2010–2019
Kuna Nguvu katika Kitabu
Oktoba 2016


Kuna Nguvu katika Kitabu

Nguvu kubwa zaidi ya Kitabu cha Mormoni ni uwezo wake wa kutuleta karibu zaidi na Yesu Kristo.

Mnamo Juni 14, 1989, kutokana na taarifa potofu kuhusu Kanisa, serikali ya Ghana ilipiga marufuku shughuli zote za Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ndani ya nchi ile ya Kiafrika. Serikali ikatwaa majengo yote ya Kanisa na shughuli zote za kimisionari zikasimamaishwa. Waumini wa Kanisa ambao waliuita wakati huu kama “katazo,” walifanya kadiri walivyoweza kuishi injili pasipo mikutano ya matawi au pasipo msaada wa wamisionari. Kuna hadithi nyingi za kuvutia juu ya namna waumini walivyodumisha nuru ya injili ikiwaka kwa kuabudu majumbani mwao na wakihudumiana kama walimu wa nyumbani na walimu watembeleaji.

Hatimaye kutoelewana huko kulitatuliwa, na mnamo Novemba  29, 1990, katazo hilo liliondolewa na shuhuli za kawaida za Kanisa zikaanza upya.1 Tangu hapo, kumekuwa na mahusiano mazuri sana baina ya Kanisa na serikali ya Ghana.

Waumini walioishi katika kipindi hicho cha katazo ni wepesi kuelezea baraka zilizokuja kutokana na kipindi hicho kisicho cha kawaida. Imani za wengi iliimarishwa, kupitia taabu ambayo walipambana nao. Lakini baraka moja ya katazo hilo ilikuja kwa namna isiyo ya kawaida.

Nicholas Ofosu-Hene alikuwa polisi kijana aliyepangiwa kulinda jengo la mikutano la Kanisa wakati huu wa katazo. Kazi yake ilikuwa kulinda Kanisa usiku. Nicholas alipofika kwenye nyumba hiyo, aliona vitu vimetawanyika huku na kule, makaratasi, vitabu, na samani zikiwa katika mchafukoge. Kati kati ya vurugu hiyo, yeye aliona nakala ya Kitabu cha Mormoni. Alijaribu kukipuuza kitabu hicho kwa sababu aliambiwa ni kiovu. Lakini alishangaa kuwa alikuwa akivutiwa nacho. Mwishowe, Nicholas hakuweza kukipuuza zaidi. Akakiokota. Akajiona kama analazimika kuanza kukisoma. Alikisoma usiku kucha, na kuona machozi yakimtiririka mashavuni mwake wakati akikisoma.

Mara ya kwanza alipokiokota, alisoma 1 Nefiyote. Mara ya pili, yeye akasoma 2 Nefiyote. Alpofika 2 Nefi mlanngo wa 25alisoma yafuatayo: “Na tunazungumza juu ya Kristo, tunafurahi katika Kristo, tunahubiri juu ya Kristo, tunatoa unabii juu ya Kristo, na tunaandika kulingana na unabii wetu, ili watoto wetu wapate kujua ni chanzo kipi watazamie kwa ajili ya ondoleo la dhambi zao.”2

Kuna wakati Nicholas alimsikia Roho kwa nguvu mno kiasi kwamba akaanza kulia kwa sauti. Akatambua kwamba wakati wa kusoma kwake alipokea mavuvio kadhaa ya kiroho kwamba kitabu kile kilikuwa maandiko matakatifu, yaliyo sahihi kuliko yoyote aliyopata kusoma yeye. Akatambua kwamba Watakatifu wa Siku za Mwisho, kinyume na kile alichosikia, kwa nguvu sana wanaamini katika Yesu Kristo. Baada ya katazo kumalizika na wamisionari kurejea tena Ghana, Nicholas, mke wake na watoto walijiunga na Kanisa. Nilipomwona mwaka jana, alikuwa kamanda wa Polisi na alikuwa akitumikia kama rais wa Wilaya ya Kanisa ya Tamale Ghana. Yeye anasema: “Kanisa limeyabadilisha maisha yangu. … Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniongoza kwenye injili hii.”3

Alibert Davis, Mghana mwingine, alimsindikiza rafiki katika moja ya majengo ya mikutano ya Kanisa mahali ambapo rafiki yake alikuwa akienda kwenye mkutano wa urais. Wakati akimsubiri rafiki yake, Alibert alisoma kitabu alichokiona jirani karibu naye. Mkutano ulipoisha, Alibert alitaka kwenda nyumbani kitabu kile. Akapewa ruhusa sio tu ya kukichukua kitabu kile, bali pia nakala ya Kitabu cha Mormoni. Alipofika nyumbani, akaanza kusoma Kitabu cha Mormoni. Hakuweza kukiweka chini. Alikisoma kwa mwangaza wa mshumaa hadi saa 9:00 alfajiri. Alifanya hivyo kwa usiku kadhaa, alivutiwa sana na alichokisoma na alichokihisi. Alibert sasa ni muumini wa Kanisa.

