Mkutano Mkuu
Kwa Ushirikiano na Bwana
mkutano mkuu wa Oktoba 2022


Kwa Ushirikiano na Bwana

Injili ya urejesho ya Yesu Kristo inatangaza kanuni ya ushirikiano kamili kati ya mwanamke na mwanamume, kote katika maisha ya duniani na ya milele yote.

Ndani ya kipindi cha miezi michache ya ndoa yetu, mke wangu mpendwa alielezea hamu yake ya kujifunza muziki. Nikikusudia kumridhisha yeye, niliamua kuandaa mshangao mkubwa wa dhati kwa mpenzi wangu. Nilienda kwenye duka la vyombo vya muziki na kumnunulia zawadi ya kinanda. Mimi kwa msisimko niliweka risiti ya ununuzi ndani ya boksi pamoja na ua zuri na nikampa, nikitarajia majibu ya shukrani kwa mume wake mwenye upendo na makini sana.

Alipofungua lile boksi na kuona yaliyomo, kwa upendo aliniangalia na kusema, “Ee, mpenzi wangu, wewe ni wa ajabu! Lakini acha nikuulize swali: je, hii ni zawadi au deni?” Baada ya kushauriana kwa pamoja kuhusu zawadi ile, tuliamua kufuta ununuzi ule. Tulikuwa tukiishi kwenye bajeti ya mwanafunzi, kama ilivyo kwa vijana wengi waliooana hivi karibuni. Tukio hili lilinisaidia mimi kutambua umuhimu wa kanuni ya ushirikiano kamili katika uhusiano wa kindoa na jinsi matumizi yake yangeweza kutusaidia mke wangu nami kuwa wa moyo mmoja na wazo moja.1

Injili ya urejesho ya Yesu Kristo inatangaza kanuni ya ushirikiano kamili kati ya mwanamke na mwanamume, kote katika maisha ya duniani na ya milele yote. Ingawa kila mmoja ana sifa na majukumu maalumu, mwanamume na mwanamke hujaza nafasi zilizo sawa na muhimu katika mpango wa Mungu wa furaha kwa watoto Wake.2 Hii ilikuwa dhahiri kutokea mwanzoni kabisa wakati Bwana alipotangaza kwamba “sio vyema kwa huyo mtu kuwa peke yake; kwa sababu hiyo [Yeye ange] mfanyia msaidizi wa kufanana naye.”3

Katika mpango wa Mungu, “msaidizi wa kufanana naye” alikuwa ni mwenza ambaye angetembea bega kwa bega na Adamu katika ushirikiano mkamilifu.4 Ukweli ni kwamba, Hawa alikuwa ni baraka ya kimbingu katika maisha ya Adamu. Kupitia asili yake ya kiungu na sifa zake za kiroho, alimshawishi Adamu kufanya kazi kwa ushirikiano na yeye ili kufanikisha mpango wa Mungu wa furaha kwa wanadamu wote.5

Hebu tuzingatie kanuni mbili za msingi ambazo zinaimarisha ushirikiano kati ya mwanamume na mwanamke. Kanuni ya kwanza ni sisi sote ni sawa mbele za Mungu.”6 Kulingana na mafundisho ya injili, tofauti kati ya mwanamke na mwanamume haibatili ahadi za milele ambazo Mungu anazo kwa ajili ya wana na mabinti Zake. Mmoja hana uwezekano mkubwa zaidi wa utukufu wa kiselestia kuliko mwingine huko mbinguni.7 Mwokozi Mwenyewe anatualika sisi sote, watoto wa Mungu, “kuja Kwake, ili kupokea wema Wake, na hamnyimi ye yote ajaye Kwake.”8 Kwa hiyo, katika muktadha huu, sisi sote tunahesabiwa kuwa sawa mbele Zake.

Wanandoa wanapoelewa na kushirikisha kanuni hii, hawajiweki wenyewe kama rais au makamu wa rais katika familia zao. Hakuna mkuu wala mdogo katika uhusiano wao wa ndoa, na wala hatembei mbele au nyuma ya mwingine. Wanatembea bega kwa bega, kama walio sawa, na wazao watakatifu wa Mungu. Wanakuwa wamoja katika wazo, matamanio, na makusudi pamoja na Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo,9 kuiongoza na kukielekeza kikundi cha familia kwa pamoja.

