Miito ya Misheni
Sura ya 4: Mtafute na Mtegemee Roho


“Sura ya 4: Mtafute na Mtegemee Roho,” Hubiri Injili Yangu: Mwongozo wa Kushiriki Injili ya Yesu Kristo (2023)

“Sura ya 4: Mtafute na Mtegemee Roho,” Hubiri Injili Yangu

Picha
Liahona, na Arnold Friberg

Sura y a 4

Mtafute na Mtegemee Roho

Zingatia Hili

  • Ninaweza kufanya nini ili nipate nguvu za Roho Mtakatifu katika maisha yangu na katika huduma ya umisionari?

  • Je, jukumu la Roho Mtakatifu ni lipi katika uongofu?

  • Je, ni kwa jinsi gani ninaweza kuwasaidia watu tunaowafundisha wahisi ushawishi wa Roho Mtakatifu?

  • Je, ni kwa jinsi gani ninaweza kufanya sala zangu ziwe zenye maana zaidi?

  • Je, ni kwa jinsi gani ninaweza kujifunza kutambua ushawishi wa Roho Mtakatifu?

Tafuta Mwongozo wa Roho Mtakatifu

Kipawa cha Roho Mtakatifu ni mojawapo ya vipawa vikuu ambavyo Mungu amewapa watoto Wake. Ni cha muhimu katika kazi yako kama mmisionari. Unahitaji nguvu zenye kuongoza, nguvu za ufunuo za Roho Mtakatifu pale unapowasaidia watu wabatizwe, wathibitishwe na wawe waongofu.

Kuwa na mwongozo wa Roho Mtakatifu katika maisha yako kunahitaji kazi ya kiroho. Kazi hii inajumuisha sala za kusihi na kujifunza maandiko kila siku. Pia hujumuisha kushika maagano yako na amri za Mungu (ona Mafundisho na Maagano 18:8–10, 13). Hujumuisha kupokea sakramenti kwa kustahili kila wiki (ona Mafundisho na Maagano 20:77, 79).

Unakabiliana na mahitaji na hali tofauti kila siku. Misukumo kutoka kwa Roho itakusaidia ujue kipi cha kufanya na kusema. Unapotafuta na kutenda juu ya misukumo hii, Roho Mtakatifu atakuza uwezo wako na huduma yako zaidi ya vile unavyoweza kufanya wewe mwenyewe. Yeye atakusaidia katika kila kipengele cha huduma yako ya umisionari na maisha yako binafsi. (Ona pia 2 Nefi 32:2–5; Alma 17:9; Helamani 5:17–19; Mafundisho na Maagano 43:15–16; 84:85.)

Picha
Rais Russell M. Nelson

“Katika siku zijazo, haitawezekana kunusurika kiroho bila mwongozo, maelekezo, faraja na ushawishi endelevu wa Roho Mtakatifu.” (Russell M. Nelson, “Ufunuo kwa Kanisa, Ufunuo kwa Ajili ya Maisha Yetu,” Liahona,” Mei 2018, 96).

Picha
Nuru na Ukweli, na Simon Dewey

Nuru ya Kristo

Nuru ya Kristo “imetolewa kwa kila mtu, ili aweze kujua mema na maovu” (Moroni 7:16; ona mistari 14–19; ona pia Yohana1:9). Nuru ya Kristo ni kuelimishwa, maarifa, na ushawishi ambao hutolewa kupitia Yesu Kristo. Ushawishi huu ni mwanzo wa kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Utawaongoza wale ambao ni wasikivu wa kujifunza na kuishi injili ya urejesho ya Yesu Kristo.

Roho Mtakatifu

Mshiriki wa Roho Mtakatifu

Roho Mtakatifu ni mshiriki wa tatu wa Uungu. Yeye ni mtu wa kiroho na hana mwili wa nyama na mifupa (ona Mafundisho na Maagano 130:22). Yeye ni mfariji, ambaye Mwokozi aliahidi angeweza kuwafundisha wafuasi Wake vitu vyote na kuleta katika kumbukumbu yao kile ambacho Yesu alikuwa amekifundisha (ona Yohana 14:26).

Nguvu ya Roho Mtakatifu

Ushahidi ambao huja kwa watafutaji wa ukweli waaminifu kabla ya ubatizo huja kupitia nguvu ya Roho Mtakatifu. Watu wote wanaweza kupokea ushuhuda wa Yesu Kristo na injili Yake ya urejesho kupitia uwezo wa Roho Mtakatifu. “Na kwa uwezo wa Roho Mtakatifu [sisi] tunaweza kujua ukweli wa vitu vyote.” (Moroni 10:45).

