Miito ya Misheni
Sura ya 12: Wasaidie Watu Wajiandae kwa ajili ya Ubatizo na Uthibitisho


“Sura ya 12: Wasaidie Watu Wajiandae kwa ajili ya Ubatizo na Uthibitisho,” Hubiri Injili Yangu: Mwongozo wa Kushiriki Injili ya Yesu Kristo (2023)

“Sura ya 12,” Hubiri Injili Yangu

Picha
Yohana Mbatizaji Akimbatiza Yesu, na Greg K. Olsen.

Sura ya 12

Wasaidie Watu Wajiandae kwa ajili ya Ubatizo na Uthibitisho

Zingatia Hili

  • Ni kwa jinsi gani ninaweza kuwasaidia watu wajiandae kwa ajili ya ubatizo na uthibitisho?

  • Ni kwa jinsi gani ninaweza kuendesha mahojiano ya ubatizo?

  • Ni kwa jinsi gani ibada ya ubatizo yenye kuinua inapangwa na kuendeshwa?

  • Kwa nini ni muhimu kujaza na kuwasilisha fomu ya ubatizo na uthibitisho?

  • Ni kwa jinsi gani ninaweza kuwasaidia waumini wapya?

Ubatizo ni ibada ya shangwe ya tumaini ambalo huleta nguvu ya Mungu katika maisha ya mtu. Nguvu hiyo huja kupitia kipawa cha Roho Mtakatifu. Itaendelea mtu anapovumilia hadi mwisho katika kushika agano la ubatizo.

Dhumuni la ufundishaji wako ni kuwasaidia wengine wakuze imani katika Yesu Kristo, watubu dhambi zao, na kubatizwa wakiwa na nia ya dhati ya kumfuata Kristo. Kama vile Mormoni alivyofundisha, “Na matokeo ya kwanza ya toba ni ubatizo” (Moroni 8:25). Watu unaowafundisha wanapotimiza ahadi unayowaalika waiweke, watakuwa wamejiandaa kufanya na kushika maagano na Mungu na kufurahia baraka zilizoahidiwa.

Ubatizo na uthibitisho siyo mwisho wa safari. Badala yake, ibada hizi ni lango ambalo kwalo watoto wa Mungu wanaingia katika njia ya agano. Njia hii huongoza hadi kwenye ibada, maagano, na baraka zenye shangwe za hekalu—na hatimaye uzima wa milele (ona 3 Nefi 11:20–40).

Sifa kwa ajili ya Ubatizo na Uthibitisho

Mungu anawaalika watoto Wake wote waje Kwake kupitia ubatizo na uthibitisho” (ona 2 Nefi 26:33; 3 Nefi 27:20). Sifa kwa ajili ya ubatizo ni sawa kwa wote.

Kutoka kwenye Mafundisho na Maagano 20:37:

  • Jinyenyekeze mwenyewe mbele za Mungu.

  • Nia ya kubatizwa.

  • Njoo kwa moyo uliovunjika na roho iliyopondeka.

  • Tubu dhambi zako zote na usali kwa ajili ya msamaha.

  • Uwe radhi kujichukulia juu yako jina la Kristo.

  • Uwe na ari ya kumtumikia Kristo hadi mwisho.

  • Onesha kwa matendo yako kwamba umempokea Roho wa Kristo aongozaye kwenye ondoleo la dhambi zako.

Kutoka kwa Urais wa Kwanza na Akidi ya Mitume Kumi na Wawili:

  • Jibu kwa usahihi maswali ya mahojiano ya ubatizo.

  • Pokea masomo yote ya wamisionari.

  • Kutana na rais wa akidi ya wazee, rais wa Muungano wa Usaidizi, na askofu.

  • Hudhuria mikutano kadhaa ya sakramenti.

Sifa hizi ni viashiria vya mchakato wa uongofu wa kiroho. Wakati watu wanapokidhi sifa hizi, wanakuwa tayari kwa ajili ya ibada za ubatizo na uthibitisho.

Wakati mtu akiwa ameweka tarehe thabiti ya ubatizo:

  • Kwa makini pitia tena kumbukumbu yake katika app ya Hubiri Injili Yangu ili kuhakikisha kwamba umefundisha mafundisho na amri zinazohitajika.