Katika ushirikiano wa usawa, “upendo si kumiliki bali ni ushiriki … sehemu ya ule uumbaji-pamoja ambao ndio wito wetu kibinadamu.”10 “Kwa ushirikiano wa kweli, mume na mke wanaungana katika umoja wa umoja wa ‘utawala usio na mwisho’ kwamba ‘pasipo njia za kulazimisha’ utatiririka pamoja na maisha ya kiroho kwao na vizazi vyao ‘milele na milele.’”11

Kanuni ya pili inayofaa ni Kanuni ya Dhahabu, iliyofundishwa na Mwokozi katika Mahubiri ya Mlimani: “Basi yo yote mtakayo kutendewa na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo.”12 Kanuni hii inaonyesha mtazamo wa kuheshimiana, umoja, na kutegemeana na imejengwa juu ya amri kuu ya pili, “Mpende jirani kama nafsi yako.”13 Inaungana na sifa nyingine za Kikristo kama vile uvumilivu, upole, unyenyekevu, na ukarimu.

Ili kuelewa vyema matumizi ya kanuni hii, tunaweza kutazama kwenye mkataba mtakatifu na wa milele uliowekwa na Mungu kati ya wazazi wetu wa kwanza, Adamu na Hawa. Wakawa mwili mmoja,14 wakitengeneza ukubwa wa umoja ambao uliwaruhusu wao kutembea kwa pamoja kwa heshima, shukrani, na upendo, wakisahau kuhusu wao wenyewe na kila mmoja akitafuta ustawi wa mwenzake kwanza kwenye safari yao ya milele.

Sifa za aina hizo hizo ndizo tunazojitahidi kuzitafuta katika umoja wa ndoa hivi leo. Kupitia kuunganishwa hekaluni, mwanamke na mwanamume wanaingia kwenye utaratibu mtakatifu wa ndoa katika agano jipya na lisilo na mwisho. Kwa njia ya utaratibu huu wa ukuhani, wanapewa baraka za milele, na nguvu za kiungu ili kuelekeza masuala yao ya kifamilia kadiri wanavyoishi kulingana na maagano waliyofanya. Kuanzia wakati huo na kuendelea wanasonga mbele wakiwa wenye kutegemeana na katika ushirikiano mkamilifu na Bwana, hususani katika kila moja ya majukumu yao yaliyoainishwa kiungu ya malezi na uongozi katika familia yao.15 Kulea na kuongoza yanaingiliana na ni majukumu mtambuka, ambako inamaanisha kwamba wakina mama na wakina baba “wanawajibika kusaidiana kama wenza walio sawa”16 na wanashiriki uongozi ulio na uwiano sawa wa nyumba yao.

“Kulea kunamaanisha kulisha, kufundisha, na kusaidia” wanafamilia, ambako kunafanyika kwa kuwasaidia “kujifunza kweli za injili na kukuza imani katika Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo” katika mazingira ya upendo. Kuongoza inamaanisha “kusaidia kuiongoza familia kurudi kuishi katika uwepo wa Mungu. Hii inafanyika kwa kuhudumu na kufundisha kwa upole, unyenyekevu, na upendo safi.” Pia inajumuisha “kuwaongoza wanafamilia katika sala za kila siku, kujifunza injili, na vipengele vingine vya kuabudu. Wazazi wanafanya kazi katika umoja,” wakifuata mfano wa Yesu Kristo, “ili kutimiza majukumu haya [mawili makubwa].”17

Ni muhimu kuzingatia kwamba serikali katika familia inafuata mpangilio wa kipatriaki, ukitofautiana katika baadhi ya vipengele na uongozi wa ukuhani katika kanisa.18 Mpangilio wa kipatriaki unahitaji kwamba wake na waume wawajibike moja kwa moja kwa Mungu kwa utimizaji wa majukumu yao matakatifu katika familia. Unahitaji ushirikiano mkamilifu—utiifu wa hiari kwa kila kanuni ya haki na uwajibikaji—na inatoa fursa kwa ajili ya kukua ndani ya mazingira ya upendo na usaidizi wa heshima.19 Majukumu haya maalumu hayaonyeshi mfumo wa ngazi za madaraka na yanazuia kabisa aina yo yote ya unyanyasaji au matumizi ya madaraka kupita kiasi.