Kipawa cha Roho Mtakatifu

Kipawa cha Roho Mtakatifu ni haki ya kuwa na wenza wa kila mara wa Roho Mtakatifu kadiri tunavyokuwa wenye kustahili. Tunapokea kipawa cha Roho Mtakatifu baada ya kubatizwa kwa maji. Kinatunukiwa juu yetu kupitia ibada ya uthibitisho.

Nabii Joseph Smith alisema: “kuna tofauti kati ya Roho Mtakatifu na kipawa cha Roho Mtakatifu. Kornelio alipokea Roho Mtakatifu kabla ya kubatizwa, ambayo ilikuwa ni nguvu ya kushawishi ya Mungu kwake ya ukweli wa injili, lakini hangeweza kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu mpaka baada ya kubatizwa” (Teachings of Presidents of the Church: Joseph Smith [2007], 97).

Ni kwa kipawa na nguvu za Roho Mtakatifu kwamba tunatakaswa—kufanywa watakatifu zaidi, wakamilifu zaidi, wazima zaidi, zaidi kama Mungu. Ni kupitia ukombozi wa Kristo na nguvu ya kutakasa ya Roho Mtakatifu kwamba tunaweza kuzaliwa tena kiroho wakati tunaposhika maagano tuliyofanya na Mungu (ona Mosia 27:25–26).

Roho Mtakatifu wa Ahadi

Roho Mtakatifu pia anajulikana kama Roho Mtakatifu wa Ahadi (ona Mafundisho na Maagano 88:3). Katika nafasi hii, Roho Mtakatifu huthibitisha kwamba ibada za ukuhani tunazopokea na maagano tunayofanya yanakubalika kwa Mungu. Wale wanaounganishwa na Roho Mtakatifu wa Ahadi watapokea yote ambayo Baba anayo (ona Mafundisho na Maagano 76:51–60; Waefeso 1:13–14; Mafundisho na Maagano, “Roho Mtakatifu wa Ahadi”).

Ibada na maagano yote lazima yaunganishwe na Roho Mtakatifu wa Ahadi ili kuwa halali baada ya maisha haya (ona Mafundisho na Maagano 132:7, 18–19, 26). Uunganishaji huo hutegemea uaminifu wetu endelevu.

Vipawa vya Kiroho

Bwana hutupatia vipawa vya Roho ili kutubariki na kuvitumia katika kuwabariki wengine (ona Mafundisho na Maagano 46:8–9, 26). Kwa mfano, wamisionari ambao wanajifunza lugha mpya wanaweza kupokea kipawa cha ndimi ili kuwapatia msaada wa kuwafundisha wengine katika lugha yao ya asili.

Vipawa vya Roho kadhaa vinaelezewa katika Moroni 10:8–18, Mafundisho na Maagano 46:11–33, na 1 Wakorintho 12:1–12. Hivi ni baadhi tu ya vipawa vingi vya Roho. Bwana anaweza kutubariki kwa vipawa vingine kutegemea uaminifu wetu, mahitaji yetu, na mahitaji ya wengine.

Mwokozi anatualika tutafute kwa biidi vipawa vya roho (ona Mafundisho na Maagano 46:8; 1 Wakorintho 14:1, 12). Vipawa hivi vinakuja kwa sala, imani, na juhudi—kulingana na mapenzi ya Mungu.

Kujifunza Binafsi au na Mwenza

Katika Kamusi ya Biblia, soma “Roho Mtakatifu,” “Nuru ya Kristo,” na “Roho, Mtakatifu.” Andika maelezo ya asili na wajibu wa Roho Mtakatifu.

Soma Matendo ya Mitume 4:1–33.

  • Ni kwa jinsi gani Petro na Yohana walitafuta vipawa vya roho?

  • Ni jinsi gani Mungu alijibu sala zao?

  • Ni kipi unaweza kujifunza kutokana na uzoefu huu kuhusu kazi yako wewe mwenyewe?

Picha
kundi likisali

Nguvu ya Roho katika Uongofu

Uongofu hutokea kupitia nguvu ya Roho Mtakatifu. Wajibu wako ni kusaidia kuleta nguvu ya Roho katika maisha ya mtu. Baadhi ya njia unazoweza kufanya hili zimependekezwa hapo chini.

  • Tafuta kuwa na Roho pamoja nawe kupitia sala, kuyachunguza maandiko, na kushika maagano yako.

  • Fundisha kwa Roho kuhusu Mwokozi na ujumbe wa Urejesho. Fuata mwongozo wa Roho katika kutohoa ujumbe wako kwa mahitaji ya kila mtu.