Angelo Scarpulla alianza mafunzo yake ya kiteolojia katika nchi yake ya asili ya Italia akiwa na umri wa miaka 10. Mwishowe akawa kasisi na akalitumikia kanisa lake kwa kujitolea. Wakati fulani imani yake ikaanza kuyumba, akatafuta na kupokea fursa ya kusoma zaidi. Kadiri alivyoendelea kujifunza zaidi, hata hivyo, ndivyo alivyozidiwa na shaka. Kile alichokisoma na kujisikia kilimshawishi kwamba kuna ukengeufu mkubwa kutoka kwenye mafundisho yaliyofundishwa na Yesu na Mitume wa kale. Angelo alifanya uchunguzi juu ya dini ya kweli ya Mungu katika imani nyingi tofauti lakini aliachwa akiwa hajaridhika kwa miaka mingi.

Siku moja alikutana na waumini wawili wa Kanisa ambao walikuwa wakiwasaidia wamisionari kutafuta watu zaidi wa kuwafundisha. Akajisikia kuvutika kwao na kwa furaha akasikiliza ujumbe wao. Angelo kwa hiari kabisa akakubali kupokea nakala ya Kitabu cha Mormoni.

Jioni ile akaanza kusoma kitabu kile. Akajisikia kuzidiwa na furaha. Kupitia Roho Mtakatifu, Mungu alimpa Angelo hakikisho kwamba katika Kitabu cha Mormoni yeye angepata ukweli wa kile alichokuwa amekitafuta kwa miaka mingi. Hisia tamu zilimfurika. Kile alichokisoma na kile alichojifunza kutoka kwa wamisionari kilithibitisha hitimisho lake kwamba pamekuwepo na ukengeufu mkubwa, lakini yeye pia alijifunza kwamba Kanisa la kweli la Mungu limerejeshwa duniani. Muda mfupi baadaye Angelo alibatizwa katika Kanisa.4 Nilipokutana naye kwa mara ya kwanza, yeye alikuwa rais wa Tawi la Kanisa la Rimini huko Italia.

Kile Nicholas, Alibert na Angelo walichokiona katika Kitabu cha Mormoni ni mfano wa uzoefu wa Parley  P. Pratt:

“Nilifungua [kitabu] kwa shauku … nikakisoma siku nzima: kula kukawa mzigo, sikuwa na hamu ya chakula; kulala kukawa mzigo usiku ulipoingia, kwani nilichagua kusoma kuliko kulala.

“Nilipokuwa nikisoma roho wa Bwana alikuwa juu yangu, na nilijua na kuelewa kwamba kitabu kile kilikuwa cha kweli, kwa uwazi zaidi na kudhihirisha kama vile mtu anapotambua kwamba yeye anaishi. Furaha yangu sasa ikawa imekamilika, kama ilivyokuwa, na nilifurahi vya kutosha kuliko kama ningelipwa kwa ajili ya huzuni, dhabihu na mateso ya maisha yangu yote.5

Baadhi wanaguswa kwa nguvu sana na Kitabu cha Mormoni mara ya kwanza tu wanapokifungua, lakini kwa wengine ushahidi wa ukweli wake huja taratibu kadiri wanavyosoma na kusali juu yake. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwangu. Kwanza nilikisoma Kitabu cha Mormoni kama kijana mwanafunzi wa seminari. Hii ndiyo nakala ya Kitabu cha Mormoni niliosoma. Siwezi kuwaambia hasa ni wakati gani au mahali iliponitokea, lakini mahali fulani wakati wa kusoma huko, nilianza kuhisi kitu fulani. Kulikuwa na joto na roho fulani ambavyo vilikuja kila wakati nikifungua kitabu hiki. Hisia hii iliendelea kukua kadiri nilivyoendelea na kusoma kwangu. Hisia hiyo inaendelea hadi leo hii. Kila wakati nifunguapo Kitabu cha Mormoni, ni kama ninawasha swichi—Roho hutiririka moyoni na nafsini mwangu.

