2010–2019
Wasichana Kazini
Aprili 2018


Wasichana Kazini

Kila msichana Kanisani anapaswa kuhisi kuwa anathaminiwa, ana fursa ya kuhudumu, na kuhisi kuwa yeye ana kitu cha thamani anachoweza kuchangia kwenye kazi hii.

Mwaka mmoja uliopita, katika kikao cha ukuhani cha mkutano mkuu Askofu Gerald Caussé alinena na wanaume wa Kanisa akieleza jinsi wenye Ukuhani wa Haruni na Melkizedeki ni washirika wasiotengana katika kutimiza kazi ya wokovu.1 Ujumbe huo umekuwa baraka kuu katika kuwasaidia wavulana walio na Ukuhani wa Haruni kuona sehemu yao wanayofanya katika kujenga ufalme wa Mungu hapa duniani. Huduma yao ya pamoja huimarisha kanisa na kuleta wongofu wa kina na ahadi ya kujitolea katika mioyo ya vijana wanapoona jinsi mchango wao ulivyo wa thamani na jinsi gani kazi hii ilivyo tukufu.

Hivi leo, ningependa maneno yangu yawe kiegemezi kwa ujumbe huo ninaponena kuhusu jinsi wasichana wa Kanisa pia wanavyohitajika na walivyo muhimu katika kutekeleza kazi ya Bwana katika familia zao na kwenye Kanisa Lake.

Kama Askofu Caussé, niliishi kwenye tawi dogo la Kanisa kwa muda wa ujana wangu, na kila mara nilikuwa nikiombwa kutekeleza kazi na miito ambayo kwa kawaida ingefanywa na watu wazima. Kwa mfano wale miongoni mwetu kwenye mipango ya vijana mara nyingi tuliongoza katika kupanga na kutekeleza shughuli zetu wenyewe na matukio maalumu. Tuliandika tamthilia, tuliunda kikundi cha kuimba ili kuburudisha katika shughuli za tawi, na tulikuwa washiriki kamili wa shughuli zote za tawi. Niliitwa kuwa kiongozi wa muziki kwenye tawi na kuongoza uimbaji wakati wa mkutano wa sakramenti kila wiki. Ilikuwa jambo kubwa kwa mtu mwenye umri wa miaka16 kusimama mbele ya watu kwenye tawi kila Jumapili na kuwaongoza katika kuimba nyimbo. Nijisikia kuwa nilihitajika, na nilijua kwamba nilikuwa na kitu cha kuchangia. Watu walinitegemea kuwepo kwangu, na nilifurahia hisia hiyo. Uzoefu huo ulinisiaidia kujenga ushuhuda wangu juu ya Yesu Kristo, kama ulivyofanya kwa Askofu Causse, ulitia nanga maisha yangu ndani ya huduma ya injili.

Kila muumini anapaswa kufahamu ni kwa kiasi gani wanavyohitajika. Kila mtu ana kitu muhimu cha kuchangia na ana talanta na uwezo maalumu ambao unasaidia kupeleka kazi hii muhimu mbele. Vijana wetu wana wajibu wa Ukuhani wa Haruni unaoelezewa kwenye Mafundisho na Maagano ambao wa wazi kabisa. Inaweza kuwa si wazi sana kwa wasichana wa Kanisa, wazazi wao, na viongozi wao, kutoka wakati wanapobatizwa, wasichana wanayo majukumu ya kimaagano “kuomboleza na wale wanaoomboleza; ndio, na kuwafariji wale ambao wanahitaji kufarijiwa, na kusimama kama mashahidi wa Mungu nyakati zote na katika vitu vyote, na katika mahali popote [wa]lipo, hata hadi kifo”2 Wasichana wana fursa ya kutimiza majukumu haya katika kata na matawi yao na wanapohudumu kwenye urais wa madarasa, katika mabaraza ya vijana, na kwenye miito mingine. Kila msichana Kanisani anapaswa kujiona kuwa anathaminiwa, ana fursa ya kuhudumu, na kujiona kuwa yeye ana kitu cha thamani anachoweza kuchangia kwenye kazi hii

Kwenye Handbook 2: Administering the Church tunajifunza kwamba kazi ya wokovu kwenye kata zetu inajumuisha “Kazi ya Muumini mmisionari, kuhakikisha waongofu wanadumu, na kuamsha wale wasio shiriki kikamilifu, kazi ya hekalu na historia ya familia, na kufundisha injili”3 Kazi hii kwenye kata huongozwa na maaskofu wetu waamininfu, walio na funguo za ukuhani kwa ajili ya kata zao. Kwa miaka mingi sasa urais wetu umekuwa ukiuliza swali, “Ni zipi kati ya sehemu zilizotajwa haipaswi wasichana wetu kujihusisha?” Jibu ni kwamba wana kitu cha kuchangia kwenye sehemu hizi zote za kazi hii.

