2010–2019
Dada Watatu
Oktoba 2017


Dada Watatu

Tunawajibika katika uanafunzi wetu wenyewe na inahusika kidogo—kwa vyovyote—na jinsi gani watu hututendea.

Kina dada, marafiki wapendwa, kuanza mkutano mkuu na kikao cha wanawake cha duniani kote ni muhimu na ajabu. Fikirieni tu: kina dada wa kila rika, tabaka, taifa, na lugha wakiunganishwa na imani na upendo kwa Bwana Yesu Kristo.

Tulipokutana hivi karibuni na nabii wetu mpendwa, Rais Thomas S. Monson, alituambia jinsi anavyompenda Bwana. Na mimi najua kwamba Rais Monson ana shukrani sana kwa ajili ya upendo wenu, maombi yenu, ucha mungu wenu kwa Bwana.

Zamani za kale katika nchi ya mbali iliishi familia ya dada watatu.

Dada wa kwanza alikuwa na huzuni. Kila kitu kuanzia puani kwake hadi kwenye kidevu na kuanzia ngozi yake mpaka vidole vyake vya miguu vilionekana si sawa kwake. Alipoongea, maneno yake wakati mwingine yalitoka vibaya, na watu walimcheka. Wakati mtu alipomkosoa au “kusahau” kumwalika kwenye kitu fulani, angekuwa na uso mwekundu, alienda zake, na kutafuta mahali pa faragha ambapo angetoa pumzi nzito ya huzuni na kushangaa kwa nini maisha yalikuwa kiza na ya kuhuzunisha.

Dada wa pili alikuwa na wazimu. Alijifikiria kuwa kama mwenye akili, lakini mara zote kulikuwa na mwingine ambaye alipata zaidi katika majaribio shuleni. Alijichukulia kama mcheshi, mzuri, mtanashati, na wakuvutia. Lakini mara zote ilionekana kuwa kuna mwingine ambaye ni mcheshi zaidi, mzuri zaidi, mtamashati zaidi, au wa kuvutia zaidi.

Hakuwahi kuwa wa kwanza kwenye chochote, na hii hakuweza kuvumilia. Maisha hayakutakiwa kuwa namna hii!

Wakati mwingine aliwashambulia wengine kwa hasira na hii ilionekana kuwa mara zote alikuwa hatua moja katika kuzidiwa na kitu kimoja au kingine.

Bila shaka, hii haikumfanya kupendeka au kuwa maarufu. Wakati mwingine aliuma meno yake, akakunja ngumi kwa nguvu, na kufikiri, “Maisha hayana usawa!”

Basi kulikuwa na dada wa tatu. Tofauti na dada yake, mwenye huzuni na mwenye wazimu, yeye alikuwa —kweli, mwenye shukrani. Na haikuwa kwa sababu alikuwa na akili zaidi au mzuri zaidi au mweza zaidi kuliko dada zake. Hapana, Watu wakati mwingine walimkwepa au kumpuuza. Wakati mwingine walimtania kuhusu alivyovaa au vitu alivyosema. Wakati mwingine walisema vibaya kumhusu. Lakini hakuruhusu chochote kati ya hivyo kumsumbua sana.

Dada huyu alipenda kuimba. Hakuwa na toni nzuri, na watu walicheka kuhusu hilo, lakini hiyo haikumzuia. Angesema, “sitaacha watu wengine na mawazo yao yanizuie kuimba!”

Ukweli kwamba aliendelea kuimba ulimfanya dada yake wa kwanza kuwa na huzuni na wa pili kuwa na wazimu.

Miaka mingi ilipita, na mwishowe kila dada alifikia mwisho wa muda wake katika dunia.

Dada wa kwanza, ambaye aligundua tena na tena kuwa hakukuwa na upungufu wa mambo ya kuvunja moyo katika maisha, hatimaye alikufa akiwa mwenye huzuni.

Wa pili, ambaye kila siku alipata kitu kipya cha kutopenda, alikufa akiwa mwenye wazimu.

Na dada wa tatu aliyeishi maisha yake akiimba wimbo kwa juhudi zake zote na tabasamu la kujiamini usoni mwake, alikufa akiwa mwenye furaha.