  • Tengeneza ratiba kwa ajili ya matukio ambayo yanahitajika kujiandaa kwa ajili ya ubatizo na uthibitisho. Pitia tena ratiba hii na mtu huyu.

  • Kama inawezekana, mwalike mtu huyu kuhudhuria kwenye ibada ya ubatizo kabla ya ubatizo wake mwenyewe.

Kujifunza Maandiko

Jifunze maandiko yafuatayo. Ni kwa jinsi gani unaweza kuwasaidia wale unaowafundisha wajiandae kwa ajili ya ubatizo na uthibitisho? Andika kile ulichojifundisha kutokana na kusoma kwako.

Picha
Mponyaji Mpole, na Greg K. Olsen

Wasaidie Watu Wajiandae kwa ajili ya Mahojiano ya Ubatizo

Mahojiano ya ubatizo ni hatua muhimu ya kuhakikisha kwamba mtu anafikia sifa za Bwana kwa ajili ya ubatizo. Ratibu mahojiano ya ubatizo pale tu wakati mtu huyu yuko tayari.

Wasaidie watu unaowafundisha kwa ajili ya mahojiano haya ili wahisi faraja kuyahusu. Eleza vile mahojiano yatakavyokuwa. Waambie kwamba watakutana na mmisionari mwingine kama wewe.

Eleza dhumuni la mahojiano haya. Ni fursa kwa ajili yao ya kushuhudia kwamba “wametubu dhambi zao zote, [na] wakithibitisha kwa matendo yao kwamba wamempokea Roho wa Kristo aongozaye kwenye ondoleo la dhambi zao” (Mafundisho na Maagano 20:37).

Shiriki maswali ambayo mwendesha mahojiano atauliza (ona hapo chini). Hii humsaidia mtu ajiandae kuyajibu.

Hakikisha mtu anaelewa kile ambacho wewe umefundisha na agano ambalo yeye atafanya kwenye ubatizo. Agano hili ni:

  • Kuwa radhi kujichukulia juu yake jina la Yesu Kristo.

  • Kushika amri za Mungu.

  • Kumtumikia Mungu na wengine.

  • Kuvumilia hadi mwisho. (Ona somo la 4.)

Toa ushuhuda kuhusu baraka kuu ambazo zinatokana na kubatizwa na kuthibitishwa na kushika agano la ubatizo. Baraka hizi zinajumuisha ondoleo la dhambi na kipawa Roho Mtakatifu.

Kuendesha mahojiano ya Ubatizo

Kila mtu ambaye anatamani kubatizwa anasailiwa na kiongozi wa ukuhani aliyeidhinishwa. Katika misheni, mtu huyu ni kiongozi wa wilaya au kanda. Yeye huendesha mahojiano kwa:

  • Watu wenye umri wa miaka 9 na zaidi ambao kamwe hawajabatizwa na kuthibitishwa.

  • Watoto wenye umri wa miaka 8 na zaidi ambao wazazi wao si waumini wa Kanisa.

  • Watoto wenye umri wa miaka 8 ambao wana mzazi ambaye pia anabatizwa na kuthibitishwa.

Miongozo kwa ajili ya mwendesha mahojiano yametolewa hapa chini.

  • Fanya mahojiano katika mahali pa faraja, faraghani ambapo Roho anaweza kuhisiwa.

  • Wakati unamsaili mtoto, kijana, au mwanamke, mwenza wa mwendesha mahojiano anapaswa kuwa karibu katika chumba kilicho mkabala, sebuleni, au ukumbi ulio mkabala. Kama mtu atataka, mtu mzima mwingine anaweza kualikwa kushiriki katika mahojiano. Wamisionari wanapaswa kuepukana na hali zote ambao zinaweza kutoeleweka.

  • Anza kwa sala.

  • Msaidie mtu huyu ahisi faraja.

  • Fanya mahojiano yawe tukio la kiroho lenye kuinua.

  • Hakikisha kwamba mtu huyo anaelewa dhumuni la mahojiano.

  • Uliza maswali ya mahojiano ya ubatizo yaliyoorodheshwa hapa chini. Tohoa maswali kwa ajili ya umri wa mtu, ukomavu, na hali kama inavyohitajika.

  • Jibu maswali ya mtu huyu.

