2010–2019
Mtumaini Bwana
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2019


Mtumaini Bwana

Tegemeo letu pekee la uhakika ni kumtumaini Bwana na upendo Wake kwa watoto Wake.

Wapendwa kaka zangu na dada zangu, barua niliyopokea miaka kadhaa iliyopita ndiyo inatambulisha mada ya hotuba yangu. Mwandishi huyo alikuwa akitafakari juu ya ndoa ya hekaluni kwa mwanaume ambaye mwenza wake wa milele alikuwa amefariki. Yeye angekuwa mke wa pili. Aliuliza swali hili: je, yeye angeweza kuwa na nyumba yake mwenyewe katika maisha yajayo, au angeishi na mumewe huyo na yule mkewe wa kwanza? Nilimwambia tu amtumaini Bwana.

Ninaendelea na uzoefu niliousikia kutoka kwa mshirika aliyethaminiwa, ambao ninaushiriki kwa ruhusa yake. Baada ya kifo cha mkewe kipenzi na mama wa watoto wake, baba alioa tena. Baadhi ya watoto waliokuwa wakubwa walipinga ndoa ile na wakatafuta ushauri kutoka kwa ndugu wa karibu ambaye alikuwa kiongozi wa kuheshimika katika Kanisa. Baada ya kusikiliza sababu za pingamizi zao, ambazo zilizingatia hali na mahusiano katika ulimwengu wa roho au katika falme za utukufu ambazo hufuatia Hukumu ya Mwisho, kiongozi huyu alisema: “Ninyi mna hofu juu ya mambo yasiyo sahihi. Mnapaswa kuwa na hofu juu ya kama ninyi mtafika sehemu hizo. Ongezeni nguvu juu ya hilo. Kama mkifika huko, jambo hili lote litakuwa vizuri ajabu kuliko mnavyofikiria.”

Ni fundisho la faraja iliyoje! Mtumaini Bwana!

Kutoka kwenye barua nilizopokea, ninajua watu wengine wanatatizwa na maswali juu ya ulimwengu wa roho tutakakoishi baada ya kufa na kabla hatujafufuka. Wengine wanadhani kwamba ulimwengu wa roho utaendeleza nyingi ya hali za kidunia na masuala tunayopitia katika maisha haya ya duniani. Je, tunajua nini hasa juu ya hali katika ulimwengu wa roho? Ninaamini makala ya profesa wa dini wa BYU juu ya mada hii ilikuwa sahihi. “Wakati tunapojiuliza sisi wenyewe kile tunachojua juu ya ulimwengu wa roho kutoka kwenye maandiko matakatifu, jibu ni ‘si kama vile daima tunavyofikiri.’”1

Ndiyo, tunajua kutokana na maandiko matakatifu kuwa baada ya miili yetu kufa tunaendelea kuishi kama roho katika ulimwengu wa roho. Maandiko matakatifu pia yanafundisha kwamba ulimwengu huu wa roho umegawanyika kati ya wale waliokuwa “waadilifu” au “wenye haki” wakati wakiishi na wale waliokuwa waovu. Pia yanaelezea namna baadhi ya roho waaminifu wanavyofundisha injili kwa wale roho waovu au waasi (ona 1 Petro 3:19; Mafundisho na Maagano 138:19–20, 29, 32, 37). Muhimu zaidi, ufunuo wa siku za mwisho unafunua kwamba kazi ya wokovu inasonga mbele katika ulimwengu wa roho (ona Mafundisho na Maagano 138:30–34, 58), na ingawa tunahimizwa tusiahirishe toba yetu tukiwa katika mwili wenye kufa (ona Alma 13:27), tunafundishwa kwamba baadhi ya toba inawezekana huko (ona Mafundisho na Maagano 138:58).

Kazi ya wokovu katika ulimwengu wa roho inajumuisha kuziweka huru roho kutoka kwenye kile ambacho maandiko matakatifu mara kwa mara hukielezea kama “kifungo.” Wote katika ulimwengu wa roho wako chini ya aina fulani ya kifungo. Ufunuo mkuu wa Rais Joseph F. Smith, uliofanywa kuwa mtukufu katika sehemu ya 138 ya Mafundisho na Maagano, unaeleza kwamba wale wafu waadilifu, ambao walikuwa katika hali ya “amani”(Mafundisho na Magano 138:22) wakati wakitazamia Ufufuko (ona Mafundisho na Maagano 138:16), “walitazamia kutokuwepo kwa roho zao kutoka kwenye miili yao kama ni utumwa” (Mafundisho na Maagano 138:50).

