2023
Bwana Alijua
Juni 2023


SAUTI ZA WAUMINI

Bwana Alijua

Mimi ni Mzee Mpinga ninahudumu misheni ya Kinshasa East katika Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, ninatokea wilaya ya Ngandajika Misheni ya Mbuji Mayi Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo.

Mara ya kwanza kupata kulijua kanisa mnamo 2016 ilikuwa kitu cha ajabu kwangu kupokea injili kupitia rafiki zangu wawili tuliosoma darasa moja, ambao leo hii wao pia wanahudumu misheni katika misheni ninayohudumu mimi. Nilisubiri mwaka mzima ili kubatizwa kwani familia yangu walikuwa Wakatoliki na lilikuwa jambo gumu sana kwangu, lakini nashukuru kwa sababu ya sala Bwana alinisaidia na nilibatizwa mnamo Julai 2017. Nilikuwa darasa la tano na nilikuwa muumini pekee wa Kanisa kwenye familia yangu na katika ujirani wangu ambapo ilinibidi nitembee angalau kilomita 9 kila Jumapili ili kuhudhuria mikutano ya Sakramenti jambo ambalo tangu mwanzo lilikuwa gumu kwangu kila Jumapili.

Baada ya ubatizo wangu nilipoteza kazi ndogo niliyokuwa nayo na nilianza kupitia wakati mgumu, wakati wa kipindi hiki kigumu nilifanyia kazi ushauri uliotolewa katika Kumbukumbu la Torati 31:6, ikiwa tu ningeondoa hofu Bwana angenisaidia na kwa msaada wake nilimleta mmoja wa rafiki zangu kanisani ambaye alikuwa mtu wa pili katika ujirani wangu kujiunga na Kanisa na ambaye pia anahudumu misheni leo, nchini Liberia.

Baada ya kuwa nimehitimu, niliamua kutumikia misheni jambo ambalo lilikuwa gumu kwani familia yangu haikukubali mwanzoni na niliamua kufanyia kazi ushauri wa Alma 37:37 na niliomba kwa Bwana anisaidie na nilianza kujitayarisha kwa ajili ya misheni yangu kwa kuweka akiba kidogo ya pesa iliyotokana na kazi yangu ya kufundisha ili isaidie misheni yangu.

Mnamo 2018 wakati nilipotambulisha faili langu kwa ajili ya misheni, Rais Alfred Kyungu ambaye alihudumu misheni ya Mbuji Mayi Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo wakati ule alinifafanulia umuhimu wa kuhudumu misheni na akanisaidia mawazo kadhaa ya kufanyia kazi ili nifike huko. Nilifanyia kazi ushauri huu na ilinichukua takribani miaka miwili kufika huko na mara kwa mara niliwashuhudia wamisionari waliokwenda misheni. Iliniumiza wakati mwingine, pamoja na kila kitu, dhabihu ya kuendesha baiskeli kwa zaidi ya kilometa 68 ili kupata baadhi ya nyaraka nilizohitaji kwa ajili ya misheni yangu nikiwa na akina kaka wengine ambao sote tulikuwa tukijitayarisha.

Tulipokuwa tumetuma mafaili kwenye eneo, janga la ulimwengu la Uviko-19 lilikuwa tayari limeanza kuleta athari kubwa za vifo ulimwenguni kote na wamisionari kutoka nje walilazimika kurejea nyumbani na hatukuwa na uhakika ikiwa tungehudumu misheni. Wiki mbili baadaye Nabii alitangaza kwamba tunapaswa kufunga milango ya kanisa na siku 30 baadaye nilipokea wito wangu wa kuhudumu misheni huko Kinshasa East katika Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo nikiwa na miezi 6 ya kujitayarisha na nikishuhudia ongezeko la idadi ya vifo vinavyohusiana na Covid-19.

Nilikuwa bado katika hali ya kutokuwa na uhakika na nilipiga magoti na nilimwuliza Bwana ikiwa alitaka kuniruhusu niwe mmisionari kwani nilijua binafsi kwamba aliijua hali kikamilifu na tarehe yangu ya kwenda Kituo cha Mafunzo ya Umisionari ilisogezwa mbele kwa wiki tatu zaidi. Mnamo Oktoba 15, 2020 nilianza mafunzo yangu CFM Ghana Accra kupitia teknolojia na nilipitia uzoefu wa kukumbukwa sana wa maisha yangu, kufanya mafunzo kupitia Zoom kila siku kwa wiki tatu kulifanya imani yangu ikue na kuongeza tumaini langu kwa Bwana kwa sababu alijua kwamba alikuwa amenitayarisha ili nimtumikie katika wakati huu wa teknolojia katika kazi yake ili nijifunze njia bora zaidi za kutumia teknolojia na niwasaidie wengine waje kwake kupitia nyenzo hii.

Nina furaha kumtumikia katika wakati huu, ninajua kwamba Baba yetu wa Mbinguni anatujua kila mmoja binafsi na anatutayarisha kwa ajili ya wakati muafaka ili tumtumikie katika wakati wake kwa nyenzo ambazo yeye mwenyewe anazitayarisha ili atusaidie tufike pale. Sala ya dhati ndiyo njia pekee ambayo inaweza kutuleta karibu na yeye na kutusaidia tujitayarishe ili tuwe zaidi kama Mwokozi Yesu Kristo.