Mkutano Mkuu
Yesu Kristo Ni Faraja
Mkutano mkuu wa Aprili 2023


Yesu Kristo Ni Faraja

Tunaweza kushirikiana na Mwokozi ili kusaidia kutoa faraja ya kimwili na kiroho kwa wale walio na mahitaji—na katika mchakato huo kupata faraja yetu wenyewe.

Wakiwa na imani katika Yesu Kristo na kutumaini yale waliyokuwa wamesikia kuhusu miujiza Yake, waliomhudumia mtu aliyepooza walimleta kwa Yesu. Walikuwa wabunifu katika kumfikisha pale—kufunua dari na kumshusha mtu huyo, akiwa kitandani kwake, hadi mahali ambapo Yesu alikuwa akifundisha. Yesu “alipoiona imani yao, akamwambia [yule mwenye kupooza], umesamehewa dhambi zako.”1 Kisha, “Ondoka, ujitwike godoro lako, uende zako nyumbani kwako.”2 Na mara yule mtu aliyepooza akasimama, akachukua kitanda chake, akaenda zake nyumbani, “akimtukuza Mungu.”3

Je, tunajua nini zaidi kuhusu marafiki waliotoa huduma kwa mtu aliyepooza? Tunajua kwamba Yesu alitambua imani yao. Na baada ya kumwona na kumsikia Mwokozi na kuwa mashahidi wa miujiza Yake, “walishangazwa” na “wakamtukuza Mungu.”4

Yesu Kristo alikuwa ametoa uponyaji uliotumainiwa—faraja ya kimwili kutokana na matokeo yenye kulemaza ya ugonjwa sugu. Cha muhimu, Mwokozi pia alitoa faraja ya kiroho katika kumwondolea mtu huyu dhambi.

Na marafiki—katika jitihada zao za kumtunza mwenye uhitaji, walipata chanzo cha faraja; walimpata Yesu Kristo.

Ninashuhudua kwamba Yesu Kristo ni faraja. Kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo, tunaweza kuondolewa mzigo na matokeo ya dhambi na kusaidiwa katika udhaifu wetu.

Na kwa sababu tunampenda Mungu, na tumefanya agano la kumtumikia Yeye, tunaweza kushirikiana na Mwokozi kusaidia kutoa faraja ya kimwili na kiroho kwa wale walio na mahitaji—na katika mchakato huo kupata faraja yetu wenyewe katika Yesu Kristo.5

Nabii wetu mpendwa, Rais Russell M. Nelson, alitualika tuushinde ulimwengu na tupate pumziko.6 Alifafanua “pumziko la kweli” kama “faraja na amani.” Rais Nelson alisema, “Kwa sababu Mwokozi, kupitia Upatanisho Wake usio na kikomo, alimkomboa kila mmoja wetu kutokana na udhaifu, makosa, na dhambi, na kwa sababu Yeye alipitia kila maumivu, wasiwasi, na mzigo ambao umewahi kuwa nao, basi unapotubu kwa dhati na kutafuta msaada Wake, unaweza kuinuka juu ya ulimwengu huu hatari wa sasa.”7 Hii ndiyo faraja ambayo Yesu Kristo hutupatia!

Kila mmoja wetu amebeba begi la mgongoni la kisitiari. Inaweza kuwa kikapu juu ya kichwa chako au mkoba au rundo la vitu vilivyofungwa kwa kitambaa na kuwekwa juu ya bega lako. Lakini kwa mawazo yetu, hebu tuliite begi la mgongoni.

Begi hili la kisitiari ni ambalo ndani yake tunabeba mizigo ya kuishi katika ulimwengu ulioanguka. Mizigo yetu ni kama mawe kwenye begi. Kwa ujumla, kuna aina tatu:

  • Mawe yatokanayo na matendo yetu kwa sababu ya dhambi.

  • Mawe kwenye mabegi yetu kwa sababu ya chaguzi zetu duni, tabia isiyofaa au udhalimu wa wengine.

  • Na mawe tunayoyabeba kwa sababu tunaishi katika hali ya kuanguka. Hii hujumuisha mawe ya ugonjwa, maumivu, magonjwa sugu, huzuni, kukata tamaa, upweke na matokeo ya majanga ya asili.

