2010–2019
Kwamba Naye Apate Kuwa Imara Pia
Oktoba 2016


Kwamba Naye Apate Kuwa Imara Pia

Naomba kwamba tutainuka na kutimiza wito wa kuwainua wengine ili kuwaandaa kwa ajili ya huduma zao tukufu.

Ninajiona kuwa nimebarikiwa kuwa katika mkutano huu pamoja na wale wanaoshikilia ukuhani wa Mungu. Kujitolea, imani, na huduma isiyo na uchoyo ya kundi hili la wanaume na wavulana ni muujiza wa kisasa. Ninanena usiku huu na wenya ukuhani, walioungana kwa moyo wote katika huduma kwa Bwana Yesu Kristo.

Bwana hutoa nguvu Zake kwa wote walio katika ofisi zote za ukuhani ambao kwa uaminifu huhudumu katika kazi zao ya kikuhani.

Wilford Woodruff, kama Rais wa Kanisa, alielezea uzoefu wake katika ofisi za ukuhani:

“Nilisikia mahubiri ya kwanza kabisa kuyasikia katika Kanisa hili. Siku iliyofuata nilibatizwa. … Nilitawazwa kuwa Mwalimu. Misheni yangu ikaanza mara moja. … Niliendelea na misheni yangu yote kama Mwalimu Wakati wa mkutano mkuu nitawazwa kuwa Kuhani. … Baada ya kutawazwa kuwa Kuhani nilipelekwa … kwenye misheni nchi za upande wa kusini. Hiyo ilikuwa katika majira ya majani kupukutika ya 1834. Nilikuwa na mwenzangu, na tulianza pasipo kuwa na mkoba wala fedha. Nilisafiri pekee yangu kwa maili nyingi na nikahubiri Injili, na nilibatiza idadi kubwa ya watu ambao sikuweza kuwathibitisha katika Kanisa, kwa sababu mimi nilikuwa Kuhani tu. … nilisafiri kwa muda mrefu nikihubiri Injili kabla ya kutawazwa kuwa Mzee. …

“[Sasa] nimekuwa kwa takribani miaka hamsini na minne mshiriki wa wale Mitume Kumi na Wawili. Nimesafiri pamoja na hao na akidi nyingine sasa kwa miaka sitini; na ninataka kusema kwa mkutano huu kwamba nimekuwa nikisaidiwa na nguvu za Mungu wakati nikishikilia ofisi ya Mwalimu, na hasa wakati nikisimamia katika shamba la mzabibu kama Kuhani, jinsi nilivyo kama Mtume. Hakuna tofauti katika hili ilimradi sisi tunatimiza wajibu wetu.”1

Kwamba uwezekano wa kiroho huu wa ajabu wa kutokuwa tofauti unapendekezwa katika ufafanuzi wa Bwana juu ya Ukuhani wa Haruni kama “kiambatisho” cha Ukuhani wa Melkizedeki.2Neno kiambatisho humaanisha hivyo viwili vimeungana. Mwunganisho huu ni muhimu kwa ukuhani kuwa nguvu na baraka inayoweza kuwa, katika ulimwengu huu na milele yote, kwani “hauna mwanzo wa siku au mwisho wa miaka.”3

Mwunganisho huu ni rahisi. Ukuhani wa Haruni huwaandaa vijana wa kiume hata kwa kazi takatifu zaidi.

“Ile nguvu na mamlaka ya juu zaidi, au Ukuhani wa Melkizedeki, ni kushikilia funguo za baraka zote za kiroho za kanisa—

“Kuwa na haki ya kupokea siri za ufalme wa mbinguni, mbingu kufunuliwa kwao, kuwasiliana na baraza kuu na kanisa la Mzaliwa wa Kwanza, na kufurahia ushirikiano wao na uwepo wa Mungu Baba, na Yesu aliye mpatanishi wa agano jipya.”4

Funguo za ukuhani hizo hutumika ipasavyo na mtu mmoja tu kwa wakati mmoja, Rais na kuhani mkuu msimamizi wa Kanisa la Bwana. Tena, kwa kunaibishwa mamlaka na Rais, kila mwanaume mwenye Ukuhani wa Melkizedeki anaweza kupewa mamlaka na haki ya kunena na kutenda katika jina la Mwenyezi. Hakuna kikomo kwa nguvu hiyo. Inahusu uzima na mauti, familia na Kanisa, asili kuu ya Mungu Mwenyewe na kazi Yake ya milele.

