Mkutano Mkuu
Nguvu ya Msukumo wa Kiroho
Mkutano mkuu wa Aprili 2022


Nguvu ya Msukumo wa Kiroho

Ningependa kupendekeza hatua tano mahususi ambazo tunaweza kuchukua ili kutusaidia kudumisha msukumo chanya wa kiroho.

Wapendwa akina kaka na akina dada, nawapenda. Naithamini fursa hii ya kuzungumza nanyi leo? Ninaomba kila siku kwamba mlindwe kutokana na mashambulizi makali ya adui na muwe na nguvu ya kusonga mbele kupitia changamoto zo zote mnazokabiliana nazo.

Majaribio mengine ni mizigo ya kibinafsi ambayo hakuna mtu mwingine anayeweza kuona. Mengine yanatokea kwenye jukwaa la dunia. Migogoro ya kivita huko Uropa mashariki ni mojawapo ya hayo. Nimeshakuwa Ukraine na Urusi mara nyingi. Tunapenda nchi hizo, watu, na lugha zao. Ninalia na kuwaombea wote walioathiriwa na vita hivi. Kama kanisa tunafanya yote tuwezayo kuwasaidia wale wanaoteseka na kuhangaika ili kuishi. Tunawakaribisha kila mtu kuendelea kufunga na kuwaombea watu wote wanaoumizwa na janga hili. Vita vyovyote ni ukiukaji wa kutisha wa kila kitu ambacho Bwana Yesu Kristo anasimamia na anafundisha.

Hakuna hata mmoja wetu anayeweza kudhibiti mataifa au matendo ya wengine au hata washiriki wa familia zetu wenyewe. Lakini tunaweza kujidhibiti mwenyewe. Wito wangu leo, akina kaka na akina dada wapendwa ni kumaliza migogoro inayoendelea mioyoni mwenu, na nyumbani mwenu, na maishani mwenu. Zika mwelekeo wowote wa kutaka kuwaumiza wengine—iwe ni hasira, ulimi mkali, au chuki kwa mtu ambaye amekuumiza. Mwokozi alituamuru kugeuza shavu lingine,1 kuwapenda maadui zetu, na kuwaombea wale wanaotutumia vibaya.2

Inaweza kuwa vigumu sana kuachilia hasira ambayo unahisi kuwa ni ya haki. Inaweza kuonekana kuwa haiwezekani kusamehe wale ambao matendo yao ya uharibifu yamewaumiza wasio na hatia. Na bado, Mwokozi alituonya “tuwasamehe watu wote.”3

Sisi ni wafuasi wa Mfalme wa Amani. Sasa kuliko wakati mwingine wowote, tunahitaji amani ambayo Yeye pekee anaweza kuileta. Tunawezaje kutazamia amani iwepo ulimwenguni ilhali sisi binafsi hatutafuti amani na maelewano? Akina kaka na akina dada, ninajua ninachopendekeza si rahisi. Lakini wafuasi wa Yesu Kristo wanapaswa kuweka kielelezo kwa ulimwengu wote ili wakifuate. Ninawasihi mfanye yote muwezayo kumaliza mizozo ya kibinafsi ambayo kwa sasa inapamba moto mioyoni mwenu na katika maisha yenu.

Naomba nisisitize wito huu wa kuchukua hatua kwa kujadili dhana ambayo nilikumbushwa hivi majuzi nilipokuwa nikitazama mchezo wa mpira wa vikapu.

Katika mchezo huo, kipindi cha kwanza ilikuwa ni pambano la panda shuka. Kisha, katika sekunde tano za mwisho za kipindi cha kwanza, mlinzi wa timu moja alipiga shuti zuri la pointi tatu. Ikiwa imesalia sekunde moja tu, mwenzake alichukua pasi ya kuingia ndani na kutengeneza kikapu kingine kwenye kelele! Kwa hivyo timu hiyo iliingia kwenye chumba cha kubadilishia nguo kwa pointi nne mbele ikiwa na kasi inayoonekana. Waliweza kubeba msukumo huo hadi kipindi cha pili na kushinda mchezo huo.

Msukumo ni dhana ya nguvu sana. Sisi sote tumepitia hali hiyo kwa namna moja au nyingine—kwa mfano, katika gari linaloshika kasi upesi au kwa kutoelewana ambako ghafla hugeuka kuwa mabishano.

Hivyo basi, ninauliza, ni nini kinachoweza kuwasha msukumo wa kiroho? Tumeona mifano ya msukumo chanya na hasi. Tunawajua wafuasi wa Yesu Kristo walioongoka na kukua katika imani yao. Lakini pia tunajua juu ya waumini waliokuwa na msimamo imara wakati mmoja ambao baadae walianguka. Msukumo unaweza kuegemea upande wa njia yo yote ile.

