Mkutano Mkuu
Angeweza Kuniponya Mimi!
Mkutano mkuu wa Aprili 2023


Angeweza Kuniponya Mimi!

Uponyaji wa Mwokozi na nguvu ya ukombozi ipo kwa ajili ya makosa ya bahati mbaya, maamuzi mabaya, changamoto na majaribu ya kila aina—pamoja na dhambi zetu.

Moroni anaahidi kwamba ikiwa tutasoma Kitabu cha Mormoni na kisha kumwuliza Mungu Baba wa Milele kwa moyo wa kweli, na kusudi halisi, tukiwa na imani katika Kristo ikiwa ni cha kweli, Mungu, atatuonesha ukweli wake, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.1 Mamilioni ya watu wametumia ahadi hii na kupokea ushahidi wenye hakikisho wa Urejesho wa utimilifu wa injili ya Yesu Kristo.

Moroni anatusihi, tunaposoma Kitabu cha Mormoni “tukumbuke jinsi gani Bwana amekuwa na huruma kwa watoto wa watu, kutokea kuumbwa kwa Adamu hadi mpaka wakati [huu]”, … na tutafakari katika mioyo [yetu].”2 Hadithi na mafundisho ndani ya Kitabu cha Mormoni hutukumbusha na kutushuhudia juu ya upendo wa Mwokozi, huruma na rehema.

Baba yangu alifariki mnamo Aprili 2013. Nilipokuwa nikijiandaa kuzungumza kwenye mazishi yake, nilitambua jinsi gani nimebarikiwa kujua na kupenda maandiko yake pendwa. Aliyashiriki katika mikutano ya familia na aliyasoma pamoja nami wakati nilipohitaji ushauri, mwongozo au kuimarisha imani yangu. Nilimsikia akiyashiriki katika mahubiri na majukumu. Si tu kwamba niliyajua, bali bado ninaweza kukumbuka mvumo wa sauti yake na hisia za kiroho nilizopata wakati akiyashiriki. Kupitia kushiriki maandiko na hisia, baba yangu alinisaidia nijenge msingi imara wa imani katika Bwana Yesu Kristo.

Baba yangu kwa upekee alipenda tukio la matembezi ya Mwokozi kwa watu wa Nefi.3 Tukio hili takatifu ni la Bwana Yesu aliyefufuka na aliyeinuliwa. Alikuwa amekinywa kikombe kichungu na kuteseka vitu vyote ili kwamba sisi tusiteseke ikiwa tutatubu.4 Alikuwa amezuru ulimwengu wa roho na kuanzisha kuhubiriwa kwa injili huko.5 Alikuwa amefufuka kutoka wafu na alikuwa amekwenda kwa Baba na kupokea amri kutoka kwa Baba ili kushiriki maandiko kwa Wanefi ambayo yangebariki vizazi vijavyo.6 Alikuwa ameinuliwa na alikuwa na nguvu na uwezo Wake wote wa milele. Tunaweza kujifunza kutokana na kila kipengele cha mafundisho Yake.

Katika 3 Nefi 11, tunasoma jinsi Mwokozi alivyoshuka kutoka mbinguni kuwafundisha Wanefi kwamba Yeye alikuwa Yesu Kristo, ambaye manabii walishuhudia atakuja ulimwenguni. Alishuhudia kwamba Yeye alikuwa Nuru ya ulimwengu na kwamba alimtukuza Baba kwa kujivika dhambi za ulimwengu. Aliwaalika watu waje mbele na kuweka mikono yao kwenye ubavu wake na kuhisi alama za misumari katika mikono Yake na katika miguu Yake. Aliwataka wajue kwamba Yeye ndiye Mungu wa Israeli ambaye aliuwawa kwa dhambi za ulimwengu. Watu waliitikia kwa shangwe, wakienda mbele mmoja mmoja, mpaka walipoona na kujua kwamba ni Yeye, ambaye manabii waliandika kwamba atakuja.7

Yesu aliwafundisha Wanefi kuhusu umuhimu wa toba, kuhusu kuwa kama watoto wadogo na hitaji la ubatizo kutoka kwa mtu mwenye mamlaka Yake. Kisha alifundisha mengi ya mafundisho ambayo tunajifunza mwaka huu katika Agano Jipya.

Katika 3 Nefi 17, tunasoma kwamba Yesu aliwaambia watu ulikuwa wakati Wake kwenda kwa Baba, na pia kujidhihirisha kwa makabila yaliyopotea ya Israeli.8 Alipoelekeza macho yake kwa umati, aligundua walikuwa wanalia, na walikuwa wanamwangalia kwa uthabiti kama wanaotaka kumwomba akae nao kwa muda mrefu zaidi.9

Jibu la Mwokozi kwa Wanefi lilikuwa lenye kugusa na lenye maelekezo. Alisema, “Tazama, nafsi yangu imejawa na huruma juu yenu.”10

Ninaamini kwamba huruma Yake ilikuwa ni zaidi ya mwitikio kwenye kilio cha watu. Inaonekana aliweza kuwaona kupitia macho ya dhabihu ya upatanisho Wake. Aliona kila maumivu yao, mateso na majaribu. Aliyaona magonjwa yao. Aliuona udhaifu wao, na alijua kutokana na mateso Yake ya uchungu pale Gethsemane na Golgota jinsi ya kuwasaidia kulingana na unyonge wao.11

Kadhalika, Mwokozi wetu, Yesu Kristo, anapotutazama, anaona na anaelewa maumivu na mzigo wa dhambi zetu. Anauona uraibu wetu na changamoto zetu. Anayaona mahangaiko na mateso yetu ya kila aina—na amejawa na huruma kwetu.

