2023
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Inapata Mhitimu Wake wa Kwanza wa BYU-Pathway
Juni 2023


Habari za Ndani

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Inapata Mhitimu Wake wa Kwanza wa BYU-Pathway

Clovis Livu Shiku kutoka Kolwezi aliweka historia kwa kuwa mwanafunzi wa kwanza katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kutunukiwa shahada ya kwanza kupitia BYU-Pathway Worldwide. Alitunukiwa shahada ya Sayansi katika Maswala ya Teknolojia kutoka BYU-Idaho mwishoni mwa 2022. Yeye pamoja na wanafunzi wengine watano walijiandikisha kwenye PathwayConnect (kozi unganishi ya BYU-Pathway) mnamo 2019 na kupambana pasipo kuchoka, wakihudhuria madarasa mengi kila msimu.

Mwishoni mwa 2022, alitimiza vigezo vyote kwa ajili ya shahada ya kwanza. Nilipata fursa ya kukutana naye pamoja na mkewe, Raissa, ambaye anasoma ngazi ya cheti kutoka BYU-Idaho. Clovis anasema ilimchukua kufunga sana, maombi na kazi kwa bidii ili kupata shahada yake. “Ninakumbuka kukumbana na changamoto ya intaneti, kompyuta na kukatika kwa umeme mara kwa mara, lakini kwa dhamira na msaada wa Bwana, nimefanikisha,” anasema. “Ni muujiza,” anaongezea. Clovis anafanya kazi kama mhandisi wa mambo ya ufundi kwenye kampuni inayotoa huduma kwa kampuni zingine za uchimbaji madini katika eneo lake na amepandishwa cheo kutokana na ujuzi wake mpya alioupata kutoka kwenye masomo yake. Clovis anahudumu kama Mtaalamu wa Teknolojia wa Kigingi katika Kigingi cha Kolwezi. Yeye pamoja na Raissa wanawasaidia wanafunzi wengine kadhaa kupitia wito wao kama Wamisionari wa Huduma Waandamizi kwa ajili ya BYU-Pathway Worldwide. Hawa wawili ni mifano mikuu ya kile inachomaanisha kutembea na Bwana. Wamekuza imani ya kuhamisha milima katika maisha yao.

Mnamo Januari 2023, sherehe ya kuwatambua wanafunzi wote waliofikia kiwango cha juu katika safari yao ya kuboresha elimu yao ilifanyika huko Kituo cha Kigingi cha Kolwezi. Wanufaika waliopata vyeti vya EnglishConnect na PathwayConnect pamoja na shahada kutoka Chuo cha Ensign na BYU-Idaho walitambuliwa. Mzee Sylvain Kongolo, Sabini wa Eneo alisimamia tukio hilo. Waziri wa Elimu wa eneo hilo pia alihudhuria sherehe na kuongea mengi kuhusu jitihada za Kanisa za kuboresha elimu ya watu wa Kongo.

Kila muhula mpya tunashuhudia ongezeko kubwa katika uandikishaji kote Afrika. Kwa mfano, zaidi ya wanafunzi wapya 2000 walijiandikisha katika PathwayConnect katika muhula wa January 2023 katika maeneo ya Kati na Kusini mwa Afrika, ongezeko la kama 30% ukilinganisha na mwaka jana. Taarifa kuhusu kujiandikisha na vyeti na shahada zitolewazo hupatikana kwenye www.byupathway.org.