2010–2019
Kupatikana kupitia Nguvu ya Kitabu cha Mormoni
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2019


Kupatikana kupitia Nguvu ya Kitabu cha Mormoni

Wote lazima wapate uzoefu na kupatikana kwa nguvu ya kweli zilizomo ndani ya Kitabu cha Mormoni.

Nikiwa natembelea waongofu katika nyumba zao, mojawapo ya maswali ninayopenda kuwauliza mara nyingi ni jinsi gani wao na familia zao walijifunza kuhusu Kanisa na jinsi walivyofikia kubatizwa. Haijalishi ikiwa kwa wakati ule mtu ni muumini anayeshiriki kikamilifu au hajahudhuria kanisani kwa miaka mingi. Jibu mara zote ni lile lile: kwa tabasamu na uso wao mchangamfu, wanaanza kusimulia hadithi ya jinsi walivyopatikana. Kwa kweli, inaonekana kwamba hadithi ya uongofu daima ni hadithi ya jinsi tulivyopatikana.

Yesu Kristo Mwenyewe ni Bwana wa vitu vilivyopotea. Anajali vitu vilivyopotea. Ndiyo maana Alifundisha mifano mitatu ambayo tunaipata katika sura ya 15 ya Luka: mfano wa kondoo aliyepotea, sarafu iliyopotea, na, mwishowe, mwana mpotevu. Hadithi hizi zote zina asili inayofanana: Haijalishi kwa nini walipotea. Haijalishi hata ikiwa walikuwa na ufahamu kwamba walipotea. Hapo hutawala kwa wingi hisia ya shangwe ambayo hutamka, “Furahini pamoja nami; kwa kuwa nimekwisha kupata [kile] kilichopotea.”1 Mwishowe, hakika hakuna kilichopotea Kwake.2

Niruhusuni kushiriki pamoja nanyi alasiri hii mojawapo ya vitu vya thamani zaidi kwangu—hadithi ya jinsi mimi mwenyewe nilivyopatikana.

Kabla sijatimiza miaka 15, nilialikwa na mjomba wangu Manuel Bustos kuwa pamoja naye na familia yake hapa Marekani. Hii ilikuwa ni nafasi nzuri kwangu kujifunza Kiingereza. Mjomba wangu alikuwa amejiunga na Kanisa miaka mingi awali, na alikuwa na roho kuu ya umisionari. Labda hiyo ndiyo sababu mama yangu, bila mimi kujua, alizungumza naye na kusema angekubali mwaliko kwa sharti moja: kwamba asingejaribu kunishawishi kuwa muumini wa Kanisa lake. Tulikuwa Wakatoliki, na tulikuwa tokea vizazi, na hapakuwa na sababu ya kubadilika. Mjomba wangu alikuwa katika makubaliano kamili na alitimiza ahadi yake kiasi kwamba hakutaka kujibu hata maswali rahisi kuhusu Kanisa.

Ndiyo, kile mjomba wangu na mke wake mpendwa, Marjorie, hawangeweza kuepuka ilikuwa kuwa vile walivyokuwa.3

Niliwekwa kwenye chumba ambacho kilikuwa na maktaba kubwa ya vitabu. Ningeweza kuona kwamba katika maktaba hii kulikuwa na karibu nakala 200 za kitabu cha Mormoni katika lugha tofauti, 20 kati ya hivyo kwa Kihispania.

Siku moja, kwa shauku, nilichukua nakala ya Kitabu cha Mormoni cha Kihispania.

Picha
Kitabu cha Mormoni kwa Kihispania

Kilikuwa ni mojawapo ya zile nakala zenye jalada la samawati, kikiwa na picha ya malaika Moroni kwa mbele. Nilipokifungua, kwenye ukurasa wa kwanza paliandikwa ahadi ifuatayo: “Na mtakapopokea vitu hivi, ningewashauri kwamba mngemwuliza Mungu, Baba wa Milele, katika jina la Kristo, ikiwa vitu hivi si vya kweli; na ikiwa mtauliza na moyo wa kweli, na kusudi halisi, mkiwa na imani katika Kristo, atawaonyesha ukweli wake kwenu, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.”

Na kisha ikaongeza: “Na kwa uwezo wa Roho Mtakatifu mtajua ukweli wa vitu vyote.”4

Ni vigumu kuelezea matokeo ambayo maandiko haya yalileta katika akili na moyo wangu. Kusema kweli, nilikuwa sitafuti “ukweli.” Nilikuwa kijana mdogo, mwenye furaha na maisha yake, nikifurahia utamaduni huu mpya.