Mwaliko Wake wa rehema kwa Wanefi ulifuatia: “Je, mnao wowote ambao ni wagonjwa miongoni mwenu? Waleteni hapa. Mnao wowote ambao ni viwete, au vipofu, au wa kupooza, au vilema, au wenye ukoma, au walionyauka au ni viziwi, au ambao wanateseka kwa njia yoyote? Waleteni hapa na nitawaponya, kwani ninayo huruma juu yenu; nafsi yangu imejawa na huruma.”12

Watu walisonga mbele “pamoja na wote waliosumbuka kwa namna yoyote; na aliwaponya wote kila mmoja kadiri walivyoletwa kwake.”13

Mnamo mwaka 1990 tulikuwa tukiishi katika mji mdogo wa Sale, huko Victoria, Australia. Tulikuwa wenye furaha kwa shughuli nyingi za kifamilia, kanisa na majukumu ya kazi. Jumamosi ya majira ya kupendeza ya joto kabla ya Krismasi, tuliamua kutembelea baadhi ya mbuga na fuko pendwa za bahari. Baada ya kufurahia siku nzuri ya kucheza kama familia, kila mmoja aliingia ndani ya gari kuelekea nyumbani. Wakati nikiendesha gari, ghafla nilisinzia na kusababisha ajali ya uso kwa uso. Baada ya muda, niliangalia ndani ya gari. Mke wangu, Maxine, alikuwa amevunjika mguu vibaya sana na alikuwa akihangaika kupumua. Alikuwa amevunjika mfupa wa kifua. Mabinti zetu watatu walikuwa kwenye taharuki lakini nina shukrani walionekana wako SAWA. Mimi nilipata majeraha madogo madogo. Lakini mtoto wetu wa miezi mitano alikuwa kimya.

Katikati ya wasiwasi na mkanganyiko wa tukio lile la ajali, Kate binti yetu mkubwa wa miaka 11, alisema kwa dharura, “Baba, unapaswa kumpa Jarom baraka.” Baada ya mahangaiko mengi, mimi na binti zangu tuliweza kutoka ndani ya gari. Maxine hakuweza kusonga. Kwa umakini nilimnyanyua Jarom; kisha nikiwa nimelala chali ardhini, taratibu nilimweka juu ya kifua changu na kumpa baraka ya ukuhani. Wakati gari la wagonjwa lilipowasili takriban dakika 40 baadaye, Jarom alikuwa amepata fahamu.

Usiku ule, niliwaacha wanafamilia watatu hospitalini na kuchukua taksi kwenda nyumbani nikiwa na binti zangu wawili. Katika usiku mrefu, nilimsihi Baba wa Mbinguni kwamba familia yangu na wale waliopata majeraha kwenye gari nyingine waweze kupona. Kwa rehema, sala zangu na sala za dhati zilizotolewa na wengine wengi zilijibiwa. Wote walipona baada ya muda fulani, baraka kuu na huruma nyororo.

Lakini bado niliendelea kuwa na hisia nzito za hatia na majuto kwa kusababisha ajali mbaya kama ile. Ningeamka usiku na kukumbuka matukio ya kuogofya. Nilipambana kwa miaka kujisamehe mwenyewe na kupata amani. Kisha, kama kiongozi wa ukuhani, wakati nikiwasaidia wengine watubu na kuwasaidia wahisi faraja, huruma na upendo wa Mwokozi, niligundua kwamba Yeye angeweza kuniponya.

Uponyaji wa Mwokozi na nguvu ya kukomboa ipo kwa makosa ya ajali, maamuzi mabaya, changamoto na majaribu ya kila aina—vilevile kwenye dhambi zetu. Nilipomgeukia Yeye, hisia zangu za hatia na majuto zilifunikwa na amani na pumziko.

Rais Russell M. Nelson alifundisha: “Wakati Mwokozi alipolipia dhambi za wanadamu wote, Yeye alifungua njia ambayo wale wanaomfuata wanaweza kufikia nguvu Yake ya uponyaji, uimarishaji na ukombozi. Fursa hizi za kiroho zinapatikana kwa wote wanaotafuta kumsikia na kumfuata Yeye.”14

Akina kaka na akina dada, iwe unabeba mzigo wa dhambi ambayo haijatatuliwa, unateseka kwa maudhi yaliyofanywa dhidi yako muda mrefu uliopita au unahangaika kujisamehe kwa makosa ya bahati mbaya, una ufiko kwenye nguvu ya uponyaji na ya kukomboa ya Mwokozi Yesu Kristo.

Ninashuhudia kwamba Yu hai. Yeye ni Mwokozi na Mkombozi wetu. Anatupenda. Ana huruma kwetu, amejawa rehema, na Yeye anaweza kukuponya. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.