Bila shaka, maisha kamwe si rahisi, na watu kamwe si wa kadiri moja kama dada hawa watatu katika hadithi hii. Lakini hata kwa mifano ya kuzidi kiasi kama hii inaweza kutufundisha kitu kutuhusu. Kama wewe ni kama wengi wetu, utakuwa umetambua sehemu yako katika wa kwanza, wa pili au labda katika dada hawa wote watatu. Ngoja tuangalie kwa ukaribu kwa kila mmoja.

Mwathiriwa

Dada wa kwanza alijiona kama mwathiriwa—kama mtu aliyetendewa.1 Ilionekana kama kitu kimoja baada ya kingine viliendelea kutokea kwake ambavyo vilimfanya kujisikia vibaya. Kwa mtazamo huu katika maisha, alikuwa akiwapa wengine utawala juu ya jinsi gani alihisi au kutenda. Tunapofanya hivi, tunasukumwa na kila upepo wa maoni—na katika siku hii ya mitandao ya kijamii kuliko zaidi, pepo hizo huvuma kwa nguvu za kimbunga.

Kina dada wapendwa, kwa nini msalimishe furaha yenu kwa mtu fulani au kundi la watu fulani ambao hujali kidogo sana kuwahusu au furaha yenu?

Kama utajikuta una wasiwasi kuhusu kile watu wengine wanasema juu yako, naweza kupendekeza tiba hii: kumbuka wewe ni nani. Kumbuka kuwa wewe ni wa nyumba ya kifalme ya ufalme wa Mungu, mabinti wa Wazazi wa Mbinguni, ambao wanatawala katika ulimwengu wote.

Mna vinasaba vya kiroho vya Mungu. Mna vipaji vya kipekee ambavyo vimetokana na uumbaji wenu kiroho na ambavyo viliendelezwa kwa wakati mrefu kabla ya maisha ya duniani. Wewe ni mtoto wa Baba wa Mbinguni wa milele mwenye rehema, Bwana wa Majeshi, Yule ambaye aliumba ulimwengu na kusambaza nyota zizungukazo katika eneo pana la anga, na kuweka sayari katika njia zake teule.

Uko katika mikono Yake.

Mikono mizuri zaidi.

Mikono ya upendo.

Mikono yenye kujali.

Na hakuna chochote ambacho yeyote amesema juu yako kitabadili hilo. Maneno yao hayana maana kulinganisha na kile Mungu amesema juu yako.

Wewe ni mtoto Wake wa thamani.

Yeye anakupenda.

Hata wakati ukijikwaa, hata wakati ukigeuka kutoka Kwake, Mungu anakupenda. Kama unahisi kupotea, kutengwa na kusahaulika—usiogope. Mchungaji mwema atakupata. Atakubeba mabegani mwake. Na atakupeleka nyumbani.2

Dada zangu wapendwa, tafadhali acheni kweli hizi zizame kwa kina mioyoni mwenu. Na mtagundua kuwa kuna sababu nyingi za kutokuwa na huzuni, kwa kuwa mna lengo la kutimiza la milele.

Mwokozi wa ulimwengu mpendwa alitoa maisha Yake ili kwamba mngeweza kuchagua kufanya kudra hiyo kuwa halisi. Mmejitwika juu yenu jina Lake; ninyi ni wanafunzi Wake. Na kwa sababu Yake, mnaweza kujivika kwa majoho ya utukufu wa milele.

Mwenye chuki

Dada wa pili alikuwa na hasira na ulimwengu. Kama dada yake mwenye huzuni, alihisi matatizo yote katika maisha yake yalisababishwa na mtu fulani. Aliilaumu familia yake, rafiki zake, bosi wake na wafanyakazi wenzake, polisi, majirani, viongozi wa kanisa, mabadiliko katika fasheni, hata ukali wa miale ya jua na bahati mbaya za wazi. Na aliwashambulia wote kwa hasira.

Yeye hakujifikiria kama mtu katili. Kinyume chake, alihisi kuwa alikuwa akijali maslahi yake. Wengine wote, aliamini, walihamasishwa na ubinafsi, ufinyu na chuki. Yeye, kwa upande mwingine, alihamasika kwa nia nzuri—haki, uadilifu na upendo.

