Maandiko Matakatifu
Moroni 7


Mlango wa 7

Karibisho linapewa kuingia kwenye makao ya Bwana—Ombeni na nia ya kweli—Roho wa Kristo huwezesha watu kujua mema na maovu—Shetani anawashawishi watu wamkane Kristo na wafanye uovu—Manabii wanadhihirisha kuja kwa Kristo—Kwa imani, miujiza hufanyika na malaika wanahudumu—Watu wanapaswa kutumaini uzima wa milele na kuambatana kwenye hisani. Karibia mwaka 401–421 B.K.

1 Na sasa mimi, Moroni, naandika machache ya maneno ya baba yangu Mormoni, ambayo alisema kuhusu imani, tumaini, na hisani; kwani hii ndiyo njia aliyozungumza kwa watu, wakati alipowafundisha katika sinagogi ambayo walikuwa wamejenga kama mahali pa kuabudu.

2 Na sasa mimi, Mormoni, nazumgumza kwenu ndugu zangu wapendwa; na ni kwa neema ya Mungu Baba, na Bwana wetu Yesu Kristo, na mapenzi yake matakatifu, kwa sababu ya karama yake kuniita, kwamba nimekubaliwa kuzungumza kwenu wakati huu.

3 Kwa hivyo, ningewazungumzia wale ambao ni wa kanisa, ambao ni wafuasi wa imani ya Kristo, ambao wamepata tumaini la kutosha ambalo kwalo mnaweza kuingia kwenye makao ya Bwana, kutoka wakati huu kwenda mbele mpaka mtakapopumzika na yeye mbinguni.

4 Na sasa ndugu zangu, nahukumu vitu hivi kwenu kwa sababu ya matembezi yenu matulivu na watoto wa watu.

5 Kwani nakumbuka neno la Mungu ambalo linasema kwa matunda yao mtawatambua; kwani kama matunda yao ni mema, basi ni wema pia.

6 Kwani tazama, Mungu amesema mtu akiwa mwovu hawezi kufanya yale ambayo ni mema; kwani ikiwa atatoa karama, au kuomba kwa Mungu, isipokuwa aifanye kwa kusudi jema haimfaidii chochote.

7 Kwani tazama, haihesabiwi kwake kwa haki.

8 Kwani tazama, ikiwa mtu mwovu anatoa zawadi, huifanya bila kupenda; kwa hivyo inahesabiwa kwake sawa kama angeiweka ile zawadi; kwa hivyo anadhaniwa mwovu mbele ya Mungu.

9 Na kadhalika huhesibiwa pia uovu kwa mtu, ikiwa ataomba bila nia kamili ya moyo; ndiyo, na haimfaidii chochote, kwani Mungu hampokei yeyote wa aina hii.

10 Kwa hivyo, mtu akiwa mwovu hawezi kufanya kile ambacho ni chema; wala hawezi kutoa karama nzuri.

11 Kwani tazama, chimbuko chungu haliwezi kutoa maji mazuri; wala chimbuko zuri haliwezi kutoa maji chungu; kwa hivyo, mtu akiwa mtumishi wa ibilisi hawezi akamfuata Kristo; na akiwa anamfuata Kristo hapo hawezi akawa mtumishi wa ibilisi.

12 Kwa hivyo, vitu vyote vilivyo vizuri vinatoka kwa Mungu; na kile kilicho kiovu hutoka kwa ibilisi; kwani ibilisi ni adui wa Mungu, na hupigana dhidi yake siku zote, na hukaribisha na hushawishi kufanya dhambi, na kufanya kile kilicho kiovu siku zote.

13 Lakini tazama, kile kilicho cha Mungu hukaribisha na hushawishi kufanya mema siku zote; kwa hivyo, kila kitu kinachokaribisha na kushawishi kufanya mema, na kumpenda Mungu, na kumtumikia, kinaongozwa na Mungu.

14 Kwa hivyo, muwe waangalifu, ndugu zangu wapendwa, kwamba msione kile ambacho ni kiovu kuwa cha Mungu, au kile ambacho ni kizuri na cha Mungu kuwa cha ibilisi.

15 Kwani tazama, ndugu zangu, mmepewa uhuru kuhukumu, kwamba mjue mema na maovu; na njia ya kuhukumu ni wazi, kwamba mjue na ufahamu kamili, kama mwangaza wa mchana kutoka kwa giza la usiku.

16 Kwani tazama, Roho ya Kristo imetolewa kwa kila mtu, ili ajue mema na maovu; kwa hivyo, ninawaonyesha njia ya kuhukumu; kwani kila kitu kinachokaribisha kufanya mema, na kushawishi kuamini katika Kristo, kinasababishwa na uwezo na thawabu ya Kristo; kwa hivyo mngejua na ufahamu kamili kwamba ni cha Mungu.