  • Pitia tena taarifa zilizoandikwa kwenye Fomu ya Ubatizo na Uthibitisho kwa ajili ya Usahihi. Kama ni mtoto mdogo, mzazi au mlezi anahitaji kutia saini fomu kabla ya ubatizo (ona sehemu ya “Ubatizo na Uthibitisho: Maswali na Majibu” katika sura hii).

  • Mwalike mtu huyu atoe ushuhuda au ashiriki uzoefu wake.

  • Toa shukrani kwa kuweza kukutana na mtu huyu.

Maswali ya Mahojiano ya Ubatizo

Maswali ya mahojiano ya ubatizo ni kama yafuatayo:

  1. Je, unaamini kwamba Mungu ni Baba yetu wa Milele? Je, unaamini kwamba Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu, na Mwokozi na Mkombozi wa Ulimwengu?

  2. Je! Unaamini kwamba Kanisa na injili ya Yesu Kristo vimerejeshwa kupitia Nabii Joseph Smith? Je! Unaamini kwamba [Rais wa Kanisa wa sasa] ni nabii wa Mungu? Hii inamaanisha nini kwako?

  3. Kutubu inamaanisha nini kwako? Je, unahisi kwamba umetubu juu ya dhambi zako za zamani?

  4. Umefundishwa kwamba uumini katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho hujumuisha kuishi viwango vya injili. Je, unaelewa nini kuhusu viwango vifuatavyo? Je, uko radhi kuvitii?

    • Sheria ya usafi wa kimwili, ambayo inakataza uhusiano wowote wa kimapenzi nje ya mipaka ya ndoa halali kati ya mwanamume na mwanamke.

    • Sheria ya zaka

    • Neno la Hekima

    • Kuitakasa siku ya Sabato, ikijumuisha kupokea sakramenti kila wiki na kuwatumikia wengine

  5. Je, umeshawahi kutenda kosa kubwa la jinai? Kama ndivyo, sasa uko chini ya uangalizi au kifungo cha nje?

  6. Je, umewahi kushiriki katika utoaji mimba? (Ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla, 38.6.1.)

  7. Unapobatizwa, unafanya agano na Mungu kwamba wewe u tayari kujichukulia juu yako jina la Kristo, kuwatumikia wengine, kusimama kama shahidi wa Mungu nyakati zote, na kushika amri Zake maisha yako yote. Je, upo tayari kufanya agano hili na kujitahidi kuwa mwaminifu kwenye agano hilo?

Kwa maelekezo kama mtu anajibu swali la 5 au 6 kwa kukubali ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla, 38.2.8.7 na 38.2.8.8.

Kuwa mzoefu kwa sera na miongozo inayohusiana na ubatizo na uthibitisho katika Kitabu cha Maelezo ya Jumla, 38.2.8. Baadhi ya sera hizi zinahusisha hali maalum ambazo unaweza kukutana nazo.

Baada ya mahojiano, wamisionari na mtu anayetarajia kubatizwa wanajiunga na wamisionari wengine. Kama mtu yuko tayari kwa ajili ya ubatizo, wamisionari wanaeleza kile kitakachotendeka katika ibada ya ubatizo. Pia wanaeleza kwamba uthibitisho kwa kawaida hutendeka katika mkutano wa sakramenti wa kata mahali ambapo mtu huyu anaishi.

Wakati Ubatizo Unapohitaji Kuahirishwa

Wakati mwingine ubatizo unahitaji kuahirishwa kwa sababu ya changamoto za ushuhuda au ustahili. Wakati hili linapotokea, shughulikia hali kwa usikivu na faragha. Msaidie mtu huyu aelewe jinsi ya kujiandaa kwa ajili ya ubatizo katika siku zijazo.

Mtie moyo mtu huyu na toa tumaini katika Kristo na Upatanisho Wake. Waombe waumini wa kata wajenge urafiki. Endelea kufundisha kanuni za msingi za injili mpaka mtu huyu anapokuwa tayari kubatizwa na kuthibitishwa. Subiri mpaka wakati huo ili kupanga tarehe mpya ya ubatizo.

