2021
Imani ya kuwa Mwenye Kujitegemea
Agosti 2021


UJUMBE WA URAIS WA ENEO

Imani ya kuwa Mwenye Kujitegemea

Didier alirejea kutoka kwenye misheni yake kama yatima bila msaada wa kifamilia au wa kifedha. Katika hali ya kukata tamaa kabisa, alimtegemea Bwana amsaidie kupata shughuli ya kufanya na kujenga biashara yake mwenyewe yenye kuleta faida.

Ikiwa utazingatia matukio ya maisha yako mpaka kufikia hapa ulipo, utatambua kwamba msimamo imara ulikuwa nyuma ya kila jambo zuri ambalo umewahi kufanikisha. Katika kila hali, ulisukumwa na imani imara kwamba lengo lako linafikika. Ulikuwa pia na ujasiri kwamba jinsi ulivyokabiliana na hali ingekuongoza kwenye lengo lako na hili lilikupa msimamo wa kushinda vikwazo ambavyo vilikupa changamoto katika maendeleo yako.

Hiyo ndiyo nguvu ya imani, ambayo Mtume Paulo aliielezea kama “hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana” (ona Waebrania 11:1). Hiyo ni njia nyingine ya kusema kwamba kabla ya kupata chochote kupitia juhudi zetu binafsi, tunakuwa tumeonyesha imani kwamba tuweze kukipata na tulikuwa na msimamo na tulifanya mambo sahihi yaliyohitajika kukipata.

Hadithi ya kweli ya imani ya kuwa mwenye kujitegemea ambayo naona ni yenye kuvutia inamhusu kaka ambaye nitamwita Didier, si jina lake halisi. Didier alitumikia misheni huko Misheni ya Nigeria Calabar wakati mimi nikitumikia huko kama rais wa misheni. Wakati anakamilisha misheni yake, Didier alikuwa akitumikia kama kiongozi wa kanda. Alikuwa mmisionari mtiifu, mwenye msimamo na mchapa kazi. Wazazi wote wa Didier walikuwa wamefariki wakati akiwa bado mdogo. Wakati huo alikuwa chini ya uangalizi wa mjomba wake upande wa mama, ambaye alimkuza na kumtambulisha Kanisani. Lakini kabla ya Didier kukamilisha misheni yake, mjomba wake alikabiliwa na ugonjwa usiotibika na alifariki. Hali za Didier zilionekana za kuchosha na za kukatisha tamaa.

Akirejea nyumbani na bila washiriki wa karibu wa familia yake wenye uwezo wa kuweza kumsaidia, Didier aliamua kwamba angeendelea kuweka tumaini lake katika Bwana ambaye amemvusha mpaka pale alipofikia. Aliamua kutafuta kile ambacho angeweza kufanya ili kusonga mbele katika maisha yake. Kupitia sala, alipata msukumo wa kujifunza kile ambacho watu ambao walikuwa wenye kujitegemea katika mji wake walikuwa wakifanya ili kujikimu. Kwa wiki kadhaa, alitembea mtaani akiingia kutoka duka hadi duka, akiangalia biashara ilivyokuwa ikifanyika na jinsi watu walivyokuwa wakija na kuondoka.

Alifikia hitimisho kwamba pengine angeishi maisha mazuri akiwa kama fundi wa vifaa vya umeme akirekebisha TV, redio na vifaa vingine vya umeme. Tatizo lilikuwa kwamba hakuwa na ujuzi, hakuwa na pesa na hakufahamu wapi pa kuanzia. Tena, kupitia sala, alipata msukumo wa kumuuliza mmiliki wa duka la kurekebisha vifaa vya umeme jinsi ambavyo angepata mafunzo ya vitendo ili afanye kazi kama fundi. Mwanaume yule alimwambia Didier kwamba angempa mafunzo kwa takriban miaka miwili kwa malipo.

Akiwa mwenye furaha, aliwasiliana na mtaalamu wa kujitegemea wa kata na kumwomba afikiriwe kwa ajili ya mkopo wa Mfuko wa Maendeleo ya Elimu (PEF) ili apate pesa za kumlipa mwenye duka na kupata mafunzo ambayo aliamini yangemsaidia kupata pesa za kutosha kukidhi mahitaji yake ya kimwili. Kisha likaja swala lililomkatisha sana tamaa. Mtaalamu alimweleza kwamba mikopo ya PEF ilitolewa tu kwa taasisi za mafunzo zilizojulikana na pesa ya mkopo ingeweza kulipwa moja kwa moja kwenye akaunti ya benki ya taasisi ya mafunzo. Mwenye duka hakuwa taasisi ya mafunzo iliyoandikishwa na hakuwa na akaunti ya benki. Didier alikuwa kwenye mwisho usioendelea.