Bado kwa wengine, ushuhuda wa Kitabu cha Mormoni huja pole pole zaidi, baada ya kujifunza kwingi na sala. Ninaye rafiki ambaye amesoma Kitabu cha Mormoni akitafuta kujua kama ni cha kweli. Alitumia mwaliko ulioko katika Moroni wa kumwomba Mungu kwa moyo wa dhati, na kusudi la kweli na imani katika Kristo, kama Kitabu cha Mormoni ni cha kweli.6 Lakini hakupata mara moja ile ahadi ya jibu la kiroho. Hata hivyo, siku moja, akiwa katika mawazo mazito, akiendesha mteremkoni, Roho alimshuhudia juu ya ukweli wa Kitabu cha Mormoni. Akiwa na furaha nyingi na kuzidiwa na furaha kiasi kwamba alishusha kioo cha gari lake na kupaza sauti , si kwa mtu ye yote, bali kwa ulimwengu wote, “Ni cha kweli!”

Iwe ushuhuda wetu juu ya Kitabu cha Mormoni umekuja mara ya kwanza unapokifungua au baada ya muda, ushuhuda huo utatushawishi siku zote kama tutaendelea kukisoma na kuyafanyia kazi mafundisho yake. Rais Ezra Taft Benson alifundisha: “Kuna uwezo katika kitabu hiki ambao utatiririka katika maisha yako wakati utaanza kujifunza kitabu hiki kwa bidii. Utapata uwezo mkuu wa kushinda majaribu. Utapata uwezo wa kuepuka udanganyifu. Utapata nguvu ya kukaa katika ile njia nyembamba na iliyosonga.”7

Ninamhimiza kila mmoja anayepokea ujumbe huu, ikijumuisha wenye Ukuhani wa Haruni waliokutana katika mkutano huu usiku huu, kugundua nguvu ya Kitabu cha Mormoni. Kama Rais Thomas S. Monson anavyotuhimiza: “Soma Kitabu cha Mormoni Yatafakarini mafundisho yake,. Mwombe Baba wa Mbinguni kama ni cha kweli.”8 Wakati wa mchakato huu wewe utamsikia Roho wa Mungu katika maisha yako. Roho huyo atakuwa sehemu ya ushuhuda wako kwamba Kitabu cha Mormoni ni cha kweli, kwamba Joseph Smith alikuwa nabii wa Mungu, na kwamba Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni Kanisa la kweli la Mungu duniani leo. Ushuhuda huo utakusaidia wewe kushinda majaribu.9 Utakuandaa wewe kwa ajili ya “wito mkuu wa bidii … kufanya kazi kwa katika mashamba ya mizabibu ya Bwana.”10 Utasimama kama nanga ya uhakika wakati shutuma na taarifa zisizo sahihi zitakapotumika kupinga imani yako na utakuwa msingi wa mwamba imara utakapopatwa na changamoto ya maswali magumu usiyoweza kujibu mara moja. Utakuwa na uwezo wa kutambua ukweli na uongo, na utahisi uhakikisho wa Roho Mtakatifu akithibitisha ushuhuda wako tena na tena kadiri unavyoendelea kukisoma Kitabu cha Mormoni katika maisha yako yote.

Pia nakuhimia wazazi wote mnaosikiliza au mtakaosoma ujumbe huu kukifanya Kitabu cha Mormoni kuwa sehemu ya nyumba yenu. Watoto wetu walipokuwa wakikua, tulikuwa tukisoma Kitabu cha Mormoni wakati tukipata kifungua kinywa. Hii ndiyo alamisho ya kitabu tuliyotumia. Mwanzoni ni nukuu kutoka kwa Rais Benson akiahidi kwamba Mungu atamwaga baraka juu yetu tunaposoma Kitabu cha Mormoni.11 Juu ya ganda la nyuma ni ahadi hii kutoka kwa Rais Marion G. Romney mshauri wa zamani katika Urais wa Kwanza: “Ni hakika kwamba kama, katika nyumba yetu, wazazi watasoma kutoka kwa Kitabu cha Mormoni kwa maombi na kila mara, wote peke yako na pamoja na watoto wao, roho ya hicho kitabu kikuu itakuja itaenea nyumbani kwetu na kwa wale wanaoishi ndani yake. … Roho ya ubishi itaondoka. Wazazi watawashauri watoto wao kwa upendo na hekima kuu. Watoto watakuwa wasikivu na watiifu kwa ushauri wa wazazi wao. Wema utaongezeka. Imani, tumaini na hisani—upendo safi wa Kristo—utastawi katika nyumba na maishani mwetu, vikileta kila kukicha amani, shangwe na furaha.”12

Sasa, miaka mingi baada ya watoto wetu kuondoka nyumbani na wanalea familia zao wenyewe, tunaweza kuona kwa uwazi zaidi kutimia kwa ahadi ile ya Rais Romney. Familia yetu iko mbali sana na ukamilifu, lakini tunaweza kushuhudia kuwa juu ya nguvu za Kitabu cha Mormoni na baraka zilizoletwa na kule kusoma na huendelea kuleta katika maisha ya familia yetu yote.