Ubatizo na Uthibitisho: Maswali na Majibu

Je, nahitaji ruhusa kumbatiza mtoto mdogo? Kanisa linajali hali njema ya watoto na uwiano wa mazingira ya nyumbani kwao. Mtoto mdogo, kama inavyofafanuliwa na sheria za eneo husika, anaweza kubatizwa wakati masharti yafuatayo yanapokuwa yametimizwa:

  1. Mzazi anayemtunza (wanaomtunza) au mlezi (walezi) kisheria wanatoa ruhusa kwa maandishi. Wanapaswa kuwa na uelewa wa kawaida wa mafundisho ambayo mtoto wao atafundishwa kama muumini wa Kanisa. Wanapaswa pia kuwa radhi kumsaidia mtoto huyu aweke na atimize agano la ubatizo.

  2. Mtu ambaye anaendesha mahojiano anatambua kwamba mtoto anaelewa agano la ubatizo. Anapaswa kuhisi ujasiri kwamba mtoto huyu atajitahidi kushika agano hili kwa kutii amri, ikijumuisha kuhudhuria mikutano ya Kanisa.

Je, ninahitaji ruhusa ya mwenza wa ndoa ili kumbatiza mume au mke? Ndiyo. Mtu aliyeoa au kuolewa ni lazima apate ridhaa kutoka kwa mume au mke wake kabla ya kubatizwa.

Kama mzazi katika familia hayuko tayari kwa ajili ya ubatizo, je ninapaswa kuwabatiza wanafamilia wengine au nisubiri mpaka mzazi huyu atakapokuwa tayari? Inapendekezwa kwamba wanafamilia wabatizwe pamoja. Hata hivyo, kama baadhi hawako tayari, mwanafamilia mmoja mmoja wanaweza kubatizwa alimradi ridhaa inayohitajika imetolewa.

Je, ubatizo wa wanafamilia unapaswa kucheleweshwa mpaka baba aweze kupokea Ukuhani wa Haruni na kufanya ubatizo yeye mwenyewe? Hapana. Akina kaka wanaobatizwa hawapokei Ukuhani wa Haruni katika siku wanapobatizwa. Wanahitaji kwanza kufanyiwa mahojiano na askofu na kukubaliwa na waumini wa kata.

Je, ninaweza kumfundisha na kumbatiza mtu ambaye alijiuzulu kutoka kwenye uumini wa Kanisa au uumini wake uliondolewa? Watu ambao walijiuzulu uumini wa Kanisa au uumini wao uliondolewa wanaweza kukubaliwa tena kwa ubatizo na uthibitisho. Kama wangependa kufundishwa, shauriana na viongozi wa ukuhani wa eneo husika na rais wako wa misheni kuhusu wajibu wowote unaoweza kuwa nao.

Katika kigingi, kukubaliwa tena kwa ubatizo itakuwa chini ya maelekezo ya askofu au rais wa kigingi. Katika misheni, kukubaliwa tena kunakuwa chini ya maelekezo ya urais wa misheni. Viongozi hawa watapokea mwongozo kutoka kwa Urais wa Kwanza kama inavyohitajika. Wamisionari hawaendeshi mahojiano ya ubatizo huu au kujaza fomu ya ubatizo na uthibitisho. Hata hivyo, wamisionari wanaweza kualikwa kufanya ubatizo.

Waumini wa awali wa Kanisa wanaojiunga tena si waongofu. Hata hivyo, wamisionari wanaweza wakati mwingine kuwa na wajibu muhimu katika kuwasaidia wafurahie baraka za uumini wa Kanisa kwa mara nyingine.

Je, inakuwaje kama mtu ana tarehe ya ubatizo lakini hatimizi ahadi zote? Subiri kupanga ratiba ya mahojiano ya ubatizo mpaka pale mtu huyu anapotimiza ahadi na kufikia sifa za ubatizo. Ona “Wakati Gani Ubatizo Unahitaji Kuahirishwa” katika sura hii.

Je, kama wachumba wanataka kubatizwa lakini wanaishi pamoja? Wachumba wanaoishi pamoja nje ya ndoa halali kati ya mwanamume na mwanamke hawawezi kubatizwa hadi pale wanapoishi sheria ya usafi wa kimwili. Hii inamaanisha kutoishi pamoja tena—iwe wachumba wa jinsia tofauti au wachumba wa jinsia moja—au, kwa mwanamume na mwanamke, inamaanisha waoane. Pia inajumuisha kuonesha imani iongozayo kwenye toba kama ilivyoelezwa katika Mafundisho na Maagano 20:37. Ndoa kati ya mwanamume na mwanamke ni muhimu kwa mpango wa Mungu.

