Mkutano Mkuu
Wapatanishi Wanahitajika
Mkutano mkuu wa Aprili 2023


Wapatanishi Wanahitajika

Unao haki ya kujiamulia ya kuchagua ubishi au mapatano. Ninawasihi mchague kuwa wapatanishi, sasa na daima.

Akina kaka na dada zangu wapendwa, ni furaha kuwa nanyi. Miezi hii sita iliyopita, mmekuwa daima katika akili yangu na maombi yangu. Ninaomba kwamba Roho Mtakatifu atawasilisha kile Bwana anachotaka msikie ninapozungumza nanyi.

Wakati wa mafunzo yangu ya upasuaji miaka mingi iliyopita, nilimsaidia mpasuaji aliyekua akikata mguu uliokuwa umejaa maambukizi mengi. Upasuaji ulikuwa mgumu. Kisha, kuongezea kwenye uzito wa kazi, mmoja wetu alifanya kazi kizembe, na mpasuaji aligomba kwa hasira. Katikati ya hasira yake, alirusha kisu chake kilichojaa vijidudu. Kisu kilitua katika mkono wangu!

Kila mmoja kwenye chumba cha upasuaji—isipokuwa mpasuaji mwenye hasira—waliogopeshwa na kitendo hiki hatari cha kiupasuaji. Kwa shukrani, sikuambukizwa. Lakini uzoefu huu uliniachia mtazamo wa kudumu. Katika saa lile lile, nilijiahidi kwamba chochote kitokeacho katika chumba changu cha upasuaji, kamwe nisingepoteza nidhamu yangu ya hisia. Pia niliweka nadhiri siku hiyo ya kutorusha kitu chochote kwa hasira—iwe visu au maneno.

Hata sasa, miongo kadhaa baadaye, najiuliza kama kile kisu chenye maambukizo kilichotua mkononi mwangu kilikuwa hatari sana kuliko mabishano makali ambayo huikumba mijadala yetu ya kijamii na mahusiano mengi binafsi hivi leo. Ustaarabu wa kijamii na heshima huonekana kupotea katika enzi hii ya ubaguzi na kutokukubaliana.

Ufidhuli, kutafuta makosa na kuongea uovu kuhusu wengine vyote vinaonekana kuwa kawaida. Wachambuzi wengi, wanasiasa, watoa burudani na washawishi wengine hurusha matusi kila mara. Ninaumizwa kwamba inaonekana kwamba watu wengi huonekana kuamini kwamba ni halali kumlaumu, kumdhihaki na kumchafua mtu yeyote asiyekubaliana nao. Wengi wana shauku ya kuharibu heshima ya mwingine kwa upuuzi na maneno makali.

Hasira kamwe haishawishi. Uhasama haumjengi yeyote yule. Ubishi kamwe hauongozi kwenye masuluhisho yenye mwongozo. Cha kusikitisha, wakati mwingine tunaona tabia za mabishano hata katika tabaka zetu wenyewe. Tunasikia wale wanaowadunisha wenzi wao na watoto, ambao hutumia hasira kuwadhibiti wengine, na wale wanaowaadhibu wanafamilia kwa “kuacha kuzungumza nao.” Tunasikia kuhusu vijana na watoto wanaowaonea wenzao na waajiriwa wanaowakashifu wenzao.

Akina kaka na dada zangu wapendwa, haipaswi kuwa hivi. Kama wafuasi wa Yesu Kristo, tunapaswa kuwa mifano ya jinsi ya kuchangamana na wengine—hasa tunapokuwa na mitazamo tofauti. Njia moja rahisi sana ya kumtambua mfuasi wa kweli wa Yesu Kristo ni kwa huruma kiasi gani mtu huyo huwaonyesha wengine.

Mwokozi aliweka hili wazi katika mahubiri Yake kwa wafuasi Wake katika mabara yote mawili. “Wamebarikiwa wapatanishi,” Alisema.1 “Yeyote atakaye kupiga shavu la kulia, mgeuzie na la pili pia.”2 Na kisha, ndio, alitoa onyo ambalo ni changamoto kwa kila mmoja wetu “Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowahudhi, watendeeni mema wanaowachukia, na waombeeni wanaowatumia kwa hila, na kuwatesa.”3

Kabla ya kifo Chake, Mwokozi aliwaamuru Mitume Wake Kumi na Wawili kwamba wapendane kama vile Yeye alivyowapenda.4 Kisha Yeye aliongezea, “Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi.”5

Ujumbe wa Mwokozi u wazi: wafuasi Wake wa kweli hujenga, huinua, huhamasisha, hushawishi na kutia moyo—bila kujali ugumu wa hali. Wafuasi wa kweli wa Yesu Kristo ni wapatanishi.6

