2022
Kuitakasa siku ya Sabato
Agosti 2022


UJUMBE WA KIONGOZI WA ENEO HUSIKA

Kuitakasa siku ya Sabato

Jumapili moja asubuhi, tulipokuwa tukielekea kanisani, mwana wetu, Steven, aliyekuwa na umri wa takriban miaka 6 wakati huo, aligundua kwamba baadhi ya vijana walikuwa wakicheza mpira wa miguu mtaani kwetu, na alijiambia mwenyewe: “Nashangaa kwa nini watu hawa wanacheza mpira Jumapili wakati wanapaswa kuhudhuria kanisani!” Ilikuwa wazi kwamba mwanetu alifahamu kwamba Jumapili ni siku maalum ambapo tunahitajika kufanya mambo fulani, na hivyo, tunatarajiwa kujiepusha na mambo mengine. Steven alifahamu kwamba Jumapili ni siku ya Bwana na kwamba tunapaswa kuitakasa.

Katika Kutoka 20:8 tunasoma: “Ikumbuke siku ya Sabato uitakase.” Kwa Kiebrania, neno Sabato humaanisha “mapumziko”. Ni muhimu kukumbuka kwamba Jumapili ni siku ya mapumziko (ya Bwana), ambayo tunahitajika kuitakasa kwani Yeye alipumzika siku ya saba kutoka kazi zake zote1. Kwa ujumla, inaweza kuwa yenye kushawishi kufikiria Jumapili kama siku ya mapumziko, na hakika kupumzika, lakini tunapaswa kuitakasa. Tunapumzika kutoka kazi zetu lakini tunaitumia siku hii kumwabudu Mungu na kuigeuza mioyo yetu kuelekea mambo ya kiroho.

Wakati akihudumu kwenye Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, Rais Russell M. Nelson alijibu swali lifuatalo: “Ni kwa jinsi gani tunaitukuza siku ya Sabato?” Alisema: “Katika miaka yangu ya ujana, nilijifunza kutoka kwa wengine ambao walitengeneza orodha ya mambo ya kufanya na mambo ya kutofanya siku ya Sabato. Ilikuja kutokea baadaye kwamba nilijifunza kutoka kwenye maandiko kwamba mwenendo wangu na mtazamo wangu siku ya Sabato vilitengeneza ishara kati yangu na Baba yangu wa Mbinguni. Kwa uelewa huo, sikuhitaji tena orodha ya mambo ya kufanya na kutofanya”2.

Fundisho hili la Rais Nelson linarejelea andiko lililo katika Kutoka 31:13 ambalo linasema kwamba “Mtazishika Sabato zangu, kwa kuwa ni ishara ambayo kwayo mimi Bwana nawatakasa ninyi.” Rais Nelson alisema kwamba mwenendo wake na mtazamo wake wa siku ya Sabato vilitengeneza ishara kati yake na Baba yake wa Mbinguni, hili linahusika kwetu vilevile. Zaidi ya kupumzika kutoka majukumu yetu ya kila siku, ni ishara ipi tunampa Baba yetu wa Mbinguni ili kumwonesha kwamba tunaitakasa siku hii? Hizi hujumuisha kwenda kanisani kupokea sakramenti na kufanya upya maagano yetu na Mungu, kufanya mikutano ya “Njoo, Unifuate” nyumbani ili kusherehekea neno la Mungu, kuongeza ufahamu wetu juu ya kweli za kiungu, kuimarisha imani yetu katika Yesu Kristo na ushuhuda wetu wa Injili na kutenda mema3 kama vile Yesu alivyofanya siku ya Sabato4. Kwa kufanya hivyo, tunapokea wenzi wa Roho Mtakatifu, tunahisi amani na kusogea karibu zaidi kwa Bwana kupitia agano hili la kudumu5.

Muhtasari

  1. Ona Mwanzo 2:2–3.

  2. Russell M. Nelson, “Sabato ni ya Furaha,” Mkutano Mkuu wa April 2015.

  3. Ona Luka 6:1–11.

  4. Ona Luka 13:11–17; Yohana 5:1–18.

  5. Ona Kutoka 31:16–17.