  • Shuhudia kwamba unajua kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwamba kile unachofundisha ni cha kweli. Unaposhuhudia, Roho Mtakatifu anaweza kutoa ushahidi kwa wengine.

  • Waalike watu watende, na wasaidie watimize ahadi zao. Watu wanapojitolea kutimiza ahadi, watahisi nguvu ya Roho Mtakatifu kwa nguvu zaidi. Ona sura ya 11.

  • Fuatilia kwa kuwauliza watu kuhusu uzoefu wao wakati walipotendea kazi mwaliko. Imani yao itakua kadiri wanavyotubu, kutii amri, na kutimiza ahadi zao. Wasaidie wamtambue Roho akiwa anafanya kazi pamoja nao.

Picha
Rais M. Russell Ballard

Rais M. Russell Ballard alifundisha: “Uongofu huja kupitia uwezo wa Roho. Wakati Roho anapogusa moyo, mioyo inabadilika. Wakati watu binafsi … wanapomhisi Roho akifanya kazi pamoja nao, au wanapoona ushahidi wa upendo na rehema ya Bwana katika maisha yao, wanainuliwa, wanaimarishwa kiroho na imani yao Kwake inaongezeka. Uzoefu mwingi wa Roho unafuata kwa njia ya kawaida wakati mtu anapokuwa tayari kufanya majaribio juu ya neno [ona Alma 32:27). Hivi ndivyo tunavyokuja kuhisi injili ni ya kweli” (“Now Is the Time,” Ensign, Nov. 2000, 75).

Kujifunza Binafsi au na Mwenza

Kujifunza Maandiko

Je, maandiko yafuatayo yanafundisha nini kuhusu uwezo wa Roho katika kazi yako?

Je, unaweza kufanya nini ili kuwa na uwezo wa Roho katika kazi yako?

Picha
wamisionari wakisali

Sali kwa Imani katika Yesu Kristo

Ili kuwasidia wengine wawe waongofu, unahitaji kufundisha kwa uwezo wa Roho (ona Mafundisho na Maagano 50:13–14, 17–22). Bwana alisema, “Roho atatolewa kwenu kwa sala ya imani; na msipompokea roho msifundishe” (Mafundisho na Maagano 42:14).

Unaposali kwa ajili ya kufundisha kwako, uwezo wa Roho Mtakatifu utapeleka mafundisho yako “katika mioyo ya watoto wa watu” (2 Nefi 33:1). Unapofundisha kwa Roho na wengine kupokea kwa njia ya Roho, “mtaelewana kila mmoja” na “kujengana na kufurahia pamoja” (onaMafundisho na Maagano 50:22)).

Jinsi ya Kusali

Yesu alitufundisha jinsi ya kusali (ona Mathayo 6:9–13; 3 Nefi 18:19). Sali kwa uaminifu na kwa kusudi halisi la kutenda juu ya ushawishi unaopokea kutoka kwa Roho Mtakatifu. Sala zenye ufanisi huhitaji unyenyekevu, na juhudi endelevu (ona Moroni 10:3–4; Mafundisho na Maagano 8:10).

Tumia lugha ambayo inaleta uhusiano wa upendo, wa kumwabudu Mungu. Katika kiingereza, tumia lugha ya kimaandiko kama vile Thee, Thou, Thy, na Thine badala ya viwakilishi vya kawaida you, your, na yours.

Daima onesha shukrani. Juhudi za makusudi za kuwa na shukrani zitakusaidia utambue jinsi Mungu alivyo mwenye rehema katika maisha yako. Itafungua moyo wako na akili yako.

Sali “kwa nguvu zote za moyo” kwa ajili ya kujazwa hisani (Moroni 7:48). Sali kwa ajili ya wengine kwa majina. Sali kwa ajili ya wale unaowafundisha. Tafuta mwongozo kwa ajili ya jinsi utakavyowaalika na kuwasaidia waje kwa Kristo.

Kujifunza Binafsi

Jifunze sala ya Bwana katika Mathayo 6:9–13. Jiulize maswali yafuatayo, na uandike misukumo katika shajara yako ya kujifunzia.

  • Je ni kwa jinsi gani majukumu yako ya sasa kama mmisionari yanashawishi sala zako?

  • Ni kwa njia zipi sala zako zinatafuta kubariki maisha ya wengine?

  • Ni kwa jinsi gani unasali ili uweze kushinda majaribu?

  • Ni kwa jinsi gani unasali kwa ajili ya msaada ili kutimiza mahitaji yako ya kiroho na kimwili?

  • Ni kwa jinsi gani unatoa utukufu kwa Mungu wakati unaposali?

