2010–2019
Akidi ya Wazee
Aprili 2018


Akidi ya Wazee

Kuwa na akidi moja ya Ukuhani wa Melkizedeki katika kata huunganisha wenye ukuhani katika kutimiza vipengele vyote vya kazi ya ukombozi.

Si muda mrefu baada ya Kanisa kuanzishwa katika kipindi hiki cha mwisho, Bwana alisema katika ufunuo, “Na kwa sala ya imani yenu mtapokea sheria yangu, ili muweze kujua jinsi ya kulitawala kanisa langu na mambo yote yawe sawa mbele yangu”.1 Kanuni hii imekuwa ikifuatwa Kanisani—na kwamba ahadi imeheshimiwa na Bwana—tangu wakati ule. Mfumo wa mpangilio wa ukuhani na huduma umekuwa ukifunuliwa muda hadi muda kwa kuanzia na Nabii Joseph Smith wakati ofisi za ukuhani na akidi zilipoanzishwa katika siku zetu. Maboresho muhimu yalifunuliwa na kutekelezwa wakati wa uongozi wa marais Brigham Young, John Taylor, na Spencer W. Kimball,miongoni mwa wengine kwenye Akidi ya Kumi na Wawili, Sabini, makuhani wakuu, na ofisi na akidi nyingine zote katika Ukuhani wa Melkizedeki na wa Haruni.2 Sasa, katika tamko la kihistoria muda mfupi tu uliopita, Rais Russell M. Nelson ametangaza mabadiliko zaidi ambayo ni muhimu.

Kama naweza kurudia sehemu ya kauli yake: Usiku huu, tunatangaza umuhimu wa kuundwa upya kwa akidi zetu za Ukuhani wa Melkizedeki ili kukamilisha kazi ya Bwana kwa ufanisi zaidi. Katika kila kata, makuhani wakuu na wazee sasa wataunganishwa katika akidi moja ya wazee … [na] utengenezwaji wa akidi ya [makuhani wakuu wa kigingi] utategemea miito ya ukuhani ilivyo sasa.”

Rais Nelson aliongeza:

“Mabadiliko haya yamekuwa katika uchunguzi kwa miezi mingi. Tumeona hitaji la muhimu na haraka la kuboresha jinsi ya kuwahudumia watu wetu. Ili kufanya hivyo vema, tunahitaji nguvu za akidi zetu za ukuhani kutoa mwongozo mkuu zaidi katika utumishi wa upendo na msaada ambao Bwana amekusudia kwa ajili ya Watakatifu Wake.

“Mabadiliko haya yametoka kwa Bwana. Tukiyatekeleza, tutakuwa na ufanisi zaidi kuliko tulivyokuwa hapo nyuma.”3

Kwa mwongozo wa Urais wa Kwanza, Mzee Ronald A. Rasband pamoja nami tutaongezea baadhi ya maelezo ambayo tunaamini yatajibu maswali yenu ambayo mnaweza kuwa nayo.

Akidi za Wazee na Makuhani Wakuu

Kwanza, ili kusisitiza, ni mabadiliko yapi ni kwa ajili ya kundi la makuhani wakuu wa kata na akidi ya wazee? Kwenye kata, washiriki wa akidi ya wazee na kundi la makuhani wakuu sasa wataunganishwa pamoja katika akidi moja ya Ukuhani wa Melkizedeki chini akidi moja ya urais. Akidi hii, imeongezeka katika idadi na umoja, itakuwa ikiitwa kama “akidi ya wazee.” Makundi ya makuhani wakuu hayataendelea kuwepo. Akidi ya wazee inajumuisha wazee wote na wazee watarajiwa katika kata pia makuhani wakuu ambao hawahudumu kwa sasa katika uaskofu, katika urais wa kigingi, katika baraza kuu au kama mapatriaki wanaofanya kazi. Akidi ya makuhani wakuu katika kigingi itaundwa na wale makuhani wakuu ambao wana hudumu katika urais wa Kigingi, uaskofu, katika baraza kuu na kama mapatriaki wanaofanya kazi.

