2010–2019
Kuwa Mwaminifu, Siyo Asiye na Imani
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2019


Kuwa Mwaminifu, Siyo Asiye na Imani

Lazima kwa kudhamiria tuchukue muda kila siku ili kujitenga na duniani na kuungana na mbingu.

Si muda mrefu uliopita niliamka na kujiandaa kusoma maandiko. Nilichukua simu janja yangu na kukaa kwenye kiti karibu na kitanda changu nikiwa na lengo la kufungua Gospel Library app. Nilifungua simu yangu na nilikuwa karibu nianze kusoma wakati nilipoona nusu dazani ya taarifa za ujumbe na barua pepe ambazo ziliingia usiku. Niliwaza, “kwa haraka nitazipitia jumbe hizi, na kisha kurudi kwenye maandiko.” Hakika, masaa mawili baadaye nilikuwa bado nikisoma ujumbe, barua pepe, muhtasari wa habari, na machapisho kwenye mitandao ya kijamii. Nilipotambua ilikuwa saa ngapi, kwa hofu nilifanya haraka kwenda kujiandaa kwa ajili ya siku. Asubuhi ile nilikosa kusoma maandiko yangu, na kwa bahati mbaya sikupata lishe ya kiroho niliyoitegemea.

Lishe ya Kiroho

Nina hakika wengi wengu mnaweza kulinganisha. Tekinologia za kisasa zinatubariki kwa njia nyingi. Zinaweza kutuunganisha na marafiki na familia, na taarifa, na habari kuhusu matukio yanayotokea sasa ulimwenguni kote. Hata hivyo, zinaweza pia kutuvuruga kwenye muunganiko muhimu sana: muunganiko wetu na mbingu.

Ninarudia kile ambacho nabii wetu, Rais Russell M. Nelson, amesema: “Tunaishi katika ulimwengu wenye tabia changamani na wenye ongezeko la mabishano. Upatikanaji endelevu wa mitandao ya kijamii na mzunguko wa taarifa za habari za saa 24 zinatushambulia na ujumbe usiokoma. Kama tunataka kuwa na matumaini yoyote ya kuchekecha kupitia sauti nyingi na falsafa za watu ambazo zinashambulia ukweli, lazima tujifunze kupokea ufunuo.

Rais Russell M. Nelson aliendelea kuonya kwamba, “Katika siku zijazo, haitawezekana kuendelea kuishi kiroho bila mwongozo, maelekezo, faraja na ushawishi endelevu wa Roho Mtakatifu.”1

Miaka kadhaa iliyopita, Rais Boyd K. Packer alizungumzia kundi la kulungu ambao, kwa sababu ya kuanguka kwingi kwa theluji, walikwama nje ya makao yao ya asili na walikabiliwa na njaa kali. Baadhi ya watu wema, katika juhudi za kutaka kuwaokoa kulungu, walijaza nyasi kuzunguka eneo—siyo chakula ambacho kulungu huwa wanakula, lakini walitegemea kingewasaidia kwa kipindi cha baridi. Kwa masikitiko, kulungu walio wengi walipatikana wakiwa wamekufa. Walikuwa wamekula nyasi, lakini hazikuwastawisha, na walishikwa na njaa huku matumbo yao yakiwa yamejaa.2

Ujumbe mwingi ambao unatufukia katika zama za taarifa ni mlinganisho wa kiroho unafanana na kuwalisha nyasi kulungu—tunaweza kuula siku nzima, lakini hauwezi kutustawisha.

Wapi tunapata lishe ya kweli ya kiroho? Mara nyingi, haisambai kwenye mitandao ya kijamii. Tunaipata wakati “tunasonga mbele” kwenye njia ya agano, “daima kushikilia fimbo ya chuma,” na kula tunda la mti wa uzima.3 Hii ina maana kwamba lazima kwa kudhamiria tuchukue muda kila siku ili kujitenga na duniani na kuungana na mbingu.