17 Lakini kitu chochote ambacho hushawishi watu kufanya maovu, na kutoamini katika Kristo, na kumkana, na kutomtumikia Mungu, hapo mtajua na ufahamu kamili kwamba ni cha ibilisi; kwani kwa njia hii ndiyo ibilisi hufanya kazi, kwani hamshawishi mtu yeyote kufanya mema, la, sio mmoja; wala malaika wake; wala wale ambao hujiweka chini yake.

18 Na sasa, ndugu zangu, nikiona kwamba mnajua nuru ambayo kwake mnaweza kuhukumu, nuru ambayo ni nuru ya Kristo, mhakikishe kwamba hamhukumu kwa makosa; kwani hukumu ile mnayohukumu nayo ndiyo mtakayohukumiwa.

19 Kwa hivyo, ninawasihi ninyi, ndugu, kwamba mtafute kwa bidii katika nuru ya Kristo kwamba mngejua mema na maovu; na ikiwa utashikilia kila kitu kizuri, na usilaumu, hapo utakuwa bila shaka mtoto wa Kristo.

20 Na sasa, ndugu zangu, inawezekanaje kwamba mshikilie kila kitu kizuri?

21 Na sasa naja kwa ile imani, ambayo nilisema nitaizungumzia; na nitawaambia njia ambayo kwake mnaweza kushikilia kwa kila kitu kizuri.

22 Kwani tazama, Mungu akijua vitu vyote, akiwa amekuwepo kutoka milele hadi milele, tazama, alimtuma malaika kuhudumu kwa watoto wa watu, kuwajulisha kuhusu kuja kwa Kristo; na katika Kristo kutatokea kila kitu kizuri.

23 Na Mungu pia aliwatangazia manabii, kwa mdomo wake mwenyewe, kwamba Kristo sharti aje.

24 Na tazama, kulikuwa na njia tofauti ambazo kwake alijulisha vitu kwa watoto wa watu, ambavyo vilikuwa vyema; na vitu vyote ambavyo ni vyema hutoka kwa Kristo; la sivyo watu wangebaki kwenye hali ya kuanguka, na hakuna kitu chochote kizuri ambacho kingewajia.

25 Na kwa hivyo, kwa huduma ya malaika, na kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu, watu walianza kutenda imani katika Kristo; na hivyo kwa imani, walishikilia kila kitu kizuri; na hivi ndivyo ilivyokuwa mpaka kuja kwa Kristo.

26 Na baada ya yeye kuja watu pia waliokolewa kwa imani katika jina lake; na kwa kupitia kwa imani, wakawa wana wa Mungu. Na kwa kweli kadiri Kristo aishivyo alisema maneno haya kwa babu zetu, akisema: Kitu chochote mtakachomwuliza Baba katika jina langu, ambacho ni kizuri, kwa imani mkiamini kwamba mtapata, tazama, mtakipokea.

27 Kwa hivyo, ndugu zangu wapendwa, je, miujiza imekoma kwa sababu Kristo amepanda mbinguni, na ameketi mkono wa kulia wa Mungu, kudai kutoka kwa Baba haki zake za huruma ambazo anazo juu ya watoto wa watu?

28 Kwani amejibu mwisho wa sheria, na hudai wale wote ambao wana imani ndani yake; na wale ambao wana imani ndani yake watajishikilia kwa kila kitu kizuri; kwa hivyo huzungumza akipendelea watoto wa watu; na huishi mbinguni milele.

29 Na kwa sababu amefanya hivi, ndugu zangu wapendwa, je, miujiza imekoma? Tazama ninawaambia, La; wala malaika hawajakoma kuwahudumia watoto wa watu.

30 Kwani tazama, wako chini yake, kuhudumu kulingana na neno la amri yake, wakijidhihirisha kwa wale walio na imani ya nguvu na akili imara katika kila kitu cha uchamungu.

31 Na kazi ya huduma yao ni kuita watu katika toba, na kutimiza na kufanya kazi ya agano la Baba, ambalo amefanya kwa watoto wa watu, kutayarisha njia miongoni mwa watoto wa watu, kwa kutangaza neno la Kristo kwa vyombo viteule vya Bwana, kwamba wangekuwa na ushahidi kumhusu.

32 Na kwa kufanya hivyo, Bwana Mungu hutayarisha njia kwamba watu wengine wangekuwa na imani katika Kristo, kwamba Roho Mtakatifu angekuwa na mahali katika mioyo yao, kulingana na uwezo alio nao; na kwa njia hii ndiyo Baba hutimiza, maagano ambayo amefanya kwa watoto wa watu.

