2023
Kujiandaa Kuhudhuria Hekaluni
Desemba 2023


“Kujiandaa kuhudhria Hekaluni,” Liahona, Des. 2023.

Ujumbe wa kila mwezi wa Liahona, Desemba 2023

Kujiandaa Kuhudhuria Hekaluni

Picha
Watu wakitembea kuelekea Hekalu la Ogden Utah

Picha ya Hekalu la Ogden Utah na Mark Brunson

Ndani ya mahekalu ya Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, tunaweza kupokea maagano na ibada takatifu kwa ajili yetu sisi wenyewe na kwa ajili ya mababu zetu. Tunahudhuria hekaluni ili kuonyesha upendo na shukrani zetu kwa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo. Tunaweza kujiandaa kuhudhuria hekaluni kwa kujifunza na kuishi injili ya Yesu Kristo. Kwa maelezo zaidi kuhusu mahekalu, ona makala ya Misingi ya Injili “Kazi ya Hekalu” katika toleo la Oktoba 2021 la gazeti la Liahona.

Picha
maneno ya nje ya Hekalu la Durban Afrika Kusini

Picha ya Hekalu la Durban Afrika Kusini na Matthew Reier

Nyumba ya Bwana

Mahekalu yanaitwa “nyumba ya Bwana.” Mahekalu ni sehemu takatifu ambapo tunaweza kumhisi Roho wa Mungu na upendo Wake kwetu sisi. Pia ni mahali ambapo tunaweza kufanya maagano na kupokea ibada maalumu ambazo zitatuandaa sisi kupata uzima wa milele. (Maagano ni ahadi takatifu kati ya Mungu na watoto Wake.) Kuwa waaminifu kwenye maagano yetu na kupokea ibada hizi kunatusaidia sisi tuwe na uhusiano maalumu na Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo.

Picha
Kijana amesimama nje ya Helaku la Guayaquil Ecuador

Picha ya Hekalu la Guayaquil Ecuador na Janae Bingham

Nani anaweza Kuhudhuria Hekaluni?

Waumini wa Kanisa wanaweza kufanya ubatizo kwa niaba ya wafu kuanzia katika mwaka ule wanapofikisha miaka 12. Muumini anaweza kupokea endaumenti kama yeye ana angalau mika 18, amekuwa muumini wa Kanisa kwa angalau mwaka mmoja, na anatamani kufanya na kushika maagano ya hekaluni (ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla: Kuhudumu katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, 27.2.2, ChurchofJesusChrist.org). Mwanamume na mwanamke ambao tayari wameshapokea endaumenti zao za hekaluni wanaweza kuunganishwa (kufunga ndoa) kwa ajili ya milele katika hekalu.

Maagano na Ibada

Utafanya maagano na kupokea ibada ndani ya hekalu. “Kuingia katika uhusiano wa agano na Mungu kunatufungamanisha Kwake katika njia ambayo inafanya kila kitu kuhusu maisha kiwe rahisi zaidi” (Russell M. Nelson, “Ushinde Ulimwengu na Upate Pumziko,” Liahona, Nov. 2022, 97). Ibada ni tendo takatifu la kimwili linalotendwa kwa mamlaka ya ukuhani. Ibada ina maana ya kina kiroho. Kwa mfano, unaposhiriki katika ibada, unamwonyesha Mungu kwamba uko radhi kupokea na kushika maagano Yake.

Matayarisho Binafsi

Jiandae kiroho kwa kufuata mafundisho ya Yesu Kristo na kushika maagano uliyofanya na Mungu wakati wa ubatizo. Unaweza pia kujifunza nyenzo za Kanisa, kama vile maandiko na hotuba za mkutano mkuu. Temples.ChurchofJesusChrist.org inatoa taarifa kuhusu kile unachoweza kutegemea wakati unapohudhuria hekaluni. Pia inatoa maelezo ya kina zaidi kuhusu maagano ya hekaluni, ibada, na ishara.

Picha
nje ya Hekalu la Nauvoo Illinois

Picha ya Hekalu la Nauvoo Illinois na Eve Tuft

Ishara

Bwana mara nyingi anafundisha akitumia ishara. Kwa mfano, ubatizo—kuzama majini na kuinuliwa tena—ni kama uzamani wako unakufa na upya wako unazaliwa (ona Warumi 6:3–6). Ibada za hekaluni hutuelekeza kwa Yesu Kristo na Upatanisho Wake. Yawezekana ikawa vigumu kuelewa ishara zote kwa mara ya kwanza unapohudhuria hekaluni, lakini unaweza kuendelea kujifunza kadiri unavyorudi hekaluni katika maisha yako yote.

Kibali cha Hekaluni

Ili kuingia hekaluni, unahitaji kujiandaa na kuwa mwenye kustahili. Unaweza kupokea kibali cha kuingia hekaluni baada ya kuhojiwa na askofu wako au rais wa tawi na rais wa kigingi au wa misioni. Viongozi hawa watakuuliza maswali kadhaa ili kuwa na uhakika wa wewe kuishi injili ya Yesu Kristo. Viongozi wako wanaweza kuzungumza na wewe kuhusu maswali hayo kabla ya muda wa mahajiano.

Kurudi Hekaluni kwa ajili ya Mababu Zako

Baba wa Mbinguni anawataka watoto Wake wote kufanya maagano na Yeye na kupokea ibada takatifu. Ibada hizi, kama vile ubatizo na endaumenti, lazima zifanyike ndani ya mahekalu kwa ajili ya wale ambao walifariki dunia pasipo kuipokea injili. Wewe unaweza kurudi hekaluni ili kufanya ibada kwa washiriki wa familia yako waliokufa.