2010–2019
Kristo: Nuru Ing’aayo Gizani
Mkutano Mkuu wa Aprili 2019


Kristo: Nuru Ing’aayo Gizani

Ikiwa unahisi kwamba nguzo ya mwanga ya ushuhuda wako inatatarika na giza linaingia ndani, vaa ujasiri. Tunza ahadi zako kwa Mungu.

Ofisi yangu katika jengo la Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama ina upeo wa macho mkamilifu wa Hekalu la Salt Lake. Kila usiku, kama mazoea ya saa, taa za nje za hekalu zinawaka kwenye giza. Hekalu ni nguzo imara, yenye kuondoa hofu nje tu ya dirisha langu.

Picha
Vifundo vya milango ya Hekalu la Salt Lake

Usiku mmoja Februari hii iliyopita, ofisi yangu ilibaki pekee yenye giza wakati jua lilipochwea. Nilipotazama nje ya dirisha, hekalu lilikuwa na giza. Taa zilikuwa hazijawaka. Nilihisi huzuni ghafla. Sikuweza kuona minara ya hekalu niliyoitazama kila jioni kwa miaka.

Picha
Hekalu la Salt Lake na minara isiyo na mwanga

Kuona giza mahali nilipotegemea kuona nuru kulinikumbusha kwamba moja ya mahitaji muhimu tuliyonayo ili kukua ni kubaki tumeunganishwa kwenye chanzo chetu cha nuru—Yesu Kristo. Yeye ni chanzo cha nguvu zetu, Nuru na Uzima wa Ulimwengu. Bila mwunganisho imara Kwake, tunaanza kufa kiroho. Kwa kujua hilo, Shetani hujaribu kutumia mashinikizo ya ulimwengu tunayopata sote. Anafanya kazi kuzima nuru yetu, akileta shoti, akikata kusambaa kwa umeme, akituacha peke yetu gizani. Mashinikizo haya ni hali za kawaida katika maisha ya kufa, lakini shetani hujaribu kututenga na kutuambia ni sisi pekee tunaoyapitia.

Baadhi Yetu Wamepooza kwa Huzuni

Majanga yanapotuzidia, maisha yanapoumiza kiasi cha kutoweza kupumua, tunapokuwa tumepata kipigo kama mtu katika njia ya Yeriko na kuachwa kufa, Yesu huja na kumimina mafuta kwenye majeraha yetu, hutuinua juu taratibu, hutupeleka nyumba ya wageni, hututunza.1 Kwa wale kati yetu wenye huzuni, Yeye anasema, “Na pia … nitawapunguzia mizigo ambayo imewekwa mabegani yenu, hata kwamba hamtaisikia kamwe migongoni mwenu, … kwamba mjue kwa hakika kwamba mimi, Bwana Mungu, huwatembelea watu wangu katika mateso yao.”2 Kristo huponya majeraha.

Baadhi Yetu Tumechoka Sana.

Mzee Holland alisema: “Haikukusudiwa kwamba tukimbie zaidi ya uwezo tulionao. … Lakini [bila kujali] hilo, ninajua … wengi wenu mnakimbia kwa [kasi], kasi sana na kwamba akiba ya nguvu na hisia wakati mwingine huonesha karibu na kuisha.”3 Wakati matarajio yanapotuzidi, tunaweza kupiga hatua nyuma na kumwuliza Baba wa Mbinguni ni nini tuache. Sehemu ya uzoefu wetu wa maisha ni kujifunza nini cha kutofanya. Lakini hata hivyo, wakati mwingine maisha yanaweza kuchosha. Yesu anatuhakikishia, “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.”4

Kristo yu tayari kujiunga nasi katika nira na kuvuta ili kuifanya miepesi mizigo yetu. Kristo ni pumziko.

Baadhi Yetu Tunahisi Hatufai kwenye Tabia za Mila.

Kwa sababu tofauti, hatuhisi kukubaliwa au kukubalika. Agano Jipya huonesha juhudi kubwa alizofanya Yesu za kuwafikia aina tofauti za watu: wakoma, watoza ushuru, watoto, Wagalilaya, makahaba, wanawake, Mafarisayo, wenye dhambi, Wasamaria, wajane, askari wa Kirumi, wazinzi, wachafu kimila. Katika angalau kila hadithi, Yeye humfikia mtu fulani ambaye hakukubalika kimila katika jamii.