Hata hivyo, kwa ahadi ile akilini, kwa siri nilianza kusoma kitabu. Wakati niliposoma zaidi, nilielewa kuwa ikiwa nilitaka kupata chochote kutoka kwenye hili, nilipaswa kuanza kuomba. Na sote tunajua kile kinachotokea wakati unapoamua si tu kusoma bali pia kuomba kuhusu Kitabu cha Mormoni. Hakika, hicho ndicho kilichotokea kwangu. Ilikuwa ni kitu maalumu na cha kipekee sana—ndio, sawa na kile kilichotokea kwa mamilioni ya wengine kote ulimwenguni. Nilikuja kujua kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwamba Kitabu cha Mormoni kilikuwa cha kweli.

Kisha nilienda kwa mjomba wangu kumwelezea kile kilichotokea na kwamba nilikuwa tayari kubatizwa. Mjomba wangu alishindwa kuzuia mshangao wake. Aliingia katika gari lake, akaenda uwanja wa ndege, na kisha kurudi akiwa na tiketi yangu ya ndege ya kunirudisha nyumbani, pamoja na ujumbe ulioelekezwa kwa mama yangu ambao ulisema, “Mimi sikuhusika na hili!”

Kwa upande mmoja alikuwa sahihi. Nilikuwa nimepatikana moja kwa moja kupitia nguvu za Kitabu cha Mormoni.

Kunaweza kuwa na wengi ambao wamepatikana kupitia wamisionari wetu wa kupendeza ulimwenguni kote, katika kila tukio kupitia njia za kimiujiza. Au labda wamepatikana kupitia marafiki ambao Mungu amewaweka kwa makusudi kwenye njia yao. Yawezekana ikawa kwamba wamepatikana kupitia mtu kutoka katika kizazi hiki au kupitia mmoja wa mababu zao.5 Haijalishi ilitokeaje, ili kuweza kuendelea kwenye uongofu wa kweli wa kibinafsi, mapema badala ya baadaye, wote lazima wapate uzoefu na kupatikana kwa nguvu za kweli zilizomo ndani ya Kitabu cha Mormoni. Wakati huo huo, lazima waamue wao binafsi kuweka ahadi ya dhati kwa Mungu kwamba watajitahidi kutii amri Zake.

Baada ya kurudi Buenos Aires, mama yangu aligundua kwamba kiukweli nilitaka kubatizwa. Kwa kuwa nilikuwa na roho fulani ya uasi, badala ya kunipinga mimi, kwa busara zake alikuwa upande wangu. Na bila hata kujua, alinifanyia mwenyewe mahojiano yangu ya ubatizo. Kwa Hakika, ninaamini kwamba mahojiano yake yalikuwa ya kina zaidi kuliko yale yanayofanywa na wamisionari wetu. Aliniambia: “Kama unataka kubatizwa, nitakuunga mkono. Lakini kwanza nataka nikuulize maswali kadhaa, na nataka ufikirie kwa kina sana na unijibu kwa uaminifu. Je! unaweka msimamo kuhudhuria kanisani kila Jumapili?”

Nilimwambia, “Ndiyo, nitafanya hivyo.”

“Je, unajua lolote kuhusu kanisa linakuwa kwa masaa mangapi?”

“Ndiyo, ninajua,” nilisema.

Alijibu, “Sawa, kama utabatizwa, nitahakikisha kwamba unahudhuria.” Kisha akaniuliza kama kweli nilikuwa radhi kutokunywa pombe au kuvuta sigara.

Nilimjibu, “Ndiyo, nitakubaliana na hayo pia.”

Kwa hilo pia aliongeza, “kama utabatizwa, nitahakikisha kwamba unafanya hivyo.” Na aliendelea hivyo kwenye karibu kila amri.

Mjomba wangu alikuwa amempigia simu mama yangu kumwambia asiwe na wasiwasi, kwamba muda si mrefu ningeachana na hili. Miaka minne baadaye, nilipopokea wito wangu wa kuhudumu katika Misheni ya Uruguay Montevideo, mama yangu alimpigia simu mjomba wangu kumuuliza ni lini hasa ningeachana na haya yote. Ukweli ni kwamba toka wakati nilipobatizwa, mama yangu alikuwa mama mwenye furaha.