Swali la 5 na la 6 katika mahojiano ya ubatizo huuliza ikiwa mtu ameshawahi kutenda kosa kubwa la jinai au kushiriki katika utoaji mimba. Je, ninapaswa kufanya nini ikiwa mtu anajibu “ndiyo” kwa maswali haya yote? Kama ukijua mojawapo ya hali hizi wakati wa mahojiano ya ubatizo, usiulize kuhusu maelezo ya kina. Usiahidi kwamba mtu huyu atakubaliwa kwa ajili ya ubatizo. Badala yake onesha upendo na kwa upole eleza kwamba mtu mwingine aliye na ukomavu na uzoefu zaidi atazungumza na mtu huyu na kutoa msaada.

Tuma ombi la mahojiano ya ubatizo kwa rais wa misheni. Yeye au mmoja wa washauri wake atakutana na mtu huyo. Ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla, 38.2.8.7 na 38.2.8.8.

Je, ninaweza kufanya nini kama kumbukumbu za uumini zimeshatengenezwa kabla ya kuwasilisha Fomu ya Ubatizo na Uthibitisho? Wasiliana na rais wako wa misheni kwa maelekezo.

Kujifunza Binafsi

Fikiria kuhusu jinsi ambavyo ungehisi kama ulikuwa unasailiwa. Fikiria maswali yafuatayo na uandike misukumo yako.

  • Ni kwa jinsi gani mahojiano yangeonekana kuwa ya faraja kwako? Mtu anayekufanyia mahojiano angeweza kufanya nini au kusema nini ili kukufanya ujisikie uko sawa?

  • Ni jinsi gani ungetaka mtu anayekufanyia mahojiano achangamane nawe?

  • Ni kwa jinsi gani ungetaka mtu anayekufanyia mahojiano ajibu ikiwa unaonesha mashaka au kutoelewa au kama umekiri dhambi kubwa?

Picha
ubatizo

Ibada ya Ubatizo

Ibada ya ubatizo na uthibitisho inapaswa kuwa ya kiroho inayoonekana wazi kwa muumini mpya. Ibada ya ubatizo inapaswa kuratibiwa punde tu mtu anapokuwa amekidhi vigezo kwa ajili ya ubatizo. Eleza kile kilichopangwa na kwa nini kimepangwa. Jadili mavazi yanayofaa, ikijumuisha jinsi mtu atakavyopatiwa nguo nyeupe za kuvaa kwa ajili ya ubatizo.

Huduma za ubatizo kwa ajili ya waongofu zinapangwa chini ya mwongozo wa uaskofu. Kiongozi wa misheni wa kata (kama ameitwa) au mshiriki wa urais wa akidi ya wazee ambaye anaongoza kazi ya umisionari na kuendesha ibada hizi. Hufanya uratibu pamoja na wamisionari wa muda wote. Huduma za ubatizo zinapaswa kuwa rahisi, fupi, na za kuinua kiroho.

Mwalike mshiriki wa uaskofu, mshiriki wa urais wa Muungano wa Usaidizi, na mshiriki wa urais wa akidi ya wazee (kama yeye siye anayeendesha) wahudhurie ibada ya ubatizo. Wakati inapofaa, waalike viongozi wengine wa vikundi, viongozi wa vijana, na akina kaka na akina dada wahudumiaji (kama wamepangiwa). Fanya kazi na mtu anayebatizwa ili kuwaalika marafiki na jamaa kuhudhuria ibada ya ubatizo na uthibitisho.

Fikiria kuwaalika watu wengine unaowafundisha. Uzoefu huu utawasaidia wamhisi Roho na wajifunze zaidi kuhusu injili. Baada ya ibada, fuatilia kujadili uzoefu wao na waalike ili wafundishwe.

