Mkutano Mkuu
Kubarikiwa Sana na Bwana
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2020


Kubarikiwa Sana na Bwana

Nyakati za masumbuko na kuvunjika moyo hazibadilishi jicho la uangalizi la Bwana pale kwa upendeleo Anapotutazama, Anapotubariki.

Siku moja miaka iliyopita, kama wamisionari vijana tukitumikia katika tawi dogo katika kisiwa kidogo cha Amami Oshima, Japan, mimi na mmisionari mwenza tulikuwa na furaha kujua kwamba Rais Spencer W. Kimball angezuru Asia na kwamba waumini na wamisionari wote wa Japan walialikwa Tokyo ili kumsikiliza nabii kwenye mkutano wa eneo. Tukishirikiana na waumini wa tawi, mimi na mmisionari mwenza kwa furaha tulianza mipango kwa ajili ya mkutano, ambayo ingehitaji masaa 12 ya kusafiri kwa boti kuvuka Bahari ya East China mpaka nchi kavu ya Japan, ikifuatiwa na masaa 15 ya kusafiri kwa gari moshi mpaka Tokyo. Kwa huzuni, hatahivyo haikuweza kufanikiwa. Tulipokea ujumbe kutoka kwa rais wetu wa misheni kwamba kwa sababu ya umbali na muda, mimi na mwenza wangu tusingeweza kuhudhuria mkutano huko Tokyo.

Picha
Mzee Stevenson na mwenza wake mmisionari

Wakati waumini wa tawi letu dogo walipoondoka kwenda Tokyo, sisi tulibaki. Siku zilizofuatia zilionekana kuwa kimya na tupu. Tulifanya mkutano wa sakramenti peke yetu katika tawi letu dogo, wakati Watakatifu wa Siku za Mwisho na wamisionari wa Japani wakihudhuria ule mkutano.

Picha
Mkutano wa Eneo la Asia

Hisia zangu binafsi za kuvunjika moyo ziliongezeka hata pale kwa shangwe nilipowasikiliza waumini wa tawi wakirudi kutoka kwenye mkutano siku chache baadae wakisema kwamba Rais Kimball ametangaza hekalu kujengwa huko Tokyo. Walibubujikwa na msisimko walipokuwa wakisimuliana utimilifu wa ndoto yao. Walielezea jinsi, baada ya kusikia tangazo la hekalu, waumini na wamisionari walishindwa kudhibiti furaha yao na kwa pamoja walilipuka na kupiga makofi.

Picha
Rais Kimball anatangaza hekalu huko Tokyo

Miaka imepita, na bado nakumbuka kuvunjika moyo kule nilikohisi kwa kukosa mkutano ule wa kihistoria.

Katika miezi ya hivi karibuni nimetafakari juu ya uzoefu huu wakati nilipowaona wengine wakipitia kuvunjika moyo na huzuni nyingi—nyingi zaidi na kubwa kuliko yangu ilivyowahi kuwa nikiwa mmisionari kijana—iliyoletwa na janga la ulimwengu la COVID-19.

Mapema mwaka huu, wakati maradhi ya ulimwenguni kote yakishika kasi, Urais wa Kwanza uliahidi kwamba “Kanisa na waumini wake kwa uaminifu kabisa tutaonyesha msimamo wetu wa kuwa raia wema na majirani wema”1 na “tutachukua tahadhari kubwa.”2 Hivyo, tumeshuhudia kusimamishwa kwa mikusanyiko ulimwenguni kote, kurudi kwa zaidi ya nusu ya jeshi la wamisionari wa Kanisa kwenye mataifa ya nyumbani kwao, na kufungwa kwa mahekalu yote kote katika Kanisa. Maelfu yenu mlikuwa mkijitayarisha kuingia hekaluni kwa ajili ya ibada za walio hai—ikijumuisha kuunganishwa hekaluni. Wengine wenu mmemaliza huduma zenu kama wamisionari mapema au mmepumzishwa kwa muda na kupangiwa sehemu mpya.

Picha
Wamisionari wakirejea katikati ya COVID

Kwa wakati huu, viongozi wa serikali na wa elimu wamezifunga shule—hatimaye limevuruga mahafali na kulazimu kufutwa kwa shughuli za michezo, kijamii, kiutamaduni, na matukio na shughuli za kielimu. Wengi wenu mlijitayarisha kwa ajili ya shughuli ambazo hazikuhudhuriwa, maonyesho ambayo hayakusikika, na msimu wa mashindano ya riadha ambayo hayakufanyika.

