Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 33


Sehemu ya 33

Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii kwa Ezra Thayre na Northrop Sweet, huko Fayette, New York, Oktoba 1830. Katika kuutambulisha ufunuo huu, historia ya Joseph Smith inatilia mkazo kuwa “Bwana … daima yuko tayari kuwaelekeza wale wenye kumtafuta kwa bidii na katika imani.”

1–4, Wafanyakazi wameitwa kuhubiri injili katika ile saa kumi na moja; 5–6, Kanisa limeanzishwa, na wateule watakusanywa; 7–10, Tubuni, kwani ufalme wa mbingu umekaribia; 11–15, Kanisa limejengwa juu ya mwamba wa injili; 16–18, Jitayarisheni kwa ujio wa Bwana harusi.

1 Tazama, ninawaambia, watumishi wangu Ezra na Northrop, fungueni masikio yenu, na sikilizeni sauti ya Bwana Mungu wenu, ambaye neno lake li hai na lenye nguvu, tena lina ukali kuliko upanga ukatao kuwili, hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.

2 Kwani amini, amini, ninawaambia, kwamba mmeitwa kuzipaza sauti zenu kama parapanda, mkiitangaza injili yangu kwa kizazi hiki chenye ila na ukaidi.

3 Kwani tazameni, shamba li jeupe tayari kwa mavuno; na ni saa kumi na moja, na ni mara ya mwisho ambayo nitawaita wafanyakazi katika shamba langu la mizabibu.

4 Na shamba langu la mizabibu limeharibiwa kabisa; na hakuna hata mmoja atendaye mema ila wachache tu; na wao hukosea mara nyingi kwa sababu ya makuhani wa uongo, wote wamekuwa na mawazo maovu.

5 Na amini, amini, ninawaambia, kuwa kanisa hili nimelianzisha na kulitoa kutoka nyikani.

6 Na hata hivyo ndivyo nitakavyowakusanya wateule wangu kutoka pande nne za dunia, hata wengi kadiri watakaoniamini Mimi, na kuisikiliza sauti yangu.

7 Ndiyo, amini, amini, ninawaambia, kwamba shamba li jeupe tayari kwa mavuno; kwa sababu hiyo, ingizeni mundu zenu, na mvune kwa nguvu, akili na uwezo wenu wote.

8 Fumbueni vinywa vyenu navyo vitajazwa, nanyi mtakuwa kama Nefi wa kale, aliyesafiri kutoka Yerusalemu katika nyika.

9 Ndiyo, fumbueni vinywa vyenu, na wala msiache, na mtachukua miganda migongoni mwenu, kwani lo Mimi ni pamoja nanyi.

10 Ndiyo, fumbueni vinywa vyenu navyo vitajazwa, mkisema: Tubuni, tubuni na itayarisheni njia ya Bwana, na yanyoosheni mapito yake; kwani ufalme wa mbinguni u karibu;

11 Ndiyo, tubuni na mkabatizwe, kila mmoja wenu, kwa ondoleo la dhambi zenu; ndiyo, mkabatizwe hata kwa maji, na halafu waja ubatizo wa moto na wa Roho Mtakatifu.

12 Tazameni, amini, amini, ninawaambia, hii ndiyo injili yangu; na kumbukeni kwamba wawe na imani katika mimi au vinginevyo hawataokolewa;

13 Na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; ndiyo, juu ya mwamba huu ninyi mmejengwa, na kama mtaendelea, milango ya jehanamu haitawashinda.

14 Na ninyi kumbukeni kushika kanuni na maagano ya kanisa.

15 Na yeyote atakayekuwa na imani mtamthibitisha katika kanisa langu, kwa kumwekea mikono, nami nitampa kipawa cha Roho Mtakatifu.

16 Na Kitabu cha Mormoni na maandiko matakatifu yanatolewa na mimi kwa ajili ya maelekezo yenu; na uwezo wa Roho wangu ndiye atiaye uzima vitu vyote.

17 Kwa sababu hiyo, kuweni waaminifu, na mkisali daima, mkitengeneza na kuziwasha taa zenu, mkiwa pamoja na mafuta yake, ili kwamba muweze kuwa tayari Bwana harusi ajapo—

18 Kwani tazameni, amini, amini, ninawaambia, kwamba naja upesi. Hivyo ndivyo. Amina.