Waovu pia huteseka utumwa wa ziada. Kwa sababu ya dhambi ambazo hazikufanyiwa toba, wao wako katika kile Mtume Petro alichokitaja kama “kifungo” cha roho (1 Petro 3:19; ona pia Mafundisho na Maagano 138:42). Roho hawa huelezewa kama “waliofungwa” au kama “mateka” (Mafundisho na Maagano 138:31, 42), au kama “waliotupwa nje gizani” pamoja na “kulia, kuomboleza, na kusaga meno” wakati wakisubiri ufufuko na hukumu (Alma 40:13–14).

Ufufuko kwa ajili ya wote katika ulimwengu wa roho ni wa hakika kutokana na Ufufuko wa Yesu Kristo (ona 1 Wakorintho 15:22), ingawa hutokea kwa nyakati tofauti kwa makundi tofauti. Hadi wakati huo ulioteuliwa, kile ambacho maandiko yanatuambia kuhusu shughuli zilizoko katika ulimwengu wa roho kimsingi zinahusu kazi ya wokovu. Mengine machache yamefunuliwa. Injili inahubiriwa kwa wasioijua, wasiotubu, na waasi ili waweze kuwekwa huru kutoka kwenye utumwa wao na kusonga mbele kuelekea kwenye baraka za Baba Mpendwa wa Mbinguni alizoziweka kwa ajili yao.

Utumwa wa ulimwengu wa roho ambao unawahusu nafsi za waongofu waadilifu ni haja yao ya kusubiri—na pengine hata kuruhusiwa kushawishi—utekelezwaji wa ibada zao kwa njia ya uwakilishi duniani ili waweze kubatizwa na kufurahia baraka za Roho Mtakatifu. (ona Mafundisho na Maagano 138:30–37, 57–58).2 Ibada hizi za uwakilishi wa wenye mwili pia huwawezesha wao kusonga mbele chini ya mamlaka ya ukuhani ili kulikuza lile jeshi kubwa la waadilifu ambao wanaweza kuhubiri injili kwa wale roho walioko kifungoni.

Zaidi ya mambo haya ya msingi, vitabu vyetu vya maandiko matakatifu vina taarifa kidogo sana juu ya ulimwengu wa roho ambao hufuatia kifo na hutangulia Hukumu ya Mwisho.3 Je, ni kitu gani kingine tunachokijua kuhusu ulimwengu wa roho? Waumini wengi wa Kanisa wamewahi kupata maono au misukumo mingine ya kiungu ili kuwajulisha wao juu ya jinsi mambo yanavyoenda au yalivyopangwa katika ulimwengu wa roho, lakini matukio haya binafsi ya kiroho hayapaswi kueleweka au kufundishwa kama ni mafundisho rasmi ya Kanisa. Na, ndiyo, kuna mengi ya kukisiwa na waumini pamoja na mengine katika vyanzo vilivyochapishwa kama vitabu juu ya matukio karibu ya mauti.4

Kwa haya yote, tahadhari ya busara ya Wazee D. Todd Christofferson na Neil L. Andersen katika ujumbe wao kwa mkutano mkuu ni muhimu kukumbukwa. Mzee Christofferson alifundisha: “Inapaswa ikumbukwe kwamba si lazima kila maelezo yanayotolewa na kiongozi wa Kanisa, aliyepita au aliyeko sasa, lazima yajumuishe mafundisho. Inaeleweka kawaida katika Kanisa kwamba maelezo yanayotolewa na kiongozi mmoja kwenye tukio moja daima yanawakilisha oni binafsi, ingawaje huwa ni oni lililozingatiwa vyema, ambalo halikukusudiwa kuwa rasmi au la kufuatwa na Kanisa lote.”5

Katika mkutano uliofuata, Mzee Andersen alifundisha kanuni hii: “Mafundisho yanafundishwa na washiriki wote15 wa Urais wa Kwanza na Akidi ya Mitume Kumi na Wawili. Hayajafichwa katika ibara isiyoonekana ya hotuba moja.”6 Tangazo la familia, lililotiwa saini na wote manabii, waonaji na wafunuzi 15 ni kielelezo cha kupendeza cha kanuni hiyo.