Leo ni Jumapili ya Mitende. Tunajiandaa kuadhimisha tukio la muhimu sana na linalopita uwezo wa binadamu lililowahi kurekodiwa duniani, ambalo ni Upatanisho na Ufufuo wa Bwana Yesu Kristo. Njia moja nzuri sana ya kumkumbuka Mwokozi ni kuwa wapatanishi.7

Upatanisho wa Mwokozi ulifanya iwezekane kwetu sisi kushinda uovu wote—ikijumuisha ubishi. Usifanye kosa kuhusu hili: ubishi ni uovu! Yesu Kristo alitangaza kwamba wale wenye “roho ya ubishi” si Wake, bali ni “wa ibilisi”, ambaye ni baba wa ubishi, na [ibilisi] huchochea mioyo ya watu kubishana na hasira mmoja kwa mwingine.”8 Wale wanaoendekeza mabishano wanaigiza kile Shetani anachokifanya, iwe wanajua au la. “Hakuna mtu ambaye anaweza kutumikia mabwana wawili.”9 Hatuwezi kukubaliana na Shetani kwa maneno yetu makali na kisha kufikiria kwamba bado tunaweza kumtumikia Mungu.

Akina kaka na dada zangu wapendwa, jinsi tunavyotendeana ndicho cha muhimu! Jinsi tunavyozungumza na wengine na kuwahusu wengine nyumbani, kanisani, kazini na mtandaoni ndio muhimu. Leo, ninawaomba kuchangamana na wengine katika njia ya juu na takatifu zaidi. Tafadhali sikilizeni kwa makini. “Kama kuna kitu chochote kilicho chema, chenye kupendeza, au chenye taarifa njema au chenye kustahili sifa”10 ambacho tunaweza kusema kuhusu mtu mwingine—mbele yake au bila uwepo wake—kinapaswa kiwe msingi wa mawasiliano yetu.

Kama wanandoa katika kata yako wakitalikiana, au mmisionari akirejea nyumbani mapema, au kijana akiwa na wasiwasi na ushuhuda wake, hawahitaji hukumu yenu. Wanahitaji kupata upendo safi wa Yesu Kristo unaoakisiwa katika maneno na matendo yenu.

Kama rafiki kwenye mtandao wa kijamii ana mitazamo mikali ya kisiasa au kijamii ambayo ni kinyume na kila kitu unachoamini, jibu la hasira na ovu havitasaidia. Kujenga madaraja ya maelewano kutahitaji jitihada zako nyingi, lakini hilo ndilo hasa rafiki yako analihitaji.

Ubishi humfukuza Roho—kila mara. Ubishi hukuza dhana potofu kwamba mifarakano ni njia ya kutatua tofauti, lakini siyo. Ubishi ni uchaguzi. Kuleta upatanishi ni uchaguzi. Unao uchaguzi wako wa kuchagua ubishi au mapatano. Ninawasihi mchague kuwa wapatanishi, sasa na daima.11

Akina kaka na dada, tunaweza kiuhalisia kuubadili ulimwengu—mtu mmoja na makutano ya aina moja kwa muda fulani. Kivipi? Kwa kujifunza jinsi ya kutatua tofauti za dhati za maoni kwa heshima sawa na mjadala wenye utu.

Tofauti za maoni ni sehemu ya maisha. Ninafanya kazi kila siku pamoja na watumishi waliojitoa wa Bwana ambao daima hawaoni jambo fulani katika hali sawa. Wanajua nahitaji kupata mawazo yao na hisia za dhati kuhusu kila kitu tunachojadili—hususani mambo nyeti.

Picha
Rais Dallin H. Oaks na Rais Henry B. Eyring

Washauri wangu wema, Rais Dallin H. Oaks na Rais Henry B. Eyring, ni mfano katika njia wanayotoa maoni yao—hasa wakati wanapoweza kutofautiana. Wanafanya hivyo kwa upendo msafi kwa kila mmoja. Hakuna anayependekeza kwamba anajua vyema na hivyo kwa nguvu atalazimika kutetea upande wake. Hakuna shuhuda zinazohitaji kushindana na zingine. Kwa sababu kila mmoja amejawa na hisani, “upendo msafi wa Kristo,”12 mapendekezo yetu yanaweza kuongozwa na Roho wa Bwana. Ninawapenda na kuwaheshimu watu hawa wawili muhimu!

Hisani ni dawa ya ubishi. Hisani ni kipawa cha kiroho ambacho hutusaidia kumtupilia mbali mwanadamu wa asili, ambaye ni mbinafsi na mwenye kujitetea, mwenye kiburi na wivu. Hisani ni tabia ya msingi ya mfuasi halisi wa Yesu Kristo.13 Hisani humfafanua mpatanishi.