Ninatamka kwa shangwe kwamba mizigo yetu ya kimwili, mawe haya kwenye mabegi yetu ya mgongoni ya kisitiari hayahitajiki kuhisiwa kuwa ni mazito.

Yesu Kristo anaweza kufanya mzigo wetu uwe mwepesi.

Yesu Kristo anaweza kuinua mizigo yetu.

Yesu Kristo anatupatia njia ya kutuondolea uzito wa dhambi.

Yesu Kristo ndiye faraja yetu.

Yeye alisema:

“Njooni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha [yaani, faraja na amani].

“Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu.

“Kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”8

Kwamba nira ni laini na mzigo ni mwepesi hudhaniwa kwamba tunaingia kwenye nira pamoja na Mwokozi, kwamba tunashiriki mizigo yetu pamoja Naye, kwamba tunamwacha Yeye aubebe mzigo wetu. Hiyo inamaanisha kuingia katika uhusiano wa agano na Mungu na kushika agano hilo, ambalo, kama Rais Nelson ambavyo ameeleza, “hufanya kila kitu kuhusu maisha kuwa rahisi.” Alisema, “Kujifunga nira na Mwokozi humaanisha kwamba unaweza kutumia nguvu Zake na uwezo Wake wa kukomboa.”9

Basi kwa nini sisi tunakuwa wachoyo kwa mawe yetu? Kwa nini mchezaji wa besiboli aliyechoka atakataa kuondoka kwenye kilima wakati msaidizi yuko pale tayari kumalizia mchezo? Kwa nini ning’ang’anie kuendelea na hali yangu nikiwa peke yangu wakati Msaidizi anasimama akiwa tayari kunisaidia?

Rais Nelson amefundisha, “Yesu Kristo … anasimama na mikono iliyonyooshwa, akitumaini na kuwa tayari kutuponya, kutusamehe, kutusafisha, kutuimarisha na kututakasa.”10

Basi kwa nini tunang’ang’ania kubeba mawe yetu peke yetu?

Hili limekusudiwa kama swali binafsi, kwa kila mmoja wenu kujiuliza.

Kwangu mimi, ni tabia mbaya ya kiburi kilichopitwa na wakati. “Nimepata hiki,” ninasema. “Hakuna wasiwasi; nitakikamilisha.” Ni yule mdanganyifu mkuu ambaye hutaka nijifiche mbali na Mungu, nigeuke mbali na uwepo Wake, na nifanye mimi mwenyewe.

Akina kaka na akina dada, siwezi kufanya peke yangu, na sihitaji iwe hivyo, na sitaki kufanya hivyo. Kuchagua kuunganishwa kwa Mwokozi wangu, Yesu Kristo, kupitia maagano niliyofanya na Mungu, “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.”11

Washika maagano wanabarikiwa kwa faraja ya Mwokozi.

Tafakari mfano huu katika Kitabu cha Mormoni: Watu wa Alma waliteswa kwa kupewa “kazi juu yao, na … wasimamizi kuwasimamia.”12 Wakiwa wamekatazwa kusali kwa sauti, “walimimina mioyo yao kwa [Mungu]; na alijua mawazo ya mioyo yao.”13

Na “sauti ya Bwana iliwafikia katika mateso yao, ikisema: lnueni vichwa vyenu na msherehekee, kwani ninajua agano ambalo mlinifanyia; na nitafanya agano na watu wangu na kuwakomboa kutoka utumwani.

“Na nitawapunguzia mizigo ambayo imewekwa mabegani mwenu, hata kwamba hamtaisikia kamwe migongoni mwenu.”14

Na mizigo yao “ilifanywa kuwa miepesi,” na “Bwana aliwatia nguvu ili waweze kubeba mizigo yao kwa urahisi, na walinyenyekea kwa furaha na subira kwa mapenzi yote ya Bwana.”15

Wale washika maagano walipokea msaada kwa njia ya faraja, kuongezeka kwa uvumilivu na uchangamfu, urahisi wa mizigo yao kwamba walihisi wepesi, na hatimaye ukombozi.16

Sasa hebu turudi kwenye mabegi yetu ya kisitiari.

