2016
Mjifunze Kwangu
Machi 2016


Ujumbe wa Urais wa Kwanza, Machi 2016

Mjifunze Kwangu

Katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, sisi sote tu walimu na sote tu wanafunzi. Kwa wote waja mwaliko ororo kutoka kwa Bwana wetu: “Mjifunze kwangu nanyi mtapata raha nafsini mwenu.”1

Mimi nawaalika Watakatifu wa Siku za Mwisho wote watafakari juu ya juhudi zao za kufundisha na kujifunza na kumtegemea Mwokozi kama Kiongozi wetu katika kufanya hivyo. Sisi tunajua kwamba huyu “mwalimu anatoka kwa Mungu”2 alikuwa zaidi ya mwalimu tu. Yeye ambaye alitufundisha kumpenda Bwana Mungu wetu kwa mioyo yetu yote, nafsi zetu zote, nguvu zetu zote, na akili zetu zote, na kumpenda jirani yetu kama tunavyojipenda, ni Mwalimu Mahiri na Mfano wa maisha kamili.

Yeye ndiye ambaye alitamka: “Njoo, unifuate.”3 “Mimi nimewapatia mfano.”4

Msipoongoka

Yesu alifunza ukweli rahisi lakini muhimu kama ilivyoandikwa katika Mathayo. Baada ya Yeye na wanafunzi Wake kushuka kutoka kwenye Mlima wa Kugeuka sura, walitua Galilaya na kisha wakaenda Kapernaumu. Hapo wanafunzi wakamwendea Yesu, wakiuliza:

“Ni nani basi aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni?

“Na Yesu akamwita mtoto mmoja, akamweka katikati yao,

“Akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka, na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.”5

Katika Kanisa, lengo la mafundisho ya injili siyo kumwaga taarifa katika vichwa vya watoto wa Mungu, iwe ni nyumbani, katika darasa, ama katika uwanja wa misheni. Siyo kuonyesha umahiri wa mzazi, mwalimu, ama mmisionari. Wala si tu kuongezea elimu kuhusu Mwokozi na Kanisa Lake.

Lengo la msingi la kufundisha ni kuwasaidia wana na mabinti wa Baba yetu wa Mbinguni kurudi katika uwepo Wake na kufurahia uzima wa milele pamoja Naye. Ili kutimiza hilo, ufundishaji wa injili sharti uwahimize katika njia ya ufuasi wa kila siku na maagano matakatifu. Lengo ni kushawishi watu kufikiria juu ya, kuhisi juu ya, na kisha kufanya kitu juu ya kuishi kanuni za Injili. Nia ni kukuza imani katika Bwana Yesu Kristo na kuongolewa katika injili Yake.

Mafundisho ambayo hubariki na huongoa na huokoa ni mafundisho ambayo yanaiga mfano wa Mwokozi. Mwalimu ambaye anaiga mfano wa Mwokozi huwapenda na kuwahudumia wale anaowafundisha…Wanawainua wasikilizaji wao kwa masomo ya milele ya ukweli mtukufu. Wanaishi maisha yanayostahili kuigwa.

Upendo na Huduma

Huduma yote ya Mwokozi inaonyesha upendo kwa jirani. Hakika, upendo na huduma Yake kila mara ilikuwa ni somo Lake. Vivyo hivyo, walimu ninaowakumbuka vyema ni walimu ambao waliwajua, wakawapenda, na kuwajali wanafunzi wao. Walimtafuta kondoo aliyepotea. Walifunza masomo ya maisha ambayo mimi daima nitayakumbuka.

Mmoja wa walimu kama hao alikuwa ni Lucy Gertsch. Alimjua kila mmoja wa wanafunzi wake. Bila kukosa aliwapigia simu wale ambao walikosa kuja Jumapili moja ama hawakuja kabisa. Sisi tulijua kwamba alitujali. Hakuna yeyote kati yetu aliyemsahau ama masomo aliyofundisha.

Miaka mingi baadaye, nilimtembelea Lucy karibu na mwisho wa maisha yake, nilizungumza naye. Tukakumbuka kuhusu siku hizo za zamani kabla hajawa mwalimu wetu. Tukaongea juu ya kila mshiriki wa darasa letu na kuzungumza kila mmoja anafanya sasa. Upendo wake na kujali kwake ni kwa maisha yote.