Wakati wa Kusali

Je, unapaswa kusali wakati gani? Bwana alisema, “Tafuteni kwa bidii, ombeni daima, na muwe wenye kuamini, na mambo yote yatafanyika kwa pamoja kwa faida yenu” (Mafundisho na Maagano 90:24).

Alma alisema, “Shauriana na Bwana kwenye matendo yako yote, na atakuongoza kwa yale mema; ndiyo, unapolala usiku lala katika Bwana, ili akulinde usingizini mwako; na ukiamka asubuhi hebu moyo wako ujazwe na shukrani kwa Mungu” (Alma 37:37; ona pia 34:17–27).

Bwana anakualika utenge nyakati za utulivu, za faragha ili usali: “Ingia kwenye chumba chako kidogo, na … sali kwa Baba yako” (3 Nefi 13:6; ona pia mstari wa 7–13).

Rais Gordon B. Hinckley alifundisha: “Kila asubuhi … , wamisionari wanapaswa kupiga magoti na kumsihi Bwana afungue ndimi zao na azungumze kupitia kwao ili kuwabariki wale watakaowafundisha. Kama watafanya hivi, nuru mpya itakuja katika maisha yao. Kutakuwa na shauku kuu kwa ajili ya kazi hii. Watakuja kujua kwamba katika hisia halisi kabisa, wao ni watumishi wa Bwana wanaozungumza kwa niaba Yake” (“Missionary Service,” First Worldwide Leadership Training Meeting, Jan. 11, 2003, 20).

Kumtumainia Mungu Wakati Tunaposali

Kuwa na imani katika Mungu humaanisha kumtumainia Yeye. Hii hujumuisha kutumaini mapenzi Yake na wakati Wake katika kujibu sala zako (ona Isaya 55:8). Rais Dallin H. Oaks alifundisha:

“Bila kujali imani yetu ni imara kiasi gani, haiwezi kuzalisha matokeo kinyume na mapenzi ya Yule ambaye kwake tunayo imani. Kumbuka hilo pale sala zako zinapoonekana kutojibiwa katika njia au wakati unaotamani. Matumizi ya imani katika Bwana Yesu Kristo daima yako chini ya utaratibu wa mbinguni, kwa wema na mapenzi na hekima na wakati wa Bwana. Tunapokuwa na aina hiyo ya imani na tumaini katika Bwana, tuna ulinzi wa kweli na utulivu maishani mwetu” (“Upatanisho na Imani,” Ensign, Aprili 2010, 30).

Kuhusu sala ambazo zinaweza kuonekana kutojibiwa, Rais Russell M. Nelson alisema:

Naijua hisia hiyo! Ninajua hofu na majonzi ya nyakati kama hizo. Lakini pia ninaelewa kuwa sala zetu kamwe huwa hazipuuzwi. Imani yetu kamwe haidharauliwi. Najua kuwa mtazamo wa Baba yetu wa Mbinguni ajuaye yote ni mpana sana kuliko wetu. Wakati tukijua matatizo yetu ya maisha ya duniani na maumivu, Yeye anajua maendeleo yetu kuelekea maisha ya milele na uwezekano wetu wa kuwa. Kama tutasali ili kujua mapenzi Yake na kujiweka chini yake kwa subira na ujasiri, uponyaji wa mbinguni unaweza kufanyika katika njia Yake na wakati Wake” (“Yesu Kristo—Bwana Mponyaji,” Liahona, Nov. 2005, 86).

Picha
Barabara ya kwenda Emau, na Greg Olsen

Kujifunza Kutambua Minong’ono ya Roho

Ni muhimu kwa ajili yako na watu unaowafundisha kujifunza kutambua mawasiliano kutoka kwa Roho. Roho kawaida huwasiliana kimyakimya, kupitia hisia zako, akili, na moyo wako. Nabii Eliya aligundua kwamba sauti ya Bwana haikuwa katika upepo, tetemeko la nchi, au moto—bali ilikuwa “sauti ndogo tulivu” (1 Wafalme 19:12). “Haikuwa sauti ya radi,” badala yake “sauti tulivu ya upole mkamilifu, kama mnong’ono,” na bado inaweza “kupenya hata kwenye roho” (Helamani 5:30).

Mawasiliano kutoka kwa Roho yanaweza kuhisiwa tofauti kwa watu tofauti. Bila kujali jinsi mawasiliano haya yanavyohisiwa, maandiko yanafundisha jinsi ya kuyatambua. Kwa mfano, Roho atakuinua na kukuongoza kwenye kutenda mema. Yeye ataiangaza akili yako. Yeye atakuongoza utembee kwa unyenyekevu, na kuhukumu kwa haki. (Ona Mafundisho na Maagano 11:12–14 na kijisanduku cha “Kujifunza Binafsi” baadaye katika sehemu hii.)