Toba, kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo, ndiyo hutuondolea uzito wa mawe ya dhambi. Na kwa zawadi hii adhimu, rehema ya Mungu hutusaidia sisi kutokana na uzito na madai mengine ya haki yasiyoweza kuondolewa.17

Upatanisho wa Yesu Kristo pia hutuwezesha sisi kupokea nguvu ya kusamehe, ambayo huturuhusu kutua mzigo tunaobeba kwa sababu ya kutendewa vibaya na wengine.18

Basi Mwokozi hutuondolea vipi mizigo ya maisha katika ulimwengu ulioanguka tukiwa wenye miili itakayokufa yenye kupata huzuni na maumivu?

Mara nyingi, Yeye huleta aina hiyo ya faraja kupitia sisi! Kama waumini wa agano wa Kanisa Lake, tunaahidi “kuomboleza pamoja na wale wanaoomboleza” na “kuwafariji wale wanaohitaji faraja.”19 Kwa sababu “tumekuja katika zizi la Mungu” na “tunaitwa watu wake,” ‘tuko tayari kubebeana mizigo, ili iwe miepesi.”20

Baraka yetu ya agano ni kushirikiana na Yesu Kristo katika kutoa faraja, ya kimwili na ya kiroho, kwa watoto wote wa Mungu. Sisi ni njia ambayo kupitia hiyo Yeye hutoa faraja.21

Na kwa hivyo, kama marafiki wa mtu aliyepooza, “tunawasaidia walio dhaifu, kuinua mikono iliyolegea, na kuimarisha magoti dhaifu.”22 “Tunabebeana … mizigo, na hivyo kuitimiza sheria ya Kristo.”23 Tunapofanya hivyo, tunakuja kumjua Yeye, na kuwa kama Yeye, na kupata faraja Yake.24

Faraja ni nini?

Ni kuondolewa au kufanywa wepesi kwa kitu chenye kuleta maumivu, kusumbua, au kulemea, au nguvu ya kustahimili. Humaanisha mtu ambaye huchukua nafasi ya mwingine. Ni marekebisho ya kosa kisheria.25 Neno la kifaransa lenye asili ya Kingereza kutoka Kifaransa cha Kale, neno relever, au “kuinua,” na kutoka Kilatini relevare, au “kuinua tena .”26

Akina kaka na akina dada, Yesu Kristo ni faraja. Ninashuhudia kwamba Yeye alifufuka tena katika siku ya tatu na, akiwa ametimiza upendo na Upatanisho usio na mwisho, anasimama mikono ikiwa wazi, akitupatia fursa ya kufufuka tena, kuokolewa, na kuinuliwa na kuwa kama Yeye. Faraja ambayo Yeye hutupatia ni ya milele.

Kama wanawake waliotembelewa na malaika asubuhi ile ya kwanza ya Pasaka, natamani “kwenda upesi” na kwa “furaha kuu” kutoa taarifa kwamba Yeye amefufuka.27 Katika jina la Mwokozi wetu, Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Luka 5:20.

  2. Marko 2:11.

  3. Luka 5:25.

  4. Luka 5:26.

  5. Ona. Todd Christofferson, “The First Commandment First” (Brigham Young University devotional, Mar. 22, 2022), 2, speeches.byu.edu: “Upendo wetu kwa Mungu huinua uwezo wetu wa kuwapenda wengine kikamilifu zaidi na kwa ukamilifu kwa sababu sisi kimsingi ni washiriki pamoja na Mungu katika uangalizi wa watoto wake” (msisitizo umeongezwa).