Ibada ya ubatizo inaweza kujumuisha yafuatayo:

  1. Muziki wa utangulizi

  2. Makaribisho mafupi kutoka kwa kiongozi wa ukuhani ambaye anaendesha ibada (mshiriki wa uaskofu anapaswa kusimamia kama inawezekana)

  3. Wimbo wa kufungua na sala ya kufungua

  4. Ujumbe mmoja au miwili mifupi juu ya mada za injili, kama vile ubatizo na kipawa cha Roho Mtakatifu

  5. Uteuzi wa muziki

  6. Ubatizo

  7. Wakati wa staha huku wale walioshiriki katika ubatizo wakibadilisha nguo za ubatizo kwa kuvaa nguo zilizokauka. (Nyimbo za dini au nyimbo za Msingi zinaweza kupigwa au kuimbwa wakati huu. Au wamisionari wanaweza kutoa wasilisho fupi la injili.)

  8. Kutoa ushuhuda kwa waumini wapya, ikiwa itafaa

  9. Wimbo wa kufunga na sala ya kufunga

  10. Muziki baada ya ibada

Kama utaratibu ubatizo Jumapili, chagua muda ambao hauitilafiani na mikutano ya kawaida ya Jumapili.

Picha
uthibitisho

Uthibitsho

Mtu hupokea ibada ya uthibitisho baada ya yeye kubatizwa (ona Mafundisho na Maagano 20:41). Muongofu mpya anachukuliwa kuwa muumini wa Kanisa baada ya ibada zote za ubatizo na uthibitisho kukamilishwa na kurekodiwa kikamilifu.

Uthibitisho upo chini ya maelekezo ya askofu. Hata hivyo, yeye haendeshi mahojiano tofauti kwa ajili ya uthibitisho.

Fanya kazi kwa ukaribu na askofu na kiongozi wa misheni wa kata (kama ameitwa) kuhakikisha kwamba waongofu wapya wamethibitishwa. Uthibitisho unapaswa kufanyika punde inapowezekana baada ya ubatizo, inapendekezwa Jumapili inayofuata. Hata hivyo, askofu anaweza kuruhusu uthibitisho ufanyike kwenye ibada ya ubatizo kama kuna hali ya upekee (ona Kitabu cha Maelekezo ya Jumla, 18.8).

Waongofu kwa kawaida wanathibitishwa katika mkutano wa sakramenti wa kata pale wanapoishi. Askofu kwa kawaida huwaalika wazee wamisionari wanaotumikia katika kata kushiriki katika uthibitisho. Kama mmisionari anafanya uthibitisho, yeye pia anahitaji idhini kutoka kwa rais wa misheni (ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla, 18.8.1). Angalau mshiriki mmoja wa uaskofu hushiriki.

Kamilisha Fomu ya Ubatizo na Uthibitisho

Ni muhimu kwamba kumbukumbu ya uumini itengenezwe punde tu baada ya mtu kubatizwa na kuthibitishwa. Kuhusu kumbukumbu kama hizo katika siku zake, Moroni aliandika kwamba waumini wapya, “walihesabiwa miongoni mwa watu wa kanisa la Kristo; na majina yao yalichukuliwa ili wakumbukwe na kulishwa na neno zuri la Mungu, kuwaweka katika njia nzuri” (Moroni 6:4).

Unapomfundisha mtu ambaye anajiandaa kubatizwa, anza kujaza Fomu ya Ubatizo na Uthibitisho katika app ya Hubiri Injili Yangu. Eleza kwamba fomu hii itatumika kutengeneza kumbukumbu ya uumini. Kumbukumbu hii itakuwa na taarifa muhimu kuhusu ibada mtu huyu anazozipokea. Wakati waumini wa Kanisa wanapohama, kumbukumbu zao za uumini zinahamishwa hadi kwenye kata yao mpya ili viongozi wenyeji na waumini waweze kuwasaidia.

Mara tu muumini mpya anapobatizwa na kuthibitishwa, sasisha fomu na taarifa kuhusu kila ibada, ikiwa ni pamoja na ni nani aliifanya. Wakati umekamilisha fomu, andika taarifa katika app ya Hubiri Injili Yangu na uiwasilishe kwa karani wa kata kieletroniki. Punde karani anapokuwa ameipokea fomu hii, anaipitia tena na anatengeneza kumbukumbu ya uumini.

Baada ya kumbukumbu ya uumini kutengenezwa, karani huandaa Cheti cha Ubatizo na Uthibitisho. Cheti hiki hutiwa saini na askofu na kutolewa kwa mtu huyu.

Jina na jinsia kwenye kumbukumbu ya uumini na cheti vinapaswa kufanana na cheti cha kuzaliwa, usajili wa uraia wa kuzaliwa, au jina la sasa kisheria.