Kwa mfano, hivi majuzi, nilikutana na baadhi ya wasichana kutoka eneo la Las Vegas walioitwa kuhudumu kama washauri wa kazi ya hekalu na historia ya familia kwenye kata. Walikuwa wanang’ara kwa shauku juu ya kuweza kufundisha na kuwasaidia washiriki wa kata yao kuwatafuta mababu zao. Walikuwa na ujuzi wa maana kuhusu kompyuta, walikuwa wamejifunza jinsi ya kutumia FamilySearch, na walikuwa na shauku ya kutoa maarifa hayo kwa wengine Ilikuwa dhahiri kuwa walikuwa na shuhuda na ufahamu wa umuhimu wa kutafuta majina ya mababu zao waliofariki ili ibada za wokovu zinaweza kufanywa hekaluni.

Miezi kadhaa iliyopita, nilipata fursa ya kujaribu dhana moja pamoja na wasichana wawili wenye umri wa miaka 14. Nilipata nakala mbili za ajenda za kata na kuwapa Emma na Maggie kila mmoja nakala moja Niliwauliza kusoma zile ajenda na kuona ikiwa kungekuwa na hatua ya kufanya kwa vipengee vya ajenda hizo za mabaraza ya kata ambamo wao wangeweza kutoa huduma. Emma aliona kuwa familia mpya ilikuwa inahamia kwenye kata hiyo, na akasema angewasaidia kuhamia na kupakua mizigo. Alifikiri kuwa angefanya urafiki na watoto kwenye familia hiyo na kuwatembeza kuona shule yao mpya. Aliona kuwa kulikuwa na chakula kikuu katika kata kilichokuwa kimepangwa na kuona njia nyingi ambazo yeye angetoa huduma yake.

Maggie aliona kuwa kulikuwa na wazee wengi kwenye kata waliohitaji kutembelewa na kujumuishwa katika usharika. Alisema angependa kuwatembelea na kuwa mwenye usaidizi kwa washiriki hawa wakongwe wapendwa. Alisema pia aliona kuwa angesaidia kuwafundisha washiriki jinsi ya kuanzisha na kutumia akaunti za mitandao ya kijamii. Kwa hakika hapakuwa na kitu hata kimoja kwenye zile ajenda ambacho hawangeweza kusaidia!

Je, wale wanaokaa kwenye mabaraza ya kata au wenye miito yo yote kwenye kata wanawaona wasichana kama nyenzo za thamani za kusaidia kukimu mahitaji mengi kwenye kata zetu? Kwa kawaida kuna orodha ndefu ya hali zinazohitaji mtu kuhudumu, na mara nyingi tunafikiria tu watu wazima kwenye kata kukimu mahitaji haya. Kama vile Wenye Ukuhani wa Haruni wamealikwa kufanya kazi na baba zao na wanaume wengine wa Ukuhani wa Melkizedeki, wasichana wetu wanaweza kuitwa kutoa huduma na kuhudumia mahitaji ya washiriki wa kata pamoja na mama zao au wakina dada wengine ambao ni mifano ya kuigwa. Wana uwezo, shauku na wako tayari kufanya hivyo kuliko kuhudhuria tu Kanisa kila Jumapili!

Picha
Msichana akisaidia kununua vyakula
Picha
msichana akihudumu
Picha
Msichana akisaidia katika Kompyuta
Picha
Msichana akisafisha
Picha
Msichana akiongoza nyimbo
Picha
Msichana akifundisha
Picha
Msichana amevaa fulana ya Helping Hands
Picha
Wasichana wakikaribisha Kanisani