Tunapojinyenyekeza mbele za Mungu na kuomba kwa nguvu zote za moyo, Mungu atatujalia hisani.14

Wale waliobarikiwa na kipawa hiki kisicho na kifani ni wastahimilivu na wema. Hawawahusudu wengine na hawajijali wao wenyewe. Hawaoni uchungu na hawahesabu mabaya.15

Akina kaka na dada, upendo msafi wa Kristo ni jibu kwa ubishi unaotusibu hivi leo. Hisani hutusukuma “kubebeana mizigo”16 kuliko kurundikiana mizigo kila mmoja kwa mwingine. Upendo msafi wa Kristo huturuhusu kusimama kama mashahidi wa Mungu nyakati zote na katika vitu vyote”17hasa katika hali tete. Hisani huturuhusu kuonyesha jinsi wanaume na wanawake wa Kristo wanavyozungumza na kutenda—hasa tunapokosolewa vikali.

Sasa, siongelei kuhusu “amani pasipo kuwajibika.”18 Ninazungumza kuhusu kuwajali wengine katika njia ambazo huendana na kushika maagano uliyoyafanya unapopokea sakramenti. Uliahidi daima kumkumbuka Mwokozi. Katika hali ambazo ni tete na zimejaa ubishi, nakualika umkumbuke Yesu Kristo. Omba ili upate ujasiri na hekima ya kusema au kufanya kile ambacho Yeye angefanya Tunapomfuata Mfalme wa Amani, tutakuwa wapatanishi Wake.

Kwa wakati huu mnaweza kufikiria kwamba ujumbe huu ungemsaidia mtu fulani unayemjua. Huenda unatumaini kwamba utamsaidia kuwa mtu mzuri zaidi kwako. Natumaini itakuwa hivyo! Lakini pia ninatumaini utatazama kwa kina ndani ya moyo wako kuona kama kuna vipande vya kiburi au wivu ambavyo hukuzuia wewe kutokuwa mpatanishi.19

Kama uko tayari kusaidia kukusanya Israeli na kujenga mahusiano yatakayodumu milele yote, sasa ndio muda wa kuachilia uchungu wote. Sasa ni muda wa kuacha kusisitiza kwamba ni kwa njia yako au la hakuna njia. Sasa ni muda wa kuacha kufanya vitu ambavyo huwafanya wengine wajizuie wakihofia kukukasirisha. Sasa ni muda wa kuzika vifaa vyako vya vita.20 Kama ghala yako ya maneno imejaa matusi na mashitaka, sasa ni wakati wa kuyatupilia mbali.21 Utakuwa imara kiroho kama mwanaume au mwanamke wa Kristo.

Hekalu linaweza kutusaidia katika tamanio hili. Huko tunapewa nguvu ya Mungu, inayotupatia uwezo wa kumshinda Shetani, mchochezi wa ubishi wote.22 Mtupeni nje ya mahusiano yenu! Kumbuka pia kwamba tunamkemea adui kila wakati tunapoponya kutoelewana au kukataa kukwazika. Badala yake, tunaweza kuonyesha huruma nyororo ambayo ni tabia ya kweli ya mfuasi wa Yesu kristo. Wapatanishi humzuia adui.

Hebu sisi kama watu tuwe nuru ya kweli kwenye kilima—nuru ambayo “haiwezi kufichwa.”23 Acha tuonyeshe kwamba kuna amani, njia ya heshima ya kutatua maswala tata na njia bora ya kutatua kutoelewana. Unapoonyesha hisani ambayo wafuasi wa kweli wa Yesu Kristo hudhihirisha, Bwana atakuza juhudi zako zaidi ya unavyoweza kufikiria.

Nyavu za injili ni nyavu kubwa sana ulimwenguni. Mungu anatualika sote tuje Kwake, “weusi na weupe, wafungwa na walio huru, wake na waume.”24 Kuna nafasi kwa ajili ya kila mmoja. Hata hivyo, hakuna nafasi kwa ajili ya chuki, lawama au ubishi wa aina yoyote.

Wapendwa akina kaka na dada, mazuri yatakuja kwa wale wanaotumia muda wao kuwajenga wengine. Leo ninawaalika kutathmini ufuasi wenu katika muktadha wa jinsi mnavyowatendea wengine. Ninawabariki katika kufanya marekebisho ambayo yanaweza kuhitajika ili kwamba tabia yako iwe ya kuinua, ya heshima na ya kumwakilisha mfuasi wa kweli wa Yesu Kristo.

Ninawabariki ili kusihi kuchukue nafasi ya ugomvi, maelewano badala ya chuki na amani badala ya ubishi.

Mungu yu hai! Yesu ndiye Kristo. Anasimama kwenye kichwa cha Kanisa hili. Sisi ni watumishi Wake. Atatusaidia sisi kuwa wapatanishi Wake. Ninashuhudia hivyo katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.