Luka 19 huelezea hadithi ya mtoza ushuru mkuu katika Yeriko aliyeitwa Zakayo. Alipanda mti ili aweze kumwona Yesu akipita. Zakayo alikuwa ameajiriwa na serikali ya Rumi na alichukuliwa kama mla rushwa na mdhambi. Yesu alimwona juu ya mti na kumwita, akisema, “Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako.”5 Na Yesu alipoona wema wa moyo wa Zakayo na mambo aliyofanya kwa wengine, Yeye alikubali dhabihu yake, akisema, “Leo wokovu umefika nyumbani humu, [kwa sababu] huyu naye ni mwana wa Ibrahimu.”6

Kristo kwa upole aliwaambia Wanefi, “Nimeamuru kwamba yeyote miongoni mwenu asiende.”7 Petro alikuwa na epifania hiyo yenye nguvu katika Matendo ya Mitume 10 wakati alipotangaza, “Mungu amenionya nisimwite [mtu] awaye yote mchafu wala najisi.”8 Ni kigezo kisichotetereka cha mfuasi wa Kikristo na Mtakatifu wa Siku za Mwisho kuonesha upendo wa kweli kwa kila mmoja.9 Yesu anatoa mwaliko sawa na huo kwetu ambao Aliutoa kwa Zakayo: “Tazama, nasimama mlangoni, nabisha: kama [wewe] utaisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia [kwako], nami nitakula pamoja [nawe], na [wewe] pamoja nami.”10 Kristo hutuona kwenye mti mwetu.

Baadhi Yetu Tunatatizika kwa Maswali

Si miaka mingi iliyopita, nilikuwa nimechoshwa na kukerwa kwa maswali ambayo sikuyapatia majibu. Mapema jumamosi moja asubuhi, nilipata ndoto. Katika ndoto niliweza kuona jengo dogo, na nilielewa kwamba nilipaswa kusimama ndani yake. Lilikuwa na matao matano kulizunguka, lakini madirisha yalikuwa yamejengwa kwa mawe. Nililalamika ndotoni, kwa kutotaka kuingia ndani kwa sababu lilikuwa la kuogopesha. Kisha wazo likanijia akilini kwamba kaka wa Yaredi kwa uvumilivu aliyeyusha mawe kuwa kioo angavu. Kioo ni jiwe ambalo limepitia hatua ya badiliko. Wakati Bwana alipogusa mawe ya kaka wa Yaredi, yaling’aa kwa nuru ndani ya mashua zenye giza.11 Ghafla nilijazwa na hamu ya kuwa ndani ya lile jengo kuliko sehemu nyingine yoyote. Ilikuwa mahala hasa—mahala pekee—kwa mimi “kuona” dhahiri. Maswali yaliyokuwa yakinitatiza hayakuondoka, lakini kwa uangavu zaidi katika akili yangu lilikuwa swali baada ya kuamka: “Ni kwa jinsi gani utaongeza imani yako, kama kaka wa Yaredi, ili mawe yako yaweze kugeuzwa nuru?”12

Bongo zetu zimeundwa kutafuta uelewa na maana katika vifurushi vikubwa. Sijui sababu zote za kwa nini pazia juu ya maisha ya kufa ni nene. Hii siyo hatua katika ukuaji wetu wa milele ambapo tuna majibu yote. Ni hatua ambapo tunakuza hakikisho letu (au wakati mwingine tumaini letu) katika ushahidi wa mambo yasiyoonekana. Hakikisho huja kwa njia ambazo mara zote si rahisi kuchanganua, lakini kuna nuru katika giza letu. Yesu alisema, “mimi ni mwangaza, na maisha, na ukweli wa dunia.”13 Kwa wale wanaotafuta ukweli, inaweza kuonekana mwanzo kuwa woga wa kipumbavu wa madirisha yaliyojengwa kwa mawe. Lakini kwa uvumilivu na maswali ya uaminifu, Yesu anaweza kubadili madirisha yetu ya mawe kuwa kioo na nuru. Kristo ni nuru ya kutazama.

Baadhi Yetu Tunahisi Hatuwezi Kuwa Wazuri Vya Kutosha

Nakshi yenye rangi nyekundu ya Agano la Kale haikuwa tu iliyosharabu rangi lakini pia haraka kushika rangi, ikimaanisha kwamba rangi yake ya kuonekana ilishika kwenye sufu na isingepauka bila kujali imefuliwa mara ngapi.14 Shetani hutumia hoja hii kama rungu: sufu nyeupe iliyochafuliwa kwa rangi nyekundu haiwezi kamwe kurudia weupe. Lakini Yesu Kristo anatangaza, “Njia zangu [zi] juu sana kuliko njia zenu,”15 na muujiza wa neema Yake ni kwamba tunapotubu dhambi zetu, damu Yake nyekundu huturejesha kwenye utakaso. Si yenye mantiki, hata hivyo ni ya kweli.