Zaidi ya kitu rasmi kama vile tangazo la familia, mafundisho ya kinabii ya Marais wa Kanisa, yakiungwa mkono na manabii na mitume wengine, nayo pia ni mfano wa hili. Juu ya hali katika ulimwengu wa roho, Nabii Joseph Smith alitoa mafundisho mawili karibia na mwisho wa huduma yake ambayo mara kwa mara yamekuwa yakifundishwa na warithi wake. Moja ya hayo ni mafundisho yake katika mahubiri ya Mfalme Follet kwamba washiriki wa familia waliokuwa waadilifu watakuwa pamoja katika ulimwengu wa roho.7 Mengine ni maelezo haya kwenye mazishi katika mwaka wa mwisho wa uhai wake: “Roho za wenye haki huinuliwa kwenye kazi iliyo kuu na tukufu zaidi … [katika] ulimwengu wa roho. … Hawako mbali nasi, na wanajua na kuelewa mawazo yetu, hisia, na mienendo yetu, na mara nyingi wanaumia pamoja nasi.”8

Sasa, vipi kuhusu swali kama lile nililolitaja mwanzoni juu ya wapi roho huishi? Kama swali hilo linaonekana kuwa geni au lenye umuhimu mdogo kwako, fikiria mengi ya maswali yako mwenyewe, au hata yale ambayo umeshawishika kuyajibu kwa msingi wa kitu fulani ulichosikia kutoka kwa mtu mwingine wakati fulani kipindi cha nyuma. Kwa maswali yote juu ya ulimwengu wa roho, napendekeza majibu mawili.. Kwanza, kumbuka kwamba Mungu anawapenda watoto wake na hakika atafanya lililo bora kwa kila mmoja wetu. Pili, kumbuka fundisho hili la Biblia linalofahamika, ambalo limekuwa ni msaada mkubwa kwangu mimi kwenye mengi ya maswali yasiyo na majibu:

“Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe.

“Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako” (Mithali 3:5–6).

Vivyo hivyo, Nefi alihitimisha zaburi yake kwa maneno haya: “Ee Bwana, nimekutegemea wewe, na nitakutegemea wewe milele.” Sitaweka tumaini langu kwenye mkono wa mwanadamu.” (2 Nefi 4:34).

Sote tunaweza kujiuliza kibinafsi juu ya hali katika ulimwengu wa roho, au hata kujadili haya au maswali mengine ambayo hayajajibiwa katika familia au mikutano mingine ya ndani. Lakini tusifundishe au kutumia kama mafundisho rasmi kile ambacho hakitoshelezi viwango vya mafundisho rasmi. Kufanya hivyo hakupeleki mbele kazi ya Bwana na kunaweza hata kuwavunja moyo watu katika kutafuta faraja yao wenyewe au kujengwa kupitia ufunuo binafsi ambao mpango wa Bwana hutoa kwa kila mmoja wetu. Kutegemea kupita kiasi mafundisho binafsi au makisio kunaweza hata kutuvuta kando kutoka kwenye kujikita katika kujifunza na jitihada ambazo zitaendeleza uelewa wetu na kutusaidia kusonga mbele kuelekea njia ya agano.

Mtumaini Bwana ni fundisho linalofahamika na la kweli katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Hilo lilikuwa fundisho la Joseph Smith wakati Watakatifu wa mwanzo walipokabiliwa na mateso makali sana na vikwazo vilivyoonekena haviwezi kushindika.9 Hii bado ni kanuni nzuri zaidi tunayoweza kutumia wakati jitihada zetu za kujifunza au majaribio yetu ya kutafuta faraja yanapokutana na vikwazo katika mambo ambayo bado hayajafunuliwa au kuasiliwa kuwa mafundisho rasmi ya Kanisa.