Kwa bahati mbaya, mtazamo wa kufikiria wa dada mwenye wazimu ni wa kawaida sana. Hii ilionekana kwenye uchunguzi wa hivi karibuni kati ya makundi shindani. Kama sehemu ya uchunguzi, wachunguzi waliwasahili Wapelestina na Waisraeli katika Mashariki ya Kati na Wanajamhuri na Wanademokrasia katika Marekani. Waligundua kuwa “kila upande ulihisi kuwa kikundi chao [kilikuwa] kikihamasika kupitia upendo kuliko chuki, lakini wakati walipoulizwa kwa nini kikundi chao pinzani [kili] husika kwenye mzozo, [wali] onyesha kuwa chuki ilikuwa kigezo cha ushawishi katika kundi jingine.”3

Kwa maneno mengine, kila kundi lilijifikiria kama “watu wazuri”—watenda haki, wakarimu na wakweli. Kwa tofauti, waliwaona wapinzani wao kama “watu wabaya—wasiolewa, wasio waaminifu na hata waovu.

Katika mwaka niliozaliwa, dunia ilikuwa imezama katika vita vibaya ambavyo vilileta majonzi mazito nahuzuni ya kutisha ulimwenguni. Vita hivi vilisababishwa na taifa langu—na kundi la watu ambao waliona makundi mengine kama maovu na kuhamasisha chuki dhidi yao.

Waliwanyamazisha wale wasiowapenda. Waliwadhalilisha na kuwatendea uovu. Waliwachukulia kuwa duni—hata si binadamu. Unapoanza kushusha hadhi ya kundi la watu, una uwezekano wa kuhalalisha maneno na vitendo vya vurugu dhidi yao.

Mimi nagwaya kufikiria kuhusu kilichotokea katika Ujerumani ya karne ya 20.

Wakati mtu anapotupinga au kutokubaliana nasi, inatia ushawishi kudhani kuwa lazima kuna kitu ambacho si sawa kwao. Na kutokea hapo, ni hatua ndogo kuunganisha nia mbaya sana katika maneno yao na matendo yao.

Bila shaka, lazima mara zote tusimame kwa kile ambacho ni sahihi, na kuna nyakati ambapo lazima tuinue sauti zetu kwa ajili ya hicho. Hata hivyo, tunapofanya hivyo kwa hasira au chuki katika mioyo yetu—tunapowashambulia wengine kwa hasira kuwadhuru, kuwaaibisha, au kuwanyamazisha—kuwa uwezekano kuwa hatufanyi hivyo katika utakatifu.

Mwokozi alifundisha nini?

“Ninakuambieni, Wapendeni adui zenu, wabarikini wenye kuwalaani, watendeeni mema wale wawachukiao, na waombeeni wale wawatumiao vibaya, na kuwatesa;

“Ili mpate kuwa watoto wa Baba yenu wa Mbinguni.”4

Hii ndio njia ya Mwokozi. Ni katika hatua ya kwanza katika kuvunja vizuizi ambavyo hutengeneza hasira sana, chuki, mgawanyo na vurugu katika dunia.

“Ndio” unaweza kusema “ningekuwa tayari kuwapenda adui zangu—kama tu na wao wangekuwa tayari kufanya hivyo.”

Lakini hii haijalishi sana, au sio? Tunawajibika katika uanafunzi wetu wenyewe na inahusika kidogo—kwa vyovyote—na jinsi gani watu hututendea. Ni kawaida tunatumaini kuwa watakuwa waelewa na wenye hisani kama malipizi, lakini upendo wetu kwao hautegemei hisia zao juu yetu.

Labda juhudi zetu kuwapenda adui zetu zitalainisha mioyo yao na kuwaathiri kwa uzuri. Labda haitakuwa hivyo. Lakini hiyo haibadili msimamo wetu wa kumfuata Yesu Kristo.

Kwa hiyo, kama waumini wa Kanisa la Yesu Kristo, tutawapenda adui zetu.

Tutashinda hasira au chuki.

Tutajaza mioyo yetu na upendo kwa watoto wote wa Mungu.

