2016
Baraka za Utiifu
Oktoba 2016


Ujumbe wa Urais wa Kwanza, Oktoba 2016

Baraka za Utiifu

“Somo moja kuu tunaloweza kujifunza duniani,” Rais Thomas S. Monson amefundisha, ni kwamba wakati Mungu anapozungumza na tunatii, daima tutakuwa sahihi.”1

Nasi pia tutabarikiwa. Kama vile Rais Monson alivyosema wakati wa mkutano mkuu wa hivi karibuni: “Tunapotii amri, maisha yetu yatakuwa na furaha tele, yaliyo makamilifu, na sio ya kutatanisha sana. Changamoto na shida zetu zitakuwa rahisi kuvumilia, na tutapokea baraka za [Mungu] alizoahidi.”2

Katika dondoo zifuatazo kutoka katika mafundisho ya Rais Monson kama Rais wa Kanisa, yeye anatukumbusha kwamba amri ni mwongozo wa uhakika katika furaha na amani.

Miongozo ya Safari

Amri za Mungu hazijatolewa ili kutufisha moyo au kuwa vizuizi vya furaha yetu. Ila tu kinyume chake ni kweli. Yule ambaye alituumba sisi na ambaye anatupenda kikamilifu anajua jinsi tunavyohitaji kuishi maisha yetu ili tupate furaha kuu kadiri iwezekanavyo. Ametupa miongozo ambayo, kama tukiifuata, itatuelekeza salama katika safari hii ya maisha ya duniani ambayo mara nyingi ni ya hatari. Tunakumbuka maneno ya wimbo wa injili unaofahamika sana: ‘Keep the Commandments! Katika hii kuna usalama; katika hii kuna amani’ [ona “Keep the Commandments,” Hymns, no. 303].”3

Nguvu na Maarifa

Utiifu ni silika ya manabii; umewapa wao nguvu na maarifa katika zama zote. Ni muhimu kwetu kutambua kwamba sisi, tuna haki ya kupata chanzo hiki cha nguvu na maarifa. Kiko tayari kupatikana kwa urahisi kwa kila mmoja wetu leo pale tunapotii amri za Mungu. …

Maarifa ambayo sisi tunatafuta, majibu ambayo sisi tunayalilia, na nguvu ambazo tunazitamani leo ili kukabiliana na changamoto za ulimwengu changamani na unaobadilika zaweza kuwa zetu pale tuwapo radhi kutii amri za Bwana.4

Chagua Kutii

Mwelekeo wa nyakati zetu ni wenye kuruhusu. Majarida na runinga vinawaonyesha nyota wa sinema, mashujaa wa viwanja vya michezo—wale ambao vijana wengi huwaiga—wakikiuka sheria za Mungu na kuringia mazoea yenye dhambi, ikionekana hakuna athari mbaya. Wewe usiamini hilo! Kuna muda wa mahesabu—hata kuweka sawa kitabu cha mahesabu. Kila Cinderella ana usiku wake wa manane—kama siyo katika maisha haya, basi katika yale yajayo. Siku ya Hukumu itakuja kwa wote. … Ninawaomba mchague kutii.”5

Furaha na Amani

Inaweza kuonekana kwako wakati mwingine kuwa wale walio wa ulimwengu wana raha kukushinda wewe. Wengine wenu mnaweza kuhisi kuwa mnabanwa na mfumo wa kanuni za maadili ambayo sisi katika Kanisa tunazingatia. Kaka zangu na dada zangu, nawatangazieni, hata hivyo, kwamba hapana cho chote kinachoweza kuleta shangwe maishani mwetu au amani kuliko Roho inayoweza kutujia tunapomfuata Mwokozi na tunaposhika amri.”6

Tembea Wima

“Ninashuhudia kwenu kwamba baraka tulizoahidiwa hazina kipimo. Japokuwa dhoruba ya mawingu itajikusanya, japokuwa mvua itatunyeshea, ufahamu wetu wa injili na upendo wa Baba Yetu wa Mbinguni na wa Mwokozi utatufariji na kutuimarisha na kutuletea shangwe katika mioyo yetu tunapotembea wima na kushika amri. Hapatakuwa na kitu katika ulimwengu huu kitakacho tushinda.”7

Mfuate Mwokozi

Je! Ni nani huyu Mtu wa simanzi, aliyezoea huzuni? Je, ni nani Mfalme wa utukufu, huyu Bwana wa majeshi? Yeye ndiye Bwana wetu. Yeye ni Mwokozi wetu. Yeye ni Mwana wa Mungu. Yeye ndiye Asili ya Wokovu wetu. Anatuita ‘Nifuate.’ Anaelekeza, ‘Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo.’ Anasihi, ‘Zishikeni amri zangu.’”

Acheni tumfuate Yeye. Acheni tuige mfano Wake. Acheni tutii neno Lake. Kwa kufanya hivyo, tunampa Yeye zawadi takatifu ya shukrani.”8

Muhtasari

  1. “Waliweka Alama Njia ya Kufuata,” Liahona, Okt. 2007, 5.

  2. “Zishike Amri,” Liahona Nov. 2015, 83.

  3. “Zishike Amri.

  4. “Utiifu Huleta Baraka,” Liahona Mei 2013, 90, 92.

  5. “Amini, Tii, na Vumilia,” Liahona, Mei 2012, 129.

  6. “Stand in Holy Places,” Liahona Nov. 2011, 83.

  7. “Be of Good Cheer,” Liahona, Mei 2009, 92.

  8. “Finding Joy in the Journey,” Liahona, Nov. 2008, 88.

Kufundisha kutoka kwenye Ujumbe Huu

Rais Monson anatufundisha juu ya baraka nyingi tunazoweza kuzipata kwa kuwa watiifu, ukiwemo uwezo, maarifa, furaha, na amani. Fikiria kuwauliza wale unaowafundisha jinsi walivyo barikiwa kwa kutii amri. Unaweza kuwahamasisha kuendelea kutafakari baraka zao na kuandika mawazo yao na uzoefu wao katika shajara. Pia waweza kuwahamasisha kuonyesha shukrani kwa Mungu kwa baraka zao kwa kuendelea kuwa watiifu.