La kutia uchungu zaidi ni mawazo ya familia ambazo zimepoteza wapendwa wao wakati huu; wengi wao hawakuweza kufanya mazishi au mikusanyiko mingine kama walivyotumaini.

Kwa kifupi, wengi, wengi wenu mmekabiliana na kuvunjika moyo, huzuni, na kukata tamaa. Hivyo ni kwa jinsi gani tunapona, tunavumilia na kusonga mbele wakati vitu vinaonekana vimevunjika?

Nabii Nefi alianza kuandika bamba ndogo wakati alipokuwa mtu mzima. Alipokuwa akitafakari juu ya maisha yake na huduma yake, alitoa tafakuri muhimu, katika mstari wa kwanza tu wa Kitabu cha Mormoni. Mstari huu unatengeneza kanuni muhimu kwa ajili yetu kuzingatia katika wakati wetu. Kufuatia maneno yake yanayofahamilka, “Mimi, Nefi nikiwa nimezaliwa na wazazi wema … ,” anaandika, “na baada ya kushuhudia masumbuko mengi maishani mwangu, haidhuru, nikiwa nimebarikiwa na Bwana maishani mwangu.”3

Kama wanafunzi wa Kitabu cha Mormoni, tunafahamu masumbuko mengi ambayo Nefi anayarejelea. Bado kufuatia kukiri juu ya masumbuko katika siku zake, Nefi anatoa mtazamo wake wa kiinjili wa kubarikiwa na Bwana katika siku za maisha yake. Nyakati za masumbuko na kuvunjika moyo hazibadilishi jicho la uangalizi la Bwana pale kwa upendeleo Anapotutazama, Anapotubariki.

Picha
Mkutano wa misheni kwa njia ya mtandao
Picha
Mkutano wa misheni na Mzee na Dada Stevenson kwa njia ya mtandao
Picha
Mkutano wa misheni na Mzee na Dada Stevenson kwa njia ya mtandao

Lesa pamoja na mimi hivi karibuni kwa njia ya mtandao tumekutana na takriban wamisionari 600 wa Australia, wengi wao wakiwa chini ya kizuizi cha kutotoka nje au vikwazo vihusianavyo na COVID-19, wengi wakifanya kazi wakiwa nyumbani. Kwa pamoja tuliwafikiria watu katika Agano Jipya, Kitabu cha Mormoni, na Mafundisho na Maagano ambao Bwana aliwabariki kukamilisha mambo makubwa katika dhiki. Wote walitambulika zaidi kwa kile walichoweza kufanya kwa msaada wa Bwana kuliko kwa kile ambacho hawakuweza kufanya kama matokeo ya zuio na kikwazo.

Tulisoma juu ya Paulo na Sila, ambao, wakati wakiwa wamefungwa gerezani, walisali, waliimba, walifundisha, walishuhudia—hata walimbatiza mlinzi wa gareza.4

Na tena juu ya Paulo, katika Roma, chini ya kizuizi cha nyumbani kwa miaka miwili, wakati ambapo mara zote aliendelea “kuhubiri na kushuhudia juu ya ufalme wa Mungu,”5 “akifundisha mambo yale yahusuyo Bwana Yesu Kristo.”6

Juu ya Nefi na Lehi, wana wa Helamani, ambao baada ya kunyanyaswa na kufungwa gerezani walizingirwa na moto wa ulinzi wakati “sauti tulivu na kadiri kama mnong’ono … ilipowapenya [watekaji wao] hata kwenye roho.”7

Juu ya Alma na Amuleki huko Amoniha, ambao waliona kwamba wengi “waliamini … na kuanza kutubu, na kupekua maandiko,”8 licha ya kuwa walikejeliwa na hawakuwa na chakula, maji, au mavazi, wakiwa wamefungwa na kuzuiliwa gerezani.9

Picha
Joseph Smith katika Jela ya Liberty

Na mwishowe juu ya Joseph Smith, ambaye, wakati akilalama katika Jela ya Liberty, akihisi kutelekezwa na kusahaulika, kisha akasikia maneno ya Bwana: “Mambo haya … yatakuwa kwa faida yako”10 na “Mungu atakuwa pamoja nawe.”11

Kila mmoja wa hawa alielewa kile Nefi alichojua: kwamba ingawa walishuhudia masumbuko mengi katika siku zao, bado walikuwa wamebarikiwa na Bwana.