Katika jibu la swali “Ni kwa jinsi gani tunatambua ushawishi wa Roho?” Rais Gordon B. Hinckley alisoma Moroni 7:13, 16–17. Kisha alisema:

“Huu ndiyo mtihani, baada ya yote kusemwa na kutendwa. Je, inamshawishi mtu kufanya mema, kuinuka, kusimama wima, kufanya jambo sahihi, kuwa mkarimu, kuwa mpaji? Basi ni ushawishi wa Roho wa Mungu. …

“ … Na kama inakualika utende mema, ni ya Mungu. Kama inakualika utende uovu, ni ya Ibilisi. … Na kama unafanya kitu sahihi na kama unaishi katika njia sahihi, utajua moyoni mwako kile Roho anachosema kwako.

“Unatambua ushawishi wa Roho kwa matunda ya Roho—kile ambacho huangaza, kile ambacho hujenga, kile ambacho ni chanya na cha uhakika na cha kuinua na kutuongoza katika maneno na mawazo mazuri zaidi na matendo mazuri zaidi ni kutoka kwa Roho wa Mungu” (Teachings of Presidents of the Church: Gordon B. Hinckley [1997], 260).

Wakati unapotafuta na kufuata mwongozo wa Roho Mtakatifu, uwezo wako wa kutambua na kuelewa ushawishi Wake utakua baada ya muda (ona 2 Nefi 28:30). Katika baadhi ya njia, kuwa na usikivu zaidi kwa lugha ya Roho ni kama kujifunza lugha nyingine. Ni mchakato wa polepole ambao unahitaji bidii, juhudi yenye subira.

Tafuta mwongozo wa Roho Mtakatifu kwa kusudi kamili la moyo. Kama unajishughulisha na mambo mengine, hutaweza kuhisi mnong’ono laini wa Roho. Au anaweza kusubiri kuwasiliana mpaka unapotafuta ushawishi Wake kwa unyenyekevu kuwa radhi kutenda juu ya minong’ono Yake.

Sauti katika ulimwengu zinashindania usikuvu wako. Zinaweza kwa urahisi kuvuruga misukumo ya kiroho isipokuwa wewe utoe nafasi kwa ajili ya Roho ndani ya moyo wako. Kumbuka ushauri huu kutoka kwa Bwana: “Tulieni na jueni kuwa Mimi ni Mungu” (Zaburi 46:10; ona pia Mafundisho na Maagano 101:16).

Picha
Mzee David A. Bednar

“Mungu hutumia njia tofauti tofauti kuleta ufunuo kwa wana na mabinti Zake, kama vile fikra hadi kwenye akili na hisia kwenye moyo, ndoto, … na mwongozo. Ufunuo mwingine hupokelewa mara moja na kwa nguvu; baadhi unatambuliwa hatua kwa hatua na kwa ustadi. Kupokea, kutambua, na kujibu ufunuo kutoka kwa Mungu ni vipawa vya roho ambavyo sote tunapaswa kuvitamani na kuvitafuta kadiri inavyofaa” (David A. Bednar, “The Spirit of Revelation in the Work,” 2018 mission leadership seminar).

Kujifunza Binafsi

Jifunze maandiko katika jedwali lifuatalo. Fikiria nyakati ambapo ulipata uzoefu wa hisia yoyote, mawazo, au misukumo iliyoelezwa katika mistari hii. Unapojifunza na kupata uzoefu, ongeza maandiko mengine kwenye orodha hii. Fikiria jinsi unavyoweza kutumia kanuni hizi ili kuwasaidia wengine wamhisi na wamtambue Roho.

Mafundisho na Maagano 6:23; 11:12–14; 88:3; Yohana 14:26–27; Warumi 15:13; Wagalatia 5:22–23

Huleta hisia za upendo, furaha, amani, faraja, subira, upole, staha, imani na tumaini.

Alma 32:28; Mafundisho na Maagano 6:14–15; 8:2–3; 1 Wakorintho 2:9–11

Huangaza na huleta mawazo akilini na hisia moyoni.

Joseph Smith—Historia ya 1:11–12

Husaidia maandiko kuwa na athari kubwa.

Alma 19:6

Hubadilisha giza kuwa nuru.

Mosia 5:2-5

Huimarisha tamanio la kuepuka uovu na kutii amri.