Tunapotafakari majukumu ambayo wasichana wetu wanatarajiwa kuchukua katika siku za usoni, tunaweza kujiuliza aina ya uzoefu tunaoweza kuwapa sasa utakaowasaidia katika matayarisho yao ya kuwa wamisionari, wasomi wa injili, viongozi wa vikundi saidizi vya Kanisa, wahudumu wa hekalu, wake, wakina mama, washauri, mifano na marafiki. Wanaweza kwa kweli kuanza leo kuchukua baadhi ya majukumu haya. Vijana kwa kawaida huombwa kufundisha masomo Jumapili darasani mwao. Nafasi sasa zipo kwa wasichana kufanya huduma hekaluni ambayo hapo awali ilifanywa na wafanyakazi wa ibada, au wenye kujitolea wakati wanapohudhuria pamoja na vikundi vyao vya vijana ili kutekeleza ubatizo kwa ajili ya wafu. Wasichana wetu wa umri wa Msingi sasa wanaalikwa kuhudhuria mikutano ya Onyesho la Awali juu ya Ukuhani na Hekalu ambalo litawasaidia kuelewa kuwa wao pia ni washiriki muhimu katika kazi inayoongozwa na ukuhani. Watajifunza kuwa waume, wake, vijana na watoto wote ni wapokeaji wa baraka za ukuhani na wanaweza kuchukua majukumu ya kuendesha kazi ya Bwana.

Maaskofu, tunajua kuwa majukumu yenu huwa mazito, lakini kama mojawapo ya vipaumbele vyenu kusimamia akidi za Ukuhani wa Haruni, Handbook 2 kinaelezea ya kwamba “Askofu na washauri wake watatoa uongozi wa ukuhani kwa ajili ya kikundi cha Wasichana. Wanawalinda na kumwimarisha wasichana binafsi, wakifanya kazi kwa karibu na wazazi na viongozi katika jitihada hii. Pia kinasema kwamba “askofu na washauri wake mara kwa mara watashiriki kwenye mikutano ya Wasichana, huduma, na shughuli zao.”4 Tunawashukuru maaskofu wanaochukua nafasi kutembelea madarasa ya wasichana na wanaotoa fursa kwa wasichana kuwa zaidi ya watazamaji wa kazi. Tunawashukuru kwa kuhakikisha kuwa wasichana wao ni washiriki wanaothaminiwa katika kukimu mahitaji ya washiriki wa kata zao! Nafasi hizi za kuhudumu kwa njia za maana huwabariki zaidi ya shughuli ambazo wanaburudishwa tu.

Kwenu ninyi wasichana wa Kanisa, miaka yenu ya ujana inaweza kuwa yenye shughuli na mara nyingi yenye changamoto. Tumeona kuwa wengi wenu mnahangaika na mambo ya thamani ya nafsi, wasiwasi, mfadhaiko wa kiwango cha juu, na pengine hata huzuni. Kugeuzia mawazo yenu upande wa nje, badala ya kuyaweka matatizo yako ndani kunaweza kusitatue mambo haya yote, lakini huduma mara nyingi inaweza kufanya mizigo yako kuwa miepesi na kufanya changamoto zako kuonekana kuwa si ngumu sana. Njia mojawapo ya kuzidisha hisia za thamani ya nafsi ni kwa kuonyesha kupitia kwa kujali kwetu na huduma kwa wengine, kuwa tunayo mengi ya thamani tunayoweza kuchangia.5 Ninawahimizeni kuinua mikono yenu juu ili kujitolea na kuiweka mikono hiyo kazini pale mwonapo shida zinazowazunguka. Mnapotimiza majukumu yenu ya kimaagano na kushiriki katika kujenga ufalme wa Mungu baraka zitawatiririkia maishani mwenu na mtagundua shangwe kuu na ya kudumu ya ufuasi.

Wakina kaka na wakina dada, wasichana wetu ni wa ajabu. Wanavyo vipaji, shauku isiyo na kipimo na nguvu na wana huruma na wao wanajali. Wanataka kutoa huduma. Wanahitaji kujua kuwa wanathaminiwa na wao ni muhimu kwa kazi ya wokovu. Kama vile wavulana katika Ukuhani wa Haruni hujitayarisha kwa huduma ya juu wakati wanapoingia kwenye Ukuhani wa Melkizediki, wasichana wetu wanajitayarisha kuwa washiriki wa taasisi kubwa zaidi ya wanawake duniani—Muungano wa Usaidizi wa Wakina Mama. Kwa pamoja, wasichana hawa warembo, wenye nguvu, waaminifu na wavulana wanajitayarisha kuwa wake na waume, wakina mama na wakina baba, ambao watalea familia zenye kustahili ufalme wa Mungu wa Selestia.

Ninashuhudia kwamba kazi ya Baba yetu wa Mbinguni ni kuleta kutokufa na uzima wa milele kwa watoto wake.6 Wasichana wetu wa thamani wana nafasi muhimu katika kusaidia kutimiza kazi hii kuu. Katika jina la Yesu Kristo, amina.