33 Na Kristo amesema: Ikiwa mtakuwa na imani ndani yangu mtakuwa na uwezo wa kufanya kitu chochote ambacho ni cha kufaa kwangu.

34 Na amesema: Tubuni enyi miisho ya dunia, na mje kwangu, na mbatizwe katika jina langu, na muwe na imani ndani yangu, ili muokolewe.

35 Na sasa, ndugu zangu wapendwa, ikiwa hivi ndivyo itakuwa kwamba vitu hivi ni kweli ambavyo nimewazungumzia, na Mungu atawaonyesha, kwa uwezo na fahari kuu katika siku ya mwisho, kwamba ni kweli, na ikiwa ni kweli, je, wakati wa miujiza umekoma?

36 Au malaika wamekoma kuonekana kwa watoto wa watu? Au amesimamisha uwezo wa Roho Mtakatifu kutoka kwao? Au atasimamisha, kadiri muda utakapokuwepo au dunia itakapokuwepo, au kutakuwa na mtu mmoja juu ya uso wake kuokolewa?

37 Tazama ninawaambia, La; kwani ni kwa imani kwamba miujiza hufanyika; na ni kwa imani kwamba malaika huonekana na kuhudumia watu; kwa hivyo, kama vitu hivi vimekoma msiba uwe kwa watoto wa watu, kwani ni kwa sababu ya kutoamini, na yote ni bure.

38 Kwani hakuna atakayeokoka, kulingana na maneno ya Kristo, isipokuwa awe na imani katika jina lake; kwani, ikiwa hivi vitu vimekoma, basi imani imekoma pia; na kutisha ni hali ya mtu, kwani ni kama hakujakuwepo na ukombozi uliofanywa.

39 Lakini tazama, ndugu zangu wapendwa, ninaweza kuona vitu vyema zaidi kwenu, kwani ninaona kwamba mna imani katika Kristo kwa sababu ya uvumilivu wenu; kwani kama hamna imani ndani yake hamfai kuhesabiwa miongoni mwa watu wa kanisa lake.

40 Na tena, ndugu zangu wapendwa, ninataka kuwazungumzia kuhusu tumaini. Inawezekanaje kwamba mtafikia imani, isipokuwa muwe na tumaini?

41 Na ni kitu gani mtakachotumainia? Tazama nawaambia kwamba mtakuwa na tumaini kupitia upatanisho wa Kristo na uwezo wa kufufuka kwake, kuinuliwa kwa maisha ya milele, na hii kwa sababu ya imani yenu kwake kulingana na ile ahadi.

42 Kwa hivyo, ikiwa mtu ana imani lazima ahitaji kuwa na tumaini; kwani bila imani hakuwezi kuwepo na tumaini lolote.

43 Na tena, tazama ninawaambia kwamba hawezi kuwa na imani na tumaini, isipokuwa awe mnyenyekevu, na mpole katika moyo.

44 Ikiwa hivyo, imani na tumaini lake ni bure, kwani hakuna yeyote anayekubaliwa mbele ya Mungu, isipokuwa yule aliye myenyekevu na mpole katika moyo; na mtu akiwa myenyekevu na mpole katika moyo, na kukiri kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwamba Yesu ni Kristo, lazima awe na ahisani; kwani kama hana hisani yeye si kitu; kwa hivyo lazima awe na hisani.

45 Na hisani huvumilia, na ni karimu, na haina wivu, na haijivuni, haitafuti mambo yake, haifutuki kwa upesi, haifikirii mabaya, na haifurahii uovu lakini hufurahi katika ukweli, huvumilia vitu vyote, huamini vitu vyote, hutumaini vitu vyote, hustahamili vitu vyote.

46 Kwa hivyo, ndugu zangu wapendwa, kama hamna hisani, ninyi si kitu, kwani hisani haikosi kufaulu kamwe. Kwa hivyo, ambatana na hisani, ambayo ni kubwa kuliko yote, kwani vitu vyote lazima vishindwe—

47 Lakini hisani ni upendo msafi wa Kristo, na inavumilia milele; na yeyote atakayepatikana nayo katika siku ya mwisho, itakuwa vyema kwake.

48 Kwa hivyo, ndugu zangu wapendwa, ombeni kwa Baba kwa nguvu zote za moyo, kwamba mjazwe na upendo huu, ambao ametoa kwa wote ambao ni wafuasi wa kweli wa Mwana wake, Yesu Kristo; ili muwe wana wa Mungu; kwamba wakati atakapoonekana tutakuwa kama yeye, kwani tutamwona vile alivyo; ili tuwe na tumaini hili; ili tutakaswe hata vile alivyo mtakatifu. Amina.