Nguvu kubwa zaidi ya Kitabu cha Mormoni ni uwezo wake wa kutuleta karibu zaidi na Yesu Kristo. Ni ushahidi wenye nguvu juu Yake na huduma Yake ya kukomboa.13 Kupitia hicho tunakuja kufahamu ukuu na uweza wa Upatanisho Wake.14 Kinafundisha mafundisho Yake kwa uwazi zaidi.15 Na kwa sababu ya utukufu wa milango ikielezea kutembelea kwa Kristo mfufuka kwa Wanefi, tunatazama na kuona upendo, baraka, kuwafundisha kwake watu wale na tunakuja kuelewa kwamba Yeye atafanya kwetu vile vile kama tutakuja Kwake kwa kuishi injili Yake.16

Ndugu, nashuhudia nguvu iliyoko katika Kitabu cha Mormoni. Iwe kinasomwa kwa lugha ya Kiingereza, Kiitaliano, au Kifaransa, kama chapisho ama chombo cha elektroniki, nimeona roho ya ajabu ile ile ikitiririka kutoka kwenye milango na aya zake katika maisha yangu. Ninashuhudia juu ya uwezo wake wa kutusaidia sisi kumkaribia Kristo. Ni maombi yangu kwamba kila mmoja wetu atatumia kikamilifu nguvu hizi zilizoko katika kitabu hiki cha ajabu cha maadiko. Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Ona “‘You Can’t Close My Heart’: Ghanaian Saints and the Freeze,” Jan. 6, 2016, history.lds.org.

  2. 2 Nefi 25:26.

  3. Barua pepe kutoka kwa Nicholas Ofosu-Hene, Oct. 27, 2015.

  4. Ona Angelo Scarpulla, “My Search for the Restoration,” Tambuli, June 1993, 16–20; email from Ezio Caramia, Sept. 16, 2016.

  5. Autobiography of Parley P. Pratt, ed. Parley P. Pratt Jr. (1938), 37.

  6. Ona Alma 10:4–5

  7. Teachings of Presidents of the Church: Ezra Taft Benson (2014), 141.

  8. Thomas S. Monson, “Dare to Stand Alone,” Liahona, Nov. 2011, 62; see also Thomas S. Monson, “Priesthood Power,” Liahona, May 2011, 66; A Prophet’s Voice: Messages from Thomas S. Monson (2012), 490–94.

  9. Rais Thomas S. Monson alielezea: “Kila mwenye ukuhani anapaswa kushiriki katika kujifunza maandiko kila siku. … Nawaahidi, hata kama ninyi mna Ukuhani wa Haruni au Ukuhani wa Melkizediki, kama mtajifunza maandiko kwa bidii, uwezo wenu wa kuepuka majaribu na kupokea maelekezo ya Roho Mttakatifu katika yote mnayofanya utaongezeka” (Thomas S. Monson, “Be Your Best Self,” Liahona, May 2009, 68).

  10. Alma 28:14.

  11. “Ninawaahidi kwamba kutoka sasa na kuendelea, kama mtakunywa kutoka kwenye kurasa za [Kitabu cha Mormoni] na kushika mafunzo yake, Mungu atamwaga juu ya kila mtoto wa Sayuni na Kanisa baraka ambazo hazijapata kuonekana” (Teachings: Ezra Taft Benson, 127).

  12. Marion G. Romney, “The Book of Mormon,” Ensign, May 1980, 67.

  13. Ona, kwa mfano, ukurasa wa kichwa wa Kitabu cha Mormoni; 1 Nfi 11; 2 Nefi 25; Mosia 16; 18; Alma 5; 12; Helamani 5; 3 Nefi 9; Mormoni 7.

  14. Ona, kwa mfano, 2 Nefi 2; 9; Mosia 3; Alma 7; 34.

  15. Ona, kwa mfano, 2 Nefi 31; 3 Nephi 11; 27.

  16. Ona 3 Nefi 11–28.