Picha
Sufu iliyotiwa waa jekundu

Picha kutoka iStock.com/iinwibisono

“Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu.”16 Bwana anasema waziwazi: “yule ambaye ametubu … dhambi, huyu anasamehewa, na Mimi, Bwana, sizikumbuki tena.”17 Kiini chake: Njoo, tujadiliane pamoja.18 Umefanya makosa; wote wana mapungufu.19 Njoo kwangu na utubu.20 Sitaikumbuka tena dhambi.21 Unaweza kuwa mzima tena.22 Nina kazi ya kufanya kwa ajili yako.23 Kristo hufanya sufu kuwa nyeupe.

Lakini ni nini hatua za kiutendaji? Ni nini ufunguo wa kuunganisha tena kwenye nguvu ya Yesu Kristo wakati tunapo yumbayumba? Rais Nelson alilisema kiurahisi sana: “Ufunguo ni kufanya na kutunza maagano matakatifu. … Si njia yenye utata.”24 Mfanye Kristo kiini cha maisha yako.25

Ikiwa unahisi kwamba nguzo ya mwanga ya ushuhuda wako inatatarika na giza linaingia ndani, vaa ujasiri. Tunza ahadi zako kwa Mungu. Uliza maswali yako. Kwa uvumilivu yeyusha jiwe kuwa kioo. Mgeukie Yesu Kristo, ambaye bado anakupenda.

Yesu alisema, “Mimi ni nuru inayong’aa gizani, nalo giza halikuiweza.”26 Hiyo humaanisha bila kujali linajaribu kiasi gani, giza haliwezi kuiondoa nuru hiyo. Kamwe. Unaweza kuamini kwamba nuru Yake itakuwepo pale kwa ajili yako.

Picha
Hekalu la Salt Lake linapata mwanga tena.

Sisi, au watu tunaowapenda, tunaweza kupata giza kwa muda. Katika suala la Hekalu la Salt Lake, meneja wa nyenzo, Kaka Val White, alipigiwa simu haraka. Watu walikuwa wamegundua. Shida ilikuwa nini kwenye taa za hekalu? Kwanza, wafanyakazi walienda wao wenyewe kwenye kila paneli ndani ya hekalu na kwa mikono waliwasha taa. Kisha walibadilisha betri kwenye mkondo wa kusambaza umeme na kuzijaribu kuona nini kilishindwa.

Ni vigumu kuwasha tena taa ukiwa peke yako. Tunahitaji marafiki. Tunamuhitaji kila mmoja. Kama vile wafanyakazi wa nyenzo wa hekaluni, tunaweza kusaidiana kwa kwenda wenyewe, kuchaji tena betri zetu za kiroho, kurekebisha kilichoharibika.

Picha
Hekalu la Salt Lake wakati wa Krismasi

nuru yetu binafsi inaweza kuwa balbu moja tu ya nuru juu ya mti. Lakini bado tunaangaza nuru yetu ndogo, na sote kwa pamoja kama Temple Aquare wakati wa Krismasi, tunavutia mamilioni ya watu kwenye nyumba ya Bwana. Kizuri zaidi ya yote, kama Rais Nelson alivyohimiza, tunaweza kuleta nuru ya Mwokozi kwetu wenyewe na kwa watu muhimu kwetu kwa matendo rahisi ya kutunza maagano yetu. Katika njia tofauti, Bwana hutoa tuzo kwa tendo hilo la uaminifu kwa nguvu na kwa shangwe.27

Ninashuhudia ninyi mnapendwa. Bwana anajua ni kwa bidii kiasi gani mnajaribu. Mnaonesha maendeleo. Endeleeni kusonga. Yeye anaona dhabihu zenu zote zilizofichika na anazihesabu kwa faida yenu na faida ya wale mnaowapenda. Kazi yenu si bure. Hamko peke yenu. Jina Lake hasa, Emmanuel, humaanisha, “Mungu pamoja nasi.”28 Yeye hakika yuko nanyi.

Piga hatua chache kadhaa kwenye njia ya agano, hata kama kuna giza nene kuona mbali sana. Taa zitawaka tena. Ninashuhudia juu ya ukweli katika maneno ya Yesu, na yamejawa na nuru: “Sogeeni karibu nami na mimi nitasogea karibu na nyinyi; nitafuteni kwa bidii nanyi mtanipata; ombeni, nanyi mtapewa; bisheni, nanyi mtafunguliwa.”29 Katika Jina la Yesu Kristo, amina.