Katika ndoto yake, Lehi aliwaona watu waliokula tunda lakini wakaliacha kwa sababu ya ushawishi wa jumba kubwa na pana, kiburi cha ulimwengu.4 Inawezekana kwa vijana kulelewa katika nyumba ya Mtakatifu wa Siku za Mwisho, kuhudhuria mikutano na madarasa yote sahihi ya Kanisa, hata kushiriki katika ibada hekaluni, na kisha kwenda kwenye “njia zilizokataliwa na [kupotea].”5 Kwa nini hili linatokea? Katika hali nyingi ni kwa sababu, wakati wao wanaweza kuwa wanakwenda katika mwendo wa kiroho, walikuwa hawakuongoka kikamilifu. Walilishwa lakini hawakurutubishwa.

Picha
Shughuli ya vijana

Kinyume chake, nimekutana na wengi wenu vijana Watakatifu wa Siku za Mwisho ambao ni hodari, imara, na waaminifu. Mnajua kwamba ninyi ni wana na mabinti za Mungu na kwamba Yeye ana kazi kwa ajili yenu. Mnampenda Mungu kwa “moyo wenu wote, uwezo, akili na nguvu.”6 Mnatii maagano yenu na kuwatumikia wengine, mkianzia nyumbani. Mnaonesha imani, mnatubu, na kuendelea kufanya vizuri kila siku, na hili linawaletea furaha ya kudumu. Mnajiandaa kwa baraka za hekalu na fursa nyingine mtakazokuwa nazo kama wafuasi wa kweli wa Mwokozi. Na mnasaidia kuuandaa ulimwengu kwa ajili ya Ujio wa Pili, mkiwaalika wote kuja kwa Kristo na kupokea baraka za Upatanisho Wake. Mmeunganishwa na mbingu.

Picha
Safari ya hekaluni ya vijana

Ndiyo, mnakumbana na changamoto. Lakini ni kwa kila kizazi. Hizi ni siku zetu, na tunatakiwa kuwa waaminifu, siyo wasiyo na imani. Ninashuhudia kwamba Bwana anajua kuhusu changamoto zetu, na kupitia uongozi wa Rais Nelson, anatuandaa kukabiliana nazo. Ninaamini kwamba wito wa nabii wa hivi karibuni wa kanisa linalolenga nyumbani, na kusaidiwa na kile tunachofanya katika majengo yetu,7 umekusudiwa kutusaidia kuendelea kuishi—hata kufanikiwa—katika siku hii ya utapia mlo wa kiroho.

Inayolenga Nyumbani

Inamaanisha nini kuwa kanisa linalolenga nyumbani? Nyumbani panaweza kuonekana tofauti kote ulimwengu. Unaweza kuwa katika familia ambayo imekuwa Kanisani kwa vizazi vingi. Au unaweza kuwa ni muumini pekee wa Kanisa katika familia yako. Unaweza kuwa kwenye ndoa au mseja, una watoto nyumbani au huna.

Bila kujali hali yako, unaweza kuifanya nyumba yako iwe kitovu cha kujifunza na kuishi injili. Kwa urahisi inamaanisha kuchukua majukumu binafsi kwa ajili ya uongofu wako na ukuaji wako kiroho. Inamaanisha kufuata ushauri wa Rais Nelson “[kurekebisha] nyumba yako kuwa kimbilio la imani.”8

Adui atajaribu kukushawishi kwamba lishe ya kiroho siyo ya lazima au, kwa ujanja zaidi, kwamba inaweza kungojea. Yeye ni bwana wa kuvuruga na mjuzi wa kuahirisha. Ataleta mambo mengine ambayo yanaonekana kuwa ya haraka lakini kiuhalisia, siyo muhimu hivyo. Atakufanya “uwe na mashaka juu ya vitu vingi” hata upuuze “jambo moja [ambalo] linahitajika.”9

Ninashukuru sana kwa “wazazi wangu wema,”10 ambao waliilea familia yao katika nyumba yenye lishe endelevu ya kiroho, mahusiano ya upendo, na shughuli za kuburudisha. Mafundisho waliyonifundisha katika ujana wangu yamenifanya niwe imara. Wazazi, tafadhali jengeni mahusiano imara na watoto wenu. Wanahitaji zaidi muda wenu, na si vinginevyo.