Uzoefu wa Adamu na Hawa baada ya kuondoka kwenye Bustani ya Edeni, kwa uzuri kabisa inafafanua wazo la kutegemeana baina ya mama na baba katika kulea na kuongoza familia yao. Kama inavyofundishwa katika kitabu cha Musa, walifanya kazi kwa pamoja ya kulima nchi kwa jasho la uso wao ili kukidhi mahitaji ya ustawi wa kimwili ya familia yao;20 waliwaleta watoto ulimwenguni;21 walililingana jina la Bwana kwa pamoja na walisikia sauti Yake “kutoka njia iendayo kwenye Bustani ya Edeni”;22 wakakubali amri Bwana alizowapa na wakajitahidi kwa pamoja kuzitii.23 Wao kisha “wakafanya mambo [haya] yajulikane kwa wana na mabinti zao”24 na “hawakuchoka kumlingana Mungu” kwa pamoja kulingana na mahitaji yao.25

Wapendwa kaka zangu na dada zangu, kulea na kuongoza ni fursa, na siyo vikwazo vya kipekee. Mtu mmoja yawezekana akawa na wajibu wa kitu fulani lakini yawezekana asiwe ndiye mtu pekee wa kufanya hilo. Wazazi wenye upendo wanapokuwa wanaelewa vyema majukumu makubwa haya mawili, watajitahidi kwa pamoja kulinda na kujali ustawi wa kimwili na kihisia wa watoto wao. Pia wanawasaidia kukabiliana na hatari za kiroho za siku yetu kwa kuwalea kwa neno jema la Bwana kama lilivyofunuliwa kwa manabii Wake.

Ingawa waume na wake husaidiana katika majukumu yao yaliyowekwa kiungu, “ulemavu, kifo, au hali nyinginezo zaweza kuhitaji marekebisho ya mtu binafsi.”26 Wakati mwingine mwana ndoa mmoja au mwingine atakuwa na jukumu la kutenda katika nafasi zote mbili kwa wakati mmoja, iwe kwa muda au kwa kudumu.

Hivi karibuni nilikutana na dada na kaka ambao kila mmoja anaishi katika hali hii. Kama wazazi pekee, kila mmoja wao, katika nyanja ya familia zao na katika ushirikiano na Bwana, wameamua kujitolea maisha yao yote kwa utunzaji wa kimwili na kiroho wa watoto wao. Hawajapoteza ufahamu wa maagano yao ya hekaluni waliyofanya na Bwana na ahadi Zake za milele licha ya ugumu wa talaka zao. Wote wawili wametafuta msaada wa Bwana katika mambo yote kama wanapoendelea kujitahidi kuvumilia changamoto zao na kutembea katika njia ya agano. Wanatumaini kwamba Bwana atashughulika na mahitaji yao, siyo tu katika maisha haya, bali milele yote. Wote wawili wamelea watoto wao kwa kuwafundisha kwa upole, unyenyekevu, na upendo safi hata wakati wanapopitia hali ngumu katika maisha. Kutokana na kile ninachojua, wazazi hawa wawili walio kila mtu peke yake hawamlaumu Mungu kwa bahati mbaya zao. Badala yake, wakiwa na mng’aro mkamilifu wa tumaini na kujiamini kwa baraka za Bwana alizonazo ghalani kwa ajili yao.27

Akina kaka na akina dada, Mwokozi aliweka mfano kamili wa umoja na uwiano wa madhumuni na mafundisho na Baba yetu aliye Mbinguni. Aliomba kwa niaba ya wanafunzi Wake, akisema, “Naomba ili wote wawe kitu kimoja; kama wewe, Baba, kama vile wewe ulivyo ndani yangu, nami ndani yako, ili nao waweze kuwa kitu kimoja na sisi.”28

Ninakushuhudieni kwamba sisi—wanawake na wanaume—tunapofanya kazi kwa pamoja katika ushirikiano wa kweli na ulio sawa, tutafurahia umoja uliofundishwa na Mwokozi tunapotimiza majukumu ya kiungu katika uhusiano wa ndoa zetu. Ninawaahidi, katika jina la Kristo, kwamba mioyo yetu “itafumwa pamoja katika umoja na upendo,”29 tutaona shangwe zaidi katika safari yetu ya kwenda kwenye uzima wa milele, na uwezo wetu wa kuhudumiana utaongezeka na kuwa wa kipekee.30 Ninatoa ushahidi wangu juu ya kweli hizi katika jina takatifu la Mwokozi Yesu Kristo, amina.