Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 78


Sehemu ya 78

Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii, huko Kirtland, Ohio, 1 Machi 1832. Katika siku hiyo, Nabii pamoja na viongozi wengine walikusanyika ili kujadili shughuli ya Kanisa. Ufunuo huu awali ulikuwa ukimwelekeza Nabii, Sidney Rigdon na Newel K. Whitney kusafiri kwenda Missouri na kuanzisha duka la Kanisa na kazi za uchapishaji kwa kuunda “kampuni” ambayo ingesimamia jitihada hizi, ikizalisha fedha kwa ajili ya kuanzisha Sayuni na kwa manufaa ya watu masikini. Kampuni hii, iliyojulikana kama United Firm (Kampuni ya Ushirika) ilianzishwa Aprili 1832 na kuvunjika 1834 (ona sehemu ya 82) Wakati Fulani baada ya kuvunjika kwake, chini ya maelekezo ya Joseph Smith, sentesi kama “shughuli za ghala kwa ajili ya masikini” lilitumika badala ya “duka la bidhaa na kiwanda cha uchapishaji” katika ufunuo, na neno “shirika” lilitumika badala ya neno “kampuni.”

1–4, Watakatifu yawapasa kutengeneza na kuanzisha ghala; 5–12, Matumizi ya busara ya mali zao yatawaelekeza kwenye wokovu; 13–14, Kanisa lazima liwe huru na mamlaka ya kidunia; 15–16, Mikaeli (Adamu) hutumikia chini ya maelekezo ya Mtakatifu (Kristo); 17–22, Heri walio waaminifu, kwa maana watarithi vitu vyote.

1 Bwana alisema kwa Joseph Smith, Mdogo, akisema: Nisikilizeni, asema Bwana Mungu wenu, ninyi ambao mmetawazwa katika ukuhani mkuu wa kanisa langu, ninyi mliojikusanya wenyewe pamoja;

2 Na sikilizeni ushauri wake aliyewatawaza ninyi kutoka juu, ambaye ataongea katika masikio yenu maneno ya hekima, ili wokovu uweze kuwa kwenu katika jambo lile mlilolileta mbele zangu, asema Bwana Mungu.

3 Kwani amini ninawaambia, wakati umefika, na sasa u karibu; na tazama, na lo, hapana budi kuwe na utaratibu wa watu wangu, katika kurekebisha na kuanzisha mambo ya ghala kwa ajili ya watu wangu walio maskini, kote hapa na katika nchi ya Sayuni

4 Kwa uanzishaji na kwa utaratibu wa kudumu na usio na mwisho kwa kanisa langu, ili kuendeleza kazi, ambayo mmeahidi wenyewe, kwa ajili ya wokovu wa mwanadamu, na kwa ajili ya utukufu wa Baba yenu aliye mbinguni;

5 Ili muweze kuwa sawa katika kugawana vitu vya mbinguni, ndiyo, na vitu vya duniani pia, kwa ajili ya kupata vitu vya mbinguni.

6 Kwani msipokuwa sawa katika vitu vya duniani hamwezi kuwa sawa katika kupata vitu vya mbinguni;

7 Kwani kama mnataka kwamba niwape mahali katika ulimwengu wa selestia, lazima mjitayarishe wenyewe kwa kufanya mambo niliyo waamuru na ninayoyataka kutoka kwenu ninyi.

8 Na sasa, amini hivyo ndivyo asemavyo Bwana, ni muhimu kwamba mambo yote yafanyike kwa utukufu wangu, na ninyi ambao mmeungana pamoja katika utaratibu huu;

9 Au, kwa maneno mengine, acha mtumishi wangu Newel K. Whitney na mtumishi wangu Joseph Smith, Mdogo, na mtumishi wangu Sidney Rigdon wakae kwenye kikao pamoja na watakatifu walioko katika Sayuni;

10 Vinginevyo Shetani anatafuta kuigeuza mioyo yao mbali na ukweli, ili aweze kuwapofusha na wasielewe mambo yaliyotayarishwa kwa ajili yao.

11 Kwa hiyo, amri ninaitoa kwenu, kutayarisha na kujisimamia wenyewe kwa mkataba, au agano lisilo na mwisho ambalo haliwezi kuvunjwa.

12 Na yule alivunjaye atapoteza ofisi yake na nafasi yake katika kanisa, naye atapelekwa kwa karamu ya Shetani hadi siku ya ukombozi.

13 Tazama, hili ni tayarisho ambalo kwalo ninawatayarisha ninyi, na msingi, na utaratibu ambao ninautoa kwenu, ambao kwa huo muweze kutimiza amri mlizopewa;

14 Ili kwa majaliwa yangu, licha ya taabu itakayoshuka juu yenu, kwamba kanisa liweze kusimama huru juu ya viumbe wengine chini ya ulimwengu wa selestia.

15 Ili muweze kuja kwenye taji lililotayarishwa kwa ajili yenu, na kufanywa watawala juu ya falme nyingi, asema Bwana Mungu, Mtakatifu wa Sayuni, ambaye aliweka misingi ya Adamu-Ondi-Amani;

16 Ambaye alimteua Mikaeli mtawala wenu, na kuisimamisha miguu yake, na kumweka juu, na kutoa kwake funguo za wokovu chini ya ushauri na maelekezo ya Mtakatifu, ambaye hana mwanzo wa siku zake au mwisho wa uhai.

17 Amini, amini, ninawaambia, ninyi ni watoto wadogo, nanyi bado hamjaelewa jinsi baraka kuu Baba alizo nazo katika mikono yake mwenyewe na amezitayarisha kwa ajili yenu;

18 Na hamwezi kustahmili mambo yote kwa sasa; hata hivyo, changamkeni, kwa kuwa nitawaongoza. Ufalme ni wenu na baraka zake ni zenu na utajiri wa milele ni wenu.

19 Na yule apokeaye vitu kwa shukrani atatukuzwa; na vitu vya dunia hii ataongezewa, hata mara mia, ndiyo, na zaidi.

20 Kwa hiyo, fanyeni mambo niliyowaamuru, asema Mkombozi wenu, hata Mwana Amani, atayarishaye vitu vyote kabla ya kuwachukua;

21 Kwani ninyi ni kanisa la Mzaliwa wa Kwanza, naye atawachukua katika wingu, na kumgawia kila mtu sehemu yake.

22 Na yule aliye mwaminifu na msimamizi mwenye busara atarithi vitu vyote. Amina.