Maandiko Matakatifu
3 Nefi 15


Mlango wa 15

Yesu anatangaza kwamba sheria ya Musa imetimizwa katika Yeye—Wanefi ndiyo wale kondoo wengine ambao Yeye alizungumzia akiwa Yerusalemu—Kwa sababu ya uovu, watu wa Bwana katika Yerusalemu hawajui kuhusu kondoo waliotawanywa wa Israeli. Karibia mwaka 34 B.K.

1 Na sasa ikawa kwamba wakati Yesu alipokuwa amemaliza maneno haya alizungusha macho yake karibu hapo kwa umati, na akawaambia: Tazameni, mmesikia vitu ambavyo nilifundisha kabla ya kupaa juu kwa Baba yangu; kwa hivyo, yeyote akumbukaye maneno haya yangu na kuyafanya, yeye nitamwinua juu katika siku ya mwisho.

2 Na ikawa kwamba wakati Yesu alipokuwa amesema maneno haya aliona kwamba kulikuwa na wengine miongoni mwao ambao walistaajabu, na kushangaa kile alichotaka kufanya na sheria ya Musa; kwani hawakuelewa msemo uliosema kwamba vitu vya kale vilikuwa vimepita, na kwamba vitu vyote vilikuwa vimekuwa vipya.

3 Na akawaambia: Msistaajabu kwamba nilisema vitu vya kale vilikuwa vimepita, na kwamba vyote vilikuwa vimekuwa vipya.

4 Tazama, ninawaambia kwamba sheria imetimizwa ambayo alipewa Musa.

5 Tazama, ni mimi niliyempa ile sheria, na ni mimi niliyeagana na watu wangu Israeli; kwa hivyo, sheria imetimizwa ndani yangu, kwani nimekuja kutimiza sheria; kwa hivyo imefika mwisho.

6 Tazama, siharibu maandishi ya manabii, kwani kadiri mengi ambayo hayajatimizwa ndani yangu, kweli nawaambia, yote yatatimizwa.

7 Na kwa sababu niliwaambia kwamba vitu vya kale vimepita, siharibu ile ambayo imezungumzwa kuhusu vitu ambavyo vinakuja.

8 Kwani tazama, agano ambalo nimefanya na watu wangu lote halijatimizwa; lakini sheria ambayo ilipewa Musa imemalizika kwa sababu yangu.

9 Tazama, Mimi ndiye sheria, na nuru. Nitazameni mimi, na mvumilie hadi mwisho, na mtaishi; kwani kwa yule ambaye huvumilia hadi mwisho nitampatia uzima wa milele.

10 Tazama, nimewapatia amri; kwa hivyo tiini amri zangu. Na hii ni sheria na maandishi ya manabii, kwani walinishuhudia kwa ukweli.

11 Na sasa ikawa kwamba wakati Yesu alipokuwa amezungumza maneno haya, aliwaambia wale kumi na wawili ambao alikuwa amewachagua:

12 Ninyi ni wanafunzi wangu; na ninyi ni nuru kwa hawa watu, ambao ni baki la nyumba ya Yusufu.

13 Na tazama, hii ni nchi ya urithi wenu; na Baba amewapatia.

14 Na kamwe hakuna wakati wowote ambao Baba amenipatia amri kwamba niwaambie ndugu zenu katika Yerusalemu.

15 Wala katika muda wowote Baba hajanipa amri kwamba niwaambie kuhusu makabila mengine ya nyumba ya Israeli, ambao Baba amewaongoza mbali kutoka nje ya nchi.

16 Hiki kiasi Baba aliniamuru, kwamba ningewaambia:

17 Kwamba kondoo wengine ninao ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta, na watasikia sauti yangu; na kutakuwa na kundi moja, na mchungaji mmoja.

18 Na sasa, kwa sababu ya shingo ngumu na kutoamini, hawakuelewa maneno yangu; kwa hivyo, niliamrishwa na Baba nisiwaambie zaidi kuhusu kitu hiki.

19 Lakini kweli, nawaambia kwamba Baba ameniamuru, na nawaambia kwamba mlitenganishwa kutoka miongoni mwao kwa sababu ya uovu wao; kwa hivyo ni sababu ya uovu wao kwamba hawajui chochote kuwahusu.

20 Na kweli, nawaambia tena kwamba makabila mengine yametengwa na Baba kutoka kwao; na ni kwa sababu ya uovu wao kwamba hawajui chochote kuwahusu.

21 Na kweli nawaambia, kwamba ni ninyi ambao nilisema: Kondoo wengine ninao ambao sio wa zizi hili; hao nao ninapaswa kuwaleta, na watasikia sauti yangu; na kutakuwa na kundi moja, na mchungaji mmoja.

22 Na hawakunielewa, kwani walidhani kwamba nilizungumza kuhusu Wayunani; kwani hawakuelewa kwamba Wayunani watageuka kupitia mahubiri yao.

23 Na hawakunielewa kwamba nilisema wataelewa sauti yangu; na hawakunielewa kwamba Wayunani hawataisikia sauti yangu wakati wowote—kwamba sitajidhihirisha kwao isipokuwa kupitia kwa Roho Mtakatifu.

24 Lakini tazama, nyote mmesikia sauti yangu, na kuniona; na ninyi ni kondoo wangu, na mmehesabiwa miongoni mwa wale ambao Baba amenipatia.