Bwana humwandaa mwenye Ukuhani wa Haruni kuwa mzee akihudumu kwa imani, uweza, na kwa shukrani katika ule Ukuhani wa Melkizedeki uliotukuka.

Kwa wazee, kuwa na shukrani ya kina itakuwa muhimu kwa kucheza sehemu yako katika huduma kamilifu ya ukuhani. Utakumbuka siku zako kama shemasi, mwalimu, au kuhani wakati wale walioshikilia ukuhani wa juu walipokufikia na kukuinua na kukutia moyo katika safari yako ya kikuhani.

Kila mwenye kushikilia Ukuhani wa Melkizedeki anazo kumbukumbu hizi, lakini wazo la shukrani yawezekana likatoweka kwa miaka mingi kupita. Tumaini langu ni kuwasha tena hisia zile na kwa hizo kudhamiria kutoa kwa wote unaoweza kuwapa msaada wa aina hiyo hiyo ambao nawe wakati mmoja ulipokea.

Ninamkumbuka askofu mmoja ambaye alinitendea mimi kama vile nilikuwa tayari kile ambacho nilikusudiwa kuwa katika nguvu za ukuhani. Aliniita mimi Jumapili moja wakati nilipokuwa kuhani. Alisema alinihitaji mimi kuwa mwenza wake wakati akiwatembelea baadhi ya waumini wa kata yetu. Alifanya isikike kana kwamba mimi nilikuwa tumaini lake katika kufanikiwa. Hakunihitaji. Alikuwa na washauri wazuri sana kwenye uaskofu wake.

Tulimtembelea mjane fukara na aliyekuwa na njaa. Alinitaka mimi nimsaidie kuugusa moyo wake, nimpe changamoto ya kufanya na kutumia bajeti, na nimwahidi kuwa angeweza kuinuka na kuwa katika nafasi siyo za kujitunza bali pia kuwasaidia wengine.

Tulikwenda baadaye kuwafariji wasichana wadogo wawili waliokuwa wakiishi katika hali ngumu. Tulipokuwa tukiondoka kwao, aliniambia kimya kimya, “Watoto wale kamwe hawatasahau kwamba tulikuja kwao.”

Kwenye nyumba iliyofuata, nilijionea namna ya kumwalika mtu asiyehudhuria kikamilifu kurejea kwa Bwana kwa kumshawishi kwamba waumini katika tawi wanamhitaji yeye.

Askofu yule alikuwa mwenye Ukuhani wa Melkizedeki ambaye alikuwa akiinua uonaji wangu na kunisaidia kwa kuwa mfano. Alinifundisha kuwa na nguvu na ujasiri wa kwenda kokote katika utumishi kwa ajili ya Bwana. Yeye alikwisha enda muda mrefu kupokea tuzo yake, lakini mimi bado namkumbuka kwa sababu alinifikia nikiwa chini wakati nilipokuwa mwenye Ukuhani wa Haruni asiye na uzoefu wowote. Nilijifunza baadaye kwamba yeye aliniona mimi kwenye njia ya ukuhani yenye majukumu makubwa, hata kupita ono langu mimi mwenyewe.

Baba yangu alifanya vivyo hivyo kwa ajili yangu. Yeye alikuwa mkongwe mwenye hekima na mwenye Ukuhani wa Melkizedeki. Wakati mmoja aliombwa na Mtume mmoja kuandika juu ya ushahidi wa kisayansi juu ya umri wa dunia. Aliandika kwa uangalifu mkubwa, akijua kwamba baadhi ya wale ambao wangeweza kuisoma walikuwa na hisia kali kwamba dunia ilikuwa changa zaidi kuliko vile ushahidi wa kisayansi ulivyokuwa ukipendekeza.

Bado nakumbuka baba yangu akinikabidhi mkononi kile alichoandika na kusema, Hal, unayo hekima ya kiroho kujua kama inafaa niipeleke kwa mitume na manabii.” Siwezi kukumbuka zaidi kile ambacho ile karatasi ilisema, lakini nitabeba milele pamoja nami shukrani niliyojisikia kwa huyu mkuu mwenye Ukuhani wa Melkizedeki ambaye aliona ndani yangu hekima ya kiroho ambayo mimi sikuweza kuiona.