Urais wa Akidi ya Wazee

Ni kwa namna gani urais wa akidi ya wazee utaundwa? Urais wa kigingi utaupumzisha uongozi wa kundi la makuhani wakuu uliopo sasa na urais wa wazee na kuita rais mpya wa akidi ya wazee na washauri katika kila kata. Urais mpya wa akidi ya wazee unaweza kujumuisha wazee na makuhani wakuu, wa rika tofauti na uzoefu, wakihudumu pamoja katika urais wa akidi moja. Mzee au kuhani mkuu anaweza kuhudumu kama rais wa akidi au kama mshauri katika urais. Huu si “utaifishwaji” wa akidi ya wazee na makuhani wakuu. Tunategemea wazee na makuhani wakuu watafanya kazi kwa pamoja katika muunganiko wowote ule katika urais wa akidi na katika huduma za akidi. Mabadiliko haya katika akidi yanapaswa kutekelezwa haraka iwezekanavyo.

Ofisi za Ukuhani katika Akidi ya Wazee.

Je, mabadiliko haya katika muundo wa akidi yanabadili ofisi za ukuhani zinazoshikiliwa na washiriki wa akidi? Hapana, kitendo hiki hakibatilishi ofisi yoyote ya ukuhani ambayo mshiriki wa Akidi alikuwa ametawazwa hapo zamani. Kama mjuavyo, mwanaume anaweza kutawazwa katika ofisi tofauti za ukuhani katika maisha yake, na hapotezi au kufuta kutawazwa kokote kwa awali anapopokea utawazwaji mpya. Wakati katika hali zingine mwenye ukuhani anaweza kutumikia ofisi zaidi ya moja kwa wakati mmoja, kama vile kuhani mkuu pia kuhudumu kama patriaki au askofu, kwa kawaida, hahudumu katika ofisi zote za ukuhani kwa wakati mmoja. Maaskofu na Sabini, kwa mfano, hawahudumu moja kwa moja katika ofisi hizo mara wanapopumzishwa au wanapobakishwa kwa heshima. Hivyo, ofisi yoyote ya ukuhani au ofisi nyingine ambazo mtu huyu anaweza kuhudumu, wakati akiwa mshiriki wa akidi ya wazee, anahudumu kama mzee.

Miaka iliyopita, Rais Boyd K. Packer alieleza kwamba “ukuhani ni mkubwa kuliko ofisi yake yo yote. … Ukuhani ahuonekani kwa macho. Mzee anashikilia ukuhani sawa sawa na ule wa Mtume. (Ona M&M 20:38.) Wakati mwanaume [inapokuwa ukuhani umetunukiwa juu yake], anaupokea wote. Hata hivyo, kuna ofisi ndani ya ukuhani—mgawanyo wa mamlaka na majukumu. Wakati mwingine ofisi moja huzungumziwa kama ya ‘juu kuliko’ au ya ‘chini kuliko’ ofisi nyingine. Badala ya ‘ya juu’ au ‘ya chini,’ ofisi katika Ukuhani wa Melkizedeki huwakilisha maeneo tofauti ya huduma.”4 Natumaini kwamba sote hatutakuwa tukizungumzia tena kuhusu “kupandishwa” kwenye ofisi nyingine katika Ukuhani wa Melkizedeki.

Wazee wataendelea kutawazwa kuwa makuhani wakuu wnapoitwa kwenye urais wa kigingi, baraza kuu au uaskofu—au kwa wakati mwingine kama itakavyo amuliwa na rais wa kigingi kwa njia ya kutafakari kwa sala na mwongozo wa kiungu. Wakati muhula wao wa huduma katika urais wa kigingi, baraza kuu, au uaskofu unapomalizika, makuhani wakuu watajiunga tena na akidi ya wazee katika kata yao.

Mwongozo kwa ajli ya Rais wa Akidi ya Wazee.

