Mkutano Mkuu
Nguvu za Kudumu
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2020


Nguvu za Kudumu

Imani pekee na neno la Mungu ambavyo hujaza nafsi zetu za ndani vinatosha kutuhimili—na kuturuhusu kufikia nguvu Zake.

Katika kupitia mafundisho ya nabii wetu mpendwa, Rais Russell M. Nelson, nilipata neno ambalo amekuwa akilitumia mara nyingi katika mazungumzo mengi. Neno hili ni nguvu.

Katika mkutano mkuu wa kwanza baada ya kuidhinishwa kama Mtume, Rais Nelson alizungumzia juu ya nguvu.1 Ameendelea kufundisha kuhusu nguvu kwa miaka mingi. Tangu tulipomuidhinisha Rais Nelson kama nabii wetu, amefundisha juu ya kanuni ya nguvu—hasa, nguvu za Mungu—na jinsi tunavyoweza kuzipata. Amefundisha jinsi tunavyoweza kuvuta nguvu za Mungu wakati tunapowahudumia wengine,2 jinsi toba inavyoalika nguvu za Yesu Kristo na Upatanisho Wake maishani mwetu,3 na jinsi ukuhani — nguvu na mamlaka ya Mungu—unavyowabariki wote wanaofanya na kutunza maagano pamoja Naye.4 Rais Nelson ameshuhudia kwamba nguvu za Mungu hutiririka kwa wote ambao wamepokea endaumenti hekaluni pale wanapotunza maagano yao.5

Niliguswa hasa na changamoto ambayo Rais Nelson aliitoa katika mkutano mkuu wa Aprili 2020. Alituelekeza “tujifunze na kuomba ili kujifunza zaidi kuhusu nguvu na maarifa ambavyo kwavyo tumetunukiwa—au ambavyo kwavyo tutakuja kutunukiwa.”6

Kwa kujibu changamoto hii, nimejifunza na kuomba na nimejifunza vitu vilivyo na faida kuhusu nguvu na maarifa ambavyo kwavyo nimetunukiwa—au ambavyo kwavyo nitakuja kutunukiwa.

Kuelewa kile tunachopaswa kufanya ili kufikia nguvu za Mungu katika maisha yetu si rahisi, lakini nimekuta kwamba inawezekana kwa kukitafakari katika akili zetu na kuomba Roho Mtakatifu atuangazie.7 Mzee Richard G. Scott alitoa ufafanuzi wa wazi wa nguvu za Mungu ni nini: ni “nguvu za kufanya zaidi ya vile tunavyoweza kufanya sisi wenyewe.”8

Kujaza mioyo yetu na hata roho zetu kwa neno la Mungu na msingi wa imani katika Yesu Kristo ni muhimu sana kwenye kuvuta nguvu za Mungu kutusaidia katika nyakati hizi zenye changamoto. Bila kupata neno la Mungu na imani katika Yesu Kristo kwenye kina cha mioyo yetu, ushuhuda wetu na imani vinaweza kushindwa, na tunaweza kupoteza fursa ya kufikia nguvu ambazo Mungu anataka kutupatia. Imani ya juujuu haitoshi. Imani pekee na neno la Mungu ambavyo hujaza nafsi zetu za ndani vinatosha kutuhimili—na kuturuhusu kufikia nguvu Zake.

Wakati mimi na Dada Johnson tulipokuwa tunawalea watoto wetu, tuliwahimiza kila mmoja wao kujifunza kupiga ala ya muziki. Lakini tungewaruhusu watoto wetu kuchukua masomo ya muziki ikiwa tu watafanya sehemu yao na kufanya mazoezi ya ala yao kila siku. Jumamosi moja, binti yetu Jalynn alikuwa na furaha kwenda kucheza na marafiki, lakini alikuwa bado hajafanya mazoezi ya piano. Akijua kuwa alikuwa ameahidi kufanya mazoezi kwa dakika 30, alikusudia kuweka kipima muda kwa sababu hakutaka kufanya mazoezi hata dakika moja zaidi ya ilivyotakiwa.

