2010–2019
Tunda
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2019


Tunda

Wekeni macho yenu na mioyo yenu kufokasi kwa mwokozi Yesu Kristo, na furaha ya milele ambayo huja tu kupitia Kwake.

Ninajua nini mnachokifikiria! Hotuba moja tu zaidi na tutasikia kutoka kwa Rais Nelson. Nikitegemea kuwaweka tayari kwa dakika chache tunapomngojea nabii wetu mpendwa, Nimechagua mada yenye kuvutia sana: somo langu ni tunda.

Picha
Tunda

Pamoja na rangi, umbile la asili, na utamu wa matunda madogo, ndizi, matikiti maji, na maembe, au matunda ya kigeni zaidi kama kiwano au komamanga, tunda kwa muda mrefu limekuwa na uzuri uliopewa thamani

Wakati wa huduma Yake ulimwenguni, Mwokozi alifananisha tunda zuri na mambo ya thamani ya milele. Alisema, “Mtawatambua kwa matunda yao.”1 “Kila mti mwema huzaa matunda mazuri.”2 Alitutia moyo kukusanya “matunda kwa uzima wa milele.”3

Katika ndoto dhahiri ambayo sote tunaijua vizuri katika Kitabu cha Mormoni, nabii Lehi anajikuta katika “giza na ukiwa wa jangwa.” Kuna maji machafu, ukungu wa giza, barabara za ajabu, na njia zilizokataliwa, vilevile fimbo ya chuma4 sambamba na njia iliyosonga na nyembamba inayoongoza kwenye mti mzuri wenye “matunda [ambayo yanamfanya] mtu kuwa na furaha.” Akisimulia ndoto, Lehi anasema: “Nilionja … tunda; … lilikuwa tamu sana, zaidi ya yote ambayo [nilikuwa] nimewahi …kuonja. …. [Na] lilijaza nafsi yangu kwa shangwe tele.” Hili tunda lilikuwa “la kutamanisha [zaidi] [kuliko] matunda yote.”5

Picha
Mti wa uzima na tunda lake tamu.

Maana ya Mti naTunda

Je, mti huu pamoja na matunda yake ya thamani kubwa unaashiria nini? Unawakilisha “upendo wa Mungu”6 na unatangaza mpango wa kupendeza wa ukombozi wa Baba yetu wa Mbinguni. “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanaye wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.”7

Tunda hili la thamani linaashiria baraka za ajabu za Upatanisho wa Mwokozi usioweza kufananishwa. Si tu tutaishi tena baada ya maisha haya, lakini kupitia imani yetu katika Yesu Kristo, toba yetu, na kuzitii amri, tunaweza kusamehewa dhambi zetu na siku moja tutasimama wasafi na tusio na doa mbele ya Baba yetu na Mwanaye.

Kula tunda la mti pia kunaashiria kwamba tunakubali ibada na maagano ya injili ya urejesho—kubatizwa, kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu, na kuingia nyumba ya Bwana kupata endaumenti kwa nguvu kutoka juu. Kupitia neema ya Yesu Kristo na kwa kuheshimu maagano yetu, tunapokea ahadi isiyo na kipimo ya kuishi na familia yetu adilifu milele yote.8

Si ajabu malaika alielezea tunda kama “la kujaza nafsi kwa shangwe.”9 Kwa kweli ndivyo lilivyo!

Changamoto ya Kubaki Mkweli

Kama wote tulivyojifunza, hata baada ya kufurahia tunda la thamani la injili ya urejesho, kubaki mkweli na mwaminifu kwa Bwana Yesu Kristo bado si rahisi kufanyika. Kama ilivyosemwa mara nyingi kwenye mkutano huu, tunaendelea kukabiliana na vurugu na udanganyifu, kiwewe na ghasia, ulaghai na majaribu ambavyo hujaribu kusukuma mioyo yetu mbali kutoka kwa Mwokozi na shangwe na uzuri tuliouzoea katika kumfuata Yeye.

Kwa sababu ya dhiki hii, Ndoto ya Lehi pia inajumuisha onyo! Upande mwingine wa mto ni jengo kubwa na pana lenye watu wa umri wote wakionesha kwa vidole vyao, wakidhihaki, na kukejeli wafuasi waadilifu wa Yesu Kristo.