Hatujawahi kuhitaji msukumo chanya wa kiroho kuliko tunavyohitaji sasa, ili kukabiliana na kasi ambayo maovu na alama za giza za nyakati zinaongezeka. Msukumo chanya wa kiroho utatufanya tusonge mbele licha ya kuwako kwa hofu na kutokuwa na uhakika kunakosababishwa na majanga ya ulimwengu, tsunami, milipuko ya volkeno na uhasama wa kutumia silaha. Msukumo wa kiroho unaweza kutusaidia kustahimili mashambulio maovu yasiyo koma ya adui na kuzuia jitihada zake za kuharibu msingi wetu binafsi wa kiroho.

Matendo mengi yanaweza kuwasha msukumo chanya wa kiroho. Utiifu, upendo, unyenyekevu, huduma, na shukrani4 nimetaja chache tu.

Leo ningependa kupendekeza hatua tano mahususi ambazo tunaweza kuchukua ili kutusaidia kudumisha msukumo chanya wa kiroho.

Kwanza: Ingia kwenye njia ya agano na ukae hapo.

Sio muda mrefu uliopita, nilikuwa na ndoto dhahiri ambayo kwayo nilikutana na kundi la watu. Wao waliniuliza maswali mengi, yaliyoulizwa sana yalikuwa ni kuhusu njia ya agano na kwa nini ni muhimu sana.

Katika ndoto yangu, nilieleza kwamba tunaingia katika njia ya agano kwa kubatizwa na kufanya agano letu la kwanza na Mungu.5 Kila wakati tunapopokea sakramenti, tunaahidi tena kujichukulia jina la Mwokozi juu yetu, kumkumbuka Yeye, na kuzishika amri Zake.6 Kwa upande Wake, Mungu anatuhakikishia kwamba tunaweza kila mara kuwa na Roho wa Bwana pamoja nasi.

Baadaye tunafanya maagano ya ziada katika hekalu, ambapo tunapokea ahadi kubwa zaidi. Ibada na maagano hutupatia ufikiaji wa uwezo wa kiungu. Njia ya agano ni njia pekee inayoongoza kwenye kuinuliwa na uzima wa milele.

Katika ndoto yangu, mwanamke kisha aliuliza jinsi mtu ambaye anavunja maagano yake anaweza kurejea kwenye njia hiyo vipi. Jibu langu kwa swali lake linaongoza kwenye pendekezo langu la pili:

Gundua shangwe ya toba ya kila siku.

Je, toba ni muhimu kiasi gani? Alma alifundisha kwamba tunapaswa “tusihubiri chochote ila tu toba na imani kwa Bwana.”7 Toba inahitajika kwa kila mtu anayewajibika ambaye anatamani utukufu wa milele.8 Hakuna kuachiwa. Katika ufunuo kwa Nabii Joseph Smith, Bwana aliwaadhibu viongozi wa mapema wa Kanisa kwa kutofundisha injili kwa watoto wao.9 Kutubu ni ufunguo wa maendeleo. Imani safi hutufanya tusonge mbele kwenye njia ya agano.

Tafadhali usiogope au kuchelewa kutubu. Shetani anafurahia taabu yako. Ikatize. Tupa ushawishi wake nje ya maisha yako. Anza leo kupata furaha ya kumvua mtu wa asili.10 Mwokozi anatupenda siku zote lakini hasa wakati tunatubu. Aliahidi kwamba ingawa “kwani milima itaondoka, na vilima vitaondelewa … wema wangu hautaondoka kwako.”11

Ikiwa unahisi umepotoka nje ya njia ya agano au kwa muda mrefu sana na hauna njia ya kurudi, hiyo kwa urahisi si kweli.12 Tafadhali wasiliana na askofu wako au rais wa tawi. Yeye ni wakala wa Bwana na atakusaidia kupata furaha na msaada wa kutubu.

Sasa, tahadhari: Kurudi kwenye njia ya agano hakumaanishi kuwa maisha yatakuwa rahisi. Njia hii ni kali na wakati mwingine utahisi kama kupanda mwinuko mkali.13 Kupaa huku, hata hivyo, kumeundwa ili kutujaribu na kutufundisha, kusafisha asili zetu, na kutusaidia kuwa watakatifu. Ndiyo njia pekee inayoongoza kwenye kuinuliwa. Nabii mmoja14 alielezea “hali ya heri na furaha ya wale wanaozishika amri za Mungu. Kwani tazama, wanabarikiwa katika vitu vyote, vya kimwili na vya kiroho; na kama watavumilia kwa uaminifu hadi mwisho watapokelewa mbinguni … [na] kuishi pamoja na Mungu katika hali ya furaha isiyo na mwisho.”15

Kuenenda katika njia ya agano, pamoja na toba ya kila siku, huchochea msukumo chanya wa kiroho.

