2021
Ukuhani ni Nguvu ya Mungu
Agosti 2021


“Ukuhani ni Nguvu ya Mungu,” Liahona, Agosti 2021

Ujumbe wa Kila Mwezi wa Gazeti la Liahona Agosti 2021

Ukuhani ni Nguvu ya Mungu

Mungu hutubariki kupitia nguvu ya ukuhani. Baraka za ukuhani zinapatikana kwa kila mtu.

Ukuhani ni nguvu ya Mungu. Anatumia nguvu hii kuwabariki watoto Wake wote na kuwasaidia wao kurudi kuishi Naye. Mungu amewapa watoto Wake hapa duniani nguvu ya ukuhani. Kwa nguvu hii, viongozi wa ukuhani wanaweza kuongoza Kanisa, na wenye ukuhani wanaweza kutekeleza ibada takatifu, kama ubatizo, ambao hutusaidia kumkaribia Mungu. Kila mwanaume na mwanamke ambaye hupokea ibada za ukuhani na kutunza maagano (ahadi takatifu) anaweza kupata nguvu za Mungu.

Picha
sakramenti

Joseph Smith Alipewa Nguvu ya Ukuhani

Wakati Yesu Kristo alipokuwa duniani, aliongoza Kanisa Lake kwa nguvu ya ukuhani. Pia aliwapa nguvu hii Mitume Wake. Katika karne baada ya kufa kwao, waumini wengi waliacha Kanisa. Walibadilisha injili kimakosa na jinsi Kanisa lilivyofanya kazi. Ukuhani wa Mungu haukuwa tena duniani. Mnamo 1829, Yesu alimtuma Yohana Mbatizaji na Mitume Petro, Yakobo, na Yohana kumpa Joseph Smith ukuhani. Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni taasisi pekee duniani yenye mamlaka haya ya ukuhani kutoka kwa Mungu.

Picha
urejesho wa Ukuhani wa Melkizedeki

Sauti ya Petro, Yakobo, na Yohana, na Linda Curley Christensen na Michael T. Malm

Funguo za Ukuhani

Funguo za Ukuhani ni mamlaka ya kuelekeza matumizi ya ukuhani, kama vile kutoa ruhusa ya kufanya ibada. Yesu Kristo anashikilia funguo zote za ukuhani. Rais wa Kanisa ndiye mtu pekee duniani ambaye anaweza kutumia funguo za ukuhani kuongoza Kanisa lote. Chini ya uongozi wake, wengine wanaweza kutumia baadhi ya funguo kufanya kazi ya Mungu. Viongozi kama vile maaskofu na marais wa vigingi hutumia funguo za ukuhani kuongoza katika kata zao na vigingi. Kwa sababu miito ya kutumikia hutoka kwa viongozi walio na funguo za ukuhani, wanaume na wanawake ambao hutumikia katika miito hutumia mamlaka ya ukuhani wanapofanya majukumu yao.

Ukuhani wa Melkizedeki na Ukuhani wa Haruni

Ukuhani una sehemu mbili: Ukuhani wa Melkizedeki na Ukuhani wa Haruni. Kupitia Ukuhani wa Melkizedeki, viongozi wa Kanisa huongoza kazi zote za kiroho za Kanisa, kama vile umisionari na kazi ya hekaluni. Ukuhani wa Haruni hufanya kazi chini ya mamlaka ya Ukuhani wa Melkizedeki. Unatumika kutekeleza ibada kama vile ubatizo na sakramenti.

Picha
ubatizo

Baraka za Ukuhani

Kupitia maagano na ibada za ukuhani, Mungu hufanya baraka za ukuhani zipatikane kwa watoto Wake wote. Baraka hizi ni pamoja na ubatizo, kipawa cha Roho Mtakatifu, sakramenti, na ibada za hekaluni. Wanaume na wanawake ambao wamepata endaomenti katika hekalu hupokea zawadi ya nguvu ya ukuhani wa Mungu kupitia maagano yao. Tunaweza pia kupokea baraka za ukuhani za uponyaji, faraja na mwongozo.

Picha
wenzi wapya wakiwa hekaluni

Je, Maandiko Yanasema Nini kuhusu Ukuhani?

Ukuhani uliokuwepo katika siku za kale ni sawa na huu uliopo sasa (ona Musa 6:7).

Funguo za ukuhani zipo ili kuhakikisha kwamba tunakamilisha kazi ya Bwana katika njia sahihi (ona Mafundisho na Maagano 42:11).

Wanaume wanaoshikilia ukuhani wanaweza kuutumia “tu kwa kanuni za haki” (Mafundisho na Maagano 121:36).

Baadhi ya majukumu ya wale wanaoshikilia ukuhani yameelezewa katika Mafundisho na Maagano 20:38–67.