Alipokuwa akitembea karibu na maikrowevu akienda kwenye piano, alisimama na kubonyeza swichi kadhaa. Lakini badala ya kuweka kipima muda, aliweka maikrowevu kupika kwa dakika 30 na akabonyeza ili ianze. Baada ya dakika 20 za mazoezi, alitembea kurudi jikoni kuangalia ni muda gani ulikuwa umebakia na akakuta maikrowevu inawaka moto.

Kisha alikimbilia nyuma ya nyumba ambapo nilikuwa nikifanya kazi ya shamba, akipiga kelele kwamba nyumba ilikuwa inaungua. Haraka nilikimbia ndani ya nyumba, na, hakika, nilikuta maikrowevu kwenye mwako wa moto.

Katika kujaribu kuokoa nyumba yetu isiteketee, nilishika nyuma ya maikrowevu, nikaichomoa, na kutumia waya wa umeme kuinua maikrowevu iliyokuwa inawaka kutoka kwenye kaunta. Nikitumaini kuwa shujaa na kuokoa siku hiyo pamoja na nyumba yetu, niliizungusha maikrowevu iliyokuwa inawaka moto kwa mzunguko kwa kutumia waya wa umeme ili kuiweka mbali na mwili wangu, nikafika nyuma ya nyumba, na kwa mwendo mwingine wa kuzungusha nikavurumisha maikrowevu nje kwenye uwanja wenye nyasi. Hapo, tuliweza kuzima moto mkali kwa bomba la maji.

Ni nini kilikuwa kimeenda vibaya? Tanuri ya maikrowevu inahitaji kitu cha kufyonza nishati yake, na wakati hakuna kitu ndani cha kufyonza nishati, tanuri yenyewe inafyonza nishati hiyo, inakuwa ya moto, na inaweza kuwaka moto, ikijiharibu yenyewe katika rundo la moto na majivu.9 Maikrowevu yetu yote iliwaka moto na ikateketea kwa sababu hakukuwa na chochote ndani.

Vivyo hivyo, wale walio na imani na neno la Mungu ndani ya mioyo yao wataweza kufyonza na kushinda mishale ya moto, ambayo adui kwa hakika atatuma ili kutuangamiza.10 Kama sivyo, imani yetu, tumaini, na kusadiki kwetu hakuwezi kudumu, na kama vile maikrowevu tupu, tunaweza kuwa majeruhi.

Nimejifunza kwamba kuwa na neno la Mungu kwa kina ndani ya nafsi yangu, pamoja na imani katika Bwana Yesu Kristo na Upatanisho Wake, kunaniruhusu kuvuta nguvu za Mungu ili kumshinda adui na chochote anachoweza kunitupia. Tunapokabiliana na changamoto, tunaweza kutegemea ahadi ya Bwana iliyofundishwa na Paulo: “Kwa maana Mungu hakutupa roho ya woga; bali ya nguvu, na ya upendo, na ya akili timamu.”11

Tunajua kwamba kama mtoto Mwokozi “alikua, na kuwa na nguvu katika roho, amejaa hekima: na neema ya Mungu ilikuwa juu yake.”12 Tunajua kuwa alipoendelea kukua, “Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.”13 Na tunajua kwamba wakati huduma Yake ilipoanza, wale waliomsikia “walishangazwa na mafundisho yake: kwa kuwa neno lake lilikuwa na nguvu.”14

Kupitia maandalizi, Mwokozi alikua katika nguvu na aliweza kupinga majaribu yote ya Shetani.15 Tunapofuata mfano wa Mwokozi na kujiandaa kupitia kujifunza neno la Mungu na kuongeza imani yetu, tunaweza pia kuvuta nguvu za Mungu kupinga majaribu.