Watu katika jengo wanawabeza na kuwacheka wale wanaotii amri, wakitumaini kuwaaibisha na kudhihaki imani yao katika Yesu Kristo na katika injili Yake. Na kwa sababu ya mashambulizi ya maneno ya kutilia shaka na dharau yaliyotumwa kwa waumini, baadhi ya hao walioonja tunda wanaanza kuionea aibu injili waliyoikumbatia mwanzo. Vivutio vya uongo vya ulimwengu vinawashawishi; wanaenda mbali kutoka kwenye mti na tunda na, kwa maneno ya maandiko, “[wanaangukia] kwenye njia zilizokataliwa na [wanapotea].”10

Katika ulimwengu wetu wa leo, Wafanyakazi wa adui wanafanya kazi masaa ya ziada, kwa haraka wakijaza jengo kubwa na pana. Upanuzi umeenea ng’ambo ya mto, wakitegemea kuingia katika nyumba zetu, wakati wenye kudhihaki na kubeza wakipiga kelele mchana na usiku kwenye vipaza sauti vyao vya mtandaoni.11

Rais Nelson alielezea, “Adui anaongeza mara nne juhudi zake kuvuruga shuhuda na kukwamisha kazi ya Bwana,”12 Na tukumbuke maneno ya Lehi: “Hatukuwasikiliza.”13

Ingawa hatuhitaji kuogopa, lazima tujilinde. Nyakati zingine, mambo madogo yanaweza kushinda usawa wetu wa kiroho. Tafadhali usiruhusu maswali yako, matusi ya wengine, marafiki wasio na imani, au makosa ya bahati mbaya na masikitiko kukuondosha kwenye baraka nzuri, halisi, na za kuridhisha-nafsi ambazo huja kutoka kwenye tunda la thamani la mti. Wekeni macho yenu na mioyo yenu kufokasi kwa mwokozi Yesu Kristo, na furaha ya milele ambayo huja tu kupitia Kwake.

Imani ya Jason Hall

Katika mwezi Juni, mimi na mke wangu, Kathy, tulihudhuria mazishi ya Jason Hall. Wakati wa kufariki kwake, alikuwa na umri wa miaka 48 na akihudumu kama rais wa akidi ya wazee.

Haya ni maneno ya Jason kuhusu tukio ambalo lilibadili maisha yake:

“[Nikiwa na umri wa miaka 15] [nilipata] ajali wakati wa kupiga mbizi . … [Nilivunja ] shingo yangu na nikapooza kuanzia kifuani kwenda chini. Nilipoteza kabisa udhibiti wa miguu yangu na kwa kiasi udhibiti wa mikono yangu. Sikuweza tena kutembea, kusimama, … au kujilisha mwenyewe. Niliweza kwa shida kupumua au kuzungumza.”14

“‘Mpendwa Baba [wa Mbinguni],’ Niliomba, ’kama ningeweza tu kuwa na mikono yangu, Ninajua ningeweza kufanikiwa. Tafadhali, Baba, tafadhali. …

“… ’Baki na miguu yangu, Baba; [ninaomba] tu kwa ajili ya matumizi ya mikono yangu.”15

Jason kamwe hakupata matumizi ya mikono yake. Unaweza kusikia sauti kutoka jengo kubwa na pana? “Jason Hall, Mungu hasikii sala zako! Kama Mungu ni Mungu mwenye upendo, je, angewezaje kukuacha kama hivi? Kwa nini kuwa na imani katika Kristo?” Jason Hall alisikia sauti zao, lakini hakuwatilia maanani. Badala yake alisherehekea tunda la mti. Imani Yake Katika Yesu Kristo ikawa isiyotikisika. Alihitimu kutoka chuo kikuu na kumuoa Kollete Coleman katika Hekalu, akimwelezea kama “mpenzi wa maisha yake.”16 Baada ya miaka 16 ya ndoa, muujiza mwingine, mwana wao wa thamani, Coleman, alizaliwa.

Picha
Jason na Kolette Hall
Picha
Familia ya Hall

Waliweza vipi kukuza imani yao? Kolette alielezea: “Tuliamini katika mpango wa Mungu. Na ulitupatia tumaini. Tulijua kwamba Jason [katika siku za baadaye] angekuwa mzima. … Tulijua kwamba Mungu alitupatia Mwokozi, ambaye dhabihu yake ya upatanisho inatuwezesha kuendelea kutazama mbele wakati tunapotaka kukata tamaa.”17

Picha
Coleman Hall

Akizungumza kwenye mazishi ya Jason, Coleman mwenye umri wa miaka 10 alisema baba yake alimfundisha: “Baba wa Mbinguni [ana] mpango kwa ajili yetu, maisha ya duniani yangekuwa ya kupendeza, na tungeweza kuishi katika familia. … Lakini … tungepaswa kupitia mambo magumu na tungefanya makosa.”

Coleman aliendelea: “Baba wa Mbinguni alimtuma Mwanaye, Yesu, duniani. Kazi yake ilikuwa ni kuwa mkamilifu. Kuponya watu. Kuwapenda. Na kisha kuteseka kwa ajili ya maumivu yetu yote, huzuni, na dhambi. Kisha alikufa kwa ajili yetu. Kisha Coleman aliongeza, “Kwa sababu alifanya hivi, Yesu anajua jinsi ninavyojisikia sasa hivi.