Nani huongoza kazi ya rais wa akidi ya wazee? Rais wa kigingi huongoza Ukuhani wa Melkizedeki katika kigingi chake. Kwa hivyo, rais wa akidi ya wazee anawajibika moja kwa moja kwa rais wa kigingi, ambaye hutoa mafunzo na mwongozo kutoka kwa urais wa kigingi na kupitia baraza kuu. Askofu, kama kuhani mkuu kiongozi katika kata, pia hukutana mara kwa mara na rais wa akidi ya wazee. Askofu humshauri na kumpa mwongozo stahiki kuhusu namna bora ya kuhudumu na kuwabariki waumini wa kata, akifanya kazi kwa maelewano na makundi yote ya kwenye kata.5

Madhumuni ya Mabadiliko Haya.

Je, madhumuni ya mabdiliko katika akidi za Ukuhani wa Melkizedeki ni nini? Kuwa na akidi moja ya Ukuhani wa Melkizedeki katika kata huwaunganisha wenye ukuhani huo katika kutimiza vipengele vyote vya kazi ya ukombozi, ikijumuisha kazi ya hekaluni na historia ya familia ambazo hapo awali zilikuwa zikisimamiwa na makundi ya makuhani wakuu. Itaruhusu washiriki wa akidi wa rika na asili zote kunufaika kutokana na mtazamo na uzoefu wa kila mmoja wao na wa wale walio katika hatua tofauti za maisha. Pia itatoa nafasi zaidi kwa wenye ukuhani wenye uzoefu kufundisha wengine, ikijumuisha wale ambao wanatarajia kuwa wazee, waumini wapya, vijana wakubwa na wale wanaorudi katika kushiriki kikamilifu Kanisani. Siwezi kelezea vya kutosha jinsi gani nilivyohamasika kutafakari ongezeko la nafasi muhimu ambayo akidi za wazee zitafanya katika wakati unaokuja. Busara, uzoefu, uwezo na nguvu ambayo itapatikana kwenye akidi hizi ikiashiria siku mpya na kiwango kipya cha huduma ya kikuhani kote katika Kanisa

Miaka ishirini iliyopita katika mkutano mkuu, nilihusisha hadithi ambayo kwanza ilisemwa na Mzee Vaugh J. Featherstone wa wale Sabini ambayo naamini inastahili kurudiwa hapa.

Katika mwaka 1918, kaka George Goates alikuwa mkulima wa viazi sukari huko Lehi, Utah Majira ya baridi yakaja mapema mwaka huo na kugandisha sehemu kubwa ya mazao yake katika ardhi. Kwa George na mwanae mdogo, Francis, kuvuna kulikuwa taratibu na kugumu. Wakati huo huo ugonjwa wa mlipuko wa mafua ulikuwa unatanda. Ugonjwa huu wa kuogofya ulitwaa maisha ya mtoto wa kiume wa George Charles na watoto watatu wadogo wa Charles— mabinti wawili wadogo na mvulana mmoja. Katika kipindi cha siku sita, George Goates mwenye huzuni alisafiri safari tatu tofauti kwenda Ogden, Utah, kuleta miili nyumbani kwa ajili ya maziko. Mwisho wa pumziko kati ya haya matukio ya kuogofya, George na Francis wakafunga mikokoteni yao kwenye farasi na kurudi shambani.

“‘[Njiani] walipita mkokoteni baada ya mkokoteni-ilioibeba viazi vitamu vikiwa vinapelekwa kiwandani na ikiendeshwa na wakulima ambao ni majirani. Walipokuwa wakipita, kila mwendeshaji angetoa salamu: “Habari, kaka George,” “Pole sana, George,” “Pumziko gumu, George,” “Una marafiki wengi sana, George.”

Katika mkokoteni wa mwisho alikuwa ni … mwenye uso wenye madoa Jasper Rolfe. Alitoa salamu ya furaha na kusema kwa sauti: “Hivyo ndivyo vyote kaka George.“

“‘[Kaka Goates] akamgeukia Francis na kusema: Natamani kama vyote vingekuwa ni vyetu.”