Moroni 10:5; Mafundisho na Maagano 21:9; 100:8; Yohana 14:26; 15:26; 16:13

Hufundisha ukweli na huuleta kwenye kumbukumbu.

Mafundisho na Maagano 45:57

Huongoza na hulinda dhidi ya udanganyifu.

2 Nefi 31:18; Mafundisho na Maagano 20:27; Yohana 16:13–14

Hutukuza na hutoa ushuhuda wa Baba na Yesu Kristo.

Mafundisho na Maagano 42:16; 84:85; 100:5–8; Luka 12:11–12

Huongoza maneno ya walimu wanyenyekevu.

Moroni 10:8–17; Mafundisho na Maagano 46:8–26; 1 Wakorintho 12

Hutoa karama za Roho

Mafundisho na Maagano 46:30; 50:29–30

Hutuambia mambo ya kuyaombea.

2 Nefi 32:1–5; Mafundisho na Maagano 28:15

Hutuambia kipi cha kufanya.

1 Nefi 10:22; Alma 18:35

Huwasaidia wenye haki wazungumze kwa nguvu na mamlaka.

2 Nefi 31:17; Alma 13:12; 3 Nefi 27:20

Hutakasa na huleta ondoleo la dhambi.

1 Nefi 2:16–17; 2 Nefi 33:1; Alma 24:8

Hubeba ukweli hadi kwenye moyo wa msikilizaji.

1 Nefi 18:1–3; Kutoka 31:3–5

Huongeza ujuzi na uwezo.

1 Nefi 7:15; 2 Nefi 28:1; 32:7; Alma 14:11; Mormoni 3:16; Etheri 12:2

Huhimiza kusonga mbele au kutulia.

Mafundisho na Maagano 50:13–22

Huwainua wote, mwalimu na wanafunzi.

Mtegemee Roho

Kama mtumishi wa Bwana, unapaswa kuifanya kazi Yake katika njia Yake na kwa nguvu Zake. Nabii Joseph Smith alifundisha kwamba, “hakuna mtu anayeweza kuihubiri Injili bila kuwa na Roho Mtakatifu” (Teachings: Joseph Smith332).

Mtumainie Roho akuongoze katika kila kipengele cha kazi yako. Yeye atakuangazia na kukupa msukumo. Yeye atakusaidia upate watu wa kuwafundisha na atakuletea nguvu katika ufundishaji wako. Yeye atakusaidia unapowasaidia waumini, waumini wanaorejea, na waongofu wapya waimarishe imani yao.

Baadhi ya wamisionari wanahisi kujiamini wenyewe. Wengine wanakosa kujiamini kama huko. Kwa unyenyekevu weka kujiamini kwako na imani katika Yesu Kristo, sio kwako mwenyewe. Mtegemee Roho badala ya vipaji vyako na uwezo wako mwenyewe. Roho Mtakatifu atakuza juhudi zako zaidi ya vile unavyoweza kufanya wewe mwenyewe.

Kujifunza Maandiko

Jifunze maandiko yafuatayo na ufikirie jinsi yanavyojibu haya maswali muhimu ambayo unapaswa kuyauliza kila siku. Ni kwa jinsi gani unaweza kutumia mafundisho katika vifungu hivi katika juhudi zako za utafutaji, vikao vya kuweka mipango, na kujifunza na mmisionari mwenza? Ni kwa jinsi gani unaweza kutumia vifungu hivi katika juhudi zako za kufundisha, kuwaalika watu waweke ahadi, na kufuatilia ahadi hizo?

Je, ninapaswa kwenda wapi?

Je, ninapaswa kufanya nini?

Je, ninapaswa kusema nini?

Je, ni kwa jinsi gani ninapaswa kutumia maandiko katika kufundisha kwangu?

Baadhi ya Maneno ya Tahadhari

Thibitisha Misukumo Yako kwa Vyanzo vya Kuaminika

Unaposali kwa ajili mwongozo, linganisha misukumo yako ya kiroho na maandiko na mafundisho ya manabii walio hai. Misukumo kutoka kwa Roho itawiana na vyanzo hivi.

Tafuta Ufunuo ndani ya Jukumu Lako

Hakikisha kwamba hisia unazopokea zinaambatana na jukumu lako. Isipokuwa umeitwa kwa mamlaka sahihi, misukumo kutoka kwa Roho haitatolewa kwako kuwashauri au kuwarekebisha wengine. Kwa mfano, hautapokea ufunuo wa kumwambia askofu kile anachopaswa kufanya katika wito wake.