Sisi pia tunaweza kuwa na mfanano huu kama waumini binafsi na kama kanisa katika njia ambayo kwayo tumebarikiwa na Bwana katika kipindi cha nyakati za changamoto tulizokutana nazo kwa miezi kadhaa iliyopita. Ninaporejelea mifano hii, acha nayo pia iimarishe ushuhuda wako juu ya uonaji wa nabii wetu aliye hai, ambaye alitutayarisha sisi kwa mabadiliko kabla ya fununu yoyote ya maradhi haya ya ulimwengu, akituwezesha kuvumilia changamoto ambazo zimekuja.

Kwanza, kuwa waliolenga nyumbani wanaosaidiwa na Kanisa.

Miaka miwili iliyopita, Rais Russell M. Nelson alisema: “Tumekuwa na kawaida ya kufikiria ‘kanisa’ kama kitu fulani ambacho kinafanyika katika nyumba zetu za mikutano, kikisaidiwa na kile kinachofanyika nyumbani. Tunahitaji marekebisho kwenye mpangilio huu. … Kanisa linalolenga nyumbani, likisaidiwa na kile kinachofanyika ndani ya … majengo yetu.”12 Ni marekebisho ya kinabii yaliyoje! Masomo ya injili yaliyolenga nyumbani yamewekwa katika vitendo kwa kufungwa kwa muda kwa nyumba za mikutano. Hata ulimwengu unapoanza kurejea katika hali ya kawaida na sisi kurudi makanisani, tutataka kubaki na mpangilio wetu wa kujifunza na kusoma injili kulikolenga nyumbani ulioanzishwa wakati wa maradhi haya ya ulimwenguni kote.

Mfano wa pili wa kuwa wenye kubarikiwa na Bwana ni ufunuo kuhusu uhudumiaji katika njia ya juu na takatifu zaidi.

Picha
Uhudumiaji

Mwaka 2018, Rais Nelson alitambulisha uhudumiaji kama marekebisho “katika njia tunayojaliana sisi kwa sisi.”13 Maradhi ya ulimwenguni kote yametambulisha fursa nyingi zisizo na idadi ili kunoa ujuzi wetu wa kuhudumu. Akina kaka na dada wahudumiaji, wasichana na wavulana, na wengine wamefikia kutoa mawasiliano, mazungumzo, utunzaji wa ua, vyakula, arafa kupitia teknolojia, na ibada ya sakramenti ili kuwabariki wale wenye uhitaji. Kanisa lenyewe pia limekuwa likiwahudumia wengine wakati huu wa maradhi ya ulimwenguni kote kwa usambazaji mkubwa wa bidhaa kwenye benki za chakula, vituo vya wasio na makazi, na kwenye vituo vya wahamiaji pamoja na miradi iliyoelekezwa kwenye hali zenye njaa kali ulimwenguni. Akina dada wa Muungano wa Usaidizi na familia zao waliitikia changamoto ya kutengeneza mamilioni ya barakoa kwa ajili ya wahudumu wa afya.

Picha
Huduma za Kibinadamu
Picha
Utengenezaji barakoa

Mfano wa mwisho wa kubarikiwa wakati wa dhiki ni kupata shangwe ya juu zaidi kama matokeo ya ibada za hekaluni.

Picha
Dada Kaitlyn Palmer

Hii inaelezeka vyema zaidi kwa hadithi. Wakati Dada Kaitlyn Palmer alipopokea wito wake wa misheni Aprili iliyopita, alifurahia kuitwa kama mmisionari lakini alihisi hii ina umuhimu sawa na wa kipekee kwenda hekaluni kupokea endaomenti yake na kufanya maagano matakatifu. Muda mfupi baada ya kupanga ratiba ya endaomenti yake, tangazo likaja kwamba mahekalu yote yangefungwa kwa muda kutokana na maradhi haya ya ulimwengu mzima. Baada ya kupokea taarifa hii yenye kuvunja moyo, aligundua kwamba atahudhuria kituo cha mafunzo cha umisionari (MTC) kwa njia ya mtandao akiwa nyumbani kwake. Licha ya hali hizi za kuvunja moyo, Kaitlyn alifokasi katika kukuza roho yake.

