2010–2019
Hili Litaongoza Wapi?
Mkutano Mkuu wa Aprili 2019


Hili Litaongoza Wapi?

Tunafanya maamuzi na chaguzi nzuri ikiwa tutatazama mibadala na kutafakari wapi itatuongoza.

Injili ya urejesho ya Yesu Kristo inatuhimiza kufikiria kuhusu wakati ujao. Inaelezea lengo la maisha ya duniani na uhalisia wa maisha yajayo. Inafundisha mawazo makuu kuhusu wakati ujao ili kuongoza matendo yetu leo.

Kinyume chake, sote tunawajua watu ambao wanajihusisha tu na wakati uliopo: wanautumia leo, wanaufurahia leo na hawafikirii wakati ujao.

Wakati wetu uliopo na ujao utakuwa wenye furaha zaidi kama daima tutatambua wakati ujao. Tunapofanya maamuzi ya sasa, tunapaswa daima kujiuliza, “Hili litaongoza wapi?”

I.

Baadhi ya maamuzi ni chaguzi kati ya kufanya jambo au kutofanya jambo. Nilisikia mfano wa aina hii ya uchaguzi kwenye mkutano wa kigingi Marekani miaka mingi iliyopita.

Mazingira yalikuwa kampasi nzuri ya chuo. Kundi la wanafunzi vijana walikuwa wameketi juu ya nyasi. Mzungumzaji aliyeelezea uzoefu huu alisema walikuwa wakitazama kindi wa mtini mwenye mkia mkubwa, uliojaa manyoya akicheza kuzunguka sehemu ya chini ya mti wa kupendeza wa ubao mgumu. Wakati mwingine alikuwa ardhini, wakati mwingine juu na chini na kuzunguka shina. Lakini kwa nini muonekano ule wa kawaida ulivutia kundi la wanafunzi?

Akijinyoosha juu ya nyasi kando kidogo alikuwa mbwa wa kuwindia wa Kiairishi. Alikuwa kusudi la mvuto wa wanafunzi, na kindi alikuwa kusudi la mbwa. Kila wakati kindi alipotoka kwenye upeo kwa muda akizunguka mti, mbwa taratibu angetambaa mbele inchi chache na kisha kurejea tena mkao wake wa kawaida. Hili ndilo lililoshika mvuto wa wanafunzi. Kimya na wasiojijongeza, macho yao yalivutwa kwenye tukio ambalo matokeo yake yaliongezeka kuwa dhahiri.

Hatimaye, mbwa alikuwa karibu vya kutosha kumfunga kindi na kumshika kwa mdomo wake. Mtweto wa kuogofya uliibuka, na kundi la wanafunzi walienda mbele na kumpokonya mnyama mdogo kutoka kwa mbwa, lakini walikuwa wamechelewa. Kindi alikuwa amekufa.

Yeyote katika kundi lile angeweza kumuonya kindi wakati wowote kwa kupunga mikono yao au kupiga kelele, lakini hakuna aliyefanya hivyo. Walitazama tu wakati athari isiyoepukika iliposonga karibu taratibu. Hakuna aliyeuliza, “Hili litaongoza wapi?” Wakati ya kutarajiwa yalipotokea, wote waliharakisha kuzuia athari, lakini walikuwa wamechelewa. Machozi ya majuto ndiyo kila kitu walichoweza kutoa.

Hadithi hiyo ya kweli ni fumbo la hali nyingi. Inahusika kwenye mambo tunayoona katika maisha yetu wenyewe, na katika maisha na mazingira yanayotuzunguka. Tunapoona hatari zikitambaa kwa mtu au mambo tunayoyapenda, tuna uchaguzi wa kuzungumza au kutenda au kubaki kimya. Ni vema kujiuliza wenyewe, “Hili litaongoza wapi?” Ambapo matokeo ni ya haraka na yenye uzito, hatuwezi kuhimili kutofanya chochote. Lazima tutoe maonyo yanayofaa au kuunga mkono juhudi za ulinzi zinazofaa wakati bado kuna muda.

Maamuzi ambayo nimetoka kuelezea yanahusisha chaguzi kati ya kuchukua hatua au kutochukua hatua kabisa. Za kawaida zaidi ni zile chaguzi kati ya tendo moja na jingine. Hizi hujumuisha chaguzi kati ya mema na mabaya, lakini mara nyingi ni chaguzi kati ya mema mawili. Hapa pia ni yenye kupendeza kuuliza hili litaongoza wapi. Tunafanya chaguzi nyingi kati ya mema mawili, mara nyingi ikijumuisha ni jinsi gani tutatumia muda wetu. Hakuna chochote kibaya kuhusu kucheza michezo ya video au kutuma arafa au kuangalia TV au kuzungumza kwenye simu. Lakini kila moja ya haya hujumuisha kile kinachoitwa “gharama ya fursa,” ikimaanisha kwamba ikiwa tunatumia muda kufanya jambo moja, tunapoteza fursa ya kufanya lingine. Nina hakika mnaweza kuona kwamba tunahitaji kupima kwa uangalifu kile tunachopoteza kwa muda tunaotumia kwenye shughuli moja, hata kama yenyewe ni nzuri kikamilifu.