“‘Walipofika katika geti la shambani, Francis alishuka chini kutoka kwenye mkokoteni mkubwa mwekundu wa viazi sukari na kufungua geti wakati [baba yake] akiendesha kuingia shambani. [George] akavuta kamba, na kuwasimamisha farasi, … na kukagua shamba. … Hakukuwa na viazi sukari katika shamba lote. Ndipo kikamjia kile Jasper Rolfe alichomaanisha aliposema kwa sauti: “Hivi ndivyo vyote, kaka George!”

“‘[George] akashuka kutoka kwenye mkokoteni, akachukua kiganjani mwake udongo wenye rutuba wa rangi ya kahawia alioupenda sana, na kisha … shina la juu la kiazi sukari, na kuviangalia kwa muda alama hizi wakilishi za kazi yake, kama vile macho yake hayakuamini.

“‘Kisha [yeye] akakaa chini juu ya kusanyiko la mashina ya juu ya viazi sukari—mwanaume huyu ambaye aliwaleta nyumbani kwa ajili ya maziko wapendwa wake wanne katika kipindi cha siku sita pekee; alitengeneza majeneza, alichimba makaburi na hata kusaidia katika nguo za maziko—mwanaume huyu wa kushangaza ambaye kamwe hakusita, wala kulegea, wala kutikisika katika jaribu hili la kuhuzunisha—alikaa juu ya mkusanyiko wa mashina ya juu ya viazi vitamu akilia kama mtoto mdogo.

Kisha alinyanyuka, akafuta macho yake, … akaangalia juu angani, na kusema, “Asante Baba kwa wazee wa kata yetu.’”6

Ndio, shukrani kwa Mungu kwa sababu ya wanaume wa ukuhani na kwa huduma ambayo bado watatoa katika kuwainua watu binafsi na familia na katika kujenga Sayuni.

Urais wa Kwanza, Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, na Urais wa Sabini umetafakari mabadiliko haya kwa kipindi cha muda mrefu. Kwa sala nyingi, kuchunguza kwa makini misingi ya kimaandiko kuhusu akidi za ukuhani, na uthibitisho kwamba haya ni mapenzi ya Bwana, tunasonga mbele kwa umoja katika kile ambacho ni dhahiri kuwa ni hatua moja mbele zaidi katika kufunuliwa kwa Urejesho. Mwongozo wa Bwana umedhihirika, na ninafurahia katika hilo, kama nitoavyo ushuhuda juu Yake, Ukuhani Wake, na kutawazwa kwenu katika ukuhani huo, katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Mafundisho na Maagano 41:3.

  2. Ona kwa mfano, William G. Hartley, “The Priesthood Reorganization of 1877: Brigham Young’s Last Achievement,” in My Fellow Servants: Essays on the History of the Priesthood (2010), 227–64; To the Seventies (instruction presented at a meeting of the First Presidency, the Quorum of the Twelve Apostles, and the Presidency of the Seventy, Apr. 1965, 352); Hartley, “The Seventies in the 1880s: Revelations and Reorganizing, in My Fellow Servants, 265–300; Edward L. Kimball, Lengthen Your Stride: The Presidency of Spencer W. Kimball (2005), 254–58; Richard O. Cowan, “The Seventies’ Role in the Worldwide Church Administration,” in David J. Whittaker and Arnold K. Garr, eds., A Firm Foundation: Church Organization and Administration (2011), 139–60.

  3. Russell M. Nelson, “Maneno ya Ufunguzi,” Liahona, Mei 2018, 54.

  4. Boyd K. Packer, “What Every Elder Should Know—and Every Sister as Well: A Primer on Principles of Priesthood Government,”  Tambuli, Nov. 1994, 17, 19.

  5. Ona Handbook 2: Administering the Church (2010), 7.3.1.

  6. D. Todd Christofferson, “Akidi za Ukuhani,” Liahona, Jan. 1999; ona pia Vaughn J. Featherstone, “Now Abideth Faith, Hope, and Charity,” Ensign, Julai 1973, 36–37.