“Siku tatu baada ya Yesu kufa, Yeye … alifufuka tena, na mwili wake mkamilifu. Hii ni muhimu kwangu kwa sababu ninajua kwamba … mwili wa [baba] yangu utakuwa mkamilifu na tutakuwa pamoja kama familia.”

Picha
Familia ya Hall

Coleman alihitimisha: “Kila usiku tangu nilipokuwa mtoto, baba yangu aliniambia, ‘Baba anakupenda, Baba wa Mbinguni anakupenda, na wewe ni mvulana mzuri.’”18

Furaha Huja Kwa sababu ya Yesu Kristo

Rais Russell M. Nelson alielezea kwa nini familia ya Hall ina furaha na tumaini. Alisema:

“Furaha tunayoihisi inahusika kwa kiasi kidogo na hali ya maisha yetu na inahusika na kila kitu kinachohusu fokasi ya maisha yetu.

“Wakati fokasi ya maisha yetu ipo kwenye mpango wa Mungu wa wokovu … na Yesu Kristo na injili Yake, tunaweza kuhisi furaha bila kujali nini kinatokea—au hakitokei—katika maisha yetu. Furaha inakuja kutoka Kwake na kwa sababu Yake. Yeye ni kiini cha furaha yote. …

“Ikiwa tunautazama ulimwengu … , kamwe hatutaijua furaha. … [Furaha] ni zawadi ambayo huja kwa makusudi kujaribu kuishi maisha ya uadilifu, kama ilivyofundishwa na Yesu Kristo.”19

Ahadi pale Unaporudi

Kama umekuwa huna tunda la mti kwa muda fulani, tafadhali jua kwamba mikono ya Mwokozi daima imenyooshwa kwako. Anaita kwa upendo, “Tubuni na mje kwangu.”20 Tunda lake linapatikana kwa wingi na siku zote lipo katika msimu. Haliwezi kununuliwa kwa pesa, na hakuna yeyote anayelitamani tunda kiukweli anayenyimwa.21

Ikiwa unatamani kurudi kwenye mti na kuonja tunda kwa mara nyingine, anza kwa kusali kwa Baba yako wa Mbinguni. Amini katika Yesu Kristo na katika nguvu ya dhabihu ya upatanisho Wake. Ninakuahidi kwamba unapomtegemea Mwokozi “katika kila wazo,”22 tunda la mti litakuwa lako tena, tamu kwa ladha yako, lenye shangwe kwenye nafsi yako, “zawadi kubwa mno kuliko zote ya Mungu.”23

Picha
Mzee Andersen akiwa na Watakatifu Warreno kwenye kuwekwa wakfu kwa Hekalu la Lisbon

Wiki mbili zilizopita leo, Niliona furaha ya tunda la Mwokozi kwenye maonesho ya wazi wakati mimi na mke wangu, Kathy, tulipohudhuria kuwekwa wakfu Hekalu la Lisbon Ureno. Kweli za injili ya urejesho zilifunguliwa Ureno mnamo mwaka 1975 wakati uhuru wa kidini ulipopatikana. Watakatifu wengi waadilifu ambao mwanzo walionja tunda wakati kulikuwa hakuna mikusanyiko, hakuna makanisa, na hakuna hekalu lililo karibu na maili 1000 (km1,600) walifurahi pamoja nasi kwamba tunda la thamani la mti sasa litapatikana katika nyumba ya Bwana iliyopo Lisbon, Ureno. Ni kwa jinsi gani nina heshima na staha kwa Watakatifu hawa wa Siku za Mwisho walioweka mioyo yao imara kwa Mwokozi.

Mwokozi alisema, “Yeye akaaye ndani yangu, Nami ndani yake, huyo huzaa matunda mengi: maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote.”24

Akizungumza asubuhi hii kwa waumini wa Kanisa ulimwenguni kote, Rais Nelson alisema, “Wapendwa akina kaka na dada zangu, ninyi ni mifano hai ya matunda ambayo huja kutokana na kufuata mafundisho ya Yesu Kristo. Kisha aliongeza: “ninawashukuru! Ninawapenda!”25

Tunakupenda, Rais Nelson.

Mimi ni shahidi wa nguvu ya ufunuo ambayo ipo juu ya Rais wetu mpendwa. Yeye ni nabii wa Mungu. Kama Lehi wa kale, Rais Russell M. Nelson anatuita sisi na familia zote za Mungu kuja na kula tunda la mti. Na tuwe na unyenyekevu na nguvu kufuata ushauri wake.

Kwa unyenyekevu ninashuhudia kwamba Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu. Upendo Wake, nguvu na neema Yake huleta vitu vyote vyenye thamani isiyo na mwisho. Ninashuhudia hivyo katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Mathayo 7:16.