Kujifunza Binafsi au na Mwenza

Jifunze Mosia 6:1–3 na Moroni 6:1–4. Ni kwa jinsi gani vifungu hivi vinahusiana na kuweka kumbukumbu sahihi za uthibitisho?

Baada ya Ubatizo na Uthibitisho

Endelea Kuhudumia

Endelea kufanya urafiki na kuwasaidia waumini wapya baada ya kubatizwa na kuthibitishwa. Wasaidie wahudhurie kanisani na wajenge mahusiano na waumini. Soma Kitabu cha Mormoni pamoja nao, na wasaidie washiriki injili na wanafamilia na marafiki. Watambulishe kwenye kijitabu cha Njia Yangu ya Agano. Endelea kutumia app ya Hubiri Injili Yangu kuandika maendeleo yao, kama vile uhudhuriaji wao kwenye mkutano wa sakramenti na masomo waliyopokea.

Picha
wanaume wakikumbatiana

Baada ya uthibitisho, fundisha tena masomo ya mmisionari. Unakuwa kiongozi katika kufundisha. Hata hivyo, ratibu pamoja na viongozi wa kata ili wamisionari wa kata au waumini wengine washiriki. Unapofundisha, wahimize waumini wapya watimize ahadi zote katika masomo haya.

Katika mikutano ya uratibu ya kila wiki, shaurianeni kuhusu jinsi waumini wanavyoweza kuwaunga mkono waongofu wapya na kuwasaidia wabaki kuwa washiriki hai katika Kanisa. Panga ni nani atawatambulisha wao kwa viongozi wa akidi au viongozi wa vikundi. Ratibu ushiriki wa waumini wengine wakati unapofundisha tena masomo. Omba wapangiwe akina kaka wahudumiaji (na akina dada wahudumiaji kwa ajili ya wanawake).

Baada ya mwanamume kuthibitishwa, yeye anastahili kupokea Ukuhani wa Haruni kama atakuwa na angalau umri wa miaka 12 kufikia mwisho wa mwaka. Utawazo wa Ukuhani wa Haruni unakuwa chini ya maelekezo ya askofu (ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla, 38.2.9.1).

Kama inavyofaa, wasiliana maisha yako yote na wale ambao uliwafundisha. Wasaidie katika kupokea baraka zote za injili ya Yesu Kristo.

Picha
Mzee Gerrit W. Gong

“Wakati tunapokuja na mioyo iliyopondeka na roho iliyovunjika, tunaweza kupata sauti katika Yesu Kristo, na kuzungukwa katika mikono Yake salama ya uelewa. Ibada takatifu hutoa mjumuisho wa agano na ‘nguvu za uungu’ za kutakasa dhamira ya ndani na matendo ya nje [Mafundisho na Maagano 84:20]. Pamoja na upendo Wake wa ukarimu na ustahimilivu, Kanisa Lake linakuwa Nyumba yetu ya Wageni” (Gerrit W. Gong, “Nafasi katika Nyumba ya Wageni,” Liahona, Mei 2021, 27).

Wasaidie Waumini Wapya Washiriki katika Baraka za Hekalu

Waumini wapya wa umri unaofaa wanaweza kupokea kibali cha hekaluni ambacho kinawasaidia kubatizwa kwa niaba ya wanafamilia waliokufa (ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla, 26.4.2). Wanapokea kibali hiki kutoka kwa askofu. Wahimize na uwasaidie waumini wapya wapate kibali cha hekaluni haraka iwezekanavyo. Kama hekalu lipo karibu, fikiria kutoa mwaliko kwa ajili ya muda mahususi kwa ajili ya waumini wapya kufanya ubatizo kwa niaba ya mababu waliokufa.

Katika mikutano ya uratibu ya kila wiki, panga ni nani atawatambulisha waumini wapya kwa kiongozi wa hekalu na historia ya familia wa kata. Kiongozi huyu anaweza kuwasaidia wajiandae kupokea baraka za hekaluni kwa kufanya maagano yao wenyewe ya hekaluni.


Mawazo kwa ajili ya Kujifunza na Kutumia

Kujifunza Binafsi

  • Orodhesha changamoto ambazo anayetarajia kubatizwa anaweza kukabiliana nazo. Kwa nini ni muhimu kwamba mtu huyu ahisi upendo na urafiki wa waumini wa Kanisa?