Mimi napenda onyo la Bwana ambalo linapatikana katika Mafundisho na Maagano:

“Na ninatoa kwenu amri ya kuwa mfundishane mafundisho ya ufalme.

“Fundishaneni kwa bidii na neema yangu itakuwa pamoja nanyi.”6

Lucy Gertsch alifundisha kwa bidii kwa sababu alipenda bila kuchoka.

Toa Tumaini na Ukweli

Mtume Petro alishauri, “Muwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu.”7

Labda tumaini kuu kabisa mwalimu anaweza kutoa ni tumaini linalopatikana katika kweli za injili ya Yesu Kristo.

“Na ni kitu gani mtakachotumainia?” Mormoni aliuliza. “Tazama nawaambia kwamba mtakuwa na tumaini kupitia upatanisho wa Kristo na uwezo wa kufufuka kwake, kuinuliwa kwa maisha ya milele, na hii kwa sababu ya imani yenu kwake.”8

Walimu, inueni sauti zenu na mshuhudie juu ya asili ya kweli ya Uungu. Tangazeni ushuhuda wenu kuhusu Kitabu cha Mormoni. Semeni kweli tukufu na za ajabu zilizomo katika mpango wa wokovu? Tumieni vifaa vilivyo idhinishwa na Kanisa, hasa maandiko, kufunza kweli za injili ya urejesho ya Yesu Kristo katika uhalisi na urahisi wake. Kumbukeni onyo la Mwokozi la “kuyachunguza maandiko; kwa sababu mnadhani ninyi mna uzima wa milele ndani yake: na hayo ndiyo yanayonishuhudia.”9

Wasaidieni watoto wa Mungu kuelewa kile kilicho halisi na muhimu katika maisha haya. Wasaidieni kukuza nguvu za kuchagua njia ambazo zitawaweka salama kwenye njia ya uzima wa milele.

Fundisheni ukweli, na Roho Mtakatifu atahimili juhudi zenu.

“Mjifunze Kwangu”

Kwa sababu Yesu Kristo alikuwa mtiifu na mnyenyekevu kabisa kwa Baba Yake, Yeye “akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.”10 Je! Una azimio la kufanya vivyo? Kama vile Yesu “alivyopokea neema juu ya neema,”11 sisi sharti kwa subira na daima tutafute nuru na maarifa kutoka kwa Mungu katika juhudi zetu za kujifunza injli.

Kusikiliza ni sehemu muhimu ya kujifunza. Wakati tunajiaandaa kufundishwa, kwa maombi tutafute maongozi na uthibitisho kutoka kwa Roho Mtakatifu. Tutafakari, tunaomba, tunatumia masomo ya injili, na kutafuta mapenzi ya Baba kwetu.12

“Yesu alifundisha mambo mengi kwa mifano,”13 ambayo ilihitaji masikio ya kusikia, macho ya kuona, na mioyo ya kuelewa. Tunapoishi kwa ustahiki, tunaweza kusikia vyema mnongono wa “Roho Mtakatifu, ambaye atatufundisha[sisi] vitu vyote, na kutukumbusha yote.”14

Tunapojibu mwaliko ororo wa Bwana, “Mjifunze Kwangu,” tutakuwa wapokeaji wa nguvu Zake tukufu. Acheni sisi, kwa hivyo, twende mbele katika roho ya utiifu, tukifuata Mfano wetu kwa mafundisho jinsi Yeye angetaka tufundishe na tujifunze jinsi Yeye angependa tujifunze.

Kufundisha kutoka kwa Ujumbe huu

Rais Monson anatualika “tutafakari juu ya juhudi [zetu] za kufundisha na kujifunza na kutegemea Mwokozi kama Kiongozi wetu tunapofanya hivyo.” Unaweza kufikira kupekua maandiko pamoja na wale unaowatembea ili mpate umaizi wa njia ambazo Yesu Kristo alifundisha na kujifunza. Unaweza kuanza na baadhi ya maandiko ambayo Rais Monson alitaja, kama vile Mathayo 11:29, Marko 5:30, na Marko 4:2. Unaweza kujadili jinsi kile ulichojifunza kuhusu Kristo kinaweza kukusaidia wewe kuwa “mpokeaji wa nguvu Zake tukufu.”