Kanuni sawa na hiyo inatumika kwa maswali yasiyo na majibu juu ya kuunganishwa katika maisha yajayo au matamanio ya marekebisho mapya kwa sababu ya matukio au uvunjaji sheria duniani. Kuna mengi sana tusiyoyajua ambayo tegemeo letu pekee la uhakika ni kumtumaini Bwana na upendo Wake kwa watoto Wake.

Katika kuhitimisha, kile tunachokijua juu ya ulimwengu wa roho ni kwamba kazi ya Baba na Mwana ya wokovu inaendelea huko. Mwokozi wetu alianzisha kazi ya kutangaza uhuru kwa wafungwa (ona 1 Petro 3:18–19; 4:6; Mafundisho na Maagano 138:6–11, 18–21, 28–37), na kazi hiyo inaendelea kadiri wajumbe wenye kustahili na kufuzu wanavyoendelea kuhubiri injili, ikijumuisha toba, kwa wale ambao bado wanahitaji nguvu ya utakaso (ona Mafundisho na Maagano 138:57). Lengo la hayo yote linaelezwa katika mafundisho rasmi ya Kanisa, yaliyotolewa katika ufunuo wa siku hizi.

“Wafu wanaotubu watakombolewa, kwa njia ya utii kwa ibada za nyumba ya Mungu,

“Na baada ya kulipia adhabu ya uvunjaji wao wa sheria, na kuoshwa safi, watapokea thawabu kulingana na matendo yao, kwa kuwa wao ni warithi wa wokovu” (Mafundisho na Maagano 138:58–59).

Kazi ya kila mmoja wetu ni kufundisha mafundisho ya injili ya urejesho, kushika amri, kupendana na kusaidiana, na kufanya kazi ya wokovu katika mahekalu matakatifu.

Ninashuhudia juu ya ukweli wa yale niliyosema hapa na juu ya kweli zilizofundishwa na zitakazofundishwa katika mkutano huu. Haya yote yamefanywa yawezekane kwa sababu ya Upatanisho wa Yesu Kristo. Kama tunavyojua kutokana na ufunuo wa siku hizi, Yeye “humtukuza Baba, na anaokoa kazi zote za mikono yake” (Mafundisho na Maagano 76:43; msisitizo umeongezwa). Katika Jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Je, kuna nini Upande Mwingine? Mazungumzo na Brent L. Top juu ya Ulimwengu wa roho Religious Educator, vol. 14, no. 2 (2013), 48.

  2. Ona Mafundisho ya Nabii Joseph Smith, sel. Joseph Fielding Smith (1976), 309–10; Joseph Smith, “Shajara, Desemba 1842–Juni 1844; Book 2,” p. 246, The Joseph Smith Papers, josephsmithpapers.org.

  3. Ufunuo kwa Joseph Smith ambao mara kwa mara ulinukuliwa juu ya hali za ulimwengu wa roho unaeleza, “Uhusiano ule uliopo miongoni mwetu hapa utakuwepo miongoni mwetu kule” (Mafundisho na Maagano 130:2). Hii inaweza kuelezea ufalme wa utukufu kuliko ulimwengu wa roho, kwa vile unaendelea, “Isipokuwa utazidishiwa utukufu wa milele, utukufu ambao sasa hatuufaidi” (mstari wa 2).

  4. Kwa mfano, George G. Ritchie, Return from Tomrrow (1978) na Raymond Moody, Life after Life (1975).

  5. D. Todd Christofferson, “Mafundisho ya Kristo,” Liahona, Mei 2012, 88; ona pia Joseph F. Smith, Gospel Doctrine, 5th ed. (1939), 42. Ona, kwa mfano, maelezo katika Mafundisho na Maagano 74:5 ya mafundisho binafsi na Mtume Paulo.

  6. Neil L. Andersen, “Majaribu ya Imani Yako,” Liahona, Nov. 2012, 41.

  7. Ona Mafundisho ya Marais wa Kanisa: Joseph Smith (2007), 175.

  8. Historia ya Kanisa, 6:52; iliyojumuishwa katika Mafundisho ya Nabii Joseph Smith, 326; mara nyingi yamenukuliwa, kama katika Henry B. Eyring, To Draw Closer to God (1997), 122; ona pia Mafundisho ya Marais wa Kanisa: Brigham Young (1997), mlango wa 38, “The Spirit World.”

  9. Ona Teachings: Joseph Smith, 231–33.