Lakini Didier alikuwa amechunguza mienendo kwenye duka kiasi cha kutosha kujua kwamba hii ilikuwa biashara nzuri ikiwa angefanya kazi kwa bidii. Zaidi, alivutwa kwenye kazi na alivutiwa na jinsi ambavyo TV isiyofanya kazi punde ingeweza kurejeshewa uhai. Katika wasaa huu wa kukata tamaa zaidi na bila shaka kukosa tumaini, alimrudia tena Bwana katika sala. Msukumo ulikuja kurudi tena kwa mwenye duka, amwelezee hali yake na kujitolea kuingia kwenye mkataba wa mafunzo wakati akifanya kazi kwamba angelipa baada ya kuhitimu mafunzo yake na kuanza kufanya kazi. Hakujua jinsi mwenye duka atakavyojibu, lakini aliamua kujaribu. Baada ya tafakari ya kina, mwenye duka alikubali pendekezo lake kwa sharti kwamba Didier alete maelezo ya mdhamini kutoka uongozi wa eneo lake, kitu ambacho alikifanya kwa furaha.

Miaka miwili baadaye Didier—sasa pamoja na mkewe, mmisionari mwingine aliyemaliza misheni, pembeni yake—alimaliza mkataba wa mafunzo kwa vitendo kama fundi wa kurekebisha vifaa vya umeme. Alijenga uhusiano imara wa uaminifu na mwalimu wake, ambaye pia alikuwa mshauri wake. Didier alikuwa mwanafunzi mzuri na mwenye manufaa kwenye duka. Mwenye duka aliamua kumuajiri kama mfanyakazi, kitu ambacho Didier alikikubali kwa furaha. Hii ilimpa fursa ya kuanza kulipa kile alichokopa kwa haraka kwa ajili ya mkataba wake wa mafunzo.

Mwaka mmoja baadaye, Didier alihisi kwamba alifahamu vya kutosha kuanzisha biashara yake mwenyewe. Kwa kile alichotunza kutokana na kipato chake cha kuajiriwa, alikodi jengo sehemu nyingine ya mji. Kwa kuwa alikuwa amejulikana kwa wateja kadhaa wazuri wakati akifanya kazi pamoja na mwalimu na mshauri wake, biashara yake ilikuwa kwa uimara. Baada ya miaka miwili, alikuwa ametunza pesa za kutosha kununua kontena la futi 40 ambalo lilikuwa likiuzwa kwa makubaliano. Alikodi ardhi ambapo aliliweka kontena na kuhamishia duka lake la ufundi kwenye makazi mapya. Katika mwaka mwingine, alinunua ardhi ambapo duka lake la ufundi lilisimama.

Didier alikuwa sasa akifanya kazi peke yake, akihisi kuyaendesha kikamilifu maisha yake na mwenye shukrani ya kina kwa Bwana kwa kumthibitisha wakati alipotembea kwa bidii kupita ngome isiyo na uhakika katika maisha yake.

Kipindi cha mwaka mmoja na nusu uliopita, janga la ulimwengu la Covid-19 limesababisha uharibifu mwingi kwenye maisha yetu. Yawezekana limejaribu vibaya msingi ambao kwa maumivu makali umejaribu kuujenga kwa miaka mingi na kudidimiza hisia yako ya kuweza kuyadhibiti maisha yako, kiroho na kimwili. Yawezekana limekuzuia hata kupiga hatua ya kuanza.

Tumaini na mwaliko wangu ni kwamba licha ya kiza cha miezi 18 iliyopita na ya chochote kile ulimwengu unachoweza kukirusha kwako ili kujaribu kuharibu tumaini lako, hutaiachilia imani yako. Ninatumaini kwamba utavuta ushawishi kutoka kwenye uzoefu wa Didier, kijana mdogo ambaye nimepata kumjua na ambaye, katika hali ambazo zingeruhusu ukataji tamaa utawale maisha yake, aliamua kumtumaini Bwana na kusonga mbele licha ya uzito wa kuchosha wa kukata kwake tamaa. Leo Didier anahudumu kama mshauri mkuu wa kigingi na yeye na familia yake wako huru. Ana ujasiri kwamba ikiwa atafanya sehemu yake, Bwana atamsaidia kupita changamoto yoyote inayoweza kumkabili.

“Kujitegemea ni uwezo, msimamo na juhudi ya kukimu mahitaji muhimu ya kiroho na ya kimwili ya maisha kwa ajili ya mtu mwenyewe na familia.”1

Nabii Etheri alifundisha kwamba “kwa imani vitu vyote hutimizwa—

Kwa hivyo, yeyote aaminiye katika Mungu angeweza kwa hakika kutumaini ulimwengu bora, ndio, hata mahali katika mkono wa kulia wa Mungu, tumaini ambalo huja kutokana na imani, hutengeneza nanga kwa roho za watu, ambayo ingewafanya kuwa imara na thabiti, wakizidi sana kutenda kazi njema, wakiongozwa kumtukuza Mungu” (Etheri 12:3–4).

Acha mimi na wewe tuwe na imani ya kutambua kwamba, kwa msaada wa Bwana, na “licha ya taabu itakayoshuka juu ya [ulimwengu], . . . kwamba [tuweze] kusimama huru juu ya viumbe wengine chini ya ulimwengu wa selestia” (M&M 78:14).

Joseph W. Sitati aliidhinishwa kama Sabini Mkuu Mwenye Mamlaka mnamo Aprili 2009. Amemuoa Gladys Nangoni, wao ni wazazi wa watoto watano.

Muhtasari

  1. Kitabu cha Maelezo ya Jumla: Kuhudumu katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, sura ya 22, ChurchofJesusChrist.org.