Mkutano Mkuu
Sauti ya Furaha!
Mkutano mkuu wa Aprili 2023


Sauti ya Furaha!

Ujenzi wa mahekalu umekuwa mojawapo ya vipaumbele vya juu kabisa vya manabii wote tangu Nabii Joseph Smith.

“Sasa, tunasikia nini katika injili ambayo tumeipokea? Sauti ya furaha! Sauti ya rehema kutoka mbinguni; na sauti ya ukweli kutoka duniani; … sauti ya furaha kwa walio hai na kwa ajili ya wafu, habari njema ya shangwe kuu.”1

Akina kaka na akina dada, ni kama vile haiwezekani kusikia maneno haya kutoka kwa Nabii Joseph Smith na kisha kukosa tabasamu kubwa!

Usemi wa furaha wa Joseph unaleta ukamilifu na ukuu wa shangwe inayopatikana katika mpango mkuu wa Mungu Baba yetu wa Mbinguni, kwani kama vile alivyotuhakikishia, “wanadamu wapo ili wapate shangwe.”2

Sisi sote tulishangilia3 katika maisha yetu kabla ya kuzaliwa duniani wakati tuliposikia mpango wa furaha wa Mungu, na tunaendelea kushangilia hapa duniani tunapoishi kulingana na mpango Wake. Lakini muktadha hasa ulikuwa ni upi kwa tamko hili la furaha kutoka kwa Nabii? Ni nini kilichochea hisia hizi za kina na za kutoka moyoni?

Nabii Joseph alikuwa akifundisha kuhusu ubatizo kwa niaba ya wafu. Huu hakika ulikuwa ufunuo mtukufu ambao ulipokelewa kwa shangwe kuu. Waumini wa Kanisa walipojifunza kwa mara ya kwanza kwamba wanaweza kubatizwa kwa niaba ya wapendwa wao waliokufa, walishangilia. Wilford Woodruff alisema, “Wakati niliposikia jambo hili, nafsi yangu iliruka kwa shangwe!”4

Ubatizo kwa niaba ya wafu wetu wapendwa haukuwa ukweli pekee ambao Bwana angeufunua na kuurejesha. Kulikuwa na wingi wa vipawa vingine au endaumenti ambazo Mungu amekuwa na hamu ya kuzitoa kwa wana na mabinti Zake.

Vipawa hivi vingine vilijumuisha mamlaka ya ukuhani, maagano na ibada, ndoa ambazo zingedumu milele, kuunganisha watoto kwa wazazi wao ndani ya familia ya Mungu, na hatimaye baraka ya kurejea nyumbani kwenye uwepo wa Mungu, Baba yetu wa Mbinguni na Mwanawe, Yesu Kristo. Baraka hizi zilifanywa ziwezekane kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo.

Kwa sababu Mungu alizizingatia hizi kuwa miongoni mwa baraka Zake za juu zaidi na takatifu zaidi,5 Yeye alielekeza kwamba majengo matakatifu yajengwe mahali ambapo Yeye angeweza kutunuku vipawa hivi vya thamani juu ya watoto Wake.6 Majengo haya yangekuwa nyumba Yake hapa duniani. Majengo haya yangekuwa mahekalu ambapo kile kilichofungwa au kuunganishwa hapa duniani katika jina Lake, kwa neno Lake na Mamlaka Yake kingefungwa mbinguni.7

Kama waumini wa Kanisa leo, baadhi yetu wanaweza kuchukulia kweli hizi tukufu za milele kuwa kitu cha kawaida. Zimekuwa asili ya pili kwetu. Wakati mwingine ni ya msaada tunapozitazama kupitia macho ya wale wanaojifunza kuzihusu kwa mara yao ya kwanza. Hii ilikuwa dhahiri kwangu kupitia tukio la hivi karibuni.

Mwaka uliopita, kabla tu ya kuwekwa wakfu upya kwa Hekalu la Tokyo Japan, wageni wengi wasio wa imani yetu walizuru hekalu lile. Mojawapo ya ziara zile ilimjumuisha kiongozi makini kutoka dhehebu jingine. Tuliwafundisha wageni wetu kuhusu mpango wa furaha wa Baba wa Mbinguni, jukumu la ukombozi la Yesu Kristo katika mpango huo, na fundisho kwamba familia zinaweza kuwa pamoja milele kupitia ibada ya kuunganishwa.

Mwishoni mwa ziara yetu, nilimwalika rafiki yetu ili ashiriki hisia zake. Katika kurejelea kuunganishwa kwa familia—zilizopita, zilizopo na zijazo—mwanaume huyu mwema aliuliza kwa udhati wote, “Je, waumini wa imani yenu wanaelewa kikamilifu jinsi fundisho hili lilivyo kuu?” Aliongeza, “Hili linaweza kuwa mojawapo ya mafundisho pekee yanayoweza kuunganisha ulimwengu huu ambao umegawanyika sana.”

Ni uchunguzi wenye nguvu ulioje. Mtu huyu hakuvutiwa tu kiurahisi na ufundi wa hali ya juu wa hekalu bali kwa mafundisho ya kuvutia na ya kina kwamba familia zinaunganishwa na kufungwa kwa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo milele.8

Hatupaswi kushangazwa, pale, mtu mmoja asiye wa imani yetu anapotambua ukuu wa kile kinachotokea ndani ya hekalu. Kitu kinachoweza kuwa cha kawaida kwetu wakati mwingine huonekana cha fahari na ukuu kwa wale wanaokisikia au kukihisi kwa mara ile ya kwanza.