Picha
Kipawa cha Nuru

Tambua Ushawishi wa Kweli wa Roho

Rais Howard W. Hunter alishauri: “Acheni nitoe neno la tahadhari. … Nadhani kama hatuko makini … , tunaweza kuanza kujaribu kugushi ushawishi kamili wa Roho wa Bwana kwa njia na ujanja usiostahili. Napata wasiwasi wakati inapoonekana kwamba hisia kali au machozi yanayotiririka wazi yanalinganishwa na uwepo wa Roho. Hakika Roho wa Bwana anaweza kuleta hisia kali, ikiwemo machozi, lakini dhihirisho hilo la nje halipaswi kukanganywa na uwepo wa Roho mwenyewe” (The Teachings of Howard W. Hunter [1997], 184).

Usijaribu Kulazimisha Mambo ya Kiroho

Mambo ya kiroho hayawezi kulazimishwa. Unaweza kukuza mtazamo na mazingira ambayo yanamwalika Roho, na unaweza kujiandaa wewe mwenyewe, lakini hauwezi kushurutisha jinsi gani au wakati gani mwongozo huja. Kuwa na subira na tumainia kwamba utapokea kile unachohitaji wakati muda ni sahihi.

Fanya Uzoefu wa Kiroho Uwe Mtakatifu

Kama mmisionari, unaweza kuwa na ufahamu zaidi wa uzoefu wa kiroho kuliko ulivyowahi kuwa nao awali katika maisha yako. Uzoefu huu ni mtakatifu na kwa kawaida ni kwa ajili ya kujengwa kwako, maelekezo, au marekebisho.

Wingi wa uzoefu huu ni vyema kuwekwa faragha. Ushiriki pale tu Roho anapoonesha kwamba unaweza kuwabariki watu wengine kwa kufanya hivyo (ona Alma 12:9; Mafundisho na Maagano 63:64; 84:73).

Tumia Uamuzi Wako Mwenyewe Ulio Bora katika Baadhi ya Hali

Wakati mwingine tunataka kuongozwa na Roho katika mambo yote. Hata hivyo, kila mara Bwana hututaka sisi tutende tukitumia uamuzi wetu wenyewe ulio bora (ona Mafundisho na Maagano 60:5; 61:22; 62:27). Rais Dallin H. Oaks alifundisha:

“Hamu ya kuongozwa na Bwana ni nguvu, lakini inahitaji kuambatana na ufahamu kwamba Baba yetu wa Mbinguni hutuachia maamuzi mengi kwa ajili ya chaguzi zetu binafsi. Kufanya maamuzi binafsi ni mojawapo ya vyanzo vya kukua ambako tunatarajiwa kupitia katika maisha ya hapa duniani. Watu ambao hujaribu kuhamisha ufanyaji uamuzi wote kwa Bwana na kuomba kwa ajili ya ufunuo katika kila uchaguzi baada ya muda mfupi watapata hali ambazo kwazo wanasali kwa ajili ya mwongozo ila hawaupati. Kwa mfano, hili lina uwezekano mkubwa wa kutokea katika hali nyingi tofauti ambazo chaguzi ni ndogo au uchaguzi unakubalika.

Tunapaswa kujifunza mambo kutoka akilini mwetu, tukitumia uwezo wa kufikiri ambao Muumba wetu ameuweka ndani yetu. Kisha tunapaswa kusali kwa ajili ya mwongozo na kuufanyia kazi kama tutaupokea. Kama hatutapokea mwongozo, inatupasa kutenda kulingana na maamuzi yetu yaliyo bora. Watu ambao wanasisitiza katika kutafuta maongozi ya ufunuo juu ya mada ambayo Bwana hajaichagua kutuongoza wanaweza kubuni jibu la fikra zao au upendeleo wao, au wanaweza kupokea jibu kutoka kwenye njia ya ufunuo wa uongo” (“Our Strengths Can Become Our Downfall,” Ensign, Oct. 1994, 13–14).

Kujifunza Maandiko

Kumtegemea Roho ni muhimu sana kiasi kwamba Bwana hutuonya tusikane au kumzimisha Roho. Unajifunza nini kutoka katika vifungu vya maandiko vifuatavyo?


Mawazo kwa ajili ya Kujifunza na Kutumia

Kujifunza Binafsi

  • Gawa ukurasa katika safu mbili. Andika safu moja “Kile Ambacho Bwana Alifanya” na safu nyingine “Kile Ambacho Lehi au Nefi Alifanya.” Soma hadithi ya Liahona na upinde uliovunjika (1 Nefi 16:9–31) au hadithi ya Nefi akijenga merikebu (1 Nefi 17:7–16; 18:1–6). Orodhesha matukio kutoka kwenye hadithi katika safu sahihi. Fikiria hadithi hii inaweza kukufundisha nini kuhusu asili ya mwongozo wa kiungu.