  2. Mathayo 7:17.

  3. Yohana 4:36.

  4. Mapema Januari 2007, wakati nikijiandaa kwa ajili ya hotuba ya ibada ya Chuo Kikuu cha Brigham Young kama mshiriki wa Urais wa wale Sabini iliyopaswa kutolewa March 4, 2007, nilimuuliza Mzee David A. Bednar kile alichokuwa akiandaa kwa ajili ya hotuba ya Februari 4, 2007 mbele ya hadhira hiyo hiyo. Nilistaajabishwa wakati alipojibu kwamba hotuba yake ilikuwa kuhusu kung’ang’ania fimbo ya chuma. Hiki kilikuwa kichwa cha habari sawasawa na kile nilichokuwa nimechagua kwa ajili ya hotuba yangu. Baada ya kushiriki maandishi yetu na kila mmoja, tulitambua kwamba mbinu zetu zilikuwa tofauti. Hotuba ylake, yenye kichwa “Bwawa la Maji ya Uzima,” ilisisitiza fimbo ya chuma, au neno la Mungu, kama linavyozunguka maandiko. Katika hotuba yake aliuliza, “Je, mimi na wewe tunasoma, kujifunza, na kutafuta kila siku maandiko katika njia ambayo inatuwezesha kung’ang’ania kwenye fimbo ya chuma?” (speeches.byu.edu).

    Kisha, wiki moja tu baada ya mazungumzo yangu na Mzee Bednar, Rais Boyd K. Packer alitoa hotuba ya ibada ya BYU iliyoitwa “Wewe na Ndoto ya Lehi.” Rais Packer alisisitiza fimbo ya chuma kama ufunuo na uvuvio binafsi ambao huja kwetu kupitia Roho Mtakatifu. Alisema: “Ikiwa utang’ang’ania fimbo, unaweza kuhisi njia yako mbele kwa kipawa cha Roho Mtakatifu. … Kamata fimbo ya chuma, na usiiachie. Kupitia nguvu ya Roho Mtakatifu, unaweza kuhisi njia yako kupitia maisha” (Jan. 16, 2007, speeches.byu.edu).

    Mada yangu, “Ng’ang’ania Maneno ya Manabii,” mnamo Machi 2007 ilikuwa fimbo ya chuma kama kiwakilishi cha maneno ya manabii walio hai (Mach. 4, 2007, speeches.byu.edu).

    Muunganiko wa mahubiri haya matatu haukuwa bahati mbaya. Mkono wa Bwana ulikuwa kazini wakati mahubiri matatu, yaliyoandaliwa kwa ajili ya hadhira moja, yalipoonesha vipengele vitatu vya fimbo ya chuma, au neno la Mungu: (1) maandiko, au maneno ya manabii wa kale; (2) maneno ya manabii walio hai; na (3) nguvu ya Roho Mtakatifu. Ulikuwa ni uzoefu muhimu wa kujifunza kwangu.

  5. Ona 1 Nefi 8:4–12.

  6. 1 Nefi 11:25.

  7. Yohana 3:16.

  8. Ona David A. Bednar, “Ndoto ya Lehi: Kung’ang’ania Daima Fimbo ya chuma,” Liahona, Okt. 2011. 32–37.

  9. 1 Nefi 11:23.

  10. 1 Nefi 8:28.

  11. Ona Boyd K. Packer, “Wewe na Ndoto ya Lehi” ( ibada ya Chuo Kikuu cha Brigham Young , Jan. 16, 2007), speeches.byu.edu.

  12. Russell M. Nelson, “Tunaweza Kufanya Vizuri Zaidi na Kuwa Wazuri Zaidi,” Liahona, Mei 2019, 68.

  13. 1 Nefi 8:33.

  14. Steven Jason Hall, “The Gift of Home,” New Era Des. 1994,12.

  15. Steven Jason Hall, “Mikono Saidizi,” New Era, Okt.1995,46,47.

  16. Mawasiliano Binafsi kwa Mzee Andersen kutoka kwa Kolette Hall.

  17. Mawasiliano Binafsi kwa Mzee Andersen kutoka kwa Kolette Hall.

  18. Mahubiri ya mazishi na Coleman Hall, yaliyoshirikiwa na Mzee Andersen kutoka kwa Kolette Hall.

  19. Russell M. Nelson, “Shangwe na Kunusurika Kiroho,” Liahona, Nov. 2016, 82. 84.

  20. 3 Nefi 21:6.

  21. Ona 2 Nefi 26:25, 33.

  22. Mafundisho na Maagano 6:36.

  23. 1 Nefi 15:36.

  24. Yohana 15:5.

  25. Russell M. Nelson, “Amri Kuu ya Pili,” Liahona, Nov. 2019, 100.