Picha
Dada Kaitlyn Palmer na MTC ya nyumbani

Katika miezi iliyoingilia kati, Dada Palmer kamwe hakupoteza matumaini ya kuhudhuria hekaluni. Familia yake walifunga na kuomba kwamba mahekalu yangefunguliwa kabla ya kuondoka kwake. Kaitlyn mara nyingi angeanza mafunzo yake ya nyumbani kwa kusema, “Je, leo itakwenda kuwa siku tutakayopokea muujiza na mahekalu yakafunguliwa?”

Mnamo Agosti 10, Urais wa Kwanza ulitangaza kwamba hekalu la Kaitlyn lingefunguliwa kwa ajili ya ibada za walio hai siku ile ile ambayo safari yake ya kwenda misheni ilikuwa imepangwa. Yeye asingeweza kuhudhuria hekaluni na kufanya safari yake ya ndege pia. Akiwa na matumaini madogo ya mafanikio, familia yake iliwasiliana na rais wa hekalu hilo Michael Vellinga ili kuona kama kuna njia yoyote muujiza huu waliokuwa wameuomba ungeweza kupatikana. Kufunga na kuomba kwao kulijibiwa!

Picha
Familia ya Palmer hekaluni

Saa 8:00 usiku, masaa kadhaa kabla ya kuondoka kwa ndege yake, Dada Palmer na familia yake, kwa machozi, walisalimiwa katika milango ya hekalu na rais wa hekalu mwenye tabasamu kwa maneno, “habari za asubuhi, familia ya Palmer. Karibuni hekaluni!” Alipomaliza endaomenti yake, walisisitizwa kufanya haraka, kwani familia inayofuata ilikuwa ikisubiri mlangoni. Waliendesha moja kwa moja kwenda uwanja wa ndege na kufika kwa wakati kuwahi ndege ya kumpeleleka kwenye misioni yake.

Picha
Dada Palmer akiwa uwanja wa ndege

Ibada za hekaluni tulizozikosa kwa miezi kadhaa huonekana tamu sana kuliko tulivyofikiria awali wakati mahekalu ulimwenguni kote yanapofunguliwa kwa awamu.

Ninapohitimisha, tafadhali sikiliza maneno ya kutia moyo, yenye hamasa, ya kuinua ya Nabii Joseph Smith. Mtu kamwe asingekisia kwamba yeye aliyaandika kwa mkono akiwa katika masumbuko na upweke, kwenye kifungo na zuio la nyumbani huko Nauvoo, akijificha kutoka kwa wale waliokuwa wakitafuta kumkamata kinyume cha sheria.

“Sasa, tunasikia nini katika injili ambayo tumeipokea? Sauti ya furaha! Sauti ya rehema kutoka mbinguni; na sauti ya ukweli kutoka duniani; habari njema kwa ajili ya wafu; sauti ya furaha kwa walio hai na wafu; habari njema ya shangwe kuu. …

“… Je, sisi hatupaswi kuendelea katika kusudi hili kuu? Nenda mbele na siyo nyuma. Ujasiri … na mbele, mbele kwenye ushindi! Acheni mioyo yenu ifurahi, na kuwa na furaha kupita kiasi. Acheni nchi ipasuke kwa kuimba.”14

Akina kaka na dada, ninaamini kuwa siku moja, kila mmoja wenu ataangalia nyuma katika matukio yaliyofutwa, huzuni, kuvunjika moyo, na upweke uliokuwepo kwenye nyakati zenye changamoto tunazopitia kuona zikiwa zimefunikwa na baraka kuu na ongezeko la imani na shuhuda. Ninaamini kwamba katika maisha haya, na katika maisha yajayo, masumbuko yenu, Amoniha yenu, Jela yenu ya Liberty, vitawekwa wakfu kwa faida yenu.15 Ninaomba kwamba, sambamba na Nefi, tuweze kutambua masumbuko katika siku zetu vilevile wakati huo huo tutambue kwamba tumebarikiwa na Bwana.

Ninahitimisha kwa ushuhuda wangu wa Yesu Kristo, ambaye Yeye mwenyewe hakuwa mgeni kwenye masumbuko na kama sehemu ya Upananisho wake usio na mwisho alijishusha chini ya vitu vyote.16 yeye anaelewa huzuni yetu, maumivu na kukata kwetu tamaa. Yeye ni Mwokozi wetu, Mkombozi wetu, tumaini letu, faraja yetu, na Mtetezi wetu. Juu ya haya ninashuhudia katika jina Lake takatifu,Yesu Kristo, amina.