2010–2019
Kweli za Msingi—Haja Yetu ya Kutenda
Oktoba 2017


Kweli Muhimu—Haja Yetu ya Kutenda

Ono la Kwanza na Nabii Joseph Smith vilileta elimu ya zaida na kweli ambazo ni muhimu kwa furaha yetu katika maisha haya na kuinuliwa kwetu.

Wakati nilipokuwa takriban miaka saba, nilimwuliza mama yangu, “Wakati mimi na wewe tutakapokufa na kwenda mbinguni, wewe utakuwa bado mama yangu?” Yeye hakuwa anatarajia swali kama hili. Lakini akijibu kadiri ya uelewawake, alisema, “Hapana, mbinguni tutakuwa kaka na dada. Sitakuwa mama yako.” Hilo halikuwa jibu nililokuwa natarajia.

Muda fulani baada ya yale maongezi yetu mafupi, vijana wawili walifika kwenye lango la nyumba yetu. Kama muujiza fulani, baba yangu aliwaruhusu kuingia. Walisema walikuwa wamisionari kutoka Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

Wazee hawa, kama tulivyojifunza kuwaita, wakaanza kufundisha familia yetu. Nakumbuka wazi hisia zetu za furaha na msisimko kila muda walipokuja nyumbani kwetu. Walituambia kwamba mvulana alikwenda kwenye kijisitu kumwomba Mungu ili ajue kanisa gani lilikuwa la kweli na kwamba alimuona Mungu na Yesu Kristo.1 Wazee walituonesha mchoro wa ono lile, na wakati nilipoona, nilijua kwamba Joseph Smith hakika alikuwa kweli amemuona Mungu Baba na Yesu Kristo. Wamisionari walisema kwamba kwa sababu ya maono haya, kanisa la kweli la Yesu Kristo lilikuwa tena duniani.2

Picha
Ono la Kwanza

Wamisionari pia walitufundisha mpango wa Mungu wa furaha na walijibu maswali ya famila yetu kuhusu dini. Walitufundisha kwamba familia kwa kweli zinaweza kuwa pamoja baada ya maisha haya kama baba, mama, wana na mabinti.

Familia yetu ilibatizwa. Njia ya kubadili tabia zetu za zamani, kuacha desturi, na kuwa waumini hai wa Kanisa ilikuwa wakati mwingine ina matuta. Lakini kwa sababu ya huruma na upendo wa Mungu na kwa msaada wa viongozi wengi na waumini, tuliweza kuvuka miaka ya kwanza yenye changamoto.

Mamilioni ya watu ambao tayari wamejiunga na Kanisa, vile vile wengi wanaoongolewa na kubatizwa kila wiki, wamepata ushuhuda wa Ono la Kwanza. Roho Mtakatifu anaweza kurudia ushahidi huu kila mara kwa kila mmoja wetu pale tunapojitahidi kuishi kweli rahisi za injili ya Yesu Kristo.

Ono la Kwanza na Nabii Joseph Smith vilileta elimu ya ziada na kweli ambazo ni muhimu kwa furaha yetu katika maisha haya na kuinuliwa kwetu katika uwepo wa Mungu. Nitataja tatu kati ya kweli tulizopata na lazima tuzifanyie kazi kwa sababu mvulana mdogo alipiga magoti na kuomba kwa dhati.

Mungu Huita Manabii Kutuongoza na Kutuelekeza

Ukweli muhimu tunaojifunza kutoka katika Ono la Kwanza na Nabii Joseph Smith ni kwamba Mungu huwaita manabii,3 waonaji, na wafunuzi ili kufundisha, kuelekeza, kuonya na kutuongoza.4 Wanaume hawa ni wasemaji wa Mungu duniani,5 pamoja na mamlaka ya kusema na kutenda katika jina la Bwana.6 Kwa kufuata ushauri wao kabisa, tutakuwa tumekingwa na tutapokea baraka za kipekee katika safari yetu hapa duniani.

Wakati nikisoma katika Chuo Kikuu cha Brigham Young kama kijana, mmisionari mseja aliyerudi kutoka misheni, nilihudhuria kikao cha ukuhani cha mkutano mkuu katika Tabenakulo pale Temple Square. Rais Ezra Taft Benson, wakati huo Rais wa Kanisa, alisihi kila mmisionari aliyerudi kutoka misheni kuchukulia ndoa kwa uzito mkubwa na kuifanya kipaumbele cha kwanza katika maisha yake.7 Baada ya kikao hicho, nilijua nilikuwa nimeitwa kwenye toba na nilihitaji kufanyia kazi ushauri wa nabii.