  6. Ona Russell M. Nelson, “Ushinde Ulimwengu na Upate Pumziko,” Liahona, Nov. 2022, 95–98.

  7. Russell M. Nelson, “Ushinde Ulimwengu na Upate Pumziko,” 96.

  8. Mathayo 11:28–30.

  9. Russell M. Nelson, “Ushinde Ulimwengu na Upate Pumziko,” 97.

  10. Russell M. Nelson, “Tunaweza Kufanya Vizuri na Kuwa Bora Zaidi,” Liahona, Mei 2019, 67.

  11. Wafilipi 4:13.

  12. Mosia 24:9.

  13. Mosiah 24:12.

  14. Mosia 24:13–14; msisitizo umeongezwa.

  15. Mosia 24:15.

  16. Ona Mosia 24:13–14.

  17. Ona Alma 34:14–16; ona pia Mosia 15:8–9.

  18. Ona Russell M. Nelson, “Four Gifts That Jesus Christ Offers to You” (First Presidency Christmas devotional, Dec. 2, 2018), broadcasts.ChurchofJesusChrist.org: “Zawadi ya pili ambayo Mwokozi hutoa ni uwezo wa kusamehe. Kupitia Upatanisho Wake usio na mwisho, unaweza kuwasamehe wale waliokuudhi na ambao kamwe hawawezi kukubali kuwajibika kwa ajili ya ukatili wao kwako.

    “Daima ni rahisi kumsamehe mtu ambaye kwa dhati na kwa unyenyekevu anatafuta msamaha wako. Lakini Mwokozi atakupa uwezo wa kumsamehe yeyote ambaye amekutendea vibaya katika njia yoyote. Kisha matendo yao ya kuumiza hayawezi tena kuumiza nafsi yako.”

  19. Mosia 18:9

  20. Mosia 18:8.

  21. Muungano wa Usaidizi, shirika la wanawake la Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, lilianzishwa na Nabii Joseph Smith mnamo Machi 17, 1842, kama “kiambatisho kitakatifu cha ukuhani” (Dallin H. Oaks, “Funguo na Mamlaka ya Ukuhani,” Liahona, Mei 2014, 51). Katika kuchagua jina la shirika jipya, neno wenye ufadhili lilizingatiwa, lakini neno faraja lilipendwa na wanawake. Emma Smith, rais wa kwanza wa shirika, na Eliza R. Snow, katibu wake ambaye baadaye alihudumu kama rais wa pili wa Muungano wa Usaidizi, walieleza kwamba neno mfadhili lilikuwa neno maarufu—maarufu kwa taasisi za wakati huo—lakini umaarufu huo “ haupaswi kuwa mwongozo wetu.” Emma alieleza kwamba neno faraja lilielezea vyema misheni yao. “Tutafanya jambo lisilo la kawaida … tunatarajia matukio yasiyo ya kawaida na simu zenye uhitaji sana” (Emma Smith, in Nauvoo Relief Society Minute Book, Mar. 17, 1842, 12, josephsmithpapers.org). Hakika, jukumu la Muungano wa Usaidizi daima limekuwa kutoa faraja ya kimwili na kiroho. Joseph Smith alifundisha, “Jumuiya hii siyo tu ya kuwasaidia maskini, bali kuokoa roho” (in Nauvoo Relief Society Minute Book, June 9, 1842, 63, josephsmithpapers.org). Na hivyo Muungano wa Usaidizi unaendelea kutoa faraja: “Faraja kwa umaskini, faraja kwa magonjwa; faraja kwa mashaka, faraja kwa ujinga—faraja kwa yote yanayozuia furaha na maendeleo ya mwanamke” (John A. Widtsoe, Evidences and Reconciliations, arr. G. Homer Durham, 3 vols. in 1 [1960], 308).

  22. Mafundisho na Maagano 81:5, ona pia Waebrania 12:12.

  23. Wagalatia 6:2.

  24. Katika moja ya mikutano ya awali ya Muungano wa Usaidizi, Lucy Mack Smith, mama yake Nabii Joseph Smith, alisema, “Lazima tuthaminiane sisi kwa sisi, tulindane, tufarijiane na kupata mafundisho, ili sote tuweze kuketi pamoja mbinguni.” Mwanahistoria Jennifer Reeder aliandika kuhusu hili, “Kwa umoja wa kutoa faraja, wanawake walishirikiana na Kristo, na kwa kufanya hivyo, walipata faraja Yake” (First: The Life and Faith of Emma Smith [2021], 130).

  25. Ona Merriam-Webster.com Dictionary, “relief.”

  26. Ona Dictionary.com, “relief.”

  27. Ona Mathayo 28:1–8.