  • Tazama kote katika shajara yako na upate nyakati ulipoongozwa na Roho au kupata uzoefu wa kipawa cha Roho. Fikiria kuhusu lini, wapi, na kwa nini uzoefu huu ulitokea. Ni kwa jinsi gani mkono wa Bwana ulidhihirika? Je! ulijisikiaje? Kukumbuka uzoefu huu kunaweza kukusaidia umtambue Roho.

  • Jifunze Alma 33:1–12 na Alma 34:17–31. Ni maswali yapi Alma na Amuleki walikuwa wakijibu? (Rejelea Alma 33:1–2.) Je, ni jinsi gani walijibu maswali haya? Je, ni hakikisho lipi walilitoa?

  • Bwana ameahidi kwamba Roho atatuongoza katika njia nyingi muhimu. Unaposoma vifungu vifuatavyo, tambua vipengele vya kazi yako ambavyo vinahitaji mwongozo wa Roho. Je, kanuni katika maandiko yafuatayo zinamaanisha nini kwa ajili ya kujifunza kwako binafsi na mmisionari mwenza? Kwa ajili ya mikutano ya baraza la wilaya, mikutano ya kanda, ibada ya ubatizo, na mikutano mingine?

    Kusali

    Kuendesha mikutano

Kujifunza pamoja na Mwenza na Kubadilishana mwenza

  • Zungumzeni kuhusu sala mnazotoa kama wenza. Je, zinaongozwa na Roho Mtakatifu? Je, ni kwa jinsi gani mnapokea majibu ya sala zenu kama wenza? Mnaposali kama wenza, je:

    • Mnaamini kwamba Mungu atawapatia kile mnachoomba kwa haki na kulingana na mapenzi Yake?

    • Mnatambua na kutoa shukrani kwa ajili ya majibu ya sala zenu?

    • Mnasali kwa ajili ya watu kwa jina na kufikiria mahitaji yao?

    • Mnasali kwa ajili ya kila mmoja wenu na kwa ajili ya Roho ili awaongoze?

    • Mnatambua majibu ya sala zenu?

    • Mnasali kwa ahadi kwamba mtatendea kazi misukumo mnayoipokea?

  • Jadilini jinsi ambavyo mtamtafuta Roho kwa ari zaidi.

  • Jadilini njia tofauti ambazo watu wanaelezea kuhusu ushawishi wa Roho Mtakatifu. Wekeni kumbukumbu katika shajara zenu za kujifunzia za maoni ambayo wale mnaowafundisha wametoa kuhusu uzoefu wao na Roho. Ni kwa jinsi gani mnaweza kuwasaidia wengine wautambue ushawishi huumtakatifu?

Baraza la Wilaya, Mikutano ya Kanda na Baraza la Uongozi la Misheni

  • Kadiri inavyofaa, waruhusu wamisionari washiriki hadithi au uzoefu waliosikia katika mikutano ya ushuhuda wa hivi karibuni, uzoefu wa kufundisha, au mazingira mengine. Hadithi na uzoefu wa kiroho ambao watu wengine wanausimulia unaweza kukusaidia ukuze imani na utambue kwamba ushawishi wa Roho unadhihirishwa kwa wingi na kila mara.

  • Waombe wamisionari watoe hotuba kuhusu misheni na nguvu ya Roho Mtakatifu.

  • Jadilini ni jinsi gani kuonesha shukrani kunavyowasaidia waone njia ndogo lakini ya kipekee sana ambayo kwayo Bwana huwabariki (ona Etheri 3:5; Mafundisho na Maagano 59:21). Jadilini njia za kuonesha shukrani.

  • Fikiria kuwaomba waumini wapya wazungumze kuhusu jinsi walivyoshawishiwa na Roho wakati walipokuwa wakijifunza kuhusu Kanisa. Muombe mtu ashiriki uzoefu ule tu ambao yeye anahisi ni sahihi kueleza.

Viongozi wa Misheni na Washauri wa Misheni

  • Ungeweza kuwaomba wamisionari wajumuishe uzoefu wa kiroho unaofaa katika barua zao za kila wiki zinazokuja kwako.

  • Katika mahojiano au katika mazungumzo, mara kwa mara waulize wamisionari kuhusu sala zao za asubuhi na jioni. Kama itahitajika, washauri kuhusu jinsi ya kufanya sala zao ziwe zenye maana zaidi.

  • Waulize wamisionari jinsi wanavyowasaidia wale wanaowafundisha wamhisi na wamtambue Roho.