Nilikuja kujua kuwa Kitabu cha Mormoni kilikuwa muhimu katika mchakato wa uongofu kwa kujionea mwenyewe ahadi kwamba “mwanadamu angemkaribia Mungu zaidi kwa kufuata mafunzo yake.”6

Nefi alielezea kusudi kuu la Kitabu cha Mormoni kwa njia hii:

“Kwani tunajitahidi kuandika, kuwashawishi watoto wetu, na pia ndugu zetu, kumwamini Kristo, na kupatanishwa na Mungu. …

“Na [hivyo] tunazungumza kuhusu Kristo, tunafurahia katika Kristo, tunahubiri kuhusu Kristo, [na] tunatoa unabii kumhusu Kristo … ili watoto wetu wajue asili ya kutegemea kwa msamaha wa dhambi zao.”7

Kitabu cha Mormoni chote kimejaa kusudi hilo takatifu.

Kwa sababu hii, msomaji yeyote anayeweka msimamo wa kukisoma kwa dhati, kwa roho ya sala, si tu atajifunza kuhusu Kristo bali atajifunza kutoka kwa Kristo—hasa ikiwa wanafanya uamuzi wa “kujaribu matokeo ya neno”8 na kutolikataa katika hatua ya mwanzo kutokana na madhara ya kutoamini9 kwenye kile wengine walichosema kuhusu vitu ambavyo hawajawahi kamwe kuvisoma.

Rais Russell M. Nelson anakumbuka: “Ninapofikiria Kitabu cha Mormoni, ninafikiria neno nguvu. Kweli za Kitabu cha Mormoni zina nguvu ya kuponya, kufariji, kurejesha, kusaidia, kuimarisha, kuliwaza, na kufurahisha nafsi zetu.”10

Mwaliko wangu alasiri hii kwa kila mmoja wetu, bila kujali tumekuwa waumini wa Kanisa kwa muda gani, ni kuiruhusu nguvu ya kweli za Kitabu cha Mormoni kutupata na kutukumbatia kwa mara nyingine na siku baada ya siku tunapotafuta kwa bidii ufunuo binafsi. Itafanya hivyo ikiwa tutairuhusu.

Ninashuhudia kwa dhati kwamba Kitabu cha Mormoni kina utimilifu wa injili ya Yesu Kristo na kwamba Roho Mtakatifu atathibitisha ukweli wake muda baada ya muda kwa mtu yeyote ambaye, kwa moyo wa dhati, anatafuta maarifa kwa wokovu wa roho zao.11 Katika Jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Luka 15:6; ona pia Luka 15:9, 32.

  2. Katika hali yake pana, maandiko yana unabii ambao huzungumzia kukusanyika kwa makabila yaliyopotea ya Israeli (ona Russell M. Nelson, “Kukusanya Israeli Iliyotawanyika,” Liahona, Nov. 2006, 79–82). Japokuwa wamepotea, hawajapotea Kwake (ona 3 Nefi 17:4). Pia, ni ya kuvutia kujua hawatambui kwamba walikuwa wamepotea mpaka wakati wanapopatikana, hasa wakati wanapopokea baraka yao ya patriaki.

  3. Mzee Dieter F. Uchtdorf alimnukuu Mtakatifu Francis wa Assisi wakati aliposema, “Hubiri injili nyakati zote na ikiwezekana, tumia maneno (“Kusubiri kwenye Njia ya Dameski,” Liahona, Mei 2011, 77; ona pia William Fay na Linda Evans Shepherd, Share Jesus without Fear [1999], 22).

  4. Moroni 10:4–5.

  5. Hadithi ya uongofu ya mababu zetu ni hadithi yetu pia. Mzee William R. Walker alifundisha, “Litakuwa jambo la kupendeza ikiwa kila Mtakatifu wa Siku za Mwisho akijua hadithi za uongofu wa mababu zao” (“Ishi Mkweli katika Imani,” Liahona, Mei 2014, 97). Hivyo, sote katika njia fulani tumepatikana moja kwa moja au kupitia mababu zetu, shukrani kwa Baba yetu wa Mbinguni, anayejua mwisho kutokea mwanzo (ona Ibrahimu 2:8).

  6. Dibaji ya Kitabu cha Mormoni; ona pia Alma 31:5.

  7. 2 Nefi 25:23, 26.

  8. Alma 31:5

  9. Ona Alma 32:28.

  10. Russell M. Nelson, “Kitabu cha Mormoni: Maisha Yako Yangekuaje Bila Hicho?Liahona, Nov. 2017, 62.

  11. Ona 3 Nefi 5:20.