Tutawafikia katika kuwabariki wengine na kuwahudumia—hata wale ambao wanaweza kututumia [sisi] kwa dharau na kututesa [sisi].”5

Mwanafunzi Halisi

Dada wa tatu anamwakilisha mwanafunzi halisi wa Yesu Kristo. Alifanya kitu ambacho kilikuwa kigumu kufanya—alimuamini Mungu hata katika uso wa kejeli na hali ngumu. Kwa kiasi, aliweza kuendeleza imani yake na tumaini licha ya dharau na ubeuzi kumzunguka. Aliishi kwa furaha, si kwa sababu hali zake zilikuwa za furaha lakini kwa sababu alikuwa mwenye furaha.

Hakuna kati yetu ambaye hufaulu safari ya maisha bila upinzani. Kwa kani nyingi zinazojaribu kutuvuta mbali, ni vipi tunaendelea kuweka mtazamo wetu kwenye furaha tukufu iliyoahidiwa kwa waaminifu?

Ninaamini jibu linaweza kupatikana kwenye ndoto aliyopata nabii, maelfu ya miaka iliyopita. Jina la nabii ni Lehi na ono lake limerekodiwa kwenye Kitabu cha Mormoni cha thamani na ajabu.

Katika ono lake, Lehi aliona uwanda mpana na, humo kulikuwa na mti wa kustaajabisha, mzuri kupita maelezo. Aliona pia kundi kubwa la watu wakisonga kwenye mti. Walitaka kuonja tunda lake tukufu. Walihisi na kuamini kuwa lingewapa furaha kubwa na amani ya kudumu.

Kulikuwa na njia nyembamba kuelekea kwenye mti, na fimbo ya chuma iliyowasaidia kubaki katika njia. Lakini pia kulikuwa na ukungu wa giza ambao uliziba uwezo wao wa kuona njia na mti. Na labda hatari zaidi ilikuwa ni sauti kubwa ya kicheko na kejeli ikitokea kwenye jengo kubwa na pana lililo karibu. Cha kushangaza sana, utani uliweza hata kuwashawishi baadhi ya watu ambao walifika kwenye mti na kuonja tunda la kustaajabisha wakaanza kuhisi aibu na kutangatanga mbali.6

Labda walianza kupata shaka kama kweli mti ulikuwa mzuri kweli jinsi walivyofikiria mwanzo. Labda walianza kujiuliza juu ya uhalisia wa walichokipitia.

Labda walifikiria kama wangegeuka kwenda mbali na mti, maisha yangekuwa rahisi zaidi. Labda wasingefanyiwa kejeli au kuchekwa tena.

Hata hivyo, watu waliokuwa wakiwadhihaki walionekana kama watu waliokuwa na furaha na wakati mzuri. Kwa hiyo, labda kama wangeuacha mti, wangekaribishwa katika kusanyiko la jengo kubwa na pana na kushangiliwa kwa ajili ya uamuzi wao, werevu na ustaarabu.

Baki katika njia

Kina dada wapendwa, marafiki wapendwa, kama unaona ni vigumu kushikilia kwa nguvu fimbo ya chuma na kutembea kwa unyoofu kuelekea kwenye wokovu; kama kicheko na kejeli za wengine ambao wanaonekana wenye kujiamini zinakufanya kuyumba; kama unasumbuliwa na maswali yasiyojibika au mafundisho ambayo huyaelewi bado; kama unahisi kuhuzunishwa kwa sababu ya kuvunjika moyo, nawaasa kukumbuka ono la Lehi.

Baki katika njia!

Kamwe usiachie fimbo ya chuma—neno la Mungu!

Na wakati yeyote akijaribu kukufanya uaibike kwa kuwa umepokea upendo wa Mungu, mpuuze.

Kamwe usisahau, wewe ni mtoto wa Mungu; baraka nyingi ziko kwa ajili yako; kama utajifunza kutenda mapenzi Yake, utaishi Naye kwa mara nyingine tena!7

Ahadi za sifa na kukubalika za kidunia sio za kutegemea, si za kwelina haziridhishi. Ahadi za Mungu ni za uhakika, kweli na za furaha—sasa na milele.

Ninawaalika mfikirie dini na imani katika mtazamo wa juu. Hakuna chochote kitolewacho kwenye jengo kubwa na pana ambacho kinaweza kulingana na tunda la kuiishi injili ya Yesu Kristo.

Kwa kweli, “jicho halijapata kuona wala sikio kusikia, wala havijawahi kuingia kwenye moyo wa mwanadamu, vile vitu Mungu ameviandaa kwa wale wanaompenda.”8

Nimejifunza mimi mwenyewe kuwa njia ya uanafunzi katika injili ya Yesu Kristo ni njia kuelekea kwenye furaha. Ni njia kuelekea kwenye usalama na amani. Ni njia kuelekea kwenye ukweli.

Ninashuhudia kwa kipawa na nguvu za Roho Mtakatifu, mnaweza kujifunza hivi wenyewe.

Kwa wakati huu, kama njia imekuwa ngumu kwenu, natumaini mtapata kimbilio na nguvu katika vitengo vya ajabu vya Kanisa: Msingi, Wasichana, na Muungano wa Usaidizi wa Kina Mama. Ni kama vielekezi katika njia, ambapo unaweza kufanya upya kujiamini kwako na imani kwa ajili ya safari iliyo mbele. Ni nyumba salama, ambapo unaweza kuhisi hisia za uwepo na kupokea utiwaji moyo kutoka kwa akina dada wenzako na wanafunzi wenzako.

Vitu mnavyojifunza katika Msingi huwandaa kwa ajili ya kweli zaidi mnazojifunza katika darasa la Wasichana. Njia ya uanafunzi mtakayotembea katika madarasa ya Wasichana huongoza kwenye ushirika na udada wa Muungano wa Usaidizi wa Kina Mama. Kwa kila hatua katika njia, mnapewa nafasi zaidi za kuonyesha upendo wenu kwa wengine kupitia matendo ya imani, huruma, hisani, maadili, na huduma.

Kuchagua njia hii ya uanafunzi huongoza kwenye furaha na kutimizwa kwa asili yako takatifu.

Haitakuwa rahisi. Itahitajika kila kitu mliichonacho—maarifa yenu yote, ubunifu, imani, uadilifu, nguvu, uamuzi na upendo. Lakini siku moja mtaangalia nyuma katika juhudi zenu na oh mtashukuru kiasi gani kuwa mlibakia imara, kwamba mliamini, na kwamba hamkuacha njia.

Endeleeni Mbele

Kunaweza kuwa na vitu vingi kuhusu maisha ambavyo viko nje ya uwezo wako. Lakini mwishoni, una nguvu ya kuchagua mahali pako pa kufikia na uzoefu wako katika njia. Sio zaidi kuhusu uwezo wako lakini ni chaguzi zako ambazo ndizo huleta tofauti katika maisha.9

Hauwezi kuruhusu hali zikufanye mwenye huzuni.

Hauwezi kuziruhusu zikufanye mwenye wazimu.

Unaweza kufurahia kuwa wewe ni binti ya Mungu. Unaweza kupata shangwe na furaha katika neema ya Mungu na katika upendo wa Yesu Kristo.

Unaweza kuwa na shukrani.

Nawaasa mjaze mioyo yenu na shukrani kwa wingi na uzuri usio na kikomo wa Mungu. Dada zangu wapendwa mnaweza kufanya hivyo. Naomba kwa upendo wote nafsini mwangu kwamba mtafanya uchaguzi wa kuendelea mbele kuelekea kwenye mti wa uzima. Naomba kuwa mtachagua kuinua sauti zenu na kufanya maisha yenu simfoni tukufu ya kusifu, kufurahia kile upendo wa Mungu na maajabu ya Kanisa Lake na Injili ya Yesu Kristo inaweza kuleta duniani.

Wimbo wa mwanafunzi wa kweli unaweza kusikika usio wa toni sahihi au hata wa sauti kubwa kiasi kwa wengine. Tangu enzi za nyakati, imekuwa hivyo.

Lakini kwa Baba yetu wa Mbinguni, na kwa wale wanaompenda na kumheshimu, ni wimbo wa thamani na mzuri—wa hadhi ya juu na wa kutakasa wa pendo okozi na huduma kwa Mungu na wanadamu wenzetu.10

Ninawaachieni baraka zangu kama Mtume wa Bwana kuwa mtapata nguvu na ujasiri wa kunawiri kwa shangwe kama binti ya Mungu wakati kwa shukrani ukitembea kila siku katika njia tukufu ya uanafunzi. Katika jina takatifula Yesu Kristo, amina.