2023
Siku ya Sabato ni kwa ajili yetu
Desemba 2023


Ujumbe wa Urais wa Eneo

Siku ya Sabato ni kwa ajili yetu

Moja ya changamoto kubwa ya siku zetu ni kubaki tumefokasi kwenye mambo ambayo ni muhimu zaidi na kutoyapuuza kwa sababu ya mambo ya ulimwengu huu wenye matatizo. Mambo yenye umuhimu zaidi ni mambo yale ambayo hudumu milele na hutusaidia tufikie uwezekano wetu wa kiungu. Kile tunachokuwa hutegemea mambo tunayochagua kuyafokasia.

Rais Lorenzo Snow alifundisha:

“Tuko wepesi sana kusahau dhumuni kuu la maisha, msukumo wa Baba yetu wa Mbinguni katika kutuleta hapa kutuweka kwenye maisha ya duniani, vilevile wito mtakatifu ambao kupitia huo tumeitwa; na hivyo, badala ya kuinuka juu ya vitu vya muda … , mara nyingi tunajiruhusu kushuka chini kwenye viwango vya ulimwengu bila kujinufaisha na usaidizi wa kiungu ambao Mungu ameuweka, ambao ndiyo pekee unaweza kutuwezesha kushinda [mambo hayo ya muda].”1

Moja ya vyanzo vyenye nguvu sana vya usaidizi wa kiungu vilivyowekwa na Baba yetu wa Mbinguni ili vitusaidie tuinuke juu ya mambo ya viwango na uharibifu wa ulimwengu ni siku ya Sabato.

Aliamuru: “Ikumbuke siku ya Sabato uitakase” (Kutoka 20:8). Alimpa Musa maelekezo akisema:

“Kisha, nena wewe na wana wa Israeli, na kuwaambia, Hakika mtazishika Sabato zangu, kwa kuwa ni ishara kati ya mimi na ninyi katika vizazi vyenu vyote; ili mpate kujua ya kuwa mimi ndimi Bwana niwatakasaye ninyi.”

“Kwa ajili ya hayo wana wa Israeli wataishika Sabato, kuiangalia sana hiyo Sabato katika vizazi vyao vyote, ni agano la milele.”

“Ni ishara kati ya mimi na wana wa Israeli milele; kwani kwa siku sita Bwana alifanya mbingu na nchi, akastarehe kwa siku ya saba na kupumzika” (Kutoka 31:13, 16–17).

Katika lugha ya Kiebrania, neno Sabato lina maana ya “mapumziko.” Lengo la Sabato linaanzia kwenye Uumbaji wa ulimwengu, ambapo baada ya siku sita za kazi Bwana alipumzika kutokana na kazi ya uumbaji. Tunaelewa kwa nini Baba yetu wa Mbinguni anatualika tuitakase.

Sabato ni muda wa Mungu na siku takatifu, iliyoandaliwa kwa ajili yetu ili tuinue uoni wetu kutoka kwenye mambo ya ulimwengu hadi kwenye baraka za milele. Hivyo, tunaweza “kuelekeza jicho kwa Mungu na tuishi” (Alma 37:46, 47). Siku ya Sabato ni zawadi kutoka kwa Mungu kuja kwetu.

Katika siku zetu Bwana amesema:

“Na ili ujilinde na dunia pasipo mawaa, utakwenda kwenye nyumba ya sala na kutoa sakramenti zako katika siku yangu takatifu;

“Kwani amini hii ndiyo siku iliyoteuliwa kwako kupumzika kutokana na kazi zako, na utoe dhabihu zako za shukrani kwa Aliye Juu Sana” (M&M 59:9–10).

Ni kwa jinsi gani tunaitumia siku hii kusonga karibu na Baba yetu wa Mbinguni na Mwokozi Yesu Kristo?

Mungu amefanya siku hii takatifu iwepo kwetu na ameamuru kwamba katika siku ya sabato, tuhudhurie mikutano ya Kanisa, tupokee sakramenti ili kufanya upya maagano yetu pale tunapokumbuka Upatanisho wa Mwokozi na Mkombozi wetu Yesu Kristo na kuitakasa siku hii takatifu kama watu binafsi na familia, na kuwahudumia wengine, hususani wale ambao hawahisi vizuri, wenye upweke au wenye uhitaji (Math 25:35-40). Unapowainua na kuwaimarisha wengine na kuwasaidia wasonge karibu na Mwokozi, utakuta kwamba wewe pia unasonga karibu zaidi na zaidi Kwake vilevile.

Ni ishara ipi tunayoitoa ili kuonesha upendo wetu kwa Bwana?