Pendekezo langu la tatu: Jifunze kuhusu Mungu na jinsi Yeye anavyofanya kazi.

Mojawapo ya changamoto zetu kuu leo ni kutofautisha kati ya kweli za Mungu na bandia za Shetani. Ndiyo sababu Bwana alituonya sisi “tuombe daima, … ili [tuweze] kumshinda Shetani, na … kuepuka mikono ya watumishi wa Shetani ambao hufanya kazi zake.”16

Musa alikuwa mfano wa jinsi ya kupambanua kati ya Mungu na Shetani. Shetani alipokuja kumjaribu Musa, yeye aligundua udanganyifu huo kwa sababu alikuwa ametoka tu kukutana na Mungu uso kwa uso. Musa kwa haraka alimtambua Shetani ni nani na kumwamuru aondoke.17 Shetani alipoendelea, Musa alijua jinsi ya kumwomba Mungu msaada zaidi. Musa alipata nguvu za kiungu na akamkemea yule mwovu tena, akisema, “Ondoka kwangu, Shetani, kwa maana ni Mungu huyu mmoja tu nitakayemwabudu.”18

Tunapaswa kufuata mfano huo. Tupa ushawishi wa Shetani nje ya maisha yako. Tafadhali usimfuate hadi kwake “kwenye ghuba ya taabu na msiba usioisha.”19

Kwa kasi ya kutisha, ushuhuda ambao haulishwi kila siku “na neno jema la Mungu”20 unaweza kubomoka. Kwa hivyo, dawa ya njama ya Shetani iko wazi: Tunahitaji uzoefu wa kila siku wa kumwabudu Bwana na kusoma injili Yake. Nakusihi umruhusu Mungu ashinde maishani mwako. Mpe sehemu nzuri ya wakati wako. Unapofanya hivyo, ona kile kinachotokea kwenye msukumo wako chanya wa kiroho.

Pendekezo nambari 4: Tafuta na kutarajia miujiza

Moroni alituhakikishia kwamba “Mungu hajakoma kuwa Mungu wa miujiza”21 Kila kitabu cha maandiko kinaonyesha jinsi Bwana alivyo tayari kuingilia kati maisha ya wale wanaomwamini.22 Aligawanya Bahari ya Shamu kwa ajili ya Musa, akamsaidia Nefi kupata mabamba ya shaba, na kurejesha Kanisa Lake kupitia Nabii Joseph Smith. Kila moja ya miujiza hii ilichukua muda na huenda haikuwa kile hasa ambacho watu hao waliomba kutoka kwa Bwana.

Kwa njia hiyo hiyo, Mungu atakubariki wewe kwa miujiza ikiwa utamwaamini Yeye “pasipo mashaka.”23 Fanya kazi ya kiroho ili kutafuta miujiza. Kwa maombi mwombe Mungu akusaidie kutumia imani ya aina hiyo. Ninaahidi kwamba unaweza kujionea mwenyewe kwamba Yesu Kristo “huwapa nguvu wazimiao; humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo.”24 Mambo machache yataongeza msukumo wako wa kiroho zaidi ya kutambua kwamba Bwana anakusaidia kuhamisha mlima maishani mwako.

Pendekezo nambari 5: Komesha migogoro katika maisha yako binafsi.

Narudia wito wangu wa kumaliza migogoro ndani ya maisha yako. Onyesha unyenyekevu, ujasiri, na nguvu zinazohitajika ili kusamehe na kutafuta msamaha. Mwokozi ameahidi kwamba “maana [sisi] tukiwasamehe watu makosa yao, Baba [yetu] wa mbinguni atatusamehe [sisi] pia.”25

Wiki mbili kuanzia leo tunasherehekea Pasaka. Kati ya sasa na wakati huo, ninakualika utafute mwisho wa mzozo binafsi ambao umekulemea. Je, kunaweza kuwa na tendo linalofaa zaidi la shukrani kwa Yesu Kristo kwa Upatanisho Wake? Ikiwa msamaha unaonekana kutowezekana kwa sasa, omba nguvu kupitia damu ya upatanisho ya Yesu Kristo ili kukusaidia. Unapofanya hivyo, ninaahidi amani binafsi na mlipuko wa msukumo wa kiroho.

Wakati Mwokozi alipolipia dhambi za wanadamu wote, Yeye alifungua njia ambayo wale wanaomfuata wanaweza kupata uwezo Wake wa uponyaji, uimarishaji, na ukombozi. Fursa hizi za kiroho zinapatikana kwa wote wanaotafuta kumsikia na kumfuata Yeye.

Wapendwa kaka zangu na dada zangu, pamoja na kusihi kwa moyo wangu wote, ninawasihi muingie kwenye njia ya agano na kubaki humo. Pata shangwe ya kutubu kila siku. Jifunze kuhusu Mungu na jinsi Yeye anavyofanya kazi. Tafuta na tarajia miujiza. Jitahidi kumaliza migogoro katika maisha yako.