Kipindi hiki cha zuio la mikusanyiko ambacho hufanya kuhudhuria hekaluni mara kwa mara kutowezekana, kwa kweli nimeweka hoja ya kuendelea kusoma na kujifunza zaidi juu ya nguvu za Mungu ambazo huja kwetu tunapofanya na kutunza maagano ya hekaluni. Kama ilivyoahidiwa katika sala ya uwekaji wakfu wa Hekalu la Kirtland, tunaondoka hekaluni tukiwa tumekingwa kwa nguvu za Mungu.16 Hakuna tarehe ya kuisha muda wa matumizi inayohusishwa na nguvu ambazo Mungu huwapa wale ambao hufanya na kutunza maagano ya hekaluni, wala hakuna zuio la kufikia nguvu hizo kipindi cha janga la ulimwengu. Nguvu zake hupungua katika maisha yetu ikiwa tu tunashindwa kutunza maagano yetu na hatuishi kwa njia ambayo inatuwezesha daima kuendelea kustahili kupokea nguvu Zake.

Wakati mimi na mke wangu mpendwa tulipokuwa tukihudumu kama viongozi wa misheni nchini Thailand, Laos, na Myanmar, tulishuhudia moja kwa moja nguvu za Mungu zinazokuja kwa wale ambao hufanya na kutunza maagano matakatifu hekaluni. Mfuko wa Msaada wa Ufadhili wa Hekalu uliwezesha Watakatifu wengi katika nchi hizi tatu kuhudhuria hekaluni baada ya kufanya yote ambayo wangeweza kupitia dhabihu binafsi na kujitayarisha. Nakumbuka kukutana na kundi la Watakatifu 20 waaminifu kutoka Laos kwenye uwanja wa ndege huko Bangkok, Thailand, ili kuwasaidia kuhamia uwanja mwingine wa ndege wa Bangkok ili kupata ndege yao ya kwenda Hong Kong. Waumini hawa walikuwa wamejawa na msisimko wa hatimaye kwenda kwenye nyumba ya Bwana.

Picha
Waumini huko Laos

Tulipokutana na Watakatifu hawa wema wakati wa kurudi kwao, ongezeko la ukomavu wa injili na nguvu zinazohusiana zinazotokana na kupokea endaumanti zao za hekaluni na kuingia katika maagano na Mungu lilikuwa dhahiri. Watakatifu hawa hakika walitoka hekaluni “wakiwa wamekingwa kwa nguvu [Zake].”17 Nguvu hizi za kufanya zaidi ya vile ambavyo wangeweza wao wenyewe ziliwapa uwezo wa kuvumilia changamoto za uumini wa Kanisa katika nchi yao na kusonga mbele wakishuhudia “habari hizi zilizo kuu na tukufu kupita kiasi, katika ukweli,”18 wakati wanapoendelea kujenga ufalme wa Bwana huko Laos.

Wakati ambao hatujaweza kuhudhuria hekaluni, je! Kila mmoja wetu ametegemea maagano tuliyoyafanya hekaluni ili kuweka mwelekeo ulio wazi, usiobadilika katika maisha yetu? Maagano haya, ikiwa yatatunzwa, yanatupa maono na matarajio kuhusu siku za usoni na dhamira dhahiri ya kutustahilisha kupokea yote ambayo Bwana ameahidi kupitia uaminifu wetu.

Ninawaalika mtafute nguvu ambazo Bwana anataka kuwapa. Ninashuhudia kwamba tunapotafuta nguvu hizi, tutabarikiwa kwa uelewa mkubwa wa upendo Baba yetu wa Mbinguni alio nao kwetu.

Ninashuhudia kwamba kwa sababu Baba wa Mbinguni anatupenda mimi na wewe, alimtuma Mwanawe Mpendwa, Yesu Kristo, kuwa Mwokozi na Mkombozi wetu. Ninashuhudia juu ya Yesu Kristo, Yeye aliye na nguvu zote,19 na ninafanya hivyo katika jina la Yesu Kristo, amina.