Rais Russell M. Nelson alifundisha, “nilijifunza kutoka kwenye maandiko kwamba matendo yangu na mtazamo wangu siku ya Sabato vilibeba ishara kati yangu na Baba yangu wa Mbinguni. Kwa uelewa huo, sikuhitaji tena orodha ya mambo ya kufanya na kutofanya. Wakati nilipopaswa kufanya uamuzi ikiwa shughuli inafaa au haifai kwa ajili ya Sabato, nilijiuliza, ‘ni ishara ipi ninayotaka kumpa Mungu?’ Swali hilo lilifanya chaguzi zangu kuhusu siku ya Sabato ziwe dhahiri kabisa.”2

Ni baraka zipi zimeahidiwa kwa wale wanaoitii na kuitakasa siku ya sabato?

  • Daima tutakuwa na wenza wa Roho Mtakatifu pamoja nasi (3 Nefi 18:7, 11)

  • Tutamjua Yeye kama Bwana wao na Mungu wao (Kutoka 31:13, Ezekieli 20:20)

  • Tutasonga karibu Naye na kutakaswa ndani Yake (M&M 82:10, Moroni 10:32–33)

  • Tutaimarisha muunganiko wa familia zetu

  • Tutasimama kama mashahidi wa Mungu

  • Tutapokea baraka nyingi za kiroho na kimwili

  • Tutajawa shangwe

  • Vyote viijazavyo dunia ni vyetu (M&M 59:16–19)

  • Tutayajenga maisha yetu juu ya mwamba ambao ni Yesu Kristo

  • Tutabaki kwenye njia ya agano

Nilikuwa na miaka 10 wakati familia yangu ilipoipokea injili ya urejesho ya Yesu Kristo. Nilibatizwa siku moja pamoja na Baba na Mama yangu. Moja ya vipengele vipya vya utamaduni wa injili ambavyo tulivifurahia kilikuwa kuhudhuria Kanisani Jumapili, kufanya upya maagano yetu na kuitakasa siku hii nyumbani kwetu. Familia yangu ilikuwa ikiishi mbali sana kutoka mahali ambapo mikutano ya Kanisa ilifanyika. Nakumbuka kama familia, tulijitayarisha kwa ajili ya siku ya sabato. Wazazi wangu walitukumbusha wakati wa jioni ya familia nyumbani kile tunachopaswa kufanya ili kujitayarisha kwa ajili ya siku ya sabato. Tulisali, tulisoma maandiko na tulitayarisha nguo zetu katikati ya wiki. Jumapili, tuliamka mapema asubuhi tukiwa na jambo moja pekee akilini ambalo lilikuwa ni kujitayarisha kufika mapema kwenye eneo la kukusanyika angalau dakika 30 kabla ya mkutano kuanza.

Baba yangu alipenda kusema, ikiwa upo kwenye haraka na kufika kwenye mkutano wa sakramenti ukiwa unatokwa jasho, utakuwa na wakati mgumu kufokasi kwenye kile kilicho muhimu zaidi wakati wa sakramenti ambacho ni Mwokozi Yesu Kristo.

Mwokozi alijitambulisha Yeye mwenyewe kama Bwana wa Sabato (Mathayo 12:8; Marko 2:28; Luka 6:5). Ni siku Yake! Mwokozi Mwenyewe aliitakasa siku ya Sabato wakati wa maisha yake duniani (Math 12:9-13, Luka 4:16, Yohana 5:9).

Kamwe sitasahau masomo haya kutoka kwenye mfano wa wazazi wangu na kujitolea kwao kwa Bwana. Mimi na Dada Mutombo tunajitahidi kufundisha kanuni hizo hizo kwa watoto wetu japokuwa mara nyingi si rahisi.

Bwana amesema, “Na tena, ili mradi wazazi wanao watoto katika Sayuni … ambao hawawafundishi wao kuelewa mafundisho ya toba, imani katika Kristo Mwana wa Mungu aliye hai, na ubatizo na kipawa cha Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono, wafikapo miaka minane, dhambi zao zitakuwa juu ya vichwa vya wazazi” (M&M 68:25).

Ninawaalika wazazi na watoto waifanye siku ya Sabato iwe kipaumbele cha juu. Msiruhusu chochote kiwe kikwazo kwenu na kwa familia zenu cha kufikia baraka zilizoahidiwa kwa wale wanaotii na kuitakasa siku ya sabato. Hakuna mwingine yeyote anayeweza kufanya hilo.