Kipindi fulani kilichopita nilitoa hubiri liliokuwa na kichwa cha habari “Nzuri, Nzuri kiasi, au Nzuri zaidi.” Katika hubiri lile nilisema kwamba “kwa sababu tu jambo ni zuri hiyo si sababu ya kutosha kulifanya. Idadi ya mambo mazuri tunayoweza kufanya inazidi mbali muda uliopo wa kuyakamilisha. Baadhi ya mambo ni mazuri kiasi zaidi ya mazuri, na haya ndiyo mambo ambayo yanapaswa kudai kipaumbele cha usikivu katika maisha yetu. … Hatuna budi kuacha baadhi ya mambo mazuri ili tuchague mengine ambavyo ni mazuri kiasi au mazuri zaidi.”1

Chukua mtazamo mrefu. Ni nini matokeo ya maamuzi tunayofanya sasa kwenye wakati wetu ujao? Kumbuka umuhimu wa kupata elimu, kujifunza injili, kufanya upya maagano yetu kwa kupokea sakramenti, na kuhudhuria hekaluni.

II.

“Hili litaongoza wapi?” ni muhimu pia katika kuchagua jinsi tunavyojitambulisha au kujifikiria wenyewe. Muhimu zaidi, kila mmoja wetu ni mtoto wa Mungu mwenye uwezekano wa hatma ya maisha ya milele. Utambulisho mwingine wowote, hata ikijumuisha kazi, utaifa, sifa za kimwili au heshima, ni wa muda au usio na maana katika mambo ya milele. Usichague kujitambulisha au kujifikiria katika mambo ambayo yanaweka ukomo kwenye lengo la kile unachopaswa kukitafuta.

Kaka zangu, na dada zangu ambao mtaweza kutazama au kusoma kile ninachosema hapa, natumaini mnajua kwa nini viongozi wenu wanatoa mafundisho na ushauri tunaowapa. Tunawapenda, na Baba yetu wa Mbinguni na Mwanaye, Yesu Kristo, wanawapenda. Mpango Wao kwetu ni “mpango mkuu wa furaha” (Alma 42:8). Mpango huo na amri Zao na ibada na maagano hutuongoza kwenye furaha na shangwe kuu katika maisha haya na maisha yajayo. Kama watumishi wa Baba na Mwana, tunafunza na kushauri jinsi Wao walivyotuelekeza kwa Roho Mtakatifu. Hatuna tamanio jingine zaidi ya kuzungumza kile kilicho kweli na kuwahimiza kutenda kile Wao wameeleza kama njia ya uzima wa milele, “kipawa ambacho ni kikuu katika vipawa vyote vya Mungu” (Mafundisho na Maagano 14:7).

III.

Hapa ni mfano mwingine wa athari ya baadaye ya maamuzi yaliyofanywa sasa. Mfano huu unahusu uchaguzi wa kufanya dhabihu sasa ili kufanikisha lengo muhimu la baadaye.

Katika mkutano wa kigingi huko Cali, Colombia, dada alielezea jinsi yeye na mchumba wake walivyotamani kufunga ndoa hekaluni, lakini wakati ule hekalu la karibu lilikuwa mbali huko Peru. Kwa muda mrefu, waliweka akiba pesa zao kwa ajili ya nauli ya basi. Hatimaye walipanda basi kuelekea Bogotá, lakini walipofika huko, waligundua kwamba viti vyote ndani ya basi la kwenda Lima, Peru, vilikuwa vimejaa. Wangeweza kurudi nyumbani bila kufunga ndoa au kufunga ndoa nje ya hekalu. Kwa bahati nzuri, kulikuwa na mbadala mwingine. Wangeweza kusafiri ndani ya basi kwenda Lima ikiwa wangekuwa radhi kukaa kwenye sakafu ya basi kwa siku zote tano za safari mchana na usiku. Walichagua kufanya hili. Anasema ilikuwa vigumu, japokuwa baadhi ya wasafiri wakati mwingine waliwaruhusu wakalie viti vyao ili wao wajinyooshe sakafuni.

Kilichonivutia katika hubiri lake ilikuwa kauli ya dada huyu kwamba alikuwa na shukrani yeye na mume wake waliweza kwenda hekaluni kwa njia hii, kwa sababu ilibadilisha jinsi walivyohisi kuhusu injili na jinsi walivyohisi kuhusu ndoa ya hekaluni. Bwana alikuwa amewazawadia kwa ukuaji ambao huja kutokana na dhabihu. Aligundua pia kwamba safari yao ya siku tano kwenda hekaluni ilifanikisha kwa kiasi kikubwa zaidi katika kujenga mambo yao ya kiroho kuliko matembezi mengi ya hekaluni ambayo hayakuhitaji dhabihu.

Tangu miaka hiyo niliposikia ushuhuda ule, nimejiuliza maisha ya wanandoa wale vijana yangekuaje kama wangefanya uchaguzi mwingine—kuacha dhabihu muhimu ili kufunga ndoa hekaluni.

Tunafanya chaguzi zisizo na idadi katika maisha, baadhi kubwa na baadhi zinaonekana ndogo. Tukitazama nyuma, tunaweza kuona tofauti kubwa baadhi ya chaguzi zetu zimeleta katika maisha yetu. Tunafanya maamuzi na chaguzi nzuri ikiwa tutatazama mibadala na kutafakari wapi itatuongoza. Tunapofanya hivyo, tutakuwa tukifuata ushauri wa Rais Russell M. Nelson wa kuanza na mwisho akilini.2 Kwetu sisi, mwisho daima uko kwenye njia ya agano kupitia hekaluni hadi kwenye uzima wa milele, kipawa ambacho ni kikuu katika vipawa vyote vya Mungu.

Ninashuhudia juu ya Yesu Kristo na juu ya matokeo ya Upatanisho Wake na kweli zingine za injili Yake ya milele katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Dallin H. Oaks, “Nzuri, Nzuri kiasi, Nzuri zaidi,” Liahona, Nov. 2007, 104107.

  2. Ona Russell M. Nelson, “Tunaposonga Mbele Pamoja,” Liahona, Apr. 2018, 7.