  • Jifunze Moroni 6 na Mafundisho na Maagano 20:68–69. Ni kipi unaweza kujifunza kutoka kwenye mistari hii kuhusu kuwasaidia watu wajiandae kwa ajili ya ubatizo na uthibitisho? Andika kile unachojifunza. Shiriki mawazo yako na mwenza wako wakati wa kujifunza na mmisionari mwenza.

Kujifunza pamoja na Mwenza na Kubadilishana Mwenza

  • Rais Henry B. Eyring, alieleza kwa nini viwango vya injili ni muhimu. Jadilini ushauri ufuatao. Ni jinsi gani mnaweza kuwahimiza watu wavifikie viwango hivi?

    “Bwana aliweka viwango Vyake ili kwamba Yeye aweze kutubariki. Fikirieni kuhusu baraka hizo: Yeye anawaahidi wale ambao wanafikia viwango hivi msaada wa Roho Mtakatifu. Yeye anaahidi amani binafsi. Yeye anaahidi nafasi ya kupokea ibada takatifu katika nyumba Yake. Na Yeye anawaahidi wale ambao wanavumilia katika kuishi viwango Vyake watapata uzima wa milele. …

    “Kwa sababu tunawapenda watu tunaowatumikia, sisi sote tunataka kufanya vyema katika kuwainua watoto wa Baba yetu wa Mbinguni hadi kufikia uaminifu na usafi wanaouhitaji ili kupata baraka zote za Bwana. …

    “… Unaanza kwa kushikilia viwango vya Bwana kwa uwazi na bila kuogopa. Na kadiri zaidi ulimwengu unavyosonga mbali na viwango hivyo na kuvidharau, ndivyo zaidi unavyokuwa jasiri zaidi katika kufanya hivyo” (“Standards of Worthiness,” First Worldwide Leadership Training Meeting, Jan. 2003, 10–11).

  • Pitia tena maswali yote ya mahojiano ya ubatizo. Fikiria jinsi ambavyo ungeweza kushughulikia hali kama zifuatazo:

    • Mtu hakukuambia kwamba alikuwa chini ya uangalizi kwa ajili ya kosa la jinai.

    • Mtu hajapokea jibu la sala kwamba Joseph Smith alikuwa nabii.

    • Mtu alivuta sigara siku mbili zilizopita.

    • Mtu hana hakika kwamba amepokea jibu la sala zake.

    • Familia ilihisi shinikizo kutoka kwa marafiki na hawakuwa na uhakika wa kuwa tayari kubatizwa.

  • Pitia Tena Fomu ya Ubatizo na Uthibitisho. Kwa nini taarifa unazotoa zinapaswa kuwa sahihi na kamili?

Baraza la Wilaya, Mikutano ya Kanda na Baraza la Uongozi la Misheni

  • Pitia tena umuhimu wa mahojiano ya ubatizo. Jadili jinsi wamisionari wanavyoweza kuwasaidia watu wajiandae kwa ajili ya mahojiano.

  • Jadili jinsi ya kutumia ibada za ubatizo na uthibitisho kama fursa.

Viongozi wa Misheni na Washauri wa Misheni

  • Fanya kazi na viongozi wenyeji wa ukuhani na viongozi wa vikundi ili kuhahikisha wanatumia ripoti ya Maendeleo ya Njia ya Agano ifaavyo.

  • Wafundishe viongozi wa wilaya, viongozi wa kanda, na viongozi wa mafunzo ya akina dada jinsi ya kuwaandaa watu kwa ajili ya mahojiano ya ubatizo. Waalike wawafundishe wamisionari wengine kuwaandaa watu kwa ajili ya mahojiano haya.

  • Wafundishe viongozi wa wilaya na kanda jinsi ya kuendesha mahojiano ya ubatizo.

  • Wafundishe jinsi ya kujibu mahojiano ya ubatizo wakati mtu anapoonesha kwamba alitenda dhambi kubwa.

  • Pale inapowezekana, hudhuria ibada za ubatizo kwa ajili ya waumini wapya. Zungumza na waumini wapya na jifunze kuhusu uzoefu wa uongofu wao. Shiriki kile unachojifunza pamoja na mwenza wako na wamisionari wengine.