Japokuwa mahekalu yalikuwepo hapo kale, kwa Urejesho wa injili ya Yesu Kristo, ujenzi wa mahekalu umekuwa mojawapo ya vipaumbele vya juu kabisa vya manabii wote tangu Nabii Joseph Smith. Na ni rahisi kuelewa ni kwa nini.

Wakati Nabii Joseph alipokuwa akifundisha kuhusu ubatizo kwa niaba ya wafu, alifunua kweli nyingine kuu. Alifundisha: “Acheni nikuhakikishieni kwamba hizi ni kanuni zinazohusiana na wafu na walio hai kwamba haziwezi kupuuzwa, kwani huhusiana na wokovu wetu. Kwani wokovu wao ni wa lazima na ni muhimu kwa wokovu wetu, … wao pasipo sisi hawawezi kukamilishwa—wala sisi hatuwezi pasipo wafu wetu kufanywa wakamilifu.”9

Kama tunavyoona uhitaji wa mahekalu na kazi ambazo hufanyika kwa ajili ya wote walio hai na wafu inakuwa dhahiri zaidi.

Adui yuko macho. Nguvu zake zinatishiwa kwa ibada na maagano yanayofanyika katika mahekalu, naye anafanya kila kitu awezacho ili kujaribu kusimamisha kazi hii. Kwa nini? Kwa sababu anajua nguvu inayokuja kutokana na kazi hii takatifu. Pale hekalu jipya linapowekwa wakfu, nguvu ya kuokoa ya Yesu Kristo huongezeka kote ulimwenguni ili kupinga juhudi za adui na kutukomboa pale tunapokuja Kwake. Kadiri mahekalu na watunza maagano wanavyoongezeka katika idadi, adui anakuwa dhaifu.

Katika siku za mwanzo za Kanisa, baadhi wangekuwa na hofu ni lini hekalu jingine lingetangazwa, kwani wangesema, “Kamwe hatukuanza kujenga hekalu pasipo kengele za kuzimu kuanza kupiga.” Lakini Brigham Young kwa ujasiri alijibu, “ninataka kuzisikia zikipiga tena.”10

Katika maisha haya ya duniani, hatutaepuka vita, lakini tunaweza kuwa na nguvu juu ya adui. Kwamba uwezo na nguvu zinatoka kwa Yesu Kristo tunapofanya na kuyashika maagano yetu ya hekaluni.

Rais Russell M. Nelson amefundisha: “Wakati unakuja ambapo wale ambao hawamtii Bwana watatengwa mbali na wale wanaofanya hivyo. Bima yetu salama kabisa ni kuendelea kuwa wastahiki wa kukubaliwa kuingia katika nyumba Yake takatifu.”11

Hapa kuna baadhi ya baraka za ziada ambazo Mungu ametuahidi kupitia nabii Wake.

Je, unahitaji miujiza? Nabii wetu amesema: “Ninawaahidi kwamba Bwana ataleta miujiza Yeye anayojua mnahitaji pale mnapofanya dhabihu ya kutumikia na kuabudu katika mahekalu Yake.”12

Je, unahitaji uponyaji na nguvu ya kuimarisha ya Mwokozi Yesu Kristo? Rais Nelson anatuhakikishia kwamba “Kila kitu kinachofundishwa ndani ya hekalu … kinaongeza ufahamu wetu juu ya Yesu Kristo. … Tunaposhika maagano yetu, Yeye hutupatia nguvu Yake ya uponyaji, ya kuimarisha. Na lo, ni kiasi gani tutahitaji nguvu Yake katika siku zijazo.”13

Katika Jumapili ya kwanza ya Matawi, Yesu Kristo kwa shangwe alipoingia Yerusalemu, umati wa wafuasi Wake “wa[li]shangilia na kumsifu Mungu kwa sauti kubwa … wakisema, Abarikiwe Mfalme ajaye katika jina la Bwana.”14

Ni ya kufaa sana kwamba mnamo Jumapili ya Matawi ya 1836, Hekalu la Kirtland liliwekwa wakfu. Katika tukio hilo wafuasi wa Yesu Kristo walikuwa wakishangilia pia. Katika sala ile ya kuweka wakfu, Nabii Joseph Smith alitangaza maneno haya ya kusifu:

“Ee Bwana Mungu Mwenyezi, utusikilize sisi … na utujibu kutoka mbinguni, … mahali wewe uketipo katika kiti cha enzi, kwa utukufu, heshima, uwezo, fahari, [na] nguvu. …

“… Tusaidie kwa uwezo wa Roho wako, ili tuweze kuchanganya sauti zetu pamoja na wale maserafi wazuri na wenye kungʼara kuzunguka kiti chako cha enzi, kwa shangwe za kusifu, tukiimba Hosana kwa Mungu na kwa Mwanakondoo!

“Na hawa … watakatifu wako wapige kelele kwa shangwe.”15

Akina kaka na akina dada, leo katika Jumapili ya Matawi, sisi pia kama wafuasi wa Yesu Kristo tumsifu Mungu wetu mtakatifu na tushangilie wema Wake kwetu. “Tunasikia nini katika injili ambayo tumeipokea? Kwa kweli ni “sauti ya furaha!”16

Ninashuhudia kwamba utahisi shangwe zaidi na zaidi unapoingia mahekalu matakatifu ya Bwana. Ninashuhudia kwamba utapata furaha ambayo Yeye anayo kwa ajili yako, katika jina la Yesu Kristo, amina