2021
Amani katika Kristo: Zawadi ya Krismasi Isiyo na Gharama na Isiyopitwa na Wakati
Desemba 2021


UJUMBE WA KIONGOZI WA ENEO

Amani katika Kristo: Zawadi ya Krismasi Isiyo na Gharama na Isiyopitwa na Wakati

Kipindi cha msimu huu wa Krismasi na kote katika mwaka, na tutafute ndani ya mioyo yetu kupata uzoefu wa amani ile ya ndani ya milele ambayo huja kutoka kwa Mfalme wa Amani.

Mimi na ndugu zangu, tukiwa watoto, tumekua wakubwa pasipo kujua na kuhisi kile inachomaanisha kufurahia roho halisi ya Krismasi iliyojikita kwenye maisha na huduma ya Mwokozi, Yesu Kristo. Tulisherehekea Krismasi kama tu siku moja maalum. Katika njia nyingi uzoefu wangu wa Krismasi ulikuwa mchanganyiko wa mawazo ya matamanio ya kitoto. Kwangu mimi, siku ya Krismasi ilimaanisha jambo moja: “Zawadi ya Krismasi”. Bila zawadi, hakuna Krismasi.

Licha ya mioyo yetu ya kitoto iliyofokasi tu kwenye “zawadi ya Krismasi”, tulifahamu muda huu kati ya mapumziko ya mwaka ya shule na siku ya Krismasi isingekuwa jambo rahisi. Ungekuwa wakati mgumu ambao nitauita “muda wa kuwa na nidhamu”. Wazazi wetu wenye upendo hawakukubali kisingizio chochote na walihakikisha kwamba kila mmoja ana shughuli ya kufanya. Kila jioni baada ya mlo wa usiku, mpango kazi wa siku iliyofuata ulijadiliwa kwa ufupi na majukumu ya mtu binafsi au kundi yanayoendana na umri wetu yalitolewa. Ilikuwa katika “muda huu wa kuwa na nidhamu” ambapo tulifunzwa thamani ya kazi, umoja wa familia, kubebeana mizigo, kufanya kazi pamoja na ujuzi mwingine wa thamani. Punde kabla ya Krismasi, wazazi wetu wangetoa maamuzi ya ni vizuri jinsi gani tulionesha nidhamu kwenye kazi hizi zote za nyumbani za kujenga uwezo binafsi na shughuli za shambani na wangetoa maamuzi ikiwa tungepokea au kukosa “Zawadi ya Krismasi”. Kwa kiasi kikubwa nimenyenyekezwa na kujawa shukrani kwa “muda huu wa kuwa na nidhamu” wa mafunzo binafsi ambao umeyajenga maisha yangu kwa tabia za milele.

Miaka mingi imepita. Tumekua kutoka matamanio ya utoto kwenda kwenye matamanio ya utu uzima, tukiwa tumejikita kwenye shughuli za maisha yaliyojaa mambo mengi. Kwa uwazi nakumbuka baadhi ya nyakati hizi za kupendeza, za furaha wakati nilipopata “Zawadi yangu ya Krismasi”. Kwa upande mwingine, ni vigumu kusahau siku zisizo za kupendeza za Krismasi ambapo nilikosa “Zawadi yangu ya Krismasi” baada ya kushindwa kufikia matarajio ya wazazi wangu wenye upendo katika kipindi cha “muda wa kuwa na nidhamu”. Ilikuwa kupitia uzoefu huu wa utotoni ambapo nilipenda na kuthamini kuzaliwa kwa mwokozi na msimu wa Krismasi.

Kujua kwamba Krismasi ni msimu, si tu siku moja maalum, ni ya kufurahisha.

Ninafurahiswa kupata amani katika uelewa mtakatifu—kama ambavyo Mtume Paulo alifundisha, “Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu” (Wafilipi 4:7).

Msimu wa Krismasi hakika ni wakati maalum kwa wale wanaomwamini Yeye na kutafuta kumjua Yeye. Katika nyakati hizi zisizo za kawaida tunazoziishi, tunaweza kutumia wakati huu kutafakari vipaumbele vyetu na kugeuza fokasi yetu kumwelekea Mwokozi Yesu Kristo. Mwokozi kwa ukarimu anatusihi, “Nitegemeeni katika kila wazo; msitie shaka, msiogope” (Mafundisho na Maagano 6:36).

Yeye anatupatia hakikisho la amani Yake ya milele. “Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga.” (Yohana 14:27).

Nina shukrani kujua kwamba kuzaliwa kwa Mwokozi ni zawadi isiyo na gharama na isiyopitwa na wakati kutoka kwa Baba yetu wa Mbinguni mwenye upendo kwenda kwa watoto Wake. “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.

“Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye” (Yohana 3:16–17).

Ninanyenyekezwa kwa kiasi kikubwa na nina shukrani nyingi kwa Baba yetu wa Mbinguni kwa zawadi ya Mwanaye mpendwa. Tunapotafuta amani kutoka Kwake, hisia za faraja zitokazo kwa Roho ambazo huja kutoka kwa Mungu kwenda kwa watoto Wake waaminifu, hakika ni “Zawadi ya kweli ya Krismasi”. Tunapaswa kujitahidi kila siku kuishi katika njia ambayo itatuwezesha kupata uzoefu wa amani halisi na ya kudumu katika nyakati zote. Hisia hizi zitakuja kutoka kwa Mfalme wa Amani. Kama Nabii Isaya alivyotangaza: “Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume: na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa Amani” (Isaya 9:6).

Amani hii huja na uelewa wa ukweli rahisi lakini mtakatifu kwamba kupitia Yeye, tunaweza kushinda kifo cha mwili na roho. Kwa sababu Yake, tutaishi tena. Yeye amefanya iwezekane kwetu tusamehewe ikiwa tutatubu. Yeye anatupenda bila mipaka. Yeye anatujua zaidi ya uwezo wetu wa kibinadamu unavyoweza kufafanua. Yeye anatuelewa hata wakati tunapopitia nyakati ngumu zaidi. Yeye bila kuchoka na kwa ukarimu hutualika kutafuta amani Yake ya milele, kama vile alivyofanya katika huduma Yake ya duniani. “Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki: lakini jipeni moyo, mimi nimeushinda ulimwengu” (Yohana 16:33).

Nyakati za hivi karibuni, Bwana alisema, “Jifunze kwangu, na sikiliza maneno yangu; enenda katika unyenyekevu wa Roho wangu, na utapata amani kwangu” (M&M 19:23).

Kipindi cha msimu huu wa Krismasi na kote katika mwaka, na tutafute ndani ya mioyo yetu kupata uzoefu wa amani ile ya ndani ya milele ambayo huja kutoka kwa Mfalme wa Amani. Ndipo tutaweza kuangaza ulimwengu kwa amani na furaha inayoletwa na injili. Kama vile Bwana alivyosema “Nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni” (Mathayo 5:16).

Nina shukrani kwa kuzaliwa kwa Mwokozi, ninajua kwamba maisha Yake, mfano Wake na Upatanisho Wake hufanya zawadi ya thamani ya upendo usio na mwisho kutoka kwa Baba yetu wa Mbinguni kwenda kwa watoto Wake wote. Yeye hakika ni “Zawadi” ambayo daima nitaithamini kwa kina ndani ya moyo wangu.

Laurian P. Balilemwa aliitwa kama Sabini wa Eneo mnamo Oktoba 2020. Amemuoa Happiness Kagemulo; wao ni wazazi wa watoto wawili. Anaishi Dar es Salaam, Tanzania.