu ya majanga ya asili kama vimbunga na matetemeko.

Shughuli zingine za hisani zinazoungwa mkono na waumini wetu kwa matoleo yao na juhudi zao za hiari ni nyingi mno kuziorodhesha, lakini kutaja hizi chache kutaonesha wingi wake na umuhimu wake: kukomesha ubaguzi na chuki zingine, utafiti juu ya jinsi ya kuzuia na kutibu magonjwa, kuwasaidia walemavu; kusaidia mashirika ya muziki na makumbusho na kuboresha mazingira ya kimaadili na kimwili kwa wote.

Juhudi zote za kibinadamu za Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho zinatafuta kufuata mfano wa watu waadilifu walioelezwa katika Kitabu cha Mormoni: “Na hivyo, hata katika hali yao ya kufanikiwa hawakumfukuza yeyote aliyekuwa uchi, au walio na njaa, au walio na kiu, au wale ambao walikuwa wagonjwa, … na walikuwa … wakarimu kwa wote, wote wazee kwa vijana, wote watumwa na walio huru, wote wanaume kwa wanawake, washiriki wa kanisa na wale wasio washiriki wa kanisa.”11

Ninashuhudia juu ya Yesu Kristo, ambaye nuru na Roho wake huwaongoza watoto wote wa Mungu katika kuwasaidia masikini na wenye huzuni kote ulimwenguni. Katika jina la Yesu Kristo, amina.