Kwa hiyo, niliamua kurudi nyumbani nchini, Brazil, kutafuta mke. Kabla sijaondoka kwenda Brazil nikiwa katika mafunzo kwa muda wa miezi miwili, nilimpigia simu mama yangu na baadhi ya marafiki na kutoka kwao nikapata orodha ya takriban wasichana 10—kila mmoja wao akiwa na uwezo wa kuwa mke.

Wakati nikiwa Brazil, baada ya kuomba na kutafakari sana, nilikutana naye, nikamchumbia, na tukapanga tarehe ya kuoana na mmoja wa wasichana kutoka kwenye orodha ile.Haukuwa muda wa kuvunja rekodi kwa wanafunzi waliokuwepo Provo, Utah, kutimiza miadi na kuwa wachumba, lakini ilikuwa haraka sana kwa vigezo vya Brazil.

Miezi michache baadaye, tulioana na Elaine. Yeye ni kipenzi cha maisha yangu na ni baraka ya kipekee.

Sipendekezi kwamba kila mtu atengeneze orodha kama ile, lakini napendekeza—pengine zaidi ya kupendekeza—kwamba wakati wote manabii wetu wanaoishi wanaposema jambo, tulitende.

Picha
Mchoro wa Rais Thomas S. Monson

Nabii wa Mungu leo ni Rais Thomas S. Monson, na tutabarikiwa kwa kufuata ushauri wake kwa usahihi.

Elimu Juu ya Ukweli wa Asili ya Mungu

Ukweli mwingine tunaojifunza kwa sababu ya Ono la Kwanza na Nabii Joseph Smith ni ukweli wa asili ya Mungu. Hebu fikiria jinsi gani tumebarikiwa kujua kwamba Mungu ni kiumbe mwenye mwili wa nyama na mifupa unaoonekana kama wetu,8 kwamba tunaweza kumwabudu Mungu ambaye ni halisi, tunayeweza kumwelewa, na aliyejionesha na kujifunua Yeye Mwenyewe na Mwanawe kwa manabii Wake—wote manabii za kale na manabii katika siku hizi za mwisho.9 Yeye ni Mungu anayesikia na kujibu maombi yetu;10 Mungu ambaye anatuangalia kutoka juu mbinguni11 na anajishughulisha siku zote kuhusu ustawi wetu wa kiroho na kimwili; Mungu hutupa sisi uhuru wa kujiamulia wenyewe kumfuata na kutii amri zake bila kutushurutisha;12 Mungu anayetupa barakana kuturuhusu kukabiliana na majaribu ili tuwezekukua nakuwa kama Yeye.

Yeye ni Mungu mwenye upendo na aliyetoa mpango ambao kupitia mpango huo tunaweza kupata furaha katika maisha haya na ya milele.

Yesu Kristo Ni Mwokozi Wetu.

Kutoka katika Ono la Kwanza na Nabii Joseph Smith, tulipokea elimu ya uhalisi na huduma takatifu ya Bwana Yesu Kristo, ambaye ndiye jiwe la msingi la dini yetu.

Kwa sababu kifo kililetwa ulimwenguni, kama ilivyo hakika kuwa sasa tunaishi, siku moja wote tutakufa.Mojawapo ya athari za kifo ingekuwa kupotea kabisa kwa mwili wetu wa asili; na tusingeweza kufanya chochote kuurudisha katika hali yake. Kwa kuongezea, kwa sababu wote tunatenda dhambi wakati wa safari yetu hapa duniani, kamwe hatungeweza kurudi kwenye uwepo wa Baba yetu wa Mbinguni.

Je, unaweza kufikiria matokeo ya kunyimwa uwepo wa Mungu na tena kamwe kutokuwa na mwili?

Mwokozi na Mkombozi alihitajika kutuweka huru kutokana na kifo na dhambi. Chini ya maelekezo ya Baba wa Mbinguni, Yesu Kristo alikuja duniani, akateseka, akafamsalabani, na akafufuka ili kwamba sisi pia tuweze kufufuka na, kwa toba ya kweli na kufanya na kushika maagano matakatifu, tuweze kwa mara nyingine tena kuwa katika uwepo wa Mungu.

Yakobo aliezea,“Ee jinsi gani ulivyo mkuu wema wa Mungu wetu, anayetutayarishia njia ya kuepuka kunaswa na huyu mnyama mwovu; ndio, huyo mnyama, kifo na jahanamu, ambayo naita kifo cha mwili, na pia kifo cha roho.”13

Picha
Yesu na Mariamu Kaburini

Yesu ni Masiya mwahidiwa, Mtoa sheria, Mtakatifu wa Israel, Bwana wetu, Mwokozi wetu, Mkombozi wetu, Mfalme wetu, Kila Kitu kwetu.

Na sote tuendelee kufanyia kazi kweli hizi muhimu na elimu, tukitoa utii wetu kwa Mungu na Mwanawe Mpendwa. Katika jina la Yesu Kristo, amina.