Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 21


Sehemu ya 21

Ufunuo uliotolewa kwa Joseph Smith, Nabii, huko Fayette, New York, 6 Aprili 1830. Ufunuo huu ulitolewa wakati wa kuanzisha Kanisa, katika tarehe iliyotajwa, katika nyumba ya Peter Whitmer Mkubwa. Wanaume sita, ambao walibatizwa hapo awali, walishiriki. Kwa kura nyingi watu hawa walionyesha kutaka kwao na dhamira ya kulianzisha, kulingana na amri ya Mungu (ona sehemu ya 20). Pia walipiga kura ya kuwakubali na kuwaunga mkono Joseph Smith Mdogo na Oliver Cowdery kama maofisa viongozi wa Kanisa. Kwa njia ya kuwawekea mikono, Joseph akamtawaza Oliver kuwa mzee wa Kanisa, na Oliver naye vile vile akamtawaza Joseph. Baada ya huduma ya Sakramenti, Joseph na Oliver wakawawekea mikono kila mtu aliyeshiriki kwa ajili ya kuwapa Roho Mtakatifu na kwa ajili ya uthibitisho wa kila mmoja kama muumini wa Kanisa.

1–3, Joseph ameitwa kuwa mwonaji, mfasiri, nabii, mtume, na mzee; 4–8, Neno lake litaiongoza kusudi la Sayuni; 9–12, Watakatifu wataamini maneno yake atakavyoongea akiwa anaongozwa na Mfariji.

1 Tazama, pawepo na kumbukumbu itakayotunzwa miongoni mwenu; ambamo ndani yake utaitwa mwonaji, mfasiri, nabii, mtume wa Yesu Kristo, mzee wa kanisa kwa njia ya mapenzi ya Mungu Baba, na neema ya Bwana wenu Yesu Kristo,

2 Ukiwa unaongozwa na Roho Mtakatifu katika kuweka msingi wake, na kulijenga juu ya imani iliyo takatifu sana.

3 Kanisa ambalo liliundwa na kuanzishwa katika mwaka wa Bwana wenu elfu moja mia nane na thelathini, katika mwezi wa nne, na siku ya sita ya mwezi ambao unaitwa Aprili.

4 Kwa hivyo, nikimaanisha kanisa, nawe utayaangalia maneno yake yote na amri ambazo atazitoa kwenu kadiri atakavyozipokea, mkitembea katika utakatifu mbele zangu;

5 Kwani neno lake mtalipokea, kama vile linatoka kinywani mwangu, katika uvumilivu wote na imani yote.

6 Kwani kwa kufanya mambo haya milango ya jehanamu haitawashinda; ndiyo, na Bwana Mungu atazitawanya nguvu za giza kutoka mbele zako, naye atasababisha mbingu zitetemeke kwa ajili yenu, na kwa utukufu wa jina lake.

7 Kwani hivyo ndivyo asemavyo Bwana Mungu: Yeye nimemwongoza kuendesha kusudi la Sayuni katika uwezo mwingi kwa ajili ya mema, na juhudi yake ninaijua, na sala zake nimezisikia.

8 Ndiyo, maombolezo yake kwa ajili ya Sayuni nimeyaona, na Mimi nitasababisha kwamba asiomboleze tena kwa ajili yake; kwani siku zake za kufurahi zimekuja kwa ondoleo la dhambi zake, na kufunua baraka zangu juu ya kazi zake.

9 Kwani, tazama, Mimi nitawabariki wale wote watakaofanya kazi katika shamba langu la mizabibu kwa baraka kuu, na wao watayaamini maneno yake, ambayo yanatolewa kwake kutoka kwangu na Mfariji, ambaye hufunulia kwamba Yesu alisulubishwa na watu wenye dhambi kwa ajili ya dhambi za ulimwengu, ndiyo, kwa ajili ya ondoleo la dhambi na kwa wenye moyo uliopondeka.

10 Kwa hiyo nimeona ni muhimu kwa yeye kutawazwa na wewe, Oliver Cowdery mtume wangu;

11 Hii ikiwa ni ibada kwako wewe, kwamba wewe u mzee chini ya mkono wake, akiwa wa kwanza mbele yako wewe, kwamba uwe mzee katika kanisa hili la Kristo, lililo na jina langu—

12 Na mhubiri wa kwanza wa kanisa hili kwa ajili ya kanisa, na mbele ya ulimwengu, ndiyo, mbele ya Wayunani; ndiyo, na hivyo ndivyo asemavyo Bwana Mungu, lo, lo! na kwa Wayahudi pia. Amina.