Usiku mmoja, miaka kadhaa baadaye, baada ya kuwa nimekwisha tawazwa kuwa Mtume, nabii wa Mungu aliniita na kuniomba kusoma kitu fulani ambacho kiliandikwa juu ya mafundisho ya Kanisa. Alikuwa amesoma sura za kitabu usiku kucha. Alisema huku akicheka chini chini, “Siwezi kumaliza yote haya. Wewe hupaswi kupumzika wakati mimi nafanya kazi.” Na kisha akatumia maneno karibu yale yale ambayo baba yangu aliyatumia miaka mingi kabla: “ Hal, wewe ndiye unayepaswa kusoma haya. Wewe utajua kama ni sahihi kuchapisha haya”

Utaratibu ule ule wa wenye Ukuhani wa Melkizedeki wa kuinua uonaji na kuwapa wengine kujiamini ulikuja usiku mmoja wa sherehe za mahubiri zilizodhaminiwa na Kanisa. Katika umri wa miaka 17 niliulizwa kunena kwenye kundi kubwa la wasikilizaji. Sikuwa na wazo nini kilitarajiwa kutoka kwangu. Sikuwa nimepewa mada ya kunena, na hivyo mimi nikaandaa hotuba ambayo ilikuwa zaidi ya kile nilichokijua juu ya injili. Wakati nikizungumza, niligundua kwamba nimefanya kosa. Naweza bado kukumbuka baada ya kuongea hisia zangu za kushindwa kule.

Aliyefuata na mzungumzaji wa mwisho alikuwa Mzee Matthew Cowley wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili. Yeye alikuwa mnenaji mahiri—aliyependwa kote katika Kanisa. Bado nakumbuka nikimtazama kutoka kwenye kiti changu karibu ya mimbari.

Alianza kwa sauti yenye nguvu. Yeye alisema kwamba hotuba yangu ilimfanya yeye ajisikie kuwa yuko kwenye mkutano mkuu. Alitabasamu wakati akisema hayo. Hisia zangu za kushindwa zikaniacha na zikafuatiwa na kujiamini kwamba siku fulani nitakuwa kile alichoonekana kufikiria kuwa tayari mimi nilikuwa.

Kumbu kumbu za usiku huo bado zinaniongoza mimi kusikiliza kwa uangalifu wakati mwenye Ukuhani wa Haruni anapozungumza. Kwa sababu ya kile Mzee Cowley alichonifanyia, daima natarajia kwamba nitasikia neno la Mungu. Ni mara chache sana navunjwa moyo na daima nashangazwa, na siwezi ila kutabasamu kama vile Mzee Cowley alivyofanya.

Mambo mengi yanaweza kuwasaidia kaka zetu wadogo ili kuinuka katika ukuhani, lakini hakuna kinachoweza na chenye nguvu zaidi kuliko kuwasaidia kwetu kukuza imani yao na kujiamini kwamba wanaweza kuvuta nguvu ya Mungu katika huduma yao ya ukuhani.

Imani hiyo na kujiamini haikutakaa nao kwa tukio moja la kuinuliwa hata na mwenye Ukuhani wa Melkizedeki aliye na kipawa sana. Uwezo wa kuvuta nguvu hizo lazima hupaliliwe kwa onyesho la kuamini kutoka kwa wale walio na uzoefu mwingi katika ukuhani.

Wenye Ukuhani wa Haruni pia watahitaji kutiwa moyo kila siku na hata kila saa na marekebisho kutoka kwa Bwana Mwenyewe kwa njia ya Roho Mtakatifu. Hiyo itakuwepo kwa ajili yao kadiri wanavyochagua kubaki kuwa wenye kustahili. Hii itategemea chaguzi wanazofanya.

Hii ndiyo sababu lazima tufundishe kwa mfano na kwa ushuhuda kwamba yale maneno ya kiongozi mkuu wa Ukuhani wa Melkizedeki Mfalme Benjamini ni ya kweli.5 Ni maneno ya upendo yaliyonenwa katika jina la Bwana ambaye ukuhani huu ni Wake. Mfalme Benjamini anatufundisha nini kinahitajika ili kubaki wasafi vya kutosha ili kupokea kutiwa moyo na kurekebishwa na Bwana.

“Na mwisho, siwezi kukuambia mambo yote ambayo kwayo waweza kutenda dhambi; kwani kuna njia nyingi na namna nyingi, hata nyingi kiasi kwamba siwezi kuhesabu.