Katika Mkutano Mkuu wa Oktoba 2018, nabii wetu mpendwa Rais Russell M. Nelson alitangaza mabadiliko ya kufikia “usawa na muunganiko mpya kati ya maelekezo ya injili nyumbani na Kanisani.”3

Alisema kwamba kusudi la muda mrefu la Kanisa ni kuwasaidia waumini wote waongeze imani yao katika Bwana wetu Yesu Kristo na Upatanisho Wake, ili iwasaidie katika kufanya na kushika maagano yao na Mungu, na kuimarisha na kuziunganisha familia zao. Katika ulimwengu wa leo wenye mambo mengi, hili si rahisi. Mjaribu anaongeza mashambulizi yake kwenye imani na juu yetu na familia zetu kwa kiwango cha juu. Ili kunusurika kiroho, tunahitaji mbinu za kushambulia na mipango makini. Vivyo hivyo, tunataka sasa kuweka marekebisho ya kitaasisi ambayo yatawaimarisha zaidi waumini wetu na familia zao.”

“Kwa miaka mingi, viongozi wa Kanisa wamekuwa wakifanyia kazi mtaala jumuishi ili kuimarisha familia na watu binafsi kupitia mpango unaolenga nyumbani na kusaidiwa na Kanisa ili kujifunza mafundisho, kuimarisha imani na kuchochea ibada binafsi kwa kiwango kikubwa. Juhudi zetu kwa miaka hii ya karibuni za kuitakasa Sabato—kuifanya iwe ya furaha na ishara binafsi kwa Mungu ya upendo wetu Kwake. Asubuhi hii tutatangaza muunganiko na usawa mpya kati ya maelekezo ya injili nyumbani na Kanisani. Sote tunawajibika kwa ukuaji wetu binafsi wa kiroho. Na maandiko yanaweka wazi kwamba wazazi wana jukumu la msingi la kufundisha mafundisho kwa watoto wao. Ni jukumu la Kanisa kumsaidia kila muumini katika lengo la kiungu lililoainishwa la kuongeza ufahamu wake wa injili.”4

Ratiba ya mkutano wa Jumapili ilirekebishwa kuwa masaa mawili ili kuruhusu muda zaidi kwa ajili ya jioni ya nyumbani na kujifunza injili nyumbani siku ya Jumapili au katika nyakati zingine kadiri watu binafsi na familia watakavyochagua.

Mzee Quentin L. Cook wa Akidi ya Kumi na Wawili aliongeza:

“Kuna mengi zaidi kwenye marekebisho haya zaidi tu ya kufupisha ratiba ya mkutano wa Jumapili kwenye nyumba ya ibada. Madhumuni na baraka zinazoambatana na rekebisho hili na mabadiliko mengine ya hivi karibuni hujumuisha yafuatayo:

  • Kuongeza uongofu kwa Baba wa Mbinguni na Bwana Yesu Kristo na kuimarisha imani Kwao.

  • Kuwaimarisha watu binafsi na familia kupitia mtaala unaolenga nyumbani unaosaidiwa na Kanisa ambao huongeza kwenye shangwe ya kuishi injili, ya Njoo Unifuate.

  • Kuiheshimu siku ya Sabato, tukiwa na fokasi kwenye ibada ya sakramenti.

  • Kuwasaidia watoto wote wa Baba wa Mbinguni kwenye pande zote za pazia kupitia kazi ya umisionari na kupokea ibada na maagano na baraka za hekaluni.”5

Hakika tumebarikiwa kuongozwa na Manabii na Mitume walio hai katika siku zetu. Ninajua kwamba sote ni wana na mabinti wa Baba wa Mbinguni mwenye upendo na Anayejali. Anatamani maendeleo yetu na shangwe ambayo inawezekana kupitia Mwana Wake Yesu Kristo pekee. Injili ya Yesu Kristo na Upatanisho Wake hutoa tumaini na lengo kwenye maisha yetu. Katika jina la Yesu Kristo, Amina.

Tanbihi

  1. Teachings of Presidents of the Church: Lorenzo Snow (2012), 101-2.

  2. Russell M. Nelson “Sabato ni Takatifu”, Mkutano Mkuu wa Aprili 2015.

  3. Russell M. Nelson “Maneno ya Utangulizi”, Liahona, Novemba 2018, 8.

  4. Rais Russell M. Nelson, Maneno ya ufunguzi, Mkutano Mkuu wa Oktoba 2018.

  5. Mzee Quentin L. Cook, “Uongofu wa kina na wa kudumu kwa Baba wa Mbinguni na Bwana Yesu Kristo”, Mkutano Mkuu wa Oktoba 2018.