Unapotendea kazi malengo haya, ninakuahidi uwezo wa kusonga mbele kwenye njia ya agano kwa msukumo ulioongezeka, licha ya vikwazo vyo vyote unavyokabiliana navyo. Na ninawaahidi ninyi nguvu kubwa zaidi za kupinga majaribu, amani zaidi ya akili, uhuru kutokana na woga, na umoja mkubwa katika familia zenu.

Mungu yu hai! Yesu ndiye Kristo! Yeye yu hai! Yeye anatupenda, na atatusaidia, Juu ya haya mimi nashuhudia katika jina takatifu la Mkombozi wetu,Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Ona 3 Nefi 12:39.

  2. Ona 3 Nefi 12:44.

  3. Mafundisho na Maagano 64:10; ona pia mstari wa 9.

  4. Kama mtume Paulo alivyosema, “Shukuruni kwa kila jambo”(1 Wathesalonike 5:18.) Mojawapo ya dawa za uhakika wa kukata tamaa, kuvunjika moyo, na uchovu wa kiroho ni shukrani. Je, ni baadhi ya mambo gani tunaweza kumshukuru Mungu? Mshukuru kwa uzuri wa dunia, kwa Urejesho wa injili, na kwa njia zisizohesabika Yeye na Mwanawe hufanya nguvu Zao zipatikane kwetu hapa duniani. Mshukuru Yeye kwa maandiko, kwa malaika wanaojibu maombi yetu kwa Mungu kwa ajili ya usaidizi, kwa ufunuo, na kwa familia za milele. Na zaidi ya yote, tunamshukuru Mungu kwa zawadi ya Mwanawe na Upatanisho wa Yesu Kristo, ambao hufanya iwezekane kwetu sisi kutimiza misheni ambazo kwazo tumetumwa hapa duniani.

  5. Ili kuelewa njia ya agano, ni muhimu kuelewa kwamba agano linahusisha makubaliano ya pande mbili kati ya Mungu na mmoja wa watoto Wake. Katika agano, Mungu huweka masharti, na tunakubaliana na masharti hayo. Kwa kubadilishana, Mungu hufanya ahadi kwetu. Maagano mengi yanaambatana na ishara za nje—au ibada takatifu—ambazo tunashiriki pamoja na mashahidi waliopo. Kwa mfano, ubatizo ni ishara kwa Bwana kwamba mtu anayebatizwa amefanya agano la kushika amri za Mungu.

  6. Ona Moroni 4:3; 5:2; Mafundisho na Maagano 20:77, 79.

  7. Mosia 18:20.

  8. Ona Musa 6:50, 57.

  9. Ona Mafundisho na Maagano 93:40–48.

  10. Ona Mosia 3:19.

  11. Isaya 54:10, msisitizo umeongezwa; ona pia 3 Nefi 22:10. Ukarimu imetafsiriwa kutokana na neno la Kiebrania hesed, neno lenye nguvu lenye maana ya kina ambalo linajumuisha wema, rehema, upendo wa agano, na zaidi.

  12. Inawezekana kufanya fidia kwa baadhi ya dhambi lakini si nyingine. Ikiwa mtu mmoja anamnyanyasa au kupiga mtu mwinginei, au kama mtu atachukua maisha ya mwingine, fidia kamili haiwezi kufanywa. Mwenye dhambi katika hali hizo anaweza tu kufanya mengi, na salio kubwa linalohitajika linabaki deni. Kwa sababu ya utayari wa Bwana kusamehe salio linalostahili, tunaweza kuja Kwake bila kujali ni kwa kiasi gani tumepotoka. Tunapotubu kwa dhati, Yeye atatusamehe. Salio lolote linalonaodaiwa kati ya dhambi zetu na uwezo wetu wa kulipa kamili unaweza kulipwa tu kwa kutumia Upatanisho wa Yesu Kristo, ambaye anaweza kutoa karama ya rehema. Utayari wake wa kusamehe salio letu linalohitajia ni karama isiyokadirika.

  13. Ona 2 Nefi 31:18–20.

  14. Nabii wa Kinefi Mfalme Benyamini

  15. Mosia 2:41.

  16. Mafundisho na Maagano 10:5; msisitizo umeongezwa.

  17. Ona Musa 1:16; ona pia mistari wa 1–20.

  18. Musa 1:20.

  19. Helamani 5:12

  20. Moroni 6:4.

  21. Mormoni 9:15; ona pia mstari wa 19..

  22. Yohana Mtume alitangaza kwamba aliandika miujiza ya Mwokozi ili “kwamba [tuweze] kuamini kwamba Yesu ndiye Kristo” (Yohana 20:31).

  23. Mormoni 9:21.

  24. Isaya 40:29.

  25. Mathayo 6:14.