“Lakini kiasi hiki naweza kukuambia, kwamba kama huwezi kujihadhari mwenyewe, na mawazo yako, na maneno yako, na matendo yako, na kuzishika amri za Mungu, na kudumu katika imani juu ya yale uliyosikia juu ya kuja kwa Bwana wetu, hata mwisho wa maisha yako, lazima utaangamia. Na sasa, Ee mwanadamu, kumbuka, na usiangamie.6

Sisi wote tunafahamu juu ya mishale ya moto ya yule adui wa haki inayotumwa kama upepo mkali dhidi ya vijana wenye ukuhani ambao tunawapenda sana. Kwetu sisi wanaonekana kama wale vijana askari, ambao wenyewe walijiita wana wa Helamani. Wanaweza kunusurika kama  wale vijana askari walivyofanya, kama watajitunza salama kama Mfalme Benjamini alivyowashauri wao wafanye.

Wana wa Helamani hawakuwa na shaka. Walipigana kwa ujasiri na wakaibuka washindi kwa sababu waliamini maneno ya mama zao.7 Tunaelewa nguvu ya imani ya mama mwenye upendo. Akina mama hutoa msaada mkubwa kwa wana wao hata leo Sisi, wenye ukuhani, tunaweza, na ni lazima tuongeze kwenye msaada ule tukiwa na lengo la kutimiza wajibu kwamba kadiri tunavyoongoka, tunapaswa kushuka chini ili kuwaimarisha ndugu zetu hawa.8

Maombi yangu ni kwamba kila mwenye Ukuhani wa Melkizedeki ataipokea fursa iliyotolewa na Bwana:

“Na kama mtu yeyote miongoni mwenu akiwa imara katika Roho, na amchukue yule aliye dhaifu pamoja naye, ili aweze kuelekezwa katika unyenyekevu kamili, ili naye aweze kuwa imara pia.

“Hivyo basi, wachukueni pamoja nanyi wale waliotawazwa katika ukuhani mdogo, na watumeni mbele yenu ili kufanya ahadi, na kutayarisha njia, na kutimiza ahadi ambazo ninyi wenyewe hamtaweza kutimiza.

“Tazama, hii ndiyo njia ambayo mitume wangu, katika siku za zamani, walinijengea kanisa langu.”9

Ninyi viongozi wa ukuhani na kina baba wa wenye Ukuhani wa Haruni mnaweza kufanya miujiza. Mnaweza kujaza nafasi za wazee waaminifu pamoja na vijana ambao wanakubali wito wa kuhubiri injili na kufanya hivyo kwa kujiamini. Mtawaona wengi mliowainua na kuwatia moyo wakibaki wakiwa waaminifu, wakifunga ndoa kwa uaminifu hekaluni, na baadae nao wakiwainua wenzao na kuwaandaa wengine.

Haitahitaji programu mpya, vitabu vipya vya kufundishia, au vyombo bora zaidi vya habari. Haitahitaji wito wo wote mpya zaidi ya huu ulio nao sasa. Kiapo na agano la ukuhani linakupa nguvu, mamlaka na mwongozo. Ni maombi yangu utaenda nyumbani na kujifunza kwa uangalifu kiapo na agano la ukuhani, hupatikana katika Mafundisho na Maagano sehemu ya 84.

Sisi sote tunatumaini kwamba vijana wengi watapata uzoefu kama wa Wilford Woodruff, ambaye, akiwa mwenye Ukuhani wa Haruni, alifundisha injili ya Yesu Kristo kwa nguvu za kuongoa.

Naomba kwamba tutainuka na kutimiza wito wa kuwainua wengine ili kuwaandaa kwa ajili ya huduma zao tukufu. Ninawashukuru kwa moyo wangu wote watu wema walioniinua na kunionyesha namna ya kuwapenda na kuwainua wengine.

Ninashuhudia kwamba Thomas S. Monson anashikilia funguo zote za ukuhani duniani kwa wakati huu. Ninatoa ushuhuda kwamba yeye, kwa huduma ya maisha yake yote, amekuwa mfano wa kuwagusa kwetu wote na kuwainua wengine kama mtu mwenye Ukuhani wa Melkizedeki. Mimi binafsi ninashukuru kwa namna ambavyo ameniinua na kunionyesha namna ya kuwainua wengine.

Mungu Baba yu hai. Yesu ndiye Kristo. Hili Kanisa na ufalme Wake. Huu ni ukuhani Wake. Mimi najua mwenyewe kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Katika jina la Yesu Kristo, Amina.