2022
“Yule Aitwaye na Bwana, Bwana Humstahilisha”
Februari 2022


SAUTI ZA WAUMINI

“Yule Aitwaye na Bwana, Bwana Humstahilisha”

“Wakati tuwapo katika kazi ya Bwana, tunapokea msaada wa Bwana”.

Rais Thomas S. Monson (1927–2018) alifafanua vyema kwa waumini wa Kanisa kwamba Bwana daima atatusaidia kwenye miito yetu. Alisema, “Yeye aitwaye na Bwana, Bwana humstahilisha”.1

Mnamo 2018, niliitwa kama Mkurugenzi wa Mambo ya Umma kwa ajili ya Kenya na Tanzania. Nilikuwa nimetumikia katika Kamati ya Mambo ya Umma, lakini jukumu hili jipya lilikuwa zito sana kwangu. Nilitekeleza majukumu ya kiuongozi katika kazi yangu, lakini jukumu la kuwa Mkurugenzi wa Mambo ya Umma katika sehemu ambapo Kanisa halijulikani sana na wakati mwingine likikabiliana na vyombo vya habari katili kwa kweli iliniogopesha.

Punde baada ya kupokea wito wangu mpya, niliarifiwa kwamba nabii mpya aliyeidhinishwa, Rais Russell M. Nelson, alikuwa akijiandaa kwa safari ya ulimwenguni kote na kwamba Kenya ingekuwa sehemu mojawapo ambayo angeitembelea. Tuliarifiwa zaidi kwamba Urais wa Eneo umeelekeza kwamba kitengo cha Mambo ya Umma kingeongoza maandalizi ya ujio wa Nabii.

Nilimtembelea Rais wangu wa Kingingi. Nilimweleza jinsi nilivyohisi kutoweza kushughulikia jambo hilo. Alisikiliza kwa makini na kisha akasema, “Kama daima kungekuwa na mtu yeyote ambaye angefaa kufanya shughuli hiyo, sina shaka ni wewe, Dada Jepkemei. Zungumza na Bwana; Yeye atakuongoza na atakusaidia.” Rais wangu wa Kingingi kisha alinipa baraka niliyoihitajika sana na niliyoipokea kwa shukrani kubwa.

Kazi yetu ya kwanza ilikuwa ni kufanya mkutano na waandishi wa habari ili kuitaarifu nchi kuhusu ujio wa nabii. Hili lingekuwa tukio la kwanza la Kanisa kwa vyombo vya habari hapa Kenya. Kwa mshangao wetu, tulikuwa na vyombo vya habari zaidi ya 15 kwenye tukio hili. Pia tulipokea mialiko kutoka kwenye ofisi za matangazo ya vyombo vya habari kwenda na kuzungumza kuhusu Kanisa na ujio wa Nabii. Rais wa kigingi alipangiwa kuliwakilisha Kanisa. Katika hili, alikuwa na udhuru na hakuweza kuhudhuria. Katika dakika ya mwisho, ilikuwa ni lazima mimi nichukue nafasi yake. Siwezi kuelezea woga niliouhisi, lakini nilielekea kwenye kituo cha redio na kujiahidi kwamba nitazungumza kuhusu kile tu nilichokijua na kile nilichokuwa na uzoefu nacho ndani ya Kanisa. Nilijitokeza kwenye kipindi cha asubuhi cha programu ya matangazo ya redio na kuzungumza kwa ujasiri kuhusu Kanisa. Niliweza kujibu maswali yao kwa ujasiri. Matangazo yalienda vizuri na watu kadhaa walipiga simu studio kuwauliza ni jinsi gani wangeweza kujiunga na Kanisa.

Rais Nelson na msafara wake walipowasili, alizungumza nasi na tulihisi upendo wa nabii wa Mungu. Binafsi, nilihisi ukweli wa maneno ya Rais Monson kwamba “wakati tuwapo katika kazi ya Bwana, tunapokea msaada wa Bwana.”2

Hakuna shaka katika akili yangu kwamba mpango wa matembezi ya Nabii ulifanikiwa, si kwa sababu ya uwezo wetu, kwani hatukuwa na uwezo wowote. Ujio ulifanikiwa kwa sababu Bwana alihitaji kazi yake ifanikiwe, na tulijitoa, mapungufu yetu na kila kitu, ili kuwa vyombo katika mikono Yake kuwabariki watakatifu wa Kenya.

Kupitia uzoefu huu mtakatifu, nilijifunza somo la milele, kwamba yeye aitwaye na Bwana, Bwana humstahilisha.

Muhtasari

  1. Thomas S. Monson, “Duty Calls”, Ensign, Mei 1996, 44.

  2. Thomas S. Monson, “Duty Calls”, 44.