Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 59


Sehemu ya 59

Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii, katika Sayuni, huko Wilayani Jackson, Missouri, 7 Agosti 1831. Kabla ya ufunuo huu, ardhi ilikuwa imekwisha tengwa kwa ajili ya dini, kama vile Bwana alivyoelekeza, na kiwanja kwa ajili ya hekalu la baadaye kiliwekwa wakfu. Katika siku ambayo ufunuo huu ulipokelewa, Polly Knight mke wa Joseph Knight Mkubwa alifariki, Muumini wa kwanza wa Kanisa kufariki katika Sayuni. Waumini wa mwanzoni waliuita ufunuo huu kama “wenye kuwaelekeza Watakatifu namna ya kuishika Sabato na namna ya kufunga na kusali.”

1–4, Watakatifu waaminifu katika Sayuni watabarikiwa; 5–8, Watampenda na kumtumikia Bwana na kushika amri Zake; 9–19, Kwa kushika kitakatifu siku ya Bwana, Watakatifu wanabarikiwa kimwili na kiroho; 20–24, Wenye haki wanaahidiwa amani katika ulimwengu huu na uzima wa milele katika ulimwengu ujao.

1 Tazama, heri, asema Bwana, wale ambao wamekuja katika nchii hii jicho lao likiwa kwenye utukufu wangu pekee, kulingana na amri zangu.

2 Kwani wale waishio watairithi nchi, na wale wanaokufa watapata kupumzika kutoka kwa kazi zao zote, na matendo yao yatafuatana nao; na watapokea taji katika nyumba ya Baba yangu, ambayo nimeitayarisha kwa ajili yao.

3 Ndiyo, heri wale ambao miguu yao inasimama juu ya ardhi ya Sayuni, ambao wameitii injili yangu; kwani watapokea kama ujira wao mambo mema ya nchi, nayo itawazalia kwa wingi.

4 Nao pia watavikwa taji la baraka kutoka juu, ndiyo, na amri zisizo haba, na pamoja na mafunuo katika wakati wao—wale walio waaminifu na wenye bidii mbele zangu.

5 Kwa hiyo, ninawapa amri, nikisema: Nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa uwezo wako wote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote; na katika jina la Yesu Kristo utamtumikia yeye.

6 Nawe mpende jirani yako kama nafsi yako. Usiibe; wala usizini, wala usiue, wala usifanye chochote kinachofanana na hayo.

7 Nawe utamshukuru Bwana Mungu wako katika mambo yote.

8 Nawe utamtolea dhabihu Bwana Mungu wako katika haki, hata ile ya moyo uliovunjika na roho iliyopondeka.

9 Na ili ujilinde na dunia pasipo mawaa, utakwenda kwenye nyumba ya sala na kutoa sakramenti zako katika siku yangu takatifu;

10 Kwani amini hii ndiyo siku iliyoteuliwa kwako kupumzika kutokana na kazi zako, na utoe dhabihu zako za shukrani kwa Aliye Juu Sana;

11 Hata hivyo nadhiri zako zitatolewa katika haki siku zote na kwa nyakati zote;

12 Lakini kumbuka kuwa katika siku hii, siku ya Bwana, utatoa sadaka na sakramenti zako kwa Aliye Juu Sana, ukiungama dhambi zako kwa ndugu zako, na mbele za Bwana.

13 Na katika siku hii hutafanya kitu kingine chochote, isipokuwa chakula chako tu na kitengenezwe kwa moyo mmoja ili kufunga kwako kuweze kukamilika, au, katika maneno mengine, shangwe yako iweze kuwa timilifu.

14 Amini, huku ndiyo kufunga na kusali, au kwa maneno mengine, kufurahi na sala.

15 Na kadiri mtakavyofanya mambo haya kwa shukrani, pamoja na mioyo na nyuso zenye furaha, pasipo na vicheko vingi, kwani hii ni dhambi, bali kwa moyo wenye furaha na uso mchangamfu—

16 Amini ninasema, kwamba kadiri mtakavyofanya hivi, vyote viijazavyo dunia ni mali yenu, wanyama wa mwituni na ndege wa angani, kile kipandacho juu ya miti na kitembeacho juu ya nchi;

17 Ndiyo, na mimea, na vitu vizuri vimeavyo kutoka ardhini, viwe kwa chakula au kwa mavazi, au kwa nyumba, au kwa maghala, au kwa bustani ya miti ya matunda, au kwa bustani ya mbogamboga, au kwa shamba la mizabibu;

18 Ndiyo, vitu vyote vimeavyo kutoka ardhini, katika majira yake, vimefanywa kwa faida na matumuzi ya mwanadamu, kwa kuridhisha jicho na kufurahisha moyo;

19 Ndiyo, kwa ajili ya chakula na mavazi, kwa kuonja na kunusa, ili kuuimarisha mwili na kuchangamsha nafsi.

20 Na imempendeza Mungu kwamba ametoa vitu hivi vyote kwa mwanadamu; kwani ni kwa sababu hii vilifanywa ili vitumiwe, kwa hekima, siyo ufujaji, wala siyo kwa kutumia nguvu.

21 Na katika lolote mwanadamu hamkosei Mungu, au ghadhabu ya Mungu haiwaki kwa yeyote, isipokuwa wale tu wasiokiri mkono wake katika mambo yote, na wasiotii amri zake.

22 Tazama, hii ni kulingana na sheria na manabii; kwa hiyo, usinisumbue tena juu ya jambo hili.

23 Lakini, jifunzeni kwamba yule afanyaye kazi za haki atapokea ujira wake, hata amani katika ulimwengu huu, na uzima wa milele katika ulimwengu ujao.

24 Mimi, Bwana, nimeyasema haya, na Roho anayashuhudia. Amina.