Inayosaidiwa na Kanisa

Mkifanya hivyo, Kanisa lipo kuwasaidieni. Uzoefu wetu kanisani unaweza kuchochea lishe ya kiroho ambayo inatokea nyumbani. Hadi kufikia hapa mwaka huu, tumeona aina hii msaada wa Kanisa katika Shule ya Jumapili na Msingi. Tutaona mengi ya hayo katika Ukuhani wa Haruni na mikutano ya Wasichana pia. Kuanzia Januari hii, mtaala wa mikutano hii utarekebishwa kidogo. Bado utafokasi kwenye mada za injili, lakini mada hizo zitafungamana na Njoo, Nifuate—Kwa Ajili ya Watu binafsi na Familia. Hili ni badiliko dogo, lakini linaweza kuleta matokeo makubwa kwenye lishe ya kiroho kwa vijana wadogo.

Ni aina gani nyingine ya msaada ambayo Kanisa linatoa? Kanisani tunapokea sakramenti, ambayo inatusaidia sisi kufanya upya msimamo wetu kwa Mwokozi kila wiki. Na Kanisani tunakusanyika pamoja na waumini wengine ambao wamefanya maagano sawa na hayo. Mahusiano ya upendo tunayojenga na wafuasi wenzetu wa Yesu Kristo yanaweza kuwa msaada wenye nguvu kwenye ufuasi wetu uliolenga nyumbani.

Nilipokuwa na miaka 14, familia yangu ilihamia katika ujirani mpya. Sasa, hii inaweza kutoonekana kama janga baya kwako, lakini katika akili yangu, wakati huo, ilikuwa ya kuumiza. Ilimaanisha kuzungukwa na watu ambao sikuwajua. Ilimaanisha kwamba wavulana wengine wote katika kata yangu wangehudhuria shule tofauti na ile ambayo mimi nilihudhuria. Na katika fikra zangu za miaka 14, niliwaza, “Inawezekana vipi wazazi wangu wanifanyie hivi?” Nilihisi kana kwamba maisha yangu yameharibiwa.

Hata hivyo, kupitia shughuli zetu za Wavulana, niliweza kujenga mahusiano na waumini wengine wa akidi yangu, na wakawa rafiki zangu. Kwa kuongezea, washiriki wa uaskofu na washauri wa Ukuhani wa Haruni walianza kupendezewa na maisha yangu. Walihudhuria matukio yangu ya kimichezo. Waliniandikia ujumbe wa kunitia moyo ambao nimeutunza hadi leo hii. Waliendelea kuwasiliana na mimi baada ya kwenda chuoni na wakati nilipoondoka kwenda misheni. Mmojawapo hata alikuwepo uwanja wa ndege niliporudi nyumbani. Daima nitakuwa mwenye shukrani kwa ndugu hawa wema na mchanganyiko wao wa upendo na matarajio ya juu. Walinielekeza mbinguni, na maisha yakawa safi, yenye furaha, na shangwe.

Ni kwa jinsi gani sisi, kama wazazi na viongozi, tunawasaidia vijana kujua kwamba hawako peke yao wakati wakitembea katika njia ya agano? Mbali na kujenga mahusiano binafsi, tunawaalika kwenye mikusanyiko mikubwa na midogo—kutoka kwenye mikutano ya Kwa Nguvu ya Vijana na kambi za vijana hadi kwenye shughuli za kila wiki za akidi na darasa. Kamwe usidharau nguvu inayotokana na kukusanyika pamoja na wengine ambao pia wanajaribu kuwa imara. Maaskofu na viongozi wengine, tafadhali zingatieni katika kulisha watoto na vijana katika kata zenu. Wanahitaji zaidi muda wenu, na si vinginevyo.

Iwe wewe ni kiongozi, jirani, mshiriki wa akidi, au Mtakatifu mwenza, kama una fursa ya kugusa maisha ya kijana mdogo, msaidie kuunganika na mbingu. Ushawishi wako unaweza kuwa hasa “Msaada wa Kanisa” ambao kijana anahitaji.

Akina kaka na akina dada, ninashuhudia kwamba Yesu Kristo ndiye kiongozi wa Kanisa hili. Yeye anawavuvia viongozi wetu na kutuongoza sisi kwenye lishe ya kiroho tunayohitaji ili kuendelea kuishi na kustawi katika siku za mwisho. Lishe hiyo ya kiroho itatusaidia sisi kuwa waaminifu na siyo wasio na imani. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.