Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 93


Sehemu ya 93

Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii, huko Kirtland, Ohio, 6 Mei 1833.

1–5, Wote walio waaminifu watamwona Bwana; 6–18, Yohana anashuhudia kuwa Mwana wa Mungu alikwenda neema hadi neema mpaka yeye akapokea utimilifu wa utukufu wa Baba; 19–20, Watu waaminifu, wanaokwenda neema hadi neema, pia nao watapata utimilifu Wake; 21–22, Wale walio wazaliwa kupitia Kristo ndiyo Kanisa la Mzaliwa wa Kwanza; 23–28, Kristo alipokea utimilifu wa ukweli wote, na mwanadamu kwa utii anaweza kufanya vivyo hivyo; 29–32, Mwanadamu mwanzoni alikuwa pamoja na Mungu; 33–35, Vitu vya asili ni vya milele, na mwanadamu aweza kupokea utimilifu wa furaha shangwe katika Ufufuko; 36–37, Utukufu wa Mungu ni akili; 38–40, Watoto hawana hatia mbele za Mungu kwa sababu ya ukombozi wa Kristo; 41–53, Ndugu viongozi wanaamriwa kuziweka sawa sawa familia zao.

1 Amini, hivyo ndivyo asemavyo Bwana: Itakuwa kwamba kila mtu atakayeziacha dhambi zake na kuja kwangu, na kulilingana jina langu, na kuitii sauti yangu, na kushika amri zangu, atauona uso wangu na kujua kuwa Mimi ndiye;

2 Na kuwa Mimi ni nuru ya kweli imwangazayo kila mtu ajaye ulimwenguni;

3 Na kuwa Mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu, na kuwa Baba na Mimi tu wamoja—

4 Baba kwa sababu amenipa Mimi utimilifu wake, na Mwana kwa sababu nilikuwepo ulimwenguni na kufanya mwili kuwa hema takatifu yangu, na kuishi miongoni mwa wanadamu.

5 Nami nilikuwa ulimwenguni na nikapokea ya Baba yangu, na kazi zake zikadhihirika wazi.

6 Na Yohana aliona na kushuhudia utimilifu wa utukufu wangu, na utimilifu wa ushuhuda wa Yohana utafunuliwa hapo baadaye.

7 Na alitoa ushuhuda, akisema: Niliuona utukufu wake, kwamba alikuwepo hapo mwanzo, kabla ya ulimwengu kuwepo;

8 Kwa hiyo, hapo mwanzo Neno alikuwepo, kwani alikuwa Neno, hata mjumbe wa wokovu—

9 Nuru na Mkombozi wa ulimwengu; Roho wa kweli, aliyekuja ulimwenguni, kwa sababu ulimwengu uliumbwa naye, na ndani yake mlikuwa na uzima wa wanadamu na nuru ya wanadamu.

10 Dunia ziliumbwa naye; wanadamu waliumbwa naye; vitu vyote viliumbwa naye, na kwa njia yake, na kutoka kwake.

11 Na mimi, Yohana, ninashuhudia kwamba niliuona utukufu wake, kama utukufu wa Mzaliwa Pekee wa Baba, amejaa neema na kweli, hata Roho wa kweli, ambaye alikuja na akakaa katika mwili, na akakaa miongoni mwetu.

12 Na mimi Yohana, niliona kwamba hakupokea utimilifu mwanzoni, bali alipokea neema juu ya neema;

13 Naye hakupokea utimilifu mwanzoni, bali aliendelea kutoka neema hadi neema, mpaka akapokea utimilifu;

14 Na hivyo akaitwa Mwana wa Mungu, kwa sababu hakuwa amepokea utimilifu mwanzoni.

15 Na mimi, Yohana, ninashuhudia, na lo, mbingu zikafunguka, na Roho Mtakatifu akashuka juu yake katika umbo la njiwa, na akatua juu yake, na hapo ikaja sauti kutoka mbinguni ikisema: Huyu ni Mwanangu Mpendwa.

16 Na mimi, Yohana, ninashuhudia kwamba alipata utimilifu wa utukufu wa Baba;

17 Na akapokea uwezo wote, kote mbinguni na duniani, na utukufu wa Baba ulikuwa pamoja naye, kwa kuwa alikaa ndani yake.

18 Na itakuwa, kwamba kama ni waaminifu mtapokea utimilifu wa ushuhuda wa Yohana.

19 Ninayatoa kwenu ninyi maneno haya ili muweze kufahamu na kujua namna ya kuabudu, na kujua nini mnachokiabudu, ili muweze kuja kwa Baba katika jina langu, na kwa wakati wake mpokee utimilifu wake.

20 Kwani ikiwa mnazishika amri zangu mtaupokea utimilifu wake, na kutukuzwa ndani yangu, kama Mimi ndani ya Baba; kwa hiyo, ninawaambia, mtapokea neema juu ya neema.

21 Na sasa, amini ninawaambia, hapo mwanzo nilikuwepo kwa Baba, na Mimi ndiye Mzaliwa wa Kwanza;

22 Na wale wote walio wazaliwa kupitia mimi ni washiriki wa utukufu huo huo, na ndiyo kanisa la Mzaliwa wa Kwanza.

23 Ninyi pia mlikuwepo mwanzoni pamoja na Baba; kile ambacho ni Roho, hata Roho wa kweli;

24 Na ukweli ni maarifa ya mambo kama yalivyo, na kama yalivyokuwa, na kama yatakavyokuwa;

25 Na chochote kilicho zaidi au pungufu ya hivi ni roho wa yule mwovu ambaye alikuwa muongo kutoka mwanzo.

26 Roho wa kweli huyo ndiye wa Mungu. Mimi ni Roho wa kweli, na Yohana alitoa ushuhuda juu yangu, akisema: Alipokea utimilifu wa kweli, ndiyo, hata kweli yote;

27 Na hakuna mtu apokeaye utimilifu isipokuwa amezishika amri zake.

28 Yule azishikaye amri zake hupokea kweli na nuru, hadi ametukuzwa katika kweli na kujua mambo yote.

29 Mwanadamu pia mwanzoni alikuwa na Mungu. Akili, au nuru ya kweli, haikuumbwa au kutengenezwa, na wala kamwe haiwezekani kuwa.

30 Kweli yote ni huru katika mazingira yale ambayo Mungu ameiweka, ili kujiamulia yenyewe, kama akili yote pia; vinginevyo hakuna maisha.

31 Tazama, hapa ndipo ilipo haki ya kujiamulia ya mwanadamu, na hapa ndipo ilipo hukumu ya mwanadamu; kwa sababu kile kilichokuwepo kutoka mwanzoni kinajitokeza wazi kwao, nao hawaipokei nuru.

32 Na kila mtu ambaye roho yake haiipokei nuru iko chini ya hukumu.

33 Kwani mwanadamu ni roho. Vitu vya asili ni vya milele, na roho na vitu vya asili, ambavyo vimeungana na haviwezi kutenganishwa, hupokea shangwe kamilifu;

34 Na vikitenganishwa, mwanadamu hawezi kupokea shangwe kamilifu.

35 Vitu vya asili ni hema takatifu ya Mungu; ndiyo, mwanadamu ni hema takatifu ya Mungu, mahekalu, hata mahekalu; na lolote likichafuliwa, Mungu ataliharibu hekalu hilo.

36 Utukufu wa Mungu ni akili, au, kwa maneno mengine, nuru na kweli.

37 Nuru na kweli humkataa yule mwovu.

38 Kila roho ya mwanadamu haikuwa na dhambi hapo mwanzoni; na Mungu akiwa amekwisha mkomboa mwanadamu kutokana na anguko, wanadamu wakaja tena, katika hali yao ya uchanga, wakiwa safi mbele za Mungu.

39 Na yule mwovu huja na kuziondoa nuru na kweli, kwa kutotii, kutoka kwa wanadamu, na kwa sababu ya mapokeo ya baba zao.

40 Lakini nimewaamuru ninyi kuwalea watoto wenu katika nuru na kweli.

41 Lakini amini ninakuambia, mtumishi wangu Frederick G. Williams, umekaa katika hatia hii;

42 Hujawafundisha watoto wako nuru na kweli, kulingana na amri; na yule mwovu bado anazo nguvu juu yako, na hii ndiyo chanzo cha mateso yako.

43 Na sasa amri ninaitoa kwako—kama utakombolewa utaiweka sawa sawa nyumba yako mwenyewe, kwani kuna mambo mengi yasiyo sawa katika nyumba yako.

44 Amini, ninakuambia wewe mtumishi wangu Sidney Rigdon, kuwa katika baadhi ya mambo hajashika amri kuhusiana na watoto wake; kwa hiyo, kwanza uirekebishe nyumba yako.

45 Amini, ninamwambia mtumishi wangu Joseph Smith, Mdogo, au katika maneno mengine, nitawaita ninyi marafiki, kwa kuwa ninyi ni marafiki zangu, na mtapata urithi pamoja nami—

46 Niliwaita, ninyi watumishi kwa faida ya ulimwengu, na ninyi ni watumishi wao kwa faida yangu—

47 Na sasa, amini ninamwambia Joseph Smith, Mdogo—Hujashika amri, na inakulazimu ukemewe mbele za Bwana;

48 Familia yako lazima itubu na kuacha baadhi ya mambo, na kuyasikiliza kwa makini maneno yako, au, wataondoshwa kwenye nafasi yao.

49 Nisemacho kwa mmoja ninasema kwa wote; ombeni daima asije yule mwovu akawa na nguvu ndani yenu, na kuwaondosha kwenye nafasi yenu.

50 Pia mtumishi wangu Newel K. Whitney, askofu wa kanisa langu, inafaa akemewe, na kuirekebisha nyumba yake, na kuona kuwa wanakuwa na bidii na wenye kujali nyumbani, na kuomba daima, au vinginevyo wataondoshwa kwenye nafasi yao.

51 Sasa, ninawaambia marafiki zangu, na mtumishi wangu Sidney Rigdon aende safari yake, na afanye haraka, na pia akitangaza mwaka uliokubaliwa wa Bwana, na injili ya wokovu, vile nitakavyompa kunena; na kwa sala yenu ya imani kwa nia moja nitamsaidia.

52 Na watumishi wangu Joseph Smith, Mdogo, na Frederick G. Williams wafanye upesi pia, nao watapewa kulingana na sala ya imani; na kadiri mtakavyoshika maneno yangu hamtashindwa katika ulimwengu huu, wala katika ulimwengu ujao.

53 Na, amini ninawaambia, kwamba ni mapenzi yangu kuwa mfanye upesi kutafsiri maandiko yangu, na kupata maarifa ya historia, na ya mataifa, na ya falme, ya sheria za Mungu na mwanadamu, na hii yote ni kwa ajili ya wokovu wa Sayuni. Amina.