2015
Ushuhuda na Uongofu
Februari 2015


Ujumbe wa Urais wa Kwanza, Februari 2015

Ushuhuda na Uongofu

Picha
Rais Henry B. Eyring

Kuna tofauti kati ya kupokea ushuhuda wa ukweli na kuongoka kwa kweli. Kwa mfano, Nabii mkuu Petro alitoa ushahidi wake kwake Mwokozi kwamba alijua kuwa Yesu alikuwa Mwana wa Mungu.

“[Yesu] akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?

“Naye Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.

“Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Baryona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni (Mathayo 16:15–17).

Na bado baadaye, katika onyo lake kwake Petro, Bwana alimpa yeye na sisi mwongozo wa kuongoka kwa kweli na kufikisha uongofu huo kwa maisha yote. Yesu aliisema hivi: “Utakapoongoka waimarishe ndugu zako” (Luka 22:32).

Yesu alimfundisha Petro kwamba kulikuwa na badiliko kubwa bado ambalo lazima liwe zaidi ya kuwa na ushuhuda hadi kuwa na uwezo wa kufikiria, kuhisi na kutenda kama wafuasi walioongoka kwa kweli wa Yesu Kristo. Hilo ndilo badiliko kuu sote tunatafuta. Mara tu tunapolipokea, tunahitaji badiliko hilo liendelee hadi mwisho wa maisha yetu duniani (ona Alma 5:13–14).

Tunajua kutoka kwa uzoefu wetu wenyewe na kutoka kwa kutazama wengine kwamba, kuwa na matukio machache makuu ya nguvu ya roho hakutatosheleza. Petro alikana kumjua Mwokozi hata baada ya kupokea ushahidi kupitia Roho kwamba Yesu alikuwa ndiye Kristo. Mashahidi Watatu wa Kitabu cha Mormoni walipewa ushuhuda wa moja kwa moja kwamba Kitabu cha Mormoni kilikuwa neno la Mungu, na baadaye walianguka katika uwezo wao wa kumkubali Joseph Smith kama Nabii wa Kanisa la Bwana.

Tunahitaji badiliko katika mioyo yetu, kama ilivyoelezewa katika kitabu cha Alma: “Na wote waliwatangazia watu kitu sawa — kwamba mioyo yao ilikuwa imebadilishwa; kwamba hawakutamani tena kutenda maovu” (Alma 19:33; ona pia Mosia 5:2).

Bwana alitufundisha kwamba tunapoongoka kwa kweli kwa injili Yake, mioyo yetu itabadilishwa kutoka kwa kujijali wenyewe na kubadilika kwa huduma ya kuinua wengine wanaposonga juu kwa uzima wa milele. Ili kupokea uongofu huo, tunaweza kuomba na kutia bidii katika imani ili kuwa kiumbe kipya kilichowezeshwa na Upatanisho wa Yesu Kristo.

Tunaweza kuanza kwa kuombea imani ya kutubu ubinafsi na ya karama ya kujali wengine kuliko sisi wenyewe. Tunaweza kuombea nguvu ya kuweka kando kiburi na wivu.

Maombi yatakuwa funguo pia ya kupokea karama ya kupenda neno la Mungu na ya kumpenda Kristo (ona Moroni 7:47–48). Hayo mawili huja pamoja. Tunaposoma, tunapotafakari, na kuombea neno la Mungu, tutakuja kulipenda. Bwana hulieka katika mioyo yetu. Tunapohisi upendo huo, tutaanza kumpenda Bwana zaidi na zaidi. Na hayo utakuja upendo kwa wengine ambao tunahitaji ili kuimarisha wale ambao Mungu huwaeka kwenye njia yetu.

Kwa mfano, tunaweza kuomba ili kutambua wale ambao Bwana angewataka wamisionari Wake wawafundishe. Wamisionari wa muda wanaweza kuomba kwa imani ili kujua kupitia Roho kile cha kufundisha na kushuhudia. Wanaweza kuomba kwa imani kwamba Bwana atawawezesha kuhisi upendo Wake kwa kila mtu wanaokutana naye. Wamisionari hawatawaleta kila mtu wakutanao naye kwenye maji ya ubatizo na kwenye karama ya Roho Mtakatifu. Lakini wanaweza kuwa na Roho Mtakatifu kama mwenzi. Kupitia huduma yao na pamoja na usaidizi wa Roho Mtakatifu, wamisionari kisha, kwa muda, watabadilishwa katika mioyo yao.

Badiliko hilo litarudiwa tena na tena wao na sisi tunapoendelea bila ubinafsi kutenda kwa imani maishani mwetu mwote kuimarisha wengine na injili ya Yesu Kristo. Uongofu hautakuwa tokeo moja ama jambo litakalo kuwa tu kwa msimu mmoja wa maisha lakini utakua mchakato unaoendelea. Maisha yanaweza kung’aa zaidi hadi siku timilifu, tutakapomuona Mwokozi na kupata kuwa tumekuwa kama Yeye. Bwana alielezea safari hivi: “Kile kilicho cha Mungu ni nuru; na yule ambaye huipokea nuru, na kukaa ndani ya Mungu, hupokea nuru zaidi; na nuru hiyo huzidi kung’ara hata mchana kamilifu.” (M&M 50:24).

Ninawaahidi kwamba hili linawezekana kwa kila mmoja wetu.

Kufundisha kutoka kwa Ujumbe huu

Mzee David A. Bednar wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alitumia “fumbo la achari” kufundisha kwamba uongofu ni mchakato unaoendelea wala si tukio la mara moja: “Mstari juu ya mstari na amri juu ya amri, hatua kwa hatua na karibu bila kujua, nia zetu, fikira zetu, maneno yetu, na vitendo vyetu vinalainika na matakwa ya Mungu” (“Ye Must Be Born Again,” Liahona, Mei 2007, 19). Zingatia kurejelea fumbo hilo la achari na wale unaowafundisha. Kila mmoja wetu anaweza kufanya nini ili kusonga mbele kwa umadhubuti katika mchakato wa hatua kwa hatua wa uongofu